Ufunuo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Ufunuo ndio tukio au mchakato ambao mawasiliano kati ya Mungu na binadamu yanafanyika. Ufunuo ni pia yaliyomo katika ujumbe unaotokana na Mungu.

Ni kwamba katika dini mbalimbali kuna imani ya kwamba Mungu anaweza kujifunua kwa binadamu na kuwafunulia matakwa yake kwao.

Pengine ufunuo huo unakuja kuandikwa katika kitabu kitakatifu, kama vile Biblia kwa Wayahudi na Wakristo, na Kurani kwa Waislamu.

Ufunuo una umuhimu mdogo katika dini nyingine, isipokuwa katika Ubuddha.

Mpokeaji[hariri | hariri chanzo]

Nabii ndiye jina la mtu anayepokea ufunuo huo ili kuwajulisha wengine.

Namna za kutolewa[hariri | hariri chanzo]

Namna za ufunuo kufanyika zinaweza kuwa mbalimbali, kama vile:

Kutokana na asili yake isiyo ya kimaumbile, ufunuo hauwezi kuchunguzwa na mbinu za sayansi. Hata hivyo ni muhimu kupambanua ufunuo wa kweli na ule bandia ambao mtu anaweza kudanganyika au kudanganya.

Mada[hariri | hariri chanzo]

Ufunuo unaweza kuhusu:

  • matukio yajayo (k.mf. mwisho wa dunia);
  • mambo ya mbinguni kuhusu Mungu, malaika n.k.;
  • ufafanuzi wa matukio ya wakati uleule.

Uyahudi[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya dini ya Kiyahudi, Mungu alijifunua mara nyingi katika historia ya taifa lao kama Historia ya Wokovu, kuanzia mababu wao, lakini hasa kumpitia Musa, asili ya Torati (vitabu vitano vya kwanza vya Biblia ya Kiebrania).

Baada yake walitokea manabii wengi waliokubalika kuwa wa kweli na ambao vitabu vyao vilipokewa na wengi kama vitakatifu.

Tanakh ilikamilika kwa vitabu vingine vilivyoongezwa kabla ya Yesu Kristo.

Wayahudi wanaendelea kumsubiri Masiya atakayekamilisha ufunuo wao.

Ukristo[hariri | hariri chanzo]

Wakristo wanapokea ufunuo wa Mungu kwa taifa la Israeli, wakiona ujio wa Yesu kuwa ndio kilele chake, ambapo Mungu alijifunua si kwa njia ya manabii, bali kwa njia ya Mwana wake, aliye Neno wa milele. Katika yeye ufunuo umekamilika usiweze kuboreshwa tena. Ufunuo huo unajitokeza hasa katika Agano Jipya.

Katika teolojia ya Kikristo neno ufunuo lina maana ya jumla ya dogma zote, yaani kweli zilizofunuliwa na zinazodai imani ya kila mtu ili kupata wokovu.

Kwa Kanisa Katoliki kweli hizo zinapatikana katika Biblia pamoja na Mapokeo ya Mitume vinavyofafanuliwa na Ualimu wa kanisa.

Kanisa Katoliki linatofautisha pia huo ufunuo wa hadhara na mafunuo ya binafsi ambao si lazima watu wengine wayasadiki.

Uislamu[hariri | hariri chanzo]

Uislamu pia unakubali ufunuo wa Mungu kwa Wayahudi kupitia manabii, Isa (Yesu) akiwa mmojawao, lakini unaamini ufunuo huo umekamilishwa kupitia Muhammad, nabii wa mwisho na mkuu kuliko wote, na umeandikwa katika Kurani, inayohesabiwa "neno la Mungu" kwa maana kamili, kwa kuwa limetoka kwake na kuandikwa bila mabadiliko.