Nenda kwa yaliyomo

Injili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Papyrus P52, iliyoandikwa kwa Kigiriki mwaka 125 hivi, inahesabika kuwa andiko la zamani zaidi kutufikia kuhusu Yesu. Ina sehemu za Injili ya Yohane; mbele 18:31-33, nyuma 18;37-38.

Injili ni neno la Kiarabu lenye asili ya Kigiriki εὐαγγέλιον, evangelion, linalotafsiriwa Habari Njema, yaani habari ya Yesu Kristo kufa na kufufuka.

Jina hilo linatumika pia kuhusu vitabu vinavyoeleza maisha na mafundisho ya Yesu kufuatana na kile cha Mtakatifu Marko ambacho kwa wataalamu wengi ndiyo Injili iliyowahi kuandikwa (65-70 B.K.)

Kati ya vitabu vyote vya namna hiyo, Ukristo tangu karne ya 2 umekubali vile vinne vya kwanza tu, ambavyo viliandikwa wakati wa Mitume wa Yesu kuwepo duniani.

Hivyo vinashika nafasi ya kwanza katika orodha ya vitabu vya Agano Jipya kama ifuatavyo: Injili ya Mathayo, Injili ya Marko, Injili ya Luka na Injili ya Yohane.

Injili tatu za kwanza zinafanana kwa kiasi kikubwa katika mpangilio, habari na maneno yenyewe; kwa sababu hiyo zinaitwa Injili Ndugu. Kadiri ya wataalamu wengi mfanano unatokana na kwamba Injili ya Marko ilitumiwa na waandishi wa zile nyingine.

Ile ya Mtume Yohane ni ya pekee na inategemea ushahidi wa Mtume huyo ambaye alipendwa zaidi na Yesu akamfuata kiaminifu hadi msalabani.

Vinahesabiwa na Wakristo kuwa moyo wa Maandiko Matakatifu yote (Biblia) yanayotunza ufunuo wa Mungu, kwa kuwa ndivyo shuhuda kuu juu ya Neno aliyefanyika mwili.

Vile vingi vilivyoandikwa kuanzia karne 2 havitumiwi na Kanisa katika kufundisha imani na katika liturujia. Vinaitwa kwa kawaida apokrifa yaani "bandia".

Waislamu wanakiri Injili kuwa iliteremshwa toka mbinguni kwa nabii Isa, lakini hawakubali vitabu 4 vya Wakristo kama vilivyo.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Injili kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.