Historia ya Kanisa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Historia ya Kanisa ni fani inayochunguza historia ya Ukristo na ya miundo yake mbalimbali tangu Kanisa lilipoanzishwa na Yesu Kristo katika karne ya 1 hadi leo.

Kwa kawaida historia hiyo hugawanywa katika hatua nne:

 1. kipindi cha Mitume wa Yesu na Mababu wa Kanisa (karne I-karne IX)
 2. Karne za kati (karne IX-karne XV)
 3. kipindi cha marekebisho (karne XVI-karne XVIII)
 4. kipindi cha sasa (karne XIX-karne XXI)

Pande mbili za Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Kwa mtazamo wa imani, historia hiyo yote inaonyesha upande mmoja udhaifu na ukosefu wa Wakristo hata katika ngazi za juu, lakini pia uwezo wa neema ya Mungu wa kuleta watakatifu wapya katika mazingira yoyote.

Ni kwamba kwa Wakristo, Kanisa ni kitu kizuri na muhimu sana. Ni bibiarusi wa Yesu, ni mwili wa Kristo, ni chombo cha Mungu cha kuunganisha waumini wake kwa Roho Mtakatifu. Limepewa na Mungu wito wa kuwaletea watu Neno lake. Hivyo linatangaza Habari Njema, ambayo ni faraja kwa watu wanaotaka kukata tamaa. Linaombea watu. Linasaidia wenye dhiki. Linatetea haki za binadamu. Ndiyo sababu ya kusema: Nasadiki Kanisa takatifu.

Lakini Kanisa lina upande mwingine. Kati ya habari za siku zetu tunaweza kusikia juu ya magomvi ndani ya madhehebu fulani. Viongozi wanaweza kushindana. Vikundi vinaweza kujitokeza na kujitenga na Kanisa. Mambo ya hela yanaweza kupata uzito kuliko mambo ya kiroho. Masharti ya ajabuajabu yasiyo na msingi katika imani na mafundisho ya mitume, yanaweza kuzushwa ghafla na kutangazwa kuwa ya lazima mbele za Mungu.

Tukiingia katika historia ya Kanisa kwa undani tunapata habari nyingi za kusikitisha. Ni kwamba Wakristo ni binadamu. Waliopokea wokovu katika Kristo wako njiani kwenda mbinguni. Lakini bado ni wanadamu wenye dhambi na wenye kasoro. Kasoro hizo za kibinadamu zinaonekana katika historia ya Kanisa pia.

Mwanzilishi wa Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Komunyo ya Mitume, kadiri ya Luca Signorelli, 1512.

Mwanzo wa Kanisa ni kule Yerusalemu, mji mkuu wa nchi inayoitwa kwa majina mbalimbali katika historia yake ndefu, kama Kanaani, Israeli, Palestina au Uyahudi.

Mnamo mwaka 30 BK Yesu wa Nazareti alikufa msalabani. Aliuawa na serikali ya kikoloni ya Kiroma. Liwali (gavana) Mroma, kwa jina Pontio Pilato, alitoa dhidi yake hukumu ya mauti kwa sababu ya maombi ya viongozi wa Kiyahudi.

Yesu alishtakiwa mbele yake kuwa anataka kujipatia cheo cha Mfalme wa Wayahudi yaani kupindua utawala wa Kiroma. Viongozi Wayahudi wenyewe waliona kosa lake ni kwamba amejitangaza kwa uongo kuwa Masiya au Mwana wa Mungu. Lakini hilo halikuwa kosa machoni pa Waroma (ambao walikuwa Wapagani), hivyo wakatumia mashtaka yaliyoeleweka mbele za Pontio Pilato.

Biblia ya Kikristo inatuambia jinsi wafuasi wa Yesu walivyoanza kukata tamaa lakini baadaye wakakutana na Yesu aliyefufuka. Akaonana nao na kuwafundisha katika kipindi cha siku arobaini baada ya Pasaka na hatimaye akapaa mbinguni.

Mwanzo wa Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Pentekoste ya Mitume ilivyochorwa mnamo mwaka 586 katika Biblia ya Rabbula nchini Iraki.

Siku ya hamsini baada ya Pasaka mji wa Yerusalemu ulijaa wageni kutoka sehemu nyingi za dunia. Walikuwa Wayahudi na watu waliovutiwa na dini yao: walikuwa wamefika kushiriki sikukuu za Kiyahudi.

Siku hiyo wanafunzi wa Yesu walimpokea Roho Mtakatifu. Matokeo yake ni kwamba walitoka nje ya mkutano wao wakaanza kumshuhudia Bwana wao mbele ya watu wote. Wengi wakasikia na wengi wakaamini wakabatizwa.

Kati ya wasikilizaji wa mahubiri ya wafuasi wa Yesu walikuwepo watu kutoka Asia, Ulaya na Afrika Kaskazini, na baadhi yao wakabatizwa. Ndio mwanzo wa ushirika wa Kikristo.

Siku ile inaitwa "Pentekoste": neno hilo la Kigiriki, maana yake ni "hamsini", yaani siku 50 baada ya Pasaka. Pentekoste ni sikukuu ya kuzaliwa kwa Kanisa.

Wote waliobatizwa siku ya Pentekoste "waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu, kumega mkate na kusali".(Mdo 2:42).

"Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja".(Mdo 2:44)

"Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kukabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake". (Mdo 4:32-35).

Ushirika wa Wakristo leo unaonekana tofauti katika mambo mbalimbali. Tusishangae: Yesu alitumia mfano wa mbegu ndogo inayotarajiwa kuwa mti mkubwa baadaye. Watu 120 wa kwanza wamekuwa leo 2,500,000,000! Picha aliyotuachia Luka si sheria ambayo ni lazima tuifuate, bali ni mfano bora tu kwetu, ambao tuzingatie kwamba kila mahali mazingira ni tofauti.

Tangu miaka 2000 Wakristo wamepata kusikia tena na tena habari hizo wakapata mawazo mazuri jinsi gani ya kujenga jumuiya ya kindugu na ya kusaidiana katika mazingira yao hapa duniani.

Mpaka leo tabia kadhaa zilizotajwa katika Biblia zinakubalika kuwa alama za Kanisa:

 • a. kujifunza toka kwa mitume wa Yesu
 • b. kuishi pamoja kindugu na kuwasaidia wanyonge
 • c. kumega mkate, yaani kushiriki sakramenti
 • d. kusali

Hali ya kushirikiana mali zote haikuendelea kama utaratibu wa kawaida wa Wakristo wote. Lakini kutokana na mfano huo zimejitokeza jumuiya mbalimbali katika maisha ya Kanisa.

Maendeleo wakati wa Mitume[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa maisha ya Mitume, dhuluma zilizotabiriwa na Yesu zilianza kutoka kwa Wayahudi wasiomuamini na kutoka kwa watu wengine. Wa kwanza kuuawa alikuwa Stefano, na kati ya Mitume Yakobo Mkubwa.

Kabla ya kufa, wengi kwa kuuawa, mitume waliweka waandamizi wao, ambao kati yao walitajwa maaskofu mapadri na mashemasi. Mapema ulipatikana muundo mmoja wa uongozi kila jimbo, yaani askofu mmoja akisaidiwa na mapadri na mashemasi, badala ya mitindo mbalimbali iliyojitokeza awali. Ni hasa Ignas wa Antiokia ambaye katika barua zake anathibitisha muundo huohuo kila mahali alipopitia kutoka Siria hadi Italia mwanzoni mwa karne ya 2.

Katika barua hizo Ignas anaonyesha heshima ya pekee kwa Kanisa la Roma akiandika kuwa "linasimamia upendo". Hiyo ilichangiwa na kwamba mjini Roma ndiko Mitume Petro na Paulo walipomfia Yesu katika dhuluma ya Kaisari Nero (64-68).

Kati ya mambo muhimu zaidi yaliyojitokeza wakati wa Mitume ni maandishi mbalimbali ambayo baadhi yake yalianza kukusanywa na katika karne zilizofuata yalikuja kuunda Agano Jipya kama sehemu ya pili ya Biblia.

Maandishi ya kwanza ni barua zilizoandikwa na Mtume Paulo na wengineo tangu mwaka 50 hivi. Tangu mwaka 65 hivi zilianza kupatikana Injili, ambazo ni vitabu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Luka mwinjili aliiongezea ile ya kwake kitabu cha pili (Matendo ya Mitume) kuhusu uenezi wa Kanisa kutoka Yerusalemu hadi Roma. Hatimaye kuna kitabu cha Ufunuo ambacho peke yake ni kwa kinabii, kikitumia mtindo wa kiapokaliptiko.

Uandishi (na halafu uteuzi) wa vitabu hivyo 27 kati ya vingine vyote ni sehemu muhimu ya maendeleo ya Kanisa chini ya Roho Mtakatifu.

Baada ya hapo vitabu viliendelea kuandikwa kwa kutetea, kutangaza na kufafanua imani sahihi: hivyo havikukusanywa katika Agano Jipya, lakini ndivyo mwanzo wa teolojia kama fani maalumu. Tofauti za ufafanuzi huo, kama zile kati ya shule ya Aleksandria na shule ya Antiokia, ndizo chanzo cha mabishano yaliyochangia mafarakano makubwa yaliyotokea hasa katika karne ya 5, ingawa kuanzia mwaka 325 mitaguso mikuu ilikusanya maaskofu wengi kutoka sehemu mbalimbali ili kumaliza migogoro. Tofauti za lugha na utamaduni, pamoja na utaifa, zilichangia sana mafarakano.

Uenezi katika karne za kwanza[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilipofikia kilele cha uenezi wake mwaka 117.

Ukristo katika karne za kwanza ulienea haraka katika mabara matatu: Asia Magharibi, Afrika Kaskazini na Ulaya ya Kusini na Magharibi, mbali ya maeneo ya mbali zaidi kama Nubia, Ethiopia, Persia hadi India.

Siri mojawapo ya uenezi huo ni kuwepo kwa Dola la Roma. Serikali yake ilitawala nchi nyingi kuanzia kando ya Sahara upande wa kusini mpaka Uholanzi na Uingereza wa leo upande wa kaskazini, halafu kutoka milima ya Mesopotamia (leo Iraq) upande wa mashariki mpaka Ureno wa leo upande wa magharibi.

Watu wa Roma walifaulu kujenga dola hilo kubwa katika muda wa karne nyingi. Kwa jumla walitawala kwa hekima, hivyo wakafaulu kuendelea muda mrefu. Mwanzoni uraia ulikuwa kwa wakazi huru wa mji wa Roma tu, lakini polepole hata wakazi wa maeneo mengine chini ya Roma wakapewa haki za uraia.

Uwepo wa dola hilo ulisaidia sana uenezaji wa Ukristo. Ingawa watawala wake walijaribu muda mrefu kupinga imani mpya, kuwepo kwa utaratibu mmoja katika eneo kubwa hivyo kulisaidia kazi ya mitume na wahubiri wa Injili. Sababu ni kwamba:

 • a. katika eneo kubwa hakuna mipaka inayoweza kuzuia usafiri na mawasiliano. Ukisafiri leo kutoka Moroko kuelekea Misri unavuka mipaka minne, unahitaji pasipoti na vibali vingi kila safari.
 • b. kulikuwa na usafiri. Merikebu zilizunguka pote katika Mediteranea zikibeba mizigo na watu. Waroma pia walikuwa hodari kujenga barabara kwenye nchi kavu. Walihitaji barabara hizo kwa matumizi ya kijeshi lakini zilisaidia pia mawasiliano mengine ya kiuchumi na usafiri.
 • c. Walitumia popote hela moja, wakawasiliana katika lugha zilezile za Kigiriki na Kilatini. Mashariki Kigiriki kilikuwa lugha ya elimu ya juu na ya biashara. Magharibi walitumia zaidi lugha ya Kilatini. Mpaka leo lugha hizo ni muhimu kama lugha za elimu. Kwa mfano maneno mengi ya sayansi (fizikia, kemia, biolojia, jiografia n.k.) yanayotumiwa katika lugha mbalimbali, asili ni ileile ya Kigiriki.

Utawala wa Kiroma ulileta kipindi kirefu cha amani na cha maendeleo ya kiuchumi. Lakini maendeleo hayo yalijengwa juu ya utaratibu mkali wa unyonyaji wa nchi na mikoa ndani ya dola. Kila sehemu wakazi walipaswa kulipa kodi. Kama kabila fulani lilijaribu kupinga utawala wa Roma wanajeshi wake wakafika haraka na kuzima ghasia.

Kwa mfano Wayahudi walipojaribu kujipatia uhuru tena mnamo mwaka 70 B.K. mji wa Yerusalemu uliharibiwa kabisa na wakazi wote wakauzwa utumwani. Watoto wa watumwa wakawa watumwa vilevile. Njia nyingine ya kugeuzwa mtumwa ilikuwa kutolipa madeni. Mdaiwa aliweza kushtakiwa na aliposhindwa kulipa aliuzwa mwenyewe kama malipo ya madeni yake.

Idadi ya watumwa ilikuwa kubwa: katika mikoa kadhaa ya Dola la Roma watumwa walikuwa asilimia 20 za wakazi wote. Wengi wao walikuwa na maisha mabaya, lakini wengine waliweza kupata maendeleo na hata kupewa uhuru na mabwana wao.

Wale watumwa walifurahia sana kusikia mafundisho mapya ya kwamba kila mtu ni mtoto wa Mungu na anapendwa naye. Wakashangaa sana kusikia ya kwamba Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za watu wote, na Mungu hajali sifa au cheo cha mtu. Wakiingia katika ushirika wa Kikristo waliweza kushangaa wanavyoruhusiwa kukutana na watu huru na hata matajiri. Ibada za kipagani zilitenga matabaka ya kijamii. Haikuwa kawaida kwa tajiri kusali pamoja na watumishi wake.

Watumwa walisikia katika ibada za Wakristo nyaraka za Mtume Paulo zinazokazia usawa kati ya Wakristo wote, akisititiza ya kwamba Wakristo wote watazamane kama ndugu na viungo vya mwili mmoja. "Maana katika Roho mmoja tulibatizwa sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru"(1Kor 12:13)

Ndiyo sababu ujumbe wa Kristo ulienea hasa kati ya maskini na watumwa. Lakini hata watu wa matabaka ya juu walivutwa na neno la Injili na mfano mzuri wa maisha ya Wakristo, uhodari wao katika mateso mbalimbali na utaratibu wao wa kusaidiana.

Dhuluma za muda mrefu katika Dola lote la Roma (64-313)[hariri | hariri chanzo]

Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika nchi zinazozunguka Mediteranea katika mabara matatu. Mataifa mengi waliishi chini ya utawala wake. Utawala huo ulianza kabla ya Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya 5 baada ya Kristo upande wa magharibi wa bahari ya Kati na hadi karne ya 15 upande wa mashariki.

Kwa jumla serikali ya Roma iliwaachia watu uhuru waendelee na desturi au mila zao ila tu ilikuwa lazima walipe kodi na kukubali utawala mkuu.

Watu wengi sana walikuwa na imani ya miungu mingi. Waliabudu mahekaluni mbele ya sanamu za miungu ile. Walikuwa na imani ya kwamba miungu ilifanana kiasi na wanadamu ila ni mikubwa na yenye nguvu zaidi na inaishi milele. Vinginevyo waliamini miungu kuwa na tabia nyingi zinazofanana na tabia za kibinadamu.

Kwa upande mwingine waliamini ya kwamba hata mtu anaweza kupanda ngazi na kuwa kama mungu akiwa na sifa za kutosha zinazokubalika mbele za miungu yote na hasa mungu mkuu. Ndiyo asili ya kumtangaza mtawala mkuu au Kaisari wa Roma kuwa na sifa za kimungu.

Dhuluma ya kwanza yalitokea mwaka 64 BK, ya mwisho mwaka 309 BK. Katika kipindi hicho kirefu, vilirudia tena na tena vipindi vya mateso vikifuatana na vipindi vya amani. Lakini miaka yote Ukristo ulikuwa dini isiyo halali. Kila mara mateso yaliweza kuanza upya.

Mwishoni mwa karne ya 1 B.K. Kaisari Domitiano alianza kudai ibada za kimungu kwake mwenyewe. Popote katika eneo kubwa la Dola la Roma watu waliitwa kusimamisha sanamu zake na kumwabudu. Kwa wakazi wengi jambo halikuwa geni sana maana yake kwao jina moja liliongezeka katika orodha ya miungu iliyoabudiwa. Lakini kwa Wakristo tendo hili lilikuwa gumu mno. Imani ya Kikristo hukataa kuwepo kwa miungu mingi, vilevile hukataza kuiabudu.

Basi, Wakristo walikataa kuabudu sanamu za Kaisari. Tendo hili lilionekana kama kusaliti serikali. Wakuu wa mikoa na majimbo walianza kuwaadhibu wale wanaokataa ibada hiyo.

Lakini katika mwendo wa miaka ibada za sanamu za Kaisari zikaongezeka. Matatizo yakakua, vita vikaongezeka, uchumi na biashara vikashuka chini. Thamani ya fedha ikapungua. Watu wengi wakaanza kukata tamaa na kutafuta msaada katika dini mbalimbali. Hivyo mafundisho ya kidini yalizidi. Hapo wazo lilikua la kuwa anayekana kuwepo kwa miungu ni hatari kwa umma. Ni mwasi atakayesababisha hasira ya miungu juu ya watu wote: ni lazima aadhibiwe.

Katika hali hiyo Wakristo walijenga utaratibu mzuri wa kufundishana na kusaidiana katika matatizo. Halafu wakakaza sana mafundisho ili waumini wasimame imara katika matatizo na dhuluma. Wakaendelea kuombea serikali na watu wote. Wakajitahidi kuonyesha kwa maisha na matendo yao ya kwamba Ukristo ni imani yenye amani na upendo isiyoharibu umma. Wakakutana katika nyumba za watu binafsi, au kule Roma pia kwenye "katakombi" yaani makaburini chini ya ardhi kwani polisi haikuruhusiwa kuingia makaburini.

Pia wasomi walijitokeza kuandika vitabu ili kutetea Ukristo dhidi ya masingizio na chuki ya wengi; walifafanua imani ilivyo na kuonyesha kwamba maisha ya wafuasi wa Yesu hayaendi kinyume cha sheria za dola, hivyo dhuluma dhidi yao hazikubaliki.

Uhuru wa dini katika dola na matokeo yake[hariri | hariri chanzo]

Mozaiki ya Konstantino pamoja na bombwe la majengo ya Konstantinopoli.

Mateso ya Wakristo yaliendelea mpaka mwaka 311. Lakini idadi yao iliendelea kuongezeka kote katika Dola la Roma. Mwaka 312 B.K. mtu kwa jina Konstantino alitafuta Ukaisari (cheo cha mtawala mkuu) akishindana na mgombea mwingine. Inasemekana siku moja aliota ndoto, akaona alama ya msalaba akasikia sauti iliyosema: "Kwa alama hii utashinda". Hapo aliwaruhusu wanajeshi wake waliokuwa Wakristo kusali akamshinda mgombea mwingine katika vita. Mwaka 313 B.K. Kaisari Konstantino akatangaza sheria iliyoruhusu Wakristo kuabudu kwa uhuru. Ukristo ukawa dini inayokubaliwa katika Dola la Roma.

Kipindi kipya kikaanza katika historia ya Ukristo. Kwa wengi hali hiyo ilikuwa ajabu la Mungu mwenyewe aliyemaliza matatizo yao, jinsi Biblia ilivyosema katika kitabu cha Ufunuo. Wakristo wakazidi kujenga na kupamba makanisa kila mahali. Vilevile ibada zilizidi kupangwa kwa utaratibu mzuri wa matini na vitendo. Maaskofu waliweza kukutana bila matatizo. Mikutano ya maaskofu (mitaguso ya ngazi mbalimbali) iliamua juu ya masuala na matatizo yaliyojitokeza.

Mwaka 325 mkutano wa kwanza wa Kanisa zima ukafanyika kule Nisea (Asia Ndogo). Wakristo wa nchi mbalimbali walikuwa wanatofautiana katika maelezo yao juu ya tabia ya Kimungu na ya kibinadamu za Kristo. Yaani kiasi gani Yesu ni mwanadamu na kiasi gani yeye ni Mungu. Kama alikuwa mwanadamu, je aliumbwa kama wanadamu wote? Lakini kama anaitwa Mungu ndiye Muumba mwenyewe. Kama yeye ni Mungu - aliwezaje kuumia msalabani? Au ni Mungu aliyejificha tu katika umbo la mwili, kumbe hakuteswa kweli, ilikuwa kama igizo tu.

Maaskofu waliokutana kule Nikea wakapatana juu ya mafundisho ya "Kanuni ya Imani ya Nisea" yanayosema "Twamwamini Bwana mmoja, Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, mwana wa azali wa Baba, yu Mungu kutoka kwa Mungu, yu nuru kutoka kwa nuru, yu Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, Mwana wa azali, asiyeumbwa; aliyeshuka kutoka mbinguni kwa ajili yetu wanadamu na kwa wokovu wetu; akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika Bikira Maria, akawa mwanadamu; akasulibiwa kwa ajili yetu zamani za Pontio Pilato; aliteswa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka kama yanenavyo maandiko matakatifu; akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Baba; kutoka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu walio hai na wafu; na ufalme wake hauna mwisho." Maneno hayo hutumika mpaka leo katika ibada za kikristo (pamoja na "kanuni ya Imani ya Mitume").

Baada ya Konstantino Kanisa lilikua sana. Watu wengi walijiunga na Ukristo. Zamani ilikuwa hatari kuwa Mkristo, kumbe sasa imekuwa faida, hata watu wenye imani haba waliosita zamani wakajiunga na Kanisa. Baada ya Konstantino makaisari wenyewe walikuwa Wakristo.

Mwaka 380 mambo yaligeuka kinyume cha hali ya awali: serikali ya Kaisari Theodosi I ilitangaza Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya dola. Kanisa lilipewa hela na serikali. Kaisari mpya aliwekwa wakfu katika ibada kanisani. Kabla yake Armenia ilikuwa nchi ya kwanza kupokea Ukristo kama dini ya taifa (301). Ushindi huo ulifanya wengi watamani vyeo ndani ya Kanisa, kwa kuwa viliendana sasa na heshima na mali: hivyo ubora ulipungua.

Mwishoni serikali ilianza kufunga na kubomoa mahekalu ya Wapagani. Asiyekuwa Mkristo alianza kupata matatizo. Ilitokea mara kadhaa ya kwamba walimu wapagani walipigwa na kuuawa na umati wa Wakristo.

Katika miji mbalimbali watu walianza kuwatesa hata kuwaua Wayahudi wakiwashutumu kwamba ndio waliomwua Yesu. Sisi tunaweza kushangaa jinsi hali hiyo ilivyoweza kutokea. Yesu mwenyewe alikuwa Myahudi na mpaka msalabani alifuata taratibu za taifa la Israeli. Mtume Paulo alifundisha ya kwamba Wayahudi hawawezi kupoteza ahadi na agano la Mungu kwao hata wakimkataa Yesu Kristo.

Bila shaka Yesu hakutaka watu walazimishwe kujiunga na Kanisa lake. Lakini katika mawazo na uzoefu wa Waroma dini na serikali zilikuwa kitu kimoja. Ikiwa sasa Kaisari, wakubwa wa serikali na watu wengi walikuwa Wakristo walihisi ni kawaida kwa wote kufuata dini hiyo. Kumbe Kanisa lilianza kutumiwa na wanasiasa kwa malengo yao ya kidunia.

Atanasi na mababu wengine wa Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Ni huko Aleksandria ulikotokea uzushi mkuu wa historia yote ya Kanisa: padri Ario alikanusha umungu wa Yesu. Mafundisho yake yalienea kote mashariki na kuungwa mkono na watawala kwa nguvu za dola. Lakini ni Kanisa la Misri lililompinga kwa uimara wa pekee, bila kujali dhuluma.

Kati ya wote, alijitokeza Atanasi wa Aleksandria anayeitwa Mkuu (Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373), Patriarki wa Kanisa Katoliki la madhehebu ya Misri kati ya mitaguso mikuu miwili ya kwanza: Nisea I (325) na Konstantinopoli I (383).

Maisha yote ya Atanasi yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema “nguzo ya Kanisa” (Gregori wa Nazianzo).

Pamoja na kupatwa na vurugu nyingi maishani (hasa kufukuzwa mara tano kutoka mji wake), Atanasi aliandika sana: hotuba na barua, lakini pia vitabu juu ya imani, historia, ufafanuzi wa Biblia, pamoja na maisha ya Kiroho. Kitabu chake maarufu kimojawapo kinahusu umwilisho wa Neno; humo aliandika kuwa Neno wa Mungu “alifanyika mtu ili sisi tuweze kufanywa Mungu”.

Lakini kitabu ambacho kilienea na kuathiri zaidi maisha ya Kanisa labda ni "Maisha ya Antoni" ambacho kilieneza umonaki haraka mashariki na vilevile magharibi.

Mbali ya Atanasi, katika karne ya 4 na ya 5 Kanisa la Mashariki lilizaa mababu wengine bora: Basili Mkuu (Kaisarea wa Kapadokia, leo Kayseri, nchini Uturuki, takriban 329 – Kaisarea wa Kapadokia, 1 Januari 379, Gregori wa Nazianzo (Arianzo, leo Güzelyurt nchini Uturuki, 329 - Arianzo, 25 Januari 390) na Yohane Krisostomo (Antiokia wa Siria, leo Antakya, nchini Uturuki, 347 hivi - Comana Pontica, Uturuki, 14 Septemba 407). Wote walikuwa maaskofu na wote walipitia kwanza umonaki. Ndio waliofafanua kwa dhati zaidi mafumbo ya Ukristo, kuanzia lile la Utatu mtakatifu, na ndio waliobaki kielelezo kwa liturujia na uchungaji bora.

Umonaki - maisha ya pekee[hariri | hariri chanzo]

Watawa ni Wakristo walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile maisha ya kimya katika sala au huduma za upendo: hospitali, nyumba za mayatima, ufundishaji, uinjilishaji, misheni, au n.k. Hivyo mtawa anaweza kuwa na maisha ya kutotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya Wakristo na wasio Wakristo akiwatolea huduma zake.

Mara nyingi tumezoea kuwaona katika Kanisa Katoliki. Lakini wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa si wengi. Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptisti.

Mtawa amepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo (ambaye hakuoa): «Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo» 1Kor 7:8. Yesu mwenyewe aliwahi kueleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila familia na uzazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (Mt 19:12: "Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni»).

Kwa jumla watawa ni kundi muhimu linalosaidia sana kazi ya kiroho katika Ukristo. Wako huru kuliko wengine kujitolea katika huduma za Kanisa, kwani hawalazimiki kufikiria maendeleo ya watoto wao. Watawa wanaweza kuishi peke yao lakini mara nyingi wanajiunga na shirika au jumuiya na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu.

Asili ya jumuiya hizo iko Misri. Katika karne ya 3 mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma Wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani wakiogopa kulazimishwa kutoa sadaka kwa sanamu. Wengine waliona jinsi familia yao ilivyouawa katika dhuluma za kidini. Wengine karibu walikata tamaa wakiona Wakristo wengine walivyokana imani kwa kuogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya kawaida, wakajitenga na dunia wakaenda porini kuishi kule maisha ya kufunga na kusali.

Watawa hao waliitwa kwa jina la Kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake). Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala wa Kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Walitumia muda mwingi wakisali na kusoma Biblia. Watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao katika mambo ya kiroho au maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k. Wengine walizoea kupokea zawadi za wanavijiji wakaelekea maisha ya kuombaomba.

Antoni abati anaitwa baba wa umonaki kwa jinsi alivyovuta wengi kwenye mtindo huo mpya wa maisha ya kiroho katika Ukristo.

Wamonaki wa kwanza walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana. Antoni wa Misri alikuwa mmojawao, naye akaona umuhimu wa kuweka utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake.

Mwanafunzi wake Pakomi aliendeleza mkazo wake akawaunganisha wamonaki mahali pamoja akawapa utaratibu wa kazi na sala. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1. Useja mtakatifu: atachagua maisha bila ndoa; badala yake kujiunga na shirika la wenzake kama familia ya kiroho. 2. Ufukara: ataacha mali yake ya binafsi na hatatafuta tena utajiri wa kidunia. 3. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo aliyechaguliwa kati yao (huitwa "Abba/Abati") na kutii taratibu za ushirika wake.

Utaratibu huo wa umonaki ulienea haraka: watawa wakaanza kukaa na kufanya kazi pamoja ili kujipatia mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu ambapo sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k.

Tangu karne IV umonaki ulijitokeza magharibi pia: huko Italia, Ufaransa na Hispania kulikuwa na monasteri za kike na za kiume zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni Martino wa Tours (316-397).

Hasa maandishi ya Yohane Kasiano (360-435) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea nao.

Augustino wa Hippo (354-430), babu wa Kanisa muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake, akawashirikisha utajiri wake wa akili na roho ili wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake, iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi kote.

Benedikto wa Nursia (480-547) ndiye aliyeunda umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake, Kanuni ya Mwalimu asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu wengine wa jangwani.

Kanuni yake iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na kufufua uchumi wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.

Kutokana na kila monasteri kujitegemea, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.

Kati ya aina nyingine za umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ulaya visiwani). Hao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa Kolumbani (540-615).

Hatimaye wakaja kukubali kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la Roma.

Wamonaki wengine pia walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. Augustino wa Canterbury (+605), aliyetumwa Uingereza na Papa Gregori I (540-604), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu Bonifas (672-754), mtume wa Ujerumani na mfiadini.

Frumensyo, mmisionari wa ufalme wa Aksum (Ethiopia ya leo).

Wamisionari Wamisri katika mabara matatu[hariri | hariri chanzo]

Panteno wa Chuo cha Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri walianzisha Kanisa katika Sudan na Ethiopia za leo.

Hata sehemu mbalimbali za Ulaya zinakumbuka wamisionari kutoka Afrika waliohubiri huko Injili wakati wa Dola la Roma. Askari Wamisri katika jeshi la Roma walikaa miaka mingi Uswisi na kwingineko. Kati yao kulikuwa na Wakristo waliohubiri huko Injili kwa mara ya kwanza.

Kule Ireland Wamisri waliunda monasteri mnamo mwaka 500 na kufundisha Injili. Waireland wanafunzi wa Waafrika hao ndio wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi baadaye.

Augustino na mababu wengine wa Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Augustino wa Hippo akibatizwa na askofu Ambrosi, mwaka 387.

Augustino (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.

Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5.

Katika historia yote Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.

Kati ya mababu wa Kanisa, ndiye aliyetuachia maandishi mengi zaidi, kuanzia yale maarufu sana yanayoitwa "Maungamo", kwa kuwa humo miaka 397-400 aliungama sifa za Mungu na ukosefu wake mwenyewe kwa kusimulia alivyoishi hadi miaka ya kwanza baada ya kuongoka.

Kila wakati ulifurahia zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika kujichunguza na kutoa siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.

Uzingatifu wake wa fumbo la nafsi yake ambamo fumbo la Mungu limefichama, ni mzuri ajabu kiasi cha kubaki hata leo kilele cha kujitafiti kiroho. Aliandika: “Usiende nje, rudi ndani mwako; ukweli unakaa katika utu wa ndani; na ukiona umbile lako ni geugeu, panda juu yako. Lakini kumbuka, unapopanda juu yako, unapanda juu ya roho inayofikiri. Basi, ufikie pale mwanga wa akili unapowaka”. Tena: “Naona ni lazima wanadamu warudishiwe tumaini la kupata ukweli”.

Posidi, mtu wa kwanza kuandika habari za maisha ya Augustino (kwa Kilatini, “Vita Augustini”), alisema “waamini wanamkuta daima hai” katika vitabu vyake. Kweli havionyeshi imepita miaka 1600 tangu viandikwe: humo anaonekana kama rafiki yetu wa wakati huu anayesema nasi kwa imani isiyozeeka.

Augustino mwenyewe aliviorodhesha 1,030, ambavyo si vyote.

Kazi yake kubwa haikuwa kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali na kutoa majibu yaliyo muhimu mpaka leo.

Akilinganisha imani na akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu (Ukweli mkuu na Upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wa Mungu). Huyo katika roho yake isiyokufa, bado ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu, ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.

Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya mapokeo na kuathiri Kanisa lote la Magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi). Kitabu muhimu zaidi kuhusu Utatu (kwa Kilatini kinaitwa “De Trinitate”) alikiandika miaka 399-420. Kilichukua muda mrefu kwa kuwa alisimamisha uandishi wake miaka minane “kwa sababu ni kigumu mno na nadhani wachache tu wanaweza kukielewa; basi kuna haraka zaidi ya kuwa na vitabu vingine tunavyotumaini vitafaidisha wengi”.

Hivyo alielekeza nguvu zake kutunga vitabu vya katekesi kwa wasio na elimu (hasa “De Catechizandis Rudibus”). Akijibu hoja za Wadonati, ambao walitaka Kanisa la Kiafrika na kuchukia mambo ya Kilatini, alikubali kurahisisha lugha hata kufanya makosa ya kisarufi kusudi wamuelewe zaidi akifafanua umoja wa Kanisa ulivyo muhimu kwa mahusiano na Mungu na kwa amani duniani.

Papa Gregori I, aliyeitwa Mkuu kutokana na umuhimu wake katika historia ya Kanisa.

Hasa hotuba zake, zilizoandikwa na wengine wakati alipokuwa anazitoa kwa watu akiongea nao kirahisi, zimechangia kueneza ujumbe wake. Tunazo bado karibu 600, lakini zilikuwa zaidi ya 3,000.

Pia alifafanua upya imani kuhusu umwilisho wa Mwana wa Mungu, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451): uwepo wa hali mbili (ya Kimungu na ya kibinadamu) katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”.

Mbali ya Augustino, Kanisa la Magharibi katika karne ya 4 hadi ya 6 lilizaa mababu wa Kanisa wengine walioathiri moja kwa moja imani, maadili, liturujia na uchungaji: kwanza askofu Ambrosi (Trier, leo nchini Ujerumani, 340 hivi - Milano, Italia, 4 Aprili 397), ambaye ndiye aliyembatiza Augustino, halafu padri Jeromu (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) na Papa Gregori I (Roma, Italia, 540 hivi – Roma, 12 Machi 604) .

Mafarakano ya mataifa mazima na umoja wa Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Katika karne ya 4 dola kubwa la Roma lilianza kupata matatizo. Makabila kutoka Ulaya kaskazini yalianza kuhamia kusini. Hali ya hewa kule ilibadilika: watu wakakosa chakula cha kutosha. Hiyo ilisababisha kipindi kirefu cha vita na vurugu. Waliohama wakawasukuma majirani wao walioanza kuhamahama vilevile. Matembezi hayo yalifika kwenye mipaka ya Dola la Roma. Waroma walishindwa kuwazuia kutokana na uzazi wao kupungua na polepole mataifa yale yasiyostaarabika yakaingia katika eneo la dola na kutwaa mikoa mbalimbali. Waroma wakatumia hela nyingi sana kwa ajili ya jeshi lao lakini bila kufanikiwa.

Mwaka 395 Kaisari akagawa dola la Roma katika sehemu mbili, yaani Magharibi (makao makuu Roma) na Mashariki (makao makuu Bizanti). Mpaka wa katikati ulifuata tofauti ya utamaduni kati ya maeneo yaliyotumia zaidi lugha ya Kigiriki na maeneo yaliyotumia zaidi Kilatini. Ugawaji huo ulikuwa na kusudi la kurahisisha utawala na utetezi. Lakini mwaka 410 makabila yasiyostaarabika yaliteka na kuharibu mji wa Roma. Mwaka 476 Kaisari wa mwisho wa Magharibi aliuawa.

Ubatizo wa Chlodwig, mfalme wa Wafaranki, uliingiza kabila hilo kubwa katika Kanisa Katoliki. Tukio lilivyochongwa katika pembe ya ndovu (karne ya 9).

Makabila ya Kijerumaniki yalichukua utawala katika sehemu zote za Ulaya mpaka Afrika Kaskazini. Dola la Roma la Magharibi likagawanywa katika nchi nyingi ndogondogo. Kila sehemu makabila toka Kaskazini yalitawala kama tabaka dogo la juu wakiwategemea wenyeji kuendelea kuzalisha mali na wenyewe kupokea kodi zao. Lakini utaratibu, mawasiliano na usalama viliharibika kabisa. Uchumi na utamaduni vilirudi nyuma. Umoja wa kisiasa uliharibika, badala yake yalitokea maeneo mengi madogo ya kikabila. Ulaya Magharibi ilibaki na chombo kimoja tu chenye umoja uliovuka mipaka: Kanisa Katoliki chini ya uongozi wa Askofu wa Roma. Ndiye aliyetunza urithi wa jina kubwa la Roma akiheshimiwa pia kama mwandamizi wa Mtume Petro. Yeye kama mchungaji mkuu alilazimika kuwajibika ili kuokoa jahazi. Ndivyo walivyofanya hasa Papa Leo I na Papa Gregori I. Wafaranki, kabila kubwa la Kigermanik waliwahi kujiunga na Kanisa Katoliki wakawa msaada mkubwa kwa Mapapa. Isipokuwa, kwa kuwaachia watawale Italia ya Kati, walisababisha Papa aanze kuwa kama mfalme wa dunia hii, jambo lililoathiri sana majukumu yake ya kiroho hadi mwaka 1870.

Kwa sababu elimu ilishuka chini popote Ulaya Magharibi, ni ndani ya Kanisa tu kwamba mapadri na wamonaki wakaendelea kusoma na kutunza elimu ya kale. Kwa juhudi za wamonaki Wabenedikto na wengineo, ustaarabu wa kale uliokolewa katika vitabu vyake na uinjilishaji uliendelea katika Ulaya ya Kati. Ni kwamba watu kutoka Ulaya kaskazini hawakuwa wasomi. Hivyo watawala wao walitegemea watu wa Kanisa wakitaka kuandika au kusomewa barua au mikataba. Polepole watawala wapya pamoja na makabila yao wakapokea Ukristo. Walifundishwa kwamba mfalme hupewa madaraka yake na Mungu, hivi anapaswa kufuata shauri la Kanisa ambalo linatangaza mapenzi ya Mungu. Kutokana na hali hiyo ya kiutamaduni na ya kiroho Kanisa lilikuwa na athari kubwa sana.

Utamaduni na utaratibu wa kale viliendelea katika sehemu ya mashariki ya dola. Mtawala wa Bizanti akaendelea kutumia cheo cha Kaisari wa Roma. Taratibu za siasa, serikali na uchumi ziliendelea. Makaisari wengine wa Mashariki walijaribu kutawala tena eneo lote la zamani hata upande wa magharibi lakini ilishindikana. Kanisa huko liliendelea kuwa dini rasmi ya serikali. Kwa sababu serikali ilikuwa yenye nguvu zaidi, Kanisa lilikuwa chini yake. Kaisari alikuwa mlezi mkuu wa kanisa. Ndiye aliyemthibitisha Askofu Mkuu wa Bizanti na maaskofu wa dayosisi.

Kwa sababu ya matatizo ya ndani ya dola la Roma la Mashariki (= Bizanti) mafarakano yalitokea katika nchi za Misri na Siria zilizokuwa chini ya Kaisari wa Bizanti. Katika nchi hizo, baada ya mtaguso wa Kalsedonia (451), sehemu kubwa ya Wakristo walijitenga na kuendelea kama Kanisa la kitaifa. Kanisa la Misri lilifuatwa na Kanisa la Nubia na la Ethiopia. Kwa namna hiyo makanisa hayo ya kale ya Afrika yameendelea hadi leo kwa namna ya pekee. Ilitokea vilevile kwa Kanisa la Siria, la Armenia n.k. Hawakuwa tena waamini binafsi walioshika msimamo tofauti na ule rasmi, bali Wakristo karibu wote wa nchi fulani chini ya maaskofu wao waliojitenga na umoja wa Kanisa.

Kanisa la Mashariki kwa Dola la Roma lilipofikia kilele cha uenezi wake.

Kabla ya hapo, kufuatana na mtaguso wa Efeso (431), Wakristo wa nje ya Dola la Roma upande wa mashariki (Mesopotamia, Uajemi n.k.) walikuwa wameshajitenga na kuendeleza maisha ya Kikristo chini ya dhuluma za Dola la Uajemi, huku wakieneza habari njema mbali zaidi na zaidi, hadi China na Indonesia.

Kumbe Kanisa Katoliki liliendelea tofautitofauti katika sehemu hizo za mashariki na magharibi za Dola la Roma. Wakristo wa Magharibi (nchi za Ulaya magharibi pamoja na Afrika kaskazini) wakafuata uongozi wa Papa yaani Askofu wa Roma. Kanisani walitumia lugha ya Kilatini. Wakristo wa Mashariki wakafuata maaskofu wao waliokuwa chini ya serikali ya Kaisari wa Bizanti. Kama lugha walitumia Kigiriki.

Pamoja na magomvi katika uenezaji wa Ukristo kwenye maeneo ya Ulaya yaliyokuwa bado ya Kipagani (hasa kati ya Waslavi), tofauti hizo zilisababisha desturi na mawazo yaliyozidi kutofautiana. Ziliweka msingi wa kutokea kwa madhehebu mawili makubwa yanayoendelea mpaka leo yaani Kanisa Katoliki la Kiroma (magharibi) na Kanisa la Kiorthodoksi (mashariki).

Baada ya mafarakano ya muda (hasa la miaka 863-867 kuhusu upatriarki wa Fosyo), mwaka 1054 wajumbe wa Askofu wa Roma walimtembelea Askofu Mkuu wa Bizanti. Walianza kupingana vikali na mwishoni wakalaaniana. Tangu mwaka ule farakano lilikuwa rasmi kati ya Ukristo wa Magharibi na Waorthodoksi.

Ilichukua miaka mingi kushinda laana hizo. Mwaka 1967 Papa Paulo VI wa Roma alimtembelea Askofu Athenagoras wa Bizanti (leo: Istanbul) wakapatana tena na kusameheana makosa ya zamani. Uelewano umeanza kujengwa pia kati ya makanisa yaliyofarakana zamani na Bizanti kama vile Wakopti na Wasiria.

Uenezi wa Uislamu ulivyorudisha nyuma Ukristo na umisionari wake[hariri | hariri chanzo]

Uenezi wa Uislamu hadi mwaka 661.

Mwaka 622 B.K. Mwarabu kwa jina Muhammad alikimbia mji wa Maka. Wakazi wa Maka walikuwa wamemkasirikia Muhamad. Kwa miaka 12 aliwahi kuhubiri juu ya ufunuo aliodai ameupokea kutoka kwa malaika wa Mungu. Alipinga desturi na maadili ya watu wa mji wake. Akatangaza "Uislamu" yaani imani katika Mungu mmoja aliyetoa amri zake kwa wanadamu. Kumbe viongozi wa Maka waliona anaharibu dini ya jadi ya kuabudu sanamu za miungu. Makabila ya Waarabu walikuja kila mwaka kuabudu sanamu za Maka katika jengo la Kaaba. Wakati wa ziara hizo biashara ya Maka ilistawi vizuri sana. Muhammad alionekana anaweza kuwazibia viongozi hao riziki wakakasirika wakajaribu kumwua lakini akakimbia.

Akisafiri pamoja na marafiki wachache akaelekea mji wa Jathrib (leo Madina). Pale alipokewa vizuri, na wenyeji wakamwamini. Habari zake zikaenea haraka pande zote za Uarabuni. Makabila mbalimbali ya Waarabu walimwunga mkono. Akawa kiongozi wao kidini, kijeshi na kisiasa. Mwaka 630 akawashinda watu wa Maka kivita lakini alionyesha busara kwa kuwahurumia mradi wajiunge na Uislamu.

Alipokufa mwaka 632 B.K. karibu Waarabu wote waliunganishwa chini ya bendera ya imani mpya ya Uislamu. Katika jina la Mungu (kwa Kiarabu: Allah) wafuasi wake wakashambulia maeneo jirani ya Waroma wa Bizanti na ya Waajemi.

Dunia nzima ilishangaa kusikia habari ya kwamba Waarabu kutoka jangwani walifaulu kuwashinda wanajeshi hodari wa Kiroma na wa Kiajemi. Lakini katika miaka iliyotangulia dola hizo mbili kubwa ziliwahi kupigana vita virefu na vikali. Wananchi wote na wanajeshi wao walichoka. Uchumi ulidhoofika baada ya miaka 20 ya vita.

Tena wenyeji wa Misri na Shamu (Siria) walisikitikia utawala wa Kaisari wa Bizanti. Walidai tangu muda mrefu uhuru wa kitaifa lakini wakagandamizwa. Waarabu walikutana na maadui waliokosa nguvu. Hivyo uenezaji wao ulikuwa wa haraka sana.

Ushindi wa Wafaranki juu ya Waislamu huko Tours (732) ulizuia uenezi wa dini hiyo Ulaya Magharibi.

Mwaka 636 Waarabu wakawashinda Waroma wa Bizanti kule Shamu wakateka Dameski na Yerusalemu. Mwaka uleule wakawashinda Waajemi kule Mesopotamia (Iraq). Mwaka 639 wakaingia Misri na kuteka Aleksandria miaka mitatu baadaye. Mwaka 642 waliteka sehemu kubwa ya Uajemi wenyewe. Miaka 670/696 waliteka mkoa wa "Afrika" ya Kiroma pamoja na Karthago (Tunisia ya leo). Mwaka 711 wakavuka mlangobahari na kuingia Hispania (Ulaya Kusini). Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na wenyeji mwaka 732 lakini walitawala sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata.

Walishindwa kuteka Bizanti yenyewe iliyoendelea kutawala Asia Ndogo lakini wakaenea Asia ya Kati. Mwaka 751 walipigana na jeshi la China. Na kule Mashariki wakasimama ana kwa ana mbele ya wanajeshi wa Wahindi na Wachina. Miaka mia moja baada ya kifo cha Muhamad sehemu kubwa ya dunia kati ya Moroko na Bonde la Indus ilikuwa chini ya bendera ya Uislamu.

Utawala wa Kiislamu ulifikia nchi hizo kwa njia ya vita. Mwanzoni walikuwa Waarabu kadhaa tu: walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Walifundishwa kwamba ikiwa watakufa vitani watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.

Chini ya utawala wa Waarabu Waislamu, wenyeji waliruhusiwa kuendelea na desturi zao lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani. Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.

Masharti ya kujiunga na Uislamu yalikuwa rahisi sana. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haikuwezekana kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu iliruhusu Mkristo kugeuka Mwislamu lakini ilikataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.

Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea.

Lakini vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi, Wafuasi wa dini ya Uajemi n.k.). Lakini Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali. Hasa vipindi vya vita kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu kwa Wakristo waliokuwa chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa au kugeuzwa misikiti, n.k.

Pamoja na Wakristo wengi kugeuka Waislamu, umisionari kwa mataifa mengine ya Afrika na Asia ulizuiwa na dola la Kiislamu lililozunguka karibu pande zote nchi za Kikristo.

Athari nyingine ya Uislamu katika historia ya Kanisa, hasa la Mashariki, ilikuwa dharau kwa sanamu na picha takatifu zilizoenea tangu karne za kwanza BK. Ni kwamba, kisha kupigwa vitani na Waislamu mara kadhaa, kwenye miaka ya 720 Kaisari Leo III wa Bizanti alizikataza hizo na kuagiza zilizokuwepo ziteketezwe. Lengo lake lilikuwa kupunguza uadui wa Waislamu dhidi ya Wakristo na dola la Roma. Lakini waamini wengi wa dola lake walipinga uamuzi huo, wakiungwa mkono na Papa Gregori III. Hatimaye Mtaguso wa pili wa Nisea (787) ulitetea na kupitisha uhalali wa picha hizo katika Ukristo.

Kanisa lilivyoendelea hasa Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Tangu kuja kwa Uislamu uenezaji wa Injili katika Afrika ulikwama na kurudi nyuma. Kusini kwa Sahara ilifika kupitia Nubia lakini baada ya Nubia kuwa ndani ya eneo la Kiislamu athari hii haikuendelea. Kumbe uenezi wa Ukristo katika kipindi kile ulipatikana Ulaya na Asia.

Kule Ulaya makabila mengi yaliendelea kupokea Ukristo. Wakati mwingine watu walivutwa na mahubiri kuacha Upagani na kubatizwa. Mara nyingi waliona ya kwamba miungu ya kikabila haina msaada tena katika mazingira iliyobadilika. Waliweza kuvutwa na mfano bora wa wamonaki walioishi kati yao, au kushangazwa na elimu au maendeleo yao. Wakati mwingine wafalme waliamua kuwa Wakristo kwa sababu za kiroho au za kisiasa wakabatizwa pamoja na kabila au taifa zima. Katika mawazo ya Wazungu wa kale dini haikuwa jambo la mtu binafsi bali jambo la kijamii. Wakati mwingine washindi wa vita waliamua kuwabatiza maadui ili kujenga uhusiano wa kiroho nao. Ndiyo sababu ya ubatizo wa mabavu ulioweza kutokea katika nchi kadhaa.

Karolo Mkuu na Papa Adrian I. Karolo alitawazwa na Papa Leo III kuwa Kaisari wa magharibi (800). Ushirikiano kati ya Mapapa na Makaisari wa Dola Takatifu la Kiroma (leo Ujerumani na nchi za kandokando) ulikuwa na mafanikio kadhaa na matatizo mengi zaidi na zaidi.

Mfano mmojawapo ni ubatizo wa Wasaksoni, kabila kubwa katika eneo la Ujerumani kaskazini. Baadhi ya mababu wao walivuka bahari na kuteka Uingereza pamoja na Waangli. Wakati ule Wajerumani wengi walikuwa Wakristo lakini Wasaksoni waliendelea kutetea Upagani wao.

Mfalme wa eneo la Ufaransa na Ujerumani Magharibi aliyeitwa Karolo Mkuu alipigana nao mara kwa mara. Mwishowe aliona wakibaki Wapagani hatawashinda. Mwaka 800 B.K. aliwapa chaguo: upanga au ubatizo. Mwanzoni walikataa akawaua machifu 4000 wa Wasaksoni katika siku moja. Waliobaki wakabatizwa wakawaamuru wenzao kubatizwa vilevile. Hivyo eneo kubwa lilipokea Ukristo, lakini si kwa sababu ya imani, ila kwa kulazimishwa.

Si ajabu ya kwamba kwa muda mrefu Ukristo wa Ulaya katika nchi mbalimbali ulikuwa wa juujuu tu, ukaonyesha dalili za mchanganyiko wa Injili na desturi za kale za Upagani. Kumbe Ukristo ulikwenda njia ndefu sana tangu zamani za mashahidi wa Aleksandria na Karthago waliokufa badala ya kukana Ukristo wao mpaka wale Wakristo wapya wa Kisaksoni walioona heri wabatizwe kuliko kufa.

Maeneo mapya ya Ukristo yalifuata desturi za kule walikotokea wahubiri wao. Ndivyo makabila ya Ulaya kaskazini walivyojiunga na Kanisa Katoliki la Kilatini. Kumbe makabila ya Mashariki wakawa Waorthodoksi wakipokea ubatizo kutoka kwa wajumbe wa Askofu wa Bizanti. Mpaka leo Ulaya mataifa ya Warusi, Waukraina, Waromania, Wabulgaria na Waserbia (pamoja na Wagiriki wenyewe) ni Waorthodoksi. (Afrika ni hasa nchi za Misri, Ethiopia na Eritrea zinazofuata mapokeo ya Kiorthodoksi ya Kikopti). Mnamo mwaka 1000 karibu maeneo yote ya Ulaya yalikuwa na Wakristo, ingawa mara nyingi kwa jina tu.

Kule Asia Ukristo wa Kiorthodoksi uliendelea vizuri katika nchi nyingi. Tangu mwanzo mpaka leo lipo Kanisa la India Kusini (jimbo la Kerala). Wamisionari wa Kanisa la Mesopotamia na Uajemi walihubiri kote Asia ya Kati hadi Uchina na Indonesia. Lakini maendeleo hayo yalirudishwa nyuma na mashindano kati ya Ukristo na Uislamu. Kiasili Uislamu ulikuwa na uvumilivu kwa dini za Wakristo na Wayahudi. Katika maeneo ya Waarabu kama Misri au Siria Kanisa liliendelea kupata ustahimilivu: liliweza kuendelea na ibada ya Kikristo ingawa kwa matatizo.

Lakini huko Asia makabila na mataifa mapya walipokea Uislamu, mara nyingi kwa njia ya vita. Makabila hayo ya Waturuki na Wamongolia yalifuata imani ya Kiislamu kwa ukali kuliko Waarabu wenyewe. Walilazimisha wote waliokuwa na imani tofauti (Wakristo, Wabuddha au wafuasi wa dini za jadi) wawe Waislamu. Mtawala Mwislamu wa Wamongolia, Tamerlano, aliua Wakristo lukuki na kubomoa makanisa elfu kadhaa alipofanya vita vyake Asia ya Kati. Katika vita hivyo Ukristo wa Asia ya Kati uliharibika kabisa. Maeneo makubwa yalichomwa moto, watu walilazimishwa kwa upanga kuwa Waislamu au kuuawa. Mnamo mwaka 1400 Ukristo wa Asia ulibaki katika Mashariki ya Kati tu (Asia ya Magharibi) pamoja na India Kusini. Kumbe uzito wa Ulaya uliongezeka katika Kanisa kwani ni huko tu lilipoweza kuendelea bila maadui wa nje.

Kuingiliana kwa dini na siasa[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1200 kwa jumla Ulaya ilikuwa bara la Kikristo. Kanisa Katoliki (au: la Kiorthodoksi katika Mashariki) lilikuwa dini rasmi. Popote Kanisa lilikuwa chini ya ulinzi wa serikali. Watu wote walipaswa kuonekana Wakristo. Watu pekee wenye tofauti walikuwa Wayahudi, lakini waliruhusiwa kuishi katika nchi kadhaa tu; katika nchi nyingine walifukuzwa. Katika mila na desturi za Ulaya zilizotangulia kuja kwa Ukristo umoja huo wa dini na kabila ulikuwa kawaida.

Hivyo kwa upande mmoja Ukristo ulikuwa na nguvu sana Ulaya wakati ule. Lakini kwa ndani ulikuwa na udhaifu wa aina mbalimbali. Wataalamu wengine wa historia ya Ulaya huita kipindi hicho "Karne za Kati" au hata "Nyakati za Giza". Maana yake ni kipindi kati ya kuanguka kwa utamaduni na uchumi wa hali ya juu uliokuwapo wakati wa Dola la Roma na kipindi cha kuanzia mwaka 1500 ambacho uchumi na elimu vilianza kusonga mbele tena. Tutajaribu kuangalia pande zote mbili, yaani mafanikio na matatizo.

Katika nchi nyingi tumezoea kwamba serikali haina dini. Kila mwananchi ni huru kuchagua imani yake. Kumbe wazo hilo si la kawaida popote duniani. Mpaka leo tunasikia habari za nchi zinazotoa kipaumbele kwa dini au madhehebu fulani upande wa serikali. Taratibu hizo ni mabaki ya zile zilizokuwa kawaida katika sehemu nyingi za dunia. Zamani katika nchi nyingi ilikuwa kawaida kuangalia mambo ya dini na mambo ya dola pamoja.

Agano Jipya halina amri yoyote juu ya kuunda "serikali za Kikristo". Kinyume chake Wakristo walifundishwa na mtume Paulo kuiombea serikali ya Kipagani ya Kaisari wa Roma. Lakini baada ya viongozi wa mataifa kuwa Wakristo waliona lazima kulitumia Kanisa kama chombo kinachoongeza umoja na nguvu ya nchi.

Katika Ulaya ya Karne za Kati Kanisa na serikali vilikwenda pamoja. Katika sehemu za Waorthodoksi Kanisa lilikuwa chini ya wafalme waliokubaliwa kuwa walezi wake wakuu. Ulaya magharibi kwenye Wakatoliki wengi Kanisa lilikuwa huru zaidi. Lakini hata huko mambo yaliingiliana.

Utaratibu wa utawala wakati ule ulikuwa wa kikabaila yaani machifu na watu wa familia za wakubwa walitawala maeneo chini ya serikali kuu ya mfalme.

 • a. Wafalme na hata watawala wadogo walipewa madaraka yao katika nchi kwa ibada maalumu kanisani.
 • b. Watawala waligandamiza wapinzani wa Kanisa kwani waliona wangeleta vurugu hata kisiasa.
 • c. Watawala walikabidhi madaraka mengi kwa maaskofu. Askofu aliweza kuunganisha uongozi wa Kanisa na mamlaka ya kiserikali katika eneo lake. Viongozi wa Kanisa waliaminika kuliko machifu wa kawaida. Machifu wakikabidhiwa madaraka fulani kwa muda walijaribu mara nyingi kuyashika kama mali yao. Wakatafuta kuongeza mali yao kuwa urithi wa familia. Faida ya kutumia watu wa Kanisa ilikuwa kwamba mapadri na hasa maaskofu hawaoi, hawana watoto, hawana hamu ya kutafuta urithi kwa ajili ya watoto wao.
 • d. Maaskofu (na viongozi wengine wa Kanisa) walichaguliwa mara nyingi kutokana na sifa zao za kisiasa kuliko uwezo wa kuongoza kiroho. Kwa sababu cheo cha askofu kiliambatana na mapato makubwa, ni familia za machifu zilizopeleka wanao katika nafasi hizo. Kwa njia hiyo matabaka ya kijamii yalionekana vilevile ndani ya Kanisa: viongozi wake walitoka katika familia za wakubwa, nafasi za chini walipewa watumishi kutoka familia za matabaka ya chini.

Marekebisho ya karne IX-XII[hariri | hariri chanzo]

Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii na vya ulegevu.

Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linaathiriwa na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha.

Utawa unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika karne IX hadi XII Kanisa la magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote.

Kati ya matukio muhimu yaliyoandaa ukombozi wa Kanisa kutoka mikono ya wanasiasa kuna uundaji wa monasteri ya Cluny (leo nchini Ufaransa) mwaka 910 ikiwa chini ya Mtume Petro (yaani chini ya Papa tu), si chini ya mtawala wa dunia hii. Monasteri hiyo ilizaa nyingine nyingi kote Ulaya ambazo kwa kutoingiliwa waliweza kuongozwa na watu wa kiroho waliochaguliwa na wamonaki wenyewe kwa malengo ya imani.

Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo, mbali ya lile la Cluny (ambalo lilikazia liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi).

Wamonaki wa matawi hayo wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa, hasa Petro Damiani (1007-1072), Papa Gregori VII (1028-1085) na Bernardo wa Clairvaux (1090-1153).

Wakati huohuo Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (Wakartusi).

Kaisari Henri IV akiomba msamaha wa Papa Gregori VII huko Canossa (1077) katika mchoro wa Carlo Emanuelle.

Kutoka monasteri za namna hiyo walitokea viongozi wa Kanisa waliokomboa Upapa pia katika kuingiliwa na wanasiasa. Muhimu zaidi kati yao ni Papa Gregori VII aliyeshindana na Kaisari akitumia mamlaka ya kiroho. Mwenzake aliyesababisha Mapapa wachaguliwe na makardinali tu ni Petro Damiani, Mbenedikto wa urekebisho mwingine, ule wa Camaldoli (Italia).

Wakati huohuo, ili kuboresha maisha ya mapadri wanajimbo, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati yao, ambamo wasali na kufanya utume kwa pamoja.

Hasa kuanzia karne XI wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makubwa kama mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji.

Inavyoweza kueleweka, hao walifuata kanuni ya Augustino na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi katika yao ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa Wapremontree.

Utajiri wa Kanisa[hariri | hariri chanzo]

Kanisa lilikuwa tajiri sana. Makanisa yalijengwa na wakubwa waliotoa baadaye shamba fulani kuwa mradi wa kanisa lile. Ilikuwa kawaida kwa kanisa kumiliki mashamba yenye nia mbalimbali: moja kugharimia matengenezo ya jengo, lingine kumtunza mchungaji au paroko, lingine kumlipa msaidizi wake n.k.

Kanisa kubwa lenye watumishi wengi lilikuwa na mapato makubwa. Watu wa vijiji kadhaa walitakiwa kuchanga sehemu ya mavuno yao na kulifanyia kanisa kazi siku mbili kwa juma kama kodi kwa ajili ya gharama za jengo, mapadri kadhaa au askofu.

Mara nyingi zawadi hizo za mashamba au vijiji zilitolewa kama sadaka, kama alama ya toba au kama shukrani. Sadaka za makabaila ziliongeza utajiri wa Kanisa.

Familia za makabaila zilichagua nafasi za uaskofu kwa watoto wao. Mwana wa chifu aliyepokewa katika upadri alizuiliwa kuunda familia na kurithi cheo cha baba, lakini alipanda ngazi ndani ya Kanisa, kupata cheo cha heshima katika jamii na kuwa na mapato makubwa yaliyomwezesha kuishi maisha mazuri na tajiri kama familia yake.

Wakati wa njaa maskini waliweza kupata misaada kanisani, hasa katika nyumba za watawa. Wamonaki waliweza kuwasaidia maskini hata kwa kuuza hazina ya kanisa hata mapambo ya dhahabu yaliyopatikana wakati wa utajiri. Lakini mara nyingi maaskofu walijisikia kuwa wakubwa na wengi wao hawakujali matatizo ya wadogo.

Uhaba wa elimu[hariri | hariri chanzo]

Karne za Kati kule Ulaya zilikuwa kipindi pasipo elimu kwa watu wengi. Kwa jumla utamaduni wa juu wa Kiroma ulikuwa umeanguka chini. Karibu watu wote hawakujua kusoma wala kuandika. Katika nchi nyingi ni watawa tu waliosoma.

Tatizo mojawapo lilikuwa uhaba wa vitabu. Mashine za kupiga chapa vitabu hazikujulikana. Maana yake kila kitabu kiliandikwa kwa mkono. Nakala ya Biblia ilihitaji kuandikwa na mtu kwa muda wa mwaka au zaidi. Hivyo vitabu vilikuwa ghali sana. Mtu wa kawaida alishindwa kununua kitabu, hata kama angeweza kusoma. Kumbe Wakristo wengi sana hawakuwahi kusoma Biblia.

Zaidi ya hayo Kanisa Katoliki lilitumia popote Biblia katika lugha moja tu, yaani Kilatini, ambacho kilikuwa pia lugha ya ibada zote kwa ajili ya nyimbo, masomo na sala. Kutumia lugha moja popote kulisaidia sana kutunza umoja wa Kanisa.

Lakini watu wa kawaida hawakuelewa Kilatini, hata mapadri wengi hawakukielewa vizuri. Kidogo ingekuwa kama kusoma Biblia na kuhubiri katika makanisa ya Afrika kwa Kiingereza au Kifaransa tu.

Hali hii ilisababisha elimu ya Kikristo kuwa chini kati ya waamini wa kawaida. Hivyo walijali sana mambo ya pembeni kama vile masalia ya watakatifu. Watu wengi waliona muhimu sana kuhiji kwenye "mahali patakatifu" wakiamini ya kwamba safari za aina hii zinaleta sifa mbele za Mungu.

Ilikuwa vema kusafiri ili kusali kwenye kaburi la mtakatifu, k.mf. shahidi aliyekufa kwa ajili ya imani yake zamani, lakini mifano mbalimbali inaonyesha jinsi gani imani ya asili ya ushirikina ilikuwa bado na nguvu baada ya Ukristo kuenea.

Vita vya msalaba[hariri | hariri chanzo]

Mtawa Petro mkaapweke akihubiri vita vya msalaba mbele ya makabaila wa Ufaransa.

Wakristo waliohiji Yerusalemu kutoka Ulaya walishambuliwa njiani mara kwa mara. Naye Kaisari wa Bizanti aliomba msaada wa Wakristo wa magharibi dhidi ya mashambulio ya Waturuki Waislamu.

Kuanzia mwaka 1095 Wakristo Wakatoliki wa Ulaya walijaribu kuwaondoa Waislamu katika nchi za Mashariki ya Kati. Papa aliwaita mataifa ya Kikatoliki ya Ulaya kuikomboa nchi takatifu. Tangu mwaka 1096 hadi mwaka 1270 kampeni za kijeshi zilianzishwa Ulaya kuelekea Yerusalemu.

Kampeni hizo huitwa "Vita vya msalaba" kwani wanajeshi walipokea kanisani alama ya msalaba wa kitambaa waliobandika juu ya nguo zao. Walifundishwa kuwa vita hivyo ni vitakatifu: atakayekufa atafika mbinguni kwa hakika. Wataalamu wanahisi kama hapo athari za mafundisho ya Kiislamu juu ya "jihadi" zimeingia katika Ukristo.

Mwaka 1099 jeshi la Ulaya lilifika mbele ya kuta za Yerusalemu. Baada ya mapigano mafupi jeshi la msalaba liliwashinda wateteaji Waislamu. Katika hasira ya mapigano waliua ovyo wakazi wengi sana, wazee na watoto, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi. Mkabaila Mfaransa alipokea cheo cha "Mfalme wa Yerusalemu".

Lakini miaka 100 baadaye Sultani Salah-ed-Din wa Misri aliwafukuza wanamsalaba tena kutoka Yerusalemu. Miaka 40 baadaye alirudisha mji huo kwa hiari baada ya kupatana na Mfalme Mjerumani.

Lakini muda wote huo Wazungu walitawala sehemu ya Palestina na Siria tu. Waislamu waliwaona kama maadui. Hata Wakristo wenyeji (Waorthodoksi) hawakuwakubali kuwa wakombozi kwani walijaribu kuwaunganisha Wakristo wote chini ya Kanisa Katoliki.

Safari moja iliyoondoka Ulaya mwaka 1204 ili kuikomboa Yerusalemu, kumbe ilifika mpaka Bizanti tu ambako wanajeshi wa msalaba waliteka mji, kupora utajiri na kumfukuza Kaisari wa Bizanti. Miaka 100 baadaye Kaisari alirudi na kuunda upya Ufalme wa Roma ya Mashariki.

Mwaka 1291 jeshi la Kiislamu liliwafukuza kabisa wanajeshi wa msalaba katika nchi takatifu wasirudi tena. Lakini kabla ya kuondoka waliwahi kuvunja nguvu ya Bizanti kiasi cha kutosha. Kumbe Ulaya Magharibi iliharibu ulinzi wa dola la mashariki dhidi ya Waturuki waliofaulu baadaye kuingia Ulaya.

Badala ya kufukuzwa, jeshi la Waturuki lilianza kuishambulia Ulaya Kusini-Mashariki. Mwaka 1453 ulianguka mji wa Bizanti, na mwaka 1529 Waturuki walifika mpaka Vienna, mji mkuu wa Mfalme wa Ujerumani. Hapo walirudishwa nyuma, lakini nchi nyingi za Ulaya Kusini-Mashariki pamoja na Wakristo wao walikaa chini ya Waturuki kwa karne tatu zijazo.

Katika karne XII, ambapo baadhi ya Wakristo walipiga vita vya msalaba kuikomboa nchi takatifu, na baadhi walitekwa na Waislamu kuwa watumwa, zilianzishwa aina mpya za watawa ambao washike maisha ya Kiroho pamoja na upanga ili kusindikiza, kukaribisha, kulinda na kutibu waliohiji Yerusalemu, au wajitolee kukomboa watumwa hata kwa kubadilishana nao.

Mt. Yohane wa Matha

Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu. Kati ya waanzilishi wakumbukwe Yohane wa Matha (1154-1213) na Petro Nolasco (1180-1249).

Kwa ujumla majaribio ya vita vya msalaba ya kuikomboa nchi takatifu yalishindikana. Vita hivyo vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu. Kipindi cha vita vya kidini kilisababisha mateso mengi kwa Wakristo Waorthodoksi chini ya Waislamu. Walilipa madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.

Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengi Wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso.

Maisha haya yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea na ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza).

Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Sababu kuu ni kwamba kama Mkristo amekuwa Mwislamu hakuweza kurudi tena. Sheria ya Kiislamu inamruhusu Mkristo kugeukia Uislamu, lakini mtu aliyekuwa Mwislamu anastahili adhabu ya kifo akigeukia Ukristo au dini nyingine. Pamoja na hayo Wakristo walianza kuhamia nchi ambako watakuwa raia huru bila kasoro.

Kumbe historia inaonyesha kwamba giza lipo hata upande wa Wakristo. Wakati ule Wakristo wengi walikosa vilevile ustahimilivu kwa watu wenye imani tofauti. Hakuna Mwislamu aliyeweza kubaki katika nchi za Hispania na Ureno baada ya kuvunjwa wa utawala wa Kiarabu.

Inatosha kulinganisha hali ya Waislamu kule Hispania. Sehemu kubwa ya Hispania ilikuwa miaka mamia chini ya utawala wa Waarabu Waislamu. Katika vita vingi mfululizo Wahispania waliteka nchi yao tena. Mwaka 1492 mfalme wa mwisho Mwislamu alishindwa. Waislamu wakaishi chini ya utawala wa Wahispania Wakatoliki. Lakini miaka michache baadaye Waislamu wote walilazimishwa wapokee ubatizo, wengine waliuawa au kufukuzwa.

Bila shaka hayo ni matokeo ya hali ya vita kati ya Waislamu na Wakristo. Wahispania walionyesha tabia zinazofanana na zile za Wamongolia Waislamu walioharibu makanisa yote ya Asia ya Kati.

Lakini ipo mifano mingine: Wakristo wote walifyekwa Uarabuni kwenyewe kumbe Waislamu waliweza kubaki chini ya Waaustria Wakristo waliotawala nchi za Ulaya Kusini-Mashariki. Kweli kati ya dini hizo mbili hakuna anayeweza kujisifu tu juu ya historia ya dini yake bila kukiri makosa na kasoro pia.

Ugandamizaji wa wazushi[hariri | hariri chanzo]

Serikali ziliona ni lazima kutetea umoja wa Kanisa. Hivyo viongozi wa Kanisa walishawishika kutumia nguvu ya serikali kuhakikisha uongozi wao ufuatwe. Ikiwa walijitokeza Wakristo waliodai mabadiliko au kupinga uongozi wa Kanisa, serikali iliingilia kati na kuwagandamiza kama "wazushi". Ilikuwa hasa utajiri wa Kanisa na wa maaskofu wengi uliosababisha ugomvi.

Katika karne ya 13 Ufaransa alijitokeza mfanyabiashara Petro Waldo aliyesikia wito wa Kristo katika maisha yake. Aliwapa maskini mali yake yote akaanza maisha ya kuhubiri akijaribu kumwiga Bwana Yesu.

Papa Inosenti III ndiye aliyefikisha Upapa hadi kilele cha mamlaka zote Ulaya.

Akafundisha ya kwamba Mkristo wa kweli anapaswa kumfuata Yesu hata katika maisha ya umaskini. Akauliza: mbona Kristo alikuwa maskini, lakini maaskofu wa leo ni matajiri? Wafuasi wake kwanza waliruhusiwa, halafu wakaanza kukutana nje ya makanisa. Kanisa liliwatangaza kuwa wazushi wakatafutwa na kukamatwa na serikali. Wengine wakafungwa gerezani, wengine wakauawa.

Baadaye ilikuwa kawaida kuweka "wazushi" mbele ya mahakama za pekee na hata kuwachoma moto. Papa Inosenti III akaunda idara ya pekee "Baraza la Ulinzi wa Imani". Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kuwatafuta "wazushi" na kuwahoji juu ya imani zao. Wakionekana kuwa na makosa wasitake kutubu walikabidhiwa mikononi mwa serikali iliyotoa adhabu ya kifo. Hata hivyo mawazo yao yaliendelea kuzunguka kati ya watu wa kawaida. Wawaldo walihubiri kwa siri katika nchi nyingi.

Fransisko na tapo la mafukara[hariri | hariri chanzo]

Mchoro wa zamani wa Fransisko wa Asizi unaoaminiwa kufanana naye kuliko yote.

Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika na wengine walianza kukata tamaa juu ya hali ya Kanisa.

Pia hija na vita vya msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni.

Dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na unyofu hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai.

Katika matatizo hayo Mungu aliita watu wairudishe upya roho ya Injili. Hivyo katika karne XIII yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa Wafransisko na Wadominiko, lakini pia Waaugustino, Wakarmeli na Watumishi wa Maria) yaliyoitwa ya ombaomba kwa jinsi yalivyokaza ufukara.

Fransisko wa Asizi alizaliwa katika familia tajiri akawa kijana aliyependa sana muziki na sherehe. Vitani alifungwa mwaka mmoja akaanza kumtafuta Mungu.

Siku moja aliposali akasikia sauti, "nenda ukatengeneze Kanisa langu linalotaka kubomoka". Basi, akachukua pesa akaanza kutengeneza kanisa dogo lililokuwa bovu sana. Baba yake akakasirika akiona kijana anapoteza mali ya familia. Fransisko akakutana na baba mbele ya Askofu uwanjani akavua nguo zake na kumrudishia baba pamoja na pesa zakeː "Kuanzia sasa nitasema tu, Baba yetu uliye mbinguni".

Fransisko akaishi maisha kama mtawa akimwomba Mungu amwonyeshe njia. Siku moja kanisani alisikia somo la Mathayo 10:7-20, akajua: Hiyo ndiyo njia yangu! Alielewa maana yake "ukatengeneze Kanisa langu": kwamba si jengo lile dogo alipoanzia, lakini Kanisa la Kristo lililobomolewa kwa sababu ya ujumbe wa Injili kusahauliwa.

Alianza maisha ya ufukara akijaribu kuiga mfano wa Yesu. Akazunguka akivaa kanzu ya gunia na kuhubiri upendo wa Mungu. Vijana wengine wakamfuata wakaunda utaratibu wa maisha ya pamoja.

Fransisko akaona ya kwamba nyumba za wamonaki zilikuwa tajiri sana (mmonaki mwenyewe hakuwa na mali, lakini jumuiya yake iliweza kuwa tajiri). Kwa wafuasi wake alikataza jumuiya zisiwe na mali.

Fransisko alipendwa sana kwani alionyesha imani na furaha katika Kristo na upendo kwa watu wote. Mwenyewe alisafiri mpaka Afrika akahubiri mbele ya Sultani wa Misri. Ingawa wakati ule vita vilikuwa vinaendelea kati ya jeshi la Kikatoliki la Ulaya na Waislamu, Sultani alimpokea kwa heshima, akamsikiliza na kumruhusu kurudi kwake.

Fransisko aliamini ya kwamba majaribio yote ya kuwashinda Waislamu kwa silaha ni ya bure. Kwa Mkristo hakuna njia nyingine kuliko mfano wa Bwana Yesu, yaani upendo na unyenyekevu.

Mfumo wa Wafransisko ulienea haraka sana. Ndugu hao walitembea popote wamevaa usiku na mchana kanzu ileile na kupewa chakula kutoka kwa Wakristo wa kawaida. Tofauti na wamonaki, wakaishi kati ya watu wakihubiri na kufundisha. Walikuwa mfano wa kumtegemea Mungu kabisa katika umaskini kwani hawakuwa na mali wala mapato kuliko sadaka za hiari kutoka kwa Wakristo.

Katika maisha hayo walifanana na vikundi kama Wawaldo lakini wakawafundisha Wakristo kufuata uongozi wa Kanisa na maaskofu. Hivyo Wafransisko walikuwa silaha muhimu ya Kanisa Katoliki dhidi ya waliopinga utajiri wake. Mahali pengi Wakristo wa kawaida wakajiunga na jumuiya za kiroho zilizokuwa chini ya ulezi wa Wafransisko.

Dominiko wa Guzmán, mwanzilishi wa Shirika la Ndugu Wahubiri.

Muda uleule Mhispania kwa jina Dominiko Guzman (1170-1221) aliunda shirika la watawa. Kusudi lake lilikuwa kuhubiri. Akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.

Wafransisko na Wadominiko walinyosha kiasi kasoro za kukosa mahubiri katika Misa ya kawaida. Walifanya kazi muhimu sana ya kuwafundisha watu wadogo waliokuwa maskini na bila elimu wala uwezo wa kusoma. Baadaye Wadominiko waliogopwa pia kwa kazi ya kutafuta na kushtaki walioitwa "wazushi".

Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo. Klara wa Asizi (1193-1253), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana hadi leo kuhusu ufukara.

Giovanni di Paolo, "Mt. Katerina wa Siena", 1475 hivi. Fogg Art Museum, Cambridge, Uingereza.

Tangu karne XII wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati yao Katerina wa Siena (1347-1380), wa utawa wa tatu wa Mt. Dominiko, ametangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa.

Kuanzia karne XIII zilijitokeza pia jumuia nyingine ambazo pengine zinahusiana na mashirika ya kitawa (yaani za Utawa wa Tatu), lakini hazina nadhiri au si za hadhara. Kwa kuenea, zikaja kuwa na muundo kama wa mashirika (1401), ingawa kwa kawaida ya kwao yalikuwa na jumuia za kiume na za kike ndani yake.

Baada ya upinzani mwingi, wanawake wakaja kukubaliwa wafanye utume na kuanzisha mashirika yasiyobanwa na ugo. Kwa namna ya pekee Anjela Merici (1474-1540) alitaka wafuasi wake waishi na kutumikia kati ya watu; baada ya karne nne shirika lake likakubaliwa kutambulika kuwa la kilimwengu.

Upande wa wanaume Filipo Neri (1515-1595) ndiye maarufu zaidi kati ya walioanzisha jumuia ambapo watu wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya kuwekwa wakfu.

Farakano la Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Wengi wanaona karne ya 13 kuwa kilele cha matunda wa Kanisa Katoliki katika kulea upya Ulaya magharibi kwa kuzaa hasa mashirika ya ombaomba ya Fransisko wa Asizi na Dominiko Guzman, mitindo mipya ya sanaa, pamoja na vyuo vikuu walipostawi walimu wa Kanisa kama Thoma wa Akwino na Bonaventura.

Lakini utaifa, uliotokea Ulaya magharibi kuanzia ufalme wa Ufaransa katika karne ya 14, ulivuruga umoja wa Kanisa na matatizo yalionekana mpaka ngazi ya Upapa. Mara nyingi Papa mpya (Askofu wa Roma) alichaguliwa kufuatana na ukoo au sifa za kisiasa tu. Cheo cha Papa kiliingizwa katika siasa kubwa kati ya wafalme wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.

Mwaka 1300 Papa Bonifas VIII alidai kuwa na madaraka juu ya wafalme wote. Mfalme wa Ufaransa alikasirika akataka kulipiza kisasi.

Migongano hii ilisababisha tatizo la Mapapa kwenda kukaa miaka 68 (1309-1377) huko Avinyon (leo nchini Ufaransa) badala ya kuongoza mjini Roma. Aliyefaulu kumrudisha Papa katika jimbo lake hilo ni Katerina wa Siena, bikira mwenye karama ya unabii.

Lakini baada ya muda mfupi makardinali waliofanya uchaguzi wa Papa mpya walisababisha farakano ndani ya Kanisa lililoendelea kwa muda wa karibu miaka 40 (1378-1417). Katika hilo Farakano la Kanisa la Magharibi, baadhi ya maaskofu na waamini wengine walimfuata Papa wa Roma na baadhi Antipapa wa Avignon wakidhani ndiye Papa wa kweli.

Hali ilizidi kuwa mbaya: mwaka 1409 walikuwepo watu watatu waliojiita "Papa" na kukubaliwa na sehemu ya maaskofu. Maaskofu na Wakristo walichoka sana farakano hilo. Mwaka 1417 Mtaguso mkuu wa Konstanz (Ujerumani) ulifaulu kuwaondoa wote watatu na kumchagua Papa mpya, Martin V.

Farakano la magharibi liliisha kwa Mtaguso wa Konstanz. Viongozi mbalimbali wakajitahidi kufuta maovu ndani ya Kanisa lakini hawakufaulu sana. Walikuwepo watu wakubwa wengi mno waliofaidika na hali halisi.

Nyumba za wamonaki zilienea sana, pia kwa sababu ilikuwa kawaida kupeleka utawani watoto wasioweza kurithi.

Cheo cha uaskofu kilikuwa nafasi iliyotafutwa sana na familia za makabaila kwa ajili ya wanao wasioweza kurithi cheo cha baba. Uaskofu ulipatikana mara nyingi kwa njia ya kuwahonga wenye haki ya kumchagua au kumthibitisha askofu. Viongozi wa Kanisa katika eneo fulani walipokea hela kabla ya kumchagua askofu mpya. Papa wa Roma alidai hela kabla ya kumthibitisha askofu yeyote aliyechaguliwa. Mfalme alidai hela kabla ya kumkabidhi askofu madaraka ya kiserikali katika eneo lake.

Lakini malipo hayo yote yalifidiwa tena na watu wa kawaida, wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo waliopaswa kumlipa askofu kodi zao kila mwaka.

Maaskofu wengine walianguka kabisa wakitumia hela zao katika vita dhidi ya majirani wao, kwa ujenzi wa maboma na makanisa uliopita uwezo wao, au kwa maisha ya ulevi na uasherati. Askofu alikataliwa kuoa lakini wengi walikuwa na wapenzi wao na kuwajengea nyumba kubwa pamoja na watoto wao.

Wakristo wengi wakasikitika juu ya hali hii. Mapapa mbalimbali walijaribu kusimamisha maovu hayo lakini bila mafanikio makubwa.

Yohane Hus na Umoja wa Ndugu[hariri | hariri chanzo]

Padri Yohane Hus alikuwa mwalimu wa teolojia kwenye Chuo Kikuu. Mwaka 1412 alihubiri kwa nguvu sana kule Praha (leo mji mkuu wa Ucheki), akafundisha ya kwamba mamlaka kuu Kanisani ni katika Biblia si katika maamuzi ya maaskofu au Papa.

Maaskofu wakamtangaza kuwa mzushi. Alishtakiwa mbele ya mfalme lakini wengi walimfuata. Akahifadhiwa na kufichwa na kabaila katika boma lake.

Miaka 1414-1418 kulikuwa na Mtaguso mkuu wa Kanisa Katoliki kule Konstanz, Ujerumani. Hus akaitwa kujitetea mbele ya mkutano huo, akaahidiwa ulinzi wa mfalme, yaani kwamba ataweza kurudi tena hata akionekana kuwa mzushi. Lakini kinyume cha ahadi alikamatwa akahukumiwa kuwa mwasi na mzushi, akachomwa moto akiwa hai.

Wafuasi wake katika mikoa ya Bohemia na Moravia (leo Ucheki) wakasikitika mno. Wengine wakachukua silaha wakataka kutenga nchi yao kutoka uongozi wa Kanisa.

Vita vya miaka mingi vilianza kati ya Wahus na askari wa mfalme na maaskofu. Alama ya Wahus ilikuwa kikombe cha Ekaristi kwani Hus alifundisha ya kwamba Wakristo wote wanapaswa kupokea kikombe kanisani (katika karne XII Kanisa Katoliki lilianza desturi ya kutoa kikombe kwa mapadri tu).

Mwishoni Ukristo wa Bohemia na Moravia uligawanyika. Wahus wakali waliojaribu kuunda utaratibu wa kisiasa juu ya mahubiri ya Yesu na kuwalazimisha wote kuufuata kwa silaha wakashindwa. Wengine wakafuata Wahus wasio wakali waliopatana na wakubwa wa nchi. Wengine wakabaki ndani ya Kanisa Katoliki, wakaruhusiwa kuwa na ibada ya Misa (chakula cha Bwana) wakipokea sakramenti katika maumbo ya mkate na divai.

Mwaka 1457 kikundi kidogo cha wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini walianzisha jumuiya ya Kikristo iliyoitwa "Umoja wa Ndugu", wakajaribu kuishi kama ndugu wakikaa pamoja, kufanya kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao.

Mbinu hii ilifanana na watawa aina ya Wafransisko lakini walikuwa jumuiya ya watu wenye ndoa na watoto. Waliona muhimu wasiwe na taratibu za utawala katika Kanisa, lakini viongozi wawe kama ndugu na watumishi wa wengine. Hawakutaka kumlazimisha yeyote katika mambo ya imani kama ilivyokuwa katika maeneo ya Wakatoliki na ya Wahus wengine.

Mwanzoni walihudumiwa kiroho na mapadri wa Kanisa Katoliki, lakini mwaka 1467 waliamua kuchagua watumishi wao wenyewe, wakiwemo mpaka leo mashemasi, makasisi na maaskofu. Umoja huo ulienea Bohemia na Moravia ukawa chanzo cha madhehebu ambayo yalistawi upya kuanzia mwaka 1722 na yanaitwa ya "Wamoravia" (leo wengi wao wanaishi nchini Tanzania).

Mwisho wa Karne za Kati[hariri | hariri chanzo]

Karne za 15 na 16 zilikuwa muhimu katika historia ya Ukristo.

Huko Asia ya Kati jeshi la Wamongolia Waislamu chini ya kiongozi Timur liliteka na kuharibu nchi nyingi. Makanisa yalichomwa moto popote Asia ya Kati na Uajemi mpaka Palestina. (Wakaharibu vilevile nyumba za dini nyingine kama Wabuddha au Wahindu).

Mwaka 1453 mji mkubwa wa Bizanti ukatekwa na jeshi la Waturuki Waislamu. Ulikuwa mwisho wa Dola la Roma lilivyoendelea katika eneo la mashariki. Tangu muda ule Wakristo wote wa Mashariki ya Kati wameishi chini ya Waislamu.

Waturuki wakaendelea kuingia Ulaya ya Kusini-Mashariki. Kwa muda wakatawala eneo la nchi za Ugiriki, Bulgaria, Romania, Masedonia, Serbia, Albania, Montenegro na Hungaria za leo. Ukristo wa Kiorthodoksi ulibaki huru katika nchi za Urusi na Ethiopia tu.

Lakini Hispania wafalme Wakatoliki walifaulu kuwafukuza Waarabu kutoka rasi ile. Tangu mwaka 711 hadi 1491 sehemu za Hispania na Ureno zilikuwa chini ya Waarabu Waislamu. Baadhi ya wenyeji walisilimu.

Kumbe 1491 mji wa mwisho uliotawaliwa na Waarabu ulitekwa, na mfalme wake akakimbilia Moroko. Wakristo wa nchi hizo walichukua nafasi ya kulipiza kisasi kwa mateso yote ya nyuma. Waislamu waliobaki walilazimishwa kubatizwa, wengine waliuawa.

Ingawa uhusiano kati ya mataifa ya Waislamu na ya Wakristo ulikuwa mgumu yaliendelea kufanya biashara. Kwa jumla Waarabu walikuwa na ujuzi zaidi katika mambo ya elimu na ufundi. Vilevile walifaulu sana katika biashara. Ni Waarabu walionunua bidhaa kule India na kuzipeleka mpaka Italia.

Wazungu walisikitikia sana bei kubwa ya bidhaa hizo na hasa faida kubwa ya wafanyabiashara Waislamu lakini wakazinunua kwani wenyewe walishindwa kuzitengeneza.

Katika kipindi kilekile mawazo mapya yalienea duniani. Anguko la Bizanti mwaka 1453 lilisababisha wasomi wengi wa mashariki kukimbilia Ulaya Magharibi wakileta vitabu vyao. Wataalamu walianza kusoma tena vitabu vya Wagiriki na Waroma wa kale. Elimu ilisonga mbele. Hasa mijini shule ziliundwa.

Mjerumani kwa jina Gutenberg alitengeneza mashine ya kwanza ya kupiga chapa vitabu. Hivyo vitabu vilianza kupatikana kwa urahisi. Habari zikazunguka haraka kati ya nchi na nchi, hali isiyojulikana karne nyingi tangu anguko la Dola la Roma.

Yakaanza kusambaa tena mafundisho ya kale kuwa dunia si tambarare lakini mviringo kama chungwa. Alijitokeza nahodha Mwitalia kwa jina Kristoforo Kolombo aliyetaka kujaribisha mafundisho hayo. Ikiwa dunia kweli ina umbo la chungwa inawezekana kuelekea magharibi kutoka Hispania na kufika mashariki katika Bara Hindi. Kwa njia hiyo inawezekana kufanya biashara moja kwa moja na nchi tajiri za mashariki bila kuwapa faida wafanyabiashara Waarabu. Mfalme wa Hispania akampa Kolombo fedha za kuandaa meli tatu.

Mwaka 1492 Kolombo akaondoka Hispania akakuta bara jipya magharibi lililoitwa baadaye Amerika. (Mwenyewe alifikiri amefika Bara Hindi, hivyo akawaita wenyeji "Wahindi" na visiwa alipofika mwanzoni mpaka leo huitwa "West Indies" = India Magharibi).

Wahispania walipora utajiri wa mataifa ya Amerika yaliyokosa silaha za kushindana nao. Utajiri huo mpya ulisaidia maendeleo ya Ulaya kupiku yale ya mataifa ya Waislamu na ya Asia.

Urekebisho wa Kikatoliki na Matengenezo ya Kiprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Martin Luther mwenye umri wa miaka 46.

Umoja halisi wa Kanisa unaweza kupatikana tu katika ukweli wa Injili ya Yesu Kristo. Ni habari mbaya kwamba katika karne ya 16 kuupigania ukweli huo kulivunja umoja wa Ukristo wa magharibi. Haiwezekani kushangilia mafarakano ya wafuasi wa Yesu.

Yale ya karne hiyo yalitokana na kuelewa tofauti kweli za imani ya Kikristo na yalikuwa na ukali kwa sababu pande zote zilisadiki kwamba kushikilia kwa usahihi ufunuo wa Mungu ni suala la wokovu wa milele. Kwa mfano, Martin Luther aliandika, «Sikubali mafundisho yangu yahukumiwe na yeyote, hata kama ni malaika. Asiyekubali mafundisho yangu hawezi kufikia wokovu».[1]

Pamoja na hayo, mambo mengi yalichangia farakano, si teolojia tu, bali siasa, uchumi, jamii na utamaduni. Wakati huo mara nyingi hoja za imani na malengo ya kisiasa vilichanganyikana: wanasiasa wengi walitumia hoja hizo ili kufikia malengo ya kiutawala, na vilevile wanateolojia walitumia siasa kutetea mafundisho yao ili kuvuta watu. Ndiyo sababu Luther alichorwa kama shujaa wa taifa la Ujerumani.

Mara nyingi pande zote zilipotosha maana ya wapinzani na kuwachora vibaya wakivunja amri ya nane inayokataza uongo dhidi ya jirani. Hata waliojitahidi kusema ukweli tu juu ya wengine kwa kawaida hawakujitahidi vya kutosha kuelewa msimamo wao na kuona kwamba pengine si mbaya zaidi. Kila mmoja alitaka ushindi akachangia ugomvi uliorithishwa kwa vizazi vilivyofuata.

Hivyo, kilichosababisha zaidi farakano si masuala ya imani yaliyojadiliwa na Waprotestanti, bali lawama zao dhidi ya hali mbaya ya Kanisa la wakati huo iliyokuwa inakera wengi na kuwaelekeza kuunga mkono urekebisho.

Hapo kale neno hilo (kwa Kilatini reformatio) lilihusu badiliko la hali mbaya iliyopo ili kurudia hali nzuri zaidi ya awali. Katika Karne za Kati lilitumika mara nyingi kwa marekebisho ya umonaki.

Katika karne ya 15 haja ya urekebisho ilionekana wazi si tu kwa mashirika ya kitawa bali kwa Kanisa lote. Hasa Mtaguso wa Konstanz (1414-1418) ulidai kabisa ufanyike «katika kichwa na katika viungo». Lakini kwa jumla mitaguso yote ya Karne za Kati na mikutano mingi ya Bunge la Dola la Ujerumani ililenga urekebisho wa Kanisa.

Kwa kweli Karne za Kati zilikuwa na mchanganyiko wa mambo yaliyopingana: ibada za nje tu na za dhati kabisa; teolojia iliyoelekeza kutenda kwa msingi wa nipe nikupe na hakika ya kwamba binadamu anategemea kabisa neema ya Mungu; kutojali wajibu hata upande wa viongozi wa Kanisa na marekebisho safi ya mashirika ya kitawa.

Karne XV ilikuwa kipindi cha umotomoto wa pekee katika Kanisa, ambapo walei wengi zaidi na zaidi walipata elimu nzuri, hivyo walitamani hotuba bora na mafundisho ya kuwasaidia kuishi Kikristo zaidi. Luther aliitikia haja hizo zilizomgusa sana kama mtu wa wakati wake.

Mwenyewe alitumia kwa nadra neno urekebisho, lakini likaja kuwa jina la kawaida la matukio yale mengi ya miaka 1517 - 1555, yaani kuanzia uenezi wa hoja 95 za Martin Luther hadi amani ya Augsburg. Kati yake mabishano ya Kikanisa yaliyosababishwa na teolojia ya Luther, yalichanganyikana mapema na siasa, uchumi na utamaduni, kutokana na hali halisi ya wakati huo, mbali kuliko mwenyewe alivyofikiri.

Viongozi Wakatoliki, yaani Papa na Mfalme mkuu wa Ujerumani, waliona kwa masikitiko kutokea kwa mafarakano lakini mawazo yao yalitekwa na shughuli nyingi za siasa na vita hata wakatumia nguvu zao kushindana kati yao.

Mwanzoni walimwona Luther kuwa padri mdogo tu apaswaye kurudishwa kwenye njia iliyo halali. Papa Leo X hakuona umuhimu mkubwa katika habari zake: mwaka 1521 akamtenga Luther katika Kanisa, halafu akapokea habari za Bunge la Ujerumani lililomhukumu Luther kuwa mzushi na adui wa taifa.

Miaka 1522/1523 akafuata Papa Adriano VI: akiona uenezaji wa haraka wa mafundisho ya Luther kila mahali akakiri Kanisa lilikuwa na makosa. Lakini uongozi wake ulidumu muda mfupi mno.

Papa Klementi VII aliyefuata hakuwa na mawazo ya kiroho, akashughulikia zaidi siasa akipigana vita na Mfalme juu ya kutawala mikoa mbalimbali ya Italia.

Mwaka 1527 jeshi la Mfalme liliteka Roma, Papa akakimbia. Walipatana mwaka 1529 lakini mwaka uleule Waturuki Waislamu walifika mbele ya mji mkuu wa mfalme, Vienna. Kwa shida tu jeshi la Wakristo liliwashinda.

Mfalme Karolo V wa Ujerumani alikuwa pia Mfalme wa Hispania. Mwaka 1521 jeshi la Wahispania liliteka Meksiko, baadaye Peru katika Amerika Kusini. Dhahabu na fedha za huko zilianza kuletwa Hispania. Mfalme hakuwa na muda wala nguvu kushindana na sehemu kubwa ya makabaila wa Ujerumani waliomuunga mkono Luther.

Kivulini mwa matokeo hayo mafundisho ya Waprotestanti yalienea haraka pande nyingi za Ulaya. Kuanzia mwaka 1530 ilikuwa wazi kwamba farakano limetokea, likitenga na Papa sehemu kubwa ya Ulaya Kaskazini pamoja na matengenezo yenyewe kuvunjikavunjika katika madhehebu mbalimbali.

Sasa sauti ya wale waliodai urekebisho ndani ya Kanisa Katoliki ilisikika zaidi. Papa Paulo III akachukua hatua mbili: kwanza aliandaa mtaguso wa maaskofu wote halafu aliimarisha Baraza la Ulinzi wa Imani. Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kufuatilia habari zote za upinzani dhidi ya Kanisa Katoliki na kuomba serikali zilizokuwa mikononi mwa Wakatoliki kugandamiza wote waliotaka kufuata mafundisho ya Luther na wenzake.

Baraza hilo lilikuwa na nguvu sana: kwa jumla lilifaulu kufuta vikundi vyote vya Wainjili katika nchi kama Italia, Ureno na Hispania. Lakini ugandamizaji huo uliongeza uchungu kati ya madhehebu ukasababisha ugandamizaji wa Wakatoliki katika maeneo ya Walutheri na ya Wareformati.

Chombo kingine kilikuwa "Orodha ya vitabu vilivyopigwa marufuku" kwa kila Mkatoliki asivisome, navyo havikuruhusiwa katika nchi katoliki. Orodha hiyo ilifutwa rasmi na Papa Paulo VI mwaka 1965.

Ignas wa Loyola, mwanzilishi wa Shirika la Yesu, alivyochorwa na Peter Paul Rubens.

Chombo kingine muhimu zaidi cha urekebisho wa Kikatoliki kilikuwa Shirika la Yesu, jumuia ya mapadri iliyoongozwa na "Jenerali" wake akitumia nidhamu ya kijeshi.

Mwanzilishi wake ni Ignas wa Loyola, Mhispania ambaye alikuwa mwanajeshi. Mwaka 1521 alijeruhiwa vibaya vitani. Alipokaa hospitalini muda mrefu akasikia wito wa Mungu uliobadilisha maisha yake.

Kisha kuacha jeshi, akamtolea Bikira Maria upanga wake akawa "Mwanajeshi wa Kiroho". Alifuata kwa juhudi zote maisha ya kiroho na kutunga Mazoezi ya Kiroho ili kuongoza watu wamfuate Yesu Kristo.

Mwaka 1534, Ignas alikusanya vijana sita wakaweka nadhiri za ufukara, useja mtakatifu na utiifu, halafu ile ya kumtii daima Papa.

Kisha kusoma teolojia akapadrishwa. Akakusanya kikundi cha marafiki akiwaongoza kujenga maisha ya kiroho kwa njia ya mazoezi ya pekee. Wote walifuata utaratibu uleule. Kila mwaka walikutana kwa kipindi cha sala, kutafakari na kusoma kilichofuata hatua au mbinu maalumu. Wengi walianza kumfuata na chama chake kikakubaliwa na Papa mwaka 1540.

Shabaha kuu ilikuwa kutetea Kanisa chini ya Papa.

Kila mwanachama alitakiwa kuwa na elimu ya juu. Hivyo Kanisa Katoliki liliimarika katika teolojia, jambo lililowahi kukazwa zaidi na Waprotestanti.

Mapadri Wajesuiti walifanya hasa kazi ya ualimu wakiunda shule na kufundisha vijana elimu pamoja na upendo kwa Kanisa Katoliki.

Mkazo mwingine ulikuwa kufufua utaratibu wa maungamo. Popote Ulaya Wajesuiti walikuwa washauri hasa wa watawala Wakatoliki. Waliposikiliza ungamo la dhambi zao walipata nafasi nzuri ya kuwapa mawazo na kusababisha hatua za serikali dhidi ya Waprotestanti.

Hivyo kwa athari ya Wajesuiti polepole Uprotestanti ulirudi nyuma katika nchi za Ulaya ambako wakazi wengi walikuwa wameanza kufuata mafundisho ya Martin Luther na Calvin lakini watawala walikuwa bado Wakatoliki.

Mbali nao, mashirika mengine yalifanya kazi kubwa ya kuzuia uenezi wa Uprotestanti, kuanzia Wafransisko waliowahi kutambua hatari kabla ya viongozi wa Kanisa. Baadaye ulikuwa hasa urekebisho wa Wakapuchini uliorudisha wengi katika Kanisa Katoliki kwa upole, usikivu na ushuhuda wa maisha safi yenye kujitosa.

Miaka 1545-1563 maaskofu wa Kanisa Katoliki walikutana Trento, Italia kaskazini, wakajadiliana juu ya mafundisho na hali ya Kanisa, wakachukua hatua za kuondoa matatizo na kuimarisha imani. Maazimio yake makuu yalibaki muhimu mpaka karne ya 20:

 • a) Msingi wa imani ni Biblia pamoja na mapokeo ya Kanisa.
 • b) Sakramenti ziko saba.
 • c) Juu ya kuhesabiwa haki (jinsi ya kupata wokovu) ni kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa sababu ya matendo yake mema bali kwa neema ya Mungu, lakini lazima mwanadamu ashiriki katika kupokea na kutumia neema hiyo.
 • d) Kanisa peke yake lina mamlaka ya kueleza maana ya Biblia; Mkristo asijisomee bila mwongozo wa Kanisa; toleo pekee la Biblia linalofaa ni lile linalotolewa na Kanisa Katoliki katika lugha ya Kilatini (lililoitwa "Vulgata" - pamoja na vitabu vya "Deuterokanoni" vilivyotengwa na Luther).
 • e) Kufuta maovu katika Kanisa: kampeni za kuuza vyeti vya rehema, malipo ya maaskofu kwa Papa ili awathibitishie cheo, askofu kuwa na majimbo zaidi ya moja (walivyofanya zamani kwa sababu ya mapato).
 • f) Mapadri wawe na elimu, wote wapitie masomo ya seminari, kila mmoja afuate utaratibu wa kusoma Biblia kila siku, mahubiri yawepo katika kila Misa ya Jumapili.
 • g) Itungwe Katekisimu ya kwanza ya Kanisa Katoliki, pamoja na vitabu vipya vya liturujia.

Kwa jumla Mtaguso wa Trento ulishindwa kuwavuta Wainjili warudi, lakini uliendeleza urekebisho wa Kanisa Katoliki. Katika nchi zilizobaki chini ya Roma Kanisa lilipata nguvu tena kwa kuimarisha mafundisho ya kale pamoja na kuondoa kasoro mbalimbali. Hata hivyo haikuwezekana kufuta farakano lililotokea tayari.

Vita kati ya madhehebu ya Kikristo[hariri | hariri chanzo]

Karolo V vitani alivyochorwa na Tiziano (1548) ili kuadhimisha ushindi wake katika mapigano ya Mühlberg.

Karolo V, Kaisari wa Dola Takatifu la Kiroma, aliendesha Vita vya Schmalkald (1546-1547) dhidi ya maeneo ya Walutheri yaliyokuwa ndani ya dola hilo kubwa la Ujerumani.

Lengo lake lilikuwa kuwalazimisha watawala wadogo waliowaunga mkono Walutheri wafute matengenezo yote.

Mwanzoni alishinda (20 Julai 1547); kwenye Bunge la Augsburg (1547-1548) alidai Walutheri wakubali kuwa chini ya maaskofu na Papa wa Kanisa Katoliki. Ingawa aliruhusu ndoa ya mapadri na kupokea ekaristi kwa maumbo yote mawili (mkate na divai), maitikio hayakuwa mazuri hata kidogo: kukawa na vurugu kubwa.

Mwaka 1552, baada ya njama ya watawala hao dhidi ya Karolo V, vilianza tena vita ambavyo vilimlazimisha kukimbia Austria. Hatimaye watawala Walutheri walipatana na mwanae, mfalme Ferdinand III. Hivyo jaribio la kufuta Ulutheri kijeshi lilishindikana kabisa.

Vita vilimalizika mwaka 1555 kwa amani ya Augsburg. Mapatano hayo yalilenga kuwezesha wananchi wenye imani tofauti waishi katika taifa lilelile. Watawala walipewa haki ya kuwachagulia madhehebu ya dini raia wao. Wasiokubali kufuata imani ya mtawala, walipewa tu haki ya kuhamia eneo lingine ambapo mtawala wake alikuwa na imani yao.

Hivyo katika Dola la Kijerumani yalikubalika rasmi maeneo yaliyoshikilia Ungamo la Augsburg na yale yaliyobaki katika Kanisa Katoliki, lakini si wenye imani tofauti na hizo mbili, kama vile Wareformati na Waanabaptisti.

Amani ya Augsburg kwanza ilifaulu kuleta mahusiano imara upande wa siasa, lakini baadaye haikuweza kuzuia mlipuko wa vita vikali vya karne XVII: vita vya miaka 30 (1618-1648).

Madola ya Ujerumani yalipigana kati yao, na nchi za nje zilishiriki zikiwemo Hispania, Ufaransa, Uswidi, Uholanzi na Denmark, lakini mapigano yake yalitokea hasa katika Ujerumani kwenye eneo la Dola Takatifu la Kiroma.

Ni kwamba uhusiano kati ya madhehebu ya Kikristo ulikuwa mbaya kwa muda mrefu. Karibu katika kila nchi Wakristo walilazimishwa kufuata madhehebu rasmi, ama Ukatoliki ama Ulutheri. Ikiwa mtawala fulani aliona vema kukubali mawazo ya Luther mapadri wote walipewa chaguo la kufuata Ulutheri au kuhama nchi. Vilevile baada ya kifo chake ikiwa mtawala aliyefuata alikuwa na msimamo tofauti, mapadri wakarudi na wachungaji wa Kiinjili wakafukuzwa.

Raia hawakuulizwa wenyewe wanasadiki nini, isipokuwa katika miji iliyojitawala na kuwa na utaratibu wa kidemokrasia. Lakini hata mijini huko haikuwa kawaida kuruhusu madhehebu mawili mahali pamoja.

Mafundisho ambayo kwetu leo yanaonekana kuwa na tofauti ndogo yaliweza kumfikisha mtu gerezani au hata kifoni.

Uhusiano mbaya ulikuwepo vilevile kati ya wafuasi wa Luther na Wareformati. Katekisimu zao zilitumika kama bendera. Walishutumiana kuwa wazushi wasioelewa vizuri kiini cha imani.

Kilichofuata ni kipindi cha vita vya kidini kule Ulaya. Kilele kilikuwa Vita vya Miaka 30 ambavyo vilianza kule Bohemia na Moravia kwa sababu watawala wadogo waliokuwa karibu na Umoja wa Ndugu walijaribu kumpindua Mfalme Mkatoliki.

Vita hivyo vilianza kama mapigano ya kidini kati ya madhehebu tofauti ya dola moja la Ujerumani, lakini viliendelea kuwa vita vya Ulaya nzima ambako nchi ya Wakatoliki kama Ufaransa ilishikamana na Uswidi ya Kiprotestanti dhidi ya Kaisari Mkatoliki.

Vita hivyo vilileta uharibifu mkubwa mno katika Ujerumani. Kuna makadirio ya kwamba karibu theluthi moja ya wakazi wote walikufa kutokana na mauaji, njaa na magonjwa. Katika maeneo ya Ujerumani ya Kusini zaidi ya nusu ya watu walipotea.

Wanajeshi walikuwa askari wa kukodiwa ambao mara nyingi hawakulipwa bali walipewa uhuru wa kutwaa kwa mabavu chochote walichotaka.

Uchovu ulileta majadiliano juu ya amani. Mwaka 1648 wawakilishi wa wafalme walipatana katika amani ya Westfalia kuhusu kanuni za amani.

 • Madhehebu matatu yaliyokubaliwa Ulaya ni Wakatoliki, Walutheri na Wareformed; mengine (kama Waanabaptisti na Umoja wa Ndugu) yaliangaliwa kuwa ya kizushi popote.
 • Kila mtawala aliamua kwa dola lake ni yapi kati ya madhehebu matatu halali yatafuatwa lakini raia walikuwa na haki ya kutoka katika nchi kama mtawala alikataa dini yao. Sheria ilikuwa: "Cuius regio, eius religio" (mwenye nchi ni mwenye kuamua dini)
 • Katika maeneo kadhaa Wakristo wa madhehebu tofauti walipewa ustahimilivu, lakini katika maeneo mengine walipaswa kuhamia nchi ya madhehebu yao au kufuata madhehebu rasmi ya nchi.
 • Ikiwa mtawala atabadili madhehebu baadaye wananchi wataruhusiwa kuendelea walivyozoea.
 • Uholanzi na Uswisi zilitoka katika Dola Takatifu la Kiroma kama nchi huru za pekee.
 • Mfalme wa Uswidi alitwaa maeneo makubwa katika Ujerumani ya Kaskazini

Kumbe mapatano hayo yaliunda ramani ya kimadhehebu kule Ulaya yenye maeneo ya Wakatoliki, Walutheri au Wareformati watupu. Jumuiya ndogo ziliendelea kugandamizwa wakapata ustahimilivu mahali pachache. Hivyo wafuasi wa madhehebu madogo walilazimika kuficha imani yao au kuhamahama katika Ulaya.

Wakati ule nafasi mpya ilitokea: Mfalme wa Uingereza alikuwa na makoloni Marekani lakini alikosa watu. Akatafuta walowezi kwa ajili ya makoloni yake akiwaahidia wote kwamba watapata shamba pamoja na uhuru wa dini. Hivyo watu kutoka nchi nyingi za Ulaya walianza kuhamia Marekani, hasa wale waliokosa uhuru huo. Mpaka leo nchi mbalimbali za Ulaya zinafuata hasa madhehebu moja, na Marekani ina madhehebu makubwa ambayo hayana wafuasi wengi Ulaya, k.mf. Wabatisti.

Umisionari kupamba tena[hariri | hariri chanzo]

Fransisko Saveri akimuongoa Paravas huko Goa, India, katika picha ya karne ya 19.

Wakati wa matengenezo na mafarakano ulikuwa pia kipindi kilicholeta habari za nchi mpya kwa watu wa Ulaya. Mataifa ya Wahispania na Wareno yalijenga aina mpya za meli zilizoweza kusafiri kote duniani hata kuvuka bahari kubwa.

Wafanyabiashara na wanajeshi wao walizunguka pande zote za dunia wakiambatana na mapadri wao. Hao walikutana na wenyeji wengi wa nchi mbalimbali wasio Wakristo, au walikuwa Wakristo lakini si washiriki wa Kanisa Katoliki (kama Waethiopia au Wahindi wa Kusini).

Wakaanza kuwaeleza imani, wakahubiri mbele ya Mfalme wa China, mbele ya Negus Negesti wa Ethiopia na mbele ya watawala wa Amerika Kusini.

Tatizo la misheni hizo lilikuwa kwamba liliambatana na uenezaji wa kijeshi wa Hispania na Ureno. Hasa Amerika wamisionari walijikuta kati ya mahitaji ya walowezi, waliotaka kuhudumiwa kiroho, na mahitaji ya wazalendo, waliogandamizwa vibaya na walowezi walewale.

Serikali ya kikoloni ilikuwa vilevile serikali ya mfalme Mkatoliki. Haikuwa rahisi kwa wamisionari kutofautisha kati ya pande hizo mbili. Mara nyingi Kanisa lilibariki tu utawala wa kikoloni uliogandamiza wenyeji.

Lakini mara kwa mara walijitokeza Wakristo wengine waliopinga unyama na kuleta taarifa za kweli kule Ulaya. Mmojawao alikuwa Askofu Bartolomeo Las Casas aliyewashtaki walowezi Wahispania kwa sababu waliua wenyeji wengi wakiwalazimisha kufanya kazi zao migodini na mashambani bila kujali afya zao. Akafaulu kuleta sheria zilizolinda Waamerika na kupunguza ukali dhidi ya watumwa, lakini walowezi walijaribu kumwua.

Zaidi tena Wajesuiti walijaribu kuwalinda Waindio wa Paraguay wakiwakusanya katika vijiji vya ujamaa vilivyojitegemea kiuchumi na hata kisiasa. Lakini walishtakiwa na walowezi majirani waliotaka kuwinda watumwa, ati wanadhoofisha utawala wa kikoloni. Mwishoni Wajesuiti walifukuzwa na serikali, na vijiji vya Wakristo wenyeji waliharibiwa na wawindaji wa watumwa.

Kule Asia mapadri wa Shirika la Yesu walifaulu kupanda mbegu ya Injili mpaka Japani na China. Walijitahidi kupatanisha Injili na utamaduni wa nchi hizo ambao ni tofauti na desturi za Ulaya. Lakini uongozi wa Kanisa kule Roma uliwakataza wasitumie mbinu hizo. Hivyo Wakristo wa Japan walionekana kufuata dini ya kigeni. Kwa sababu hiyo waligandamizwa, ila wachache walishika imani yao kwa siri mpaka kutokea kwa uhuru wa dini katika karne ya 19.

Kati ya wote anakumbukwa hasa Fransisko Saveri (Francisco de Jasso y Azpilicueta) (Javier, Navarra, leo nchini Hispania, 7 Aprili 1506 - kisiwa cha Shangchuan, China, 3 Desemba 1552), padri wa Shirika la Yesu, ambalo alichangia kulianzisha pamoja na Ignas wa Loyola.

Baadaye alitangaza Injili katika nchi nyingi za Ulaya, Afrika na Asia hata akawa kati ya wamisionari maarufu zaidi ya historia ya Kanisa.

Kati ya miaka 1500 na 1850 wamisionari Wakatoliki walihubiri kwenye pwani ya Afrika, hata Afrika Mashariki. Walifuata uenezi wa Wareno waliojaribu kutawala pwani hiyo kama vituo vya biashara kati ya Ulaya na Bara Hindi. Ustawi wa pekee ulipatikana katika ufalme wa Kongo (kusini kwa mto huo) ambapo Wakristo walifikia kuwa 50% za wakazi wote, na kati yao alipatikana askofu Mwafrika wa kwanza kutoka Kusini kwa Sahara, Dom Enrique.

Kutoka kwa makao yao ya Sofala na Msumbiji walijaribu pia kutawala biashara ya dhahabu iliyochimbwa katika eneo la Mwene Mtapa (Zimbabwe).

Kati ya matunda bora ya uinjilishaji huo wanakumbukwa "Mashahidi wa Mombasa" waliomfia Yesu mwaka 1631.

Mizizi ya Kanisa Afrika ilikauka tena mnamo karne za 16-18 kwa sababu ya kuingiliana kwa hotuba ya Injili na siasa ya ukoloni. Udhaifu wa kibinadamu uliongezea ugumu wa mazingira na hali ya hewa kwa ajili ya wamisionari kutoka Ulaya.

Upietisti[hariri | hariri chanzo]

Philipp Jakob Spener (16351705) anaitwa pengine "Baba wa Upietisti".

Upietisti (kwa Kiingereza Pietism, kutoka neno la Kilatini pietas, yaani heshima kwa Mungu, kwa wazazi, kwa ndugu na kwa nchi asili) ulikuwa tapo lenye athari kubwa kati ya Walutheri, lakini pia kwa madhehebu mengine ya Uprotestanti, na hata kwa Wakatoliki huko Ulaya na Amerika Kaskazini[2] tangu mwishoni mwa karne ya 17.

Uliunganisha mikazo ya Kilutheri kuhusu mafundisho ya Biblia ya Kikristo na mikazo ya Kikalvini kuhusu maadili imara.

Asili yake ni Ujerumani ya leo na kazi ya Philipp Jakob Spener, mwanateolojia Mlutheri aliyesisitiza mabadiliko ya Mkristo kwa aina ya kuzaliwa upya. Ingawa yeye hakudai wafuasi wake wajitenge na Wakristo wenzao, mahimizo yake yalielekea huko.

Upietisti ulienea kwanza Uswisi na nchi nyingine za lugha ya Kijerumani barani Ulaya, halafu Skandinavia na Baltiki (ulipoathiri zaidi tena utamaduni wa Kikristo kupitia watu kama Hans Nielsen Hauge huko Norway, Carl Olof Rosenius huko Sweden, Katarina Asplund huko Finland na Barbara von Krüdener katika nchi za Baltiki), na hatimaye Ulaya nzima.

Kutoka huko ulipelekwa Amerika Kaskazini, hasa kwa njia ya wahamiaji kutoka Ujerumani na Skandinavia, ukaathiri Waprotestanti wenye asili tofauti ukachangia katika karne ya 18 mwanzo wa Ukristo wa Kiinjilisti, ambao leo una waumini milioni mia tatu.

Tapo la Upietisti ndani ya Ulutheri lilifikia kilele chake katikati ya karne ya 18, lilififia kati karne ya 19 na kutoweka Amerika mwishoni mwa karne ya 20.

Hata hivyo, baadhi ya misimamo yake iliathiri Uprotestanti kwa jumla, ikimchochea kasisi Mwanglikana John Wesley kuanzisha tapo la Wamethodisti, na vilevile Alexander Mack kuanzisha tapo la Schwarzenau Brethren kati ya Waanabaptisti.

Huko Marekani, Upietisti ulitawala pia kati ya Quakers, Wakalvini, Wabaptisti, Waanglikana n.k.

Umisionari wa Kiprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Tumeshaona kwamba tangu mwaka 1500 wamisionari Wakatoliki walienda sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 17 Waprotestanti walienea nje ya Ulaya, lakini bila kumtangaza Kristo kwa wenyeji, kwa mfano katika makoloni ya Marekani mashariki ya leo. Kumbe katika 18 walianza kuiga mifano ya wamisionari Wakatoliki.

Uenezaji wa Ukristo wa Kiprotestanti ulianzishwa na Wakristo kutoka nchi za Ulaya zilizoendelea kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mapinduzi ya viwandani yaliongeza sana uwezo wa kiuchumi wa mataifa hayo.

Biashara ya kimataifa ilianza kuunganisha nchi za mbali sana. Vyombo vya usafiri kama vile meli, reli na baadaye hata ndege vilifikisha watu na bidhaa kila sehemu za dunia. Watu walianza kupata habari za nchi zisizojulikana kwao mpaka wakati ule.

Wakristo wa nchi za Ulaya walitumia mawasiliano hayo. Labda tunaweza kulinganisha hali hiyo na sera za mitume ambao walitumia njia zilizofunguliwa na biashara ya Kiroma katika karne za kwanza. Wengine waliona uwezo wao kama wito wa Mungu kwa Wakristo wa Ulaya katika karne ile hasa.

Mahali pengi Ulaya Wakristo hawakuridhika tena na hali ya Kanisa. Ukristo ulikwisha kuwa sehemu ya utamaduni na jambo la kawaida. Bila kutafakari sana, mtoto alibatizwa, akafundishwa na kupewa Kipaimara, akafunga ndoa kanisani, akawabatiza watoto wake halafu akazikwa kwa ibada.

Kanisa lilikuwa kama idara ya serikali iliyosaidia taifa kuweka utaratibu wa kidini kwa manufaa ya maadili ya umma. Serikali zilihimiza watu washiriki na kuhudhuria ibada. Wasipofika kanisani waliweza kutozwa faini.

Lakini mazingira na hali ya maisha vilibadilika. Watu walianza kuhamia mijini, jumuiya za vijiji zilianza kulegea na kuvunjika.

Mahali pengi watumishi wa makanisa hawakujua kujibu maswali mapya ila tu kukumbusha mazoea ya kale na mila nzuri za zamani.

Ndiyo asili ya matapo ya uamsho yaliyotokea kwa nguvu sana. Wasioridhika na hali hiyo walikutana nje ya makanisa. Katika maeneo ya Kiprotestanti hali ilitegemea. Penye uongozi wenye busara walipewa nafasi zao shirikani. Watu waliguswa upya na neno la Mungu na Roho wake, walitafuta njia mpya za kuishi na kuonyesha imani yao. Hivyo vilijitokeza vyama vya kusaidia wagonjwa, wajane, mayatima na maskini.

Penye uongozi mkali uliokataa njia na mbinu mpya Wakristo walikutana na kusali katika nyumba za watu. Wengine walianzisha jumuiya na madhehebu ya pekee. Lakini sehemu kubwa ya Wakristo wa uamsho walielewa kazi yao ya kutengeneza upya makanisa yao badala ya kuunda vikanisa vipya.

Katika maeneo ya Wakatoliki matapo yaliyofanana na uamsho yalisababisha mara nyingi kutokea kwa shirika jipya la watawa au la walei. Muundo wa Kanisa Katoliki unasaidia kuwapa watu wenye wito au vipawa vya pekee nafasi zao katika mashirika hayo.

Kanisa la Anglikana liliunda kamati ya kupeleka Injili katika nchi za ng'ambo lakini ilishughulikia hasa Waingereza waliohamia makoloni. Polepole wazalendo wachache walianza kuwaendea pia, jambo lililokuwa gumu kutokana na hali ya ukoloni wenyewe.

Kanisa la kwanza la Kiprotestanti lililotuma wamisionari hasa kwa watu wasiomjua Kristo lilikuwa ni la Ndugu wa Herrnhut (Wamoravia).

Katika kijiji hicho kidogo cha Ujerumani waliishi wakimbizi kutoka Moravia waliopewa ustahimilivu kuanzisha upya ushirika wa Umoja wa Ndugu kufuatana na urithi wao kutoka Ucheki. Walikuwa watu wa kawaida kama wakulima na mafundi.

Siku moja katika mwaka 1732 walikutana na mgeni, kwa jina Antoni, mtumishi wa Mdenmark aliyemtembelea Mkuu wa Herrnhut, Ludwig von Zinzendorf. Antoni alikuwa mtumwa mwenye asili ya Afrika aliyenunuliwa na bwana wake katika Visiwa vya Karibi. Baadaye akapewa uhuru wake akasafiri pamoja na bwana wake hadi Denmark.

Kwa Antoni Ndugu wa Herrnhut wakasikia kwa mara ya kwanza habari za hali mbaya ya watumwa Waafrika kule Karibi, na jinsi walivyozuiwa kusikia neno la Mungu pamoja na mateso yao mengine. Usiku ule ndugu wawili wakasali pamoja na asubuhi yake wakamwendea Mkuu wa Herrnhut wakamwomba ruhusa ya kusafiri hadi Karibi ili wawahubirie wale watumwa. Katika sala hiyo ya maseremala wawili ilianza kazi ya misheni ya Umoja wa Ndugu (Wamoravia).

Baadaye Ndugu Wamoravia waliendelea kuhubiri kule Greenland, Urusi, Nikaragua, Afrika Kusini na kati ya Waindio wa Amerika. Mawasiliano mapya yakaleta habari hiyo katika kila pembe ya dunia zisizosikika zamani kwa watu wengi.

Wamoravia walihubiri mahali pengi Ulaya kati ya Wakristo wa madhehebu yote bila kuwashawishi wajiunge nao lakini walieneza sana habari za misheni.

Wakiitikia mfano wa Ndugu wa Herrnhut Wakristo kutoka vikundi mbalimbali vya uamsho walianza kuelewa wajibu wao wa kueneza Injili kote duniani.

David Livingstone (1813-1873) kutoka Uskoti ni kati ya wamisionari bora wa Afrika.

Mnamo mwaka 1800 Wakristo Waingereza waliunda vyama mbalimbali vya misheni, kama Wabatisti mwaka 1792, Chama cha Misheni cha London mwaka 1795 na Chama cha Misheni cha Kanisa (la Kianglikana = Church Missionary Society/CMS) mwaka 1799. Waprotestanti wa nchi nyingine za Ulaya walifuata.

Mara nyingi wakati ule si viongozi wa madhehebu ya Kiprotestanti (isipokuwa kwa kiasi Waanglikana) walioendesha kazi ya misheni, kwa kuwa walijali maeneo yao tu wakikosa mtazamo wa dunia nzima kama wenzao Wakatoliki.

Kumbe walikuwa walei na wachungaji wa kawaida waliounda vyama vya misheni, kuiombea kazi hiyo, kutafuta habari za nchi nyingine na kuchanga pesa wakiandaa vijana watakaokuwa tayari kuacha ndugu zao wakielekea nchi za mbali zisizojulikana nao.

Kanisa Katoliki na la Kiorthodoksi katika karne ya 18[hariri | hariri chanzo]

Wakati Ukristo ulipozidi kuenea na kuchangamka katika bara lote la Amerika, huko Ulaya Kanisa Katoliki lilipitia kipindi cha udhaifu, hasa kutokana na mashambulizi ya falsafa ya Mwangaza dhidi yake.

Falsafa hiyo ilienea katika matabaka ya juu ya nchi nyingi na kufuatwa na serikali zake, ambazo zilianza kulibana kwa njia nyingi, hasa kwa kuzuia mashirika ya kitawa.

Mambo yalizidi kuwa magumu Mapinduzi ya Ufaransa yalipopiga vita dini, kuanzia Ukatoliki. Akili ilisimikwa kama mungu mpya. Kalenda mpya ilitengenezwa ili kufuta wiki na Jumapili pamoja na sikukuu za Kikristo. Monasteri zote zilibomolewa, wengi waliuawa au kufukuzwa nchini kwa sababu ya imani yao. Mali za Kanisa zilitaifishwa na mapadri walidaiwa kula kiapo cha kufuata serikali badala ya Papa. Mnamo 1799 Papa Pius VI alitekwa hadi Ufaransa na hatimaye kufa kifungoni.

Kiongozi wa Ufaransa, Napoleon Bonaparte, alizidi kueneza misimamo mipya katika sehemu kubwa ya Ulaya aliyoiteka.

Hata Waorthodoksi walipata shida za namna hiyo hasa Urusi, ambapo mwaka 1721 Kaisari Petro I alifuta Upatriarki nchini na kuweka Kanisa moja kwa moja chini ya serikali.

Ukristo katika karne ya 19[hariri | hariri chanzo]

Pius IX, Papa aliyeongoza Kanisa kwa muda mrefu kuliko wote (1846-1878).

Baada ya Ufaransa wa Napoleon kushindwa (1815), nchi za Ulaya zilikubaliana kurudisha hali ilivyokuwa kabla ya mapinduzi, lakini haikuwa rahisi. Umati wa watu ulizidi kusogea mbali na dini.

Baada ya mateso yao, Papa na Kanisa Katoliki walipewa tena heshima, lakini siasa iliendelea kuwa dhidi yao.

Kilele chake ni Kulturkampf (kwa Kijerumani: vita vya utamaduni) iliyotangazwa na Chansela Bismarck ili kuzuia umoja wa Wakatoliki wa Ujerumani na Papa. Majimbo na parokia nyingi vilibaki bila mchungaji, mapadri wengi walifungwa n.k.

Kabla ya hapo, Papa Pius IX alikutanisha maaskofu mjini Roma kwa Mtaguso wa kwanza wa Vatikano (1869-1870) uliotangaza dogma ya karama ya Papa kutokosea anapotoa mafundisho ya moja kwa moja "ex cathedra".

Mtaguso ulikatishwa na jeshi la Italia lililovamia Roma na kuuteka moja kwa moja, likikomesha Dola la Papa (1870). Tukio hilo lilimkomboa Papa kutoka majukumu ya kisiasa na kumwezesha kuimarisha mamlaka yake ya kiroho duniani kote dhidi ya utaifa uliotesa Kanisa kwa karne kadhaa.

Karne ya 19 iliona pia Wakatoliki kuchangamkia tena umisionari, kuanzia Wafaransa.

Jambo lingine la pekee katika Kanisa Katoliki la karne hiyo ni uundaji wa mashirika ya kitawa ya kike na ya kiume zaidi ya 2000 yaliyolenga huduma maalumu, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha mafukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji habari. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa jimbo, baada ya mashirika ya zamani kuzuiwa na serikali.

Kati ya waanzilishi muhimu zaidi wakumbukwe Karolo Yosefu Mazenod (1782-1861), Vinsenti Pallotti (1795-1850), Antoni Maria Claret (1807-1870), Yohane Bosco (1815-1888), Daniele Comboni (1831-1881), Arnold Janssen (1837-1909). Kati ya wanawake, Yoana Antida Thouret (1765-1826), Magdalena wa Canossa (1774-1835), Visensya Gerosa (1784-1847) pamoja na Bartolomea Capitanio (1807-1833), Fransiska Saveri Cabrini (1850-1917).

Uprotestanti uliendelea kufaidika na uamsho, ingawa huko Marekani walifikia hatua ya kuanzisha madhehebu mengi ya aina mpya, yaliyojaribu kuanza kila kitu upya kwa msingi wa Biblia, yakidharau historia yote ya Kanisa kama upotoshaji wa imani.

Miaka ya mwisho ya karne ya 19 iliona ustawi wa elimu ya Biblia iliyoongozwa na mawazo mapya kabisa yaliyoyumbisha imani ya wengi kwa kukanusha mambo yapitayo maumbile (teolojia ya Usasa).

Karne ya 20[hariri | hariri chanzo]

Papa Yohane Paulo II (1978-2005) anahesabiwa na wanahistoria kadhaa kama mtu aliyeathiri ulimwengu kuliko watu wote wa karne ya 20, hasa kwa kusambaratisha Ukomunisti na kumaliza vita baridi.

Wakati Ulaya ulipozidi kuachana na dini, Ukristo ulienea kwa kasi ya ajabu katika bara la Afrika, na kwa kiasi tofauti katika maeneo mengine yasiyokuwa na mapokeo hayo.

Mang'amuzi ya kimisionari yalifanya Wakristo watambue upya haja ya umoja kati yao. Walianza Waprotestanti (Kongamano la Edinburgh, 1910), halafu Waorthodoksi na Wakatoliki.

Masomo ya liturujia na uchungaji pamoja na uchunguzi wa maandishi ya mababu wa Kanisa vilileta pumzi mpya katika madhehebu mbalimbali.

Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965) ulioitishwa na Papa Yohane XXIII ulielekeza Kanisa Katoliki kukabili vema ulimwengu wa kisasa badala ya kuulaumu tu.

Lakini karne ya 20 inakumbukwa hasa kwa dhuluma za kidini zisizowahi kutokea: hasa Ukomunisti, ulioteka Urusi ukaenea polepole hadi kutawala theluthi moja ya binadamu wote, ulipiga vita dini kwa namna zote na kuua mamilioni ya waamini, hasa Waorthodoksi.

Hatimaye, chini ya Papa Yohane Paulo II, wa kwanza kutoka mataifa ya Kislavi, Wapolandi walifaulu kuangusha serikali ya Kikomunisti, wakifuata na wenzao wa nchi zote za Ulaya Mashariki.

Baada ya hapo, Ukristo uliamka upya katika nchi hizo.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. Martin Luther, Weim., X, P. Il, 107, 8-11
 2. In places, such as parts of England and America, where Pietism was frequently juxtaposed with Roman Catholicism, Catholics also became naturally influenced by Pietism, helping to foster a stronger tradition of congregational hymn-singing, including among Pietists who converted to Catholicism and brought their pietistic inclination with them, such as Frederick William Faber.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]