Nenda kwa yaliyomo

Torati

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Gombo la Torati kwa Kiebrania katika sinagogi la Cologne (Ujerumani).
Torati ikisomwa sinagogini.

Torati (kwa Kiebrania: תורה, Torah), maana yake ni fundisho, mwongozo au sheria. Kwa jina hilo vinatajwa kwa pamoja vitabu vitano vya kwanza vya Tanakh, vinavyojulikana pia kwa jina lenye asili ya Kigiriki la Pentateuko (pente maana yake tano, teukhos maana yake kitabu).

Vitabu vitano vya Torati

Vitabu vya Torah ni (majina ya vitabu kwa Kiebrania yanatokana na maneno yake ya kwanza):

Torati si mkusanyo wa mpango wa sheria, bali hasa msingi wa kiteolojia wa imani ya Israeli ("Mungu mmoja, taifa moja, nchi moja") ambamo zinapatikana sheria nyingi pia pamoja na historia ya taifa la Mungu. Sheria zinaweza zikafanana na zile za makabila ya jirani, lakini zina mambo ya pekee yanayotokana hasa na imani ya kuwa Mungu ni mmoja tu.

Matumizi ya Torati

Kusoma Torah ni wajibu muhimu mmojawapo wa kila Myahudi. Ni desturi kusoma Torati nzima kwa mwaka mmoja katika ibada za sinagogi. Kwa kusudi hilo imegawiwa katika sehemu 54 (parashoth, wingi wa parasha, yaani "sehemu"), kama zilivyo siku za Sabato katika miaka mirefu (yenye miezi 13). Wakati somo la sehemu zote limekamilika, kuna sherehe ya Simhat Torah katika sinagogi ambapo wote wanacheza pamoja na magombo ya Torati.

Kwa matumizi katika ibada Torati huandikwa kwa mkono kwenye ngozi ambayo ni sharti itokane na mnyama ambaye ni kosher kwa mtazamo wa Kiyahudi. Mwandishi haruhusiwi kufanya kosa lolote akinakili matini. Gombo la Torati linaandikwa kwa herufi 304,805[1]. Ngozi hiyo inaandaliwa kwa kushona kurasa zake 62 hadi 84 pamoja kama mlia mrefu ambako maneno huandikwa kwa nguzo; urefu wake ni kati ya mita 30 na 50 kutegemeana na namna ya kuandika. Mlia huo hufungwa na fimbo la ubao kila upande na hivyo unaweza kuviringishwa. Wakati wa kusoma gombo linafunguliwa hadi ukurasa unaotafutwa na msomaji anageuza bao akimaliza ukurasa mmoja. Wakati wa kusomwa ukurasa hauguswi kwa mkono. Kuna vifaa vya kudokeza sehemu inayosomwa.

Torati hutunzwa katika kabati au chumba cha pekee ndani ya sinagogi kinachoitwa "sanduku takatifu".

Mtazamo wa Wayahudi kuhusu Torah

Kwa jina hilohilo Wayahudi wanamaanisha pia sheria ya dini yao kwa jumla, wakitofautisha Torah shebiktav (sheria iliyoandikwa yaani vitabu hivyo vitano) na Torah shebehalpeh kwa mapokeo yote yaliyokubalika baadaye.

Torah ni msingi muhimu zaidi wa dini ya Kiyahudi na ya maadili yake yanatotegemea utekelezaji wa maagizo (mitzvot) 613.

Kadiri ya mapokeo yao vitabu hivyo vilitolewa na Mwenyezi Mungu kwa Musa kwenye Mlima Sinai. Kwa hiyo hata herufi au ishara yake ndogo imewekwa na Mungu kama fundisho.

Wataalamu kuanzia mwisho wa karne ya 19 wameonyesha kuwa maandiko hayo yametokana na mapokeo mbalimbali, hasa manne yanaoitwa J, E, D na P, yaliyokuja kuunganishwa na hatimaye kupitishwa moja kwa moja katika karne ya 5 KK.

Mtazamo wa Wakristo kuhusu Torati

Wakristo walipokea Torati kutoka kwa Wayahudi, kwa kuzingatia hasa maneno ya Yesu: "Msidhani kwamba nimekuja tangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua bali kukamilisha" (Math 5:17). Hivyo Wakristo hawakubali kutekeleza maagizo yote ya Torati yanavyofundishwa na Wayahudi, bali yalivyokamilishwa na Yesu.

Sura hiyo ya Mathayo inatoa mifano 6 kuhusu tafsiri yake ya maneno juu ya upendo kwa jirani. Ni kama ifuatavyo:

17 "Msidhani ya kuwa nimekuja kutangua Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha.

18 Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya Sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.

19 Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika Ufalme wa mbiguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika Ufalme wa mbinguni.

20 Ndiyo maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa Mafarisayo na walimu wa Sheria, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni.

21 "Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.`

22 Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: `Pumbavu` atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.

23 Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe,

24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi ukatoe sadaka yako.

25 "Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani, kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani.

26 Kweli nakwambia, hutatoka humo mpaka umemaliza kulipa senti ya mwisho.

27 "Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: `Usizini!`

28 Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.

29 Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, ling`oe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu.

30 Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali zaidi kupoteza kiungo kimoja cha mwili, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.

31 "Ilikwisha semwa pia: `Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka.`

32 Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mtu akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.

33 "Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.`

34 Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu;

35 wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu.

36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37 Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.

38 "Mmesikia kwamba ilisemwa: `Jicho kwa jicho, jino kwa jino.`

39 Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili.

40 Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako.

41 Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili.

42 Akuombaye mpe, na mtu akitaka kukukopa kitu usimnyime.

43 "Mmesikia kwamba ilisemwa: `Mpende jirani yako na kumchukia adui yako.`

44 Lakini mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi

45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu.

46 Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda ninyi? Hakuna! Kwa maana hata watoza ushuru hufanya hivyo!

47 Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo.

48 Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Tena, mtaguso wa Mitume uliofanyika Yerusalemu mwaka 49 hivi uliamua watu wa mataifa wanaojiunga na Kanisa wasidaiwe kufuata vipengele vyote vya Torati (Mdo 15).

Mtazamo wa Waislamu kuhusu Torati

Kurani inazungumzia sana yaliyomo katika Torati na isisitiza sana baadhi ya sheria zake. Kuikubali ni kati ya misingi ya imani ya Uislamu. Waislamu huamini kwamba Torati ilikuwa kitabu kilishoshushwa kutoka mbinguni kwa ajili ya Musa jinsi inavyoandikwa katika Kurani 3:4[2]. Wasilamu wengu huamini kwamba Torati imebadilishwa au kuchafuliwa hivyo wanadai Wayahudi hawana tena Torati sahihi ya kiasili.[3]

Tanbihi

  1. How is the Torah made?, tovuti ya chabad.org, iliangaliwa Septemba 2022
  2. (Mungu) "aliteremsha Taurati na Injili kabla (ya hiki) kuwa mwongozo kwa watu"; tafsiri ya Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy
  3. Ahmed Deedat: Is the Bible God's Word?, "The Taurat we Muslims believe in is not the "Torah" of the Jews and the Christians though the words - one Arabic, the other Hebrew - are the same. We believe that whatever the Holy Prophet Moses (Peace be upon him) preached to his people, was the revelation from God Almighty, but that Moses was not the author of those "books" attributed to him by the Jews and the Christians."

Marejeo

Bandstra, Barry L (2004). Reading the Old Testament: an introduction to the Hebrew Bible. Wadsworth. ISBN 9780495391050.
Birnbaum, Philip (1979). Encyclopedia of Jewish Concepts. Wadsworth.
Blenkinsopp, Joseph (2004). Treasures old and new: essays in the theology of the Pentateuch. Eerdmans. ISBN 9780802826794.
Campbell, Antony F; O'Brien, Mark A (1993). Sources of the Pentateuch: texts, introductions, annotations. Fortress Press. ISBN 9781451413670.
Carr, David M (1996). Reading the fractures of Genesis. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664220716.
Clines, David A (1997). The theme of the Pentateuch. Sheffield Academic Press. ISBN 9780567431967.
Davies, G.I (1998). "Introduction to the Pentateuch". Katika John Barton (mhr.). Oxford Bible Commentary. Oxford University Press. ISBN 9780198755005.
Friedman, Richard Elliot (2001). Commentary on the Torah With a New English Translation. Harper Collins Publishers.
Gooder, Paula (2000). The Pentateuch: a story of beginnings. T&T Clark. ISBN 9780567084187.
Kugler, Robert; Hartin, Patrick (2009). The Old Testament between theology and history: a critical survey. Eerdmans. ISBN 9780802846365.
Levin, Christoph L (2005). The Old testament: a brief introduction. Princeton University Press. ISBN 9780691113944.
McEntire, Mark (2008). Struggling with God: An Introduction to the Pentateuch. Mercer University Press. ISBN 9780881461015.
Ska, Jean-Louis (2006). Introduction to reading the Pentateuch. Eisenbrauns. ISBN 9781575061221.
Van Seters, John (1998). "The Pentateuch". Katika Steven L. McKenzie, Matt Patrick Graham (mhr.). The Hebrew Bible today: an introduction to critical issues. Westminster John Knox Press. ISBN 9780664256524.
Van Seters, John (2004). The Pentateuch: a social-science commentary. Continuum International Publishing Group. ISBN 9780567080882.
Walsh, Jerome T (2001). Style and structure in Biblical Hebrew narrative. Liturgical Press. ISBN 9780814658970.

Marejeo mengine

Friedman, Richard Elliott, Who Wrote the Bible?, HarperSanFrancisco, 1997
Welhausen, Julius, Prolegomena to the History of Israel, Scholars Press, 1994 (reprint of 1885)
Kantor, Mattis, The Jewish time line encyclopedia: A year-by-year history from Creation to the present, Jason Aronson Inc., London, 1992
Wheeler, Brannon M., Moses in the Quran and Islamic Exegesis, Routledge, 2002
DeSilva, David Arthur, An Introduction to the New Testament: Contexts, Methods & Ministry, InterVarsity Press, 2004
Alcalay, Reuben., The Complete Hebrew – English dictionary, vol 2, Hemed Books, New York, 1996 ISBN 978-965-448-179-3
Scherman, Nosson, (ed.), Tanakh, Vol. I, The Torah, (Stone edition), Mesorah Publications, Ltd., New York, 2001
Heschel, Abraham Joshua, Tucker, Gordon & Levin, Leonard, Heavenly Torah: As Refracted Through the Generations, London, Continuum International Publishing Group, 2005
Hubbard, David "The Literary Sources of the Kebra Nagast" Ph.D. dissertation St Andrews University, Scotland, 1956

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu: