Upendo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Giotto, Upendo, Padua, Italia.
Maadili ya Kimungu

Wamisionari wa Upendo, shirika la kitawa la Kanisa Katoliki lililoanzishwa na Mama Teresa huko Kolkata, India, ili kusaidia watu walio fukara zaidi.

Upendo ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali kuanzia hali ya nafsi ya binadamu hadi kwa Mungu. Linatokana na kitenzi "kupenda" na kufanana na pendo, mapendo, mapenzi, n.k.

Hapa linatumika kwa maana ya juu zaidi kulingana na Kigiriki "agape" na Kilatini "caritas".

Katika Ukristo[hariri | hariri chanzo]

Kufuatana na Maandiko Matakatifu, hasa ya Mtume Paulo, katika teolojia ya Ukristo ni mojawapo kati ya maadili ya Kimungu, pamoja na imani na tumaini.

Kadiri ya dini hiyo, inatupasa tumpende Mungu pekee, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, kadiri tunavyoweza, kwa kuwa ndiye asili ya uhai wetu na ya wema wote. “Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote” (Kumb 6:4). “Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu” (Mk 10:18).

Halafu tupende viumbe vya Mungu pia kadiri anavyotaka tuwapende kwa kuwa mwenyewe anawapenda. “Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba” (Hek 11:24). “Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana... Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu’, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye: ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake” (1Yoh 4:11,20-21)[1].

Kielelezo cha upendo ni Yesu Kristo, aliyefikia hatua ya kujitoa kafara kwa ajili yetu na kutuombea sisi wakosefu tuliomtesa. “Ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Rom 5:7-8). “Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:15). “Muenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yenu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato” (Ef 5:2). “Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” (1Yoh 3:16).

Lakini tusimfuate Yesu kama kielelezo tu, bali tuishi ndani yake na kwa ajili yake, kwa kuwa ndiye uhai wetu. “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika nabyi, msipokaa ndani yangu” (Yoh 15:4). “Alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao” (2Kor 5:15). “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu” (Kol 3:3-4).

Kadiri ya madhehebu kadhaa, tunaweza kufuata mfano wa watu wengine kadiri walivyomfuata Yesu. Ndio wale tunaowaita watakatifu, kwa kuwa Kanisa limewaweka mbele yetu kama kielelezo wazi cha upendo kamili. “Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate” (2Thes 3:9). “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo” (1Kor 11:1). “Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi... Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo” (Fil 3:17; 4:9).

Upendo wa Mungu si hisia ya moyo, inayoweza kubadilikabadilika, bali ni msimamo wa dhati unaojitokeza katika matendo. “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yoh 3:17-18).

Basi, huo upendo ambao tumpende Mungu na viumbe vyake si pendo la kibinadamu tu, bali ni uleule ambao mwenyewe anajipenda, anatupenda na kutushirikisha, yaani ni Roho Mtakatifu. “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). “Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu... Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake... Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza” (1Yoh 4:7,16,19).

Tunaweza kuwa na kiasi chochote cha upendo huo wa Kimungu, lakini tuwe daima tayari kuupokea upya na kuutekeleza uzidi kustawi bila mwisho. “Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote” (1Thes 3:12). “Pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” (Fil 1:9).

Upendo unatakiwa kustawi zaidi na zaidi bila mwisho, kwa kuwa ndio mfumo wake. Upendo wa kweli haufuati kipimo: kiasi cha kupenda ni kupenda bila kiasi. “Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6:36). “Kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo” (Yoh 13:1).

Upendo utakamilika mbinguni, ambapo tutamuona Mungu alivyo na kuvutiwa naye tusiweze kubandukana naye milele. “Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika... Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1Kor 13:8,12). “Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yoh 17:3).

Hivyo Ukristo unatuelekeza kuona maisha haya kama safari ya kulenga upendo kamili, ambapo Roho Mtakatifu anatunasukuma tusonge mbele kwa hatua za upendo mkubwa zaidi na zaidi. “Nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu, katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo” (Fil 3:13-16).

Utekelezaji wa upendo unadai uendane na maadili mengine yote, la sivyo si wenyewe; sanasana ni pendo la kibinadamu tu lisilopatana na Mungu. “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote” (1Kor 13:4-7). “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu” (Math 6:2).

Maadili mengine yasipoendana na upendo, huwa yamekufa, kwa kuwa upendo ndio uhai wa hayo yote. “Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, ‘Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba’, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake” (Yak 2:14-17). “Nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu” (1Kor 13:3).

Maadili yanayoendana na upendo ni hasa imani na tumaini. “Hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu” (1Thes 1:3). “Sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu” (1Thes 5:8). “Sikuzote tukiwaombea, tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote, kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni” (Kol 1:3-5). “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo” (1Kor 13:13).

Hayo matatu yanaitwa maadili ya Kimungu kwa kuwa asili na lengo lake ni Mungu mwenyewe. Hatuwezi kujipatia hayo, bali tunamiminiwa naye kwa pamoja tuweze kumsadiki, kumtumaini na kumpenda inavyotupasa tuwe marafiki wake. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). “Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana” (1Thes 4:9).

Pamoja na imani na tumaini, upendo unadai maadili ya kiutu, ambayo yote yanategemea manne ya msingi: busara, haki, nguvu na kiasi. “Huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha” (Hek 8:7).

Ustawi wa upendo kadiri ya Kanisa Katoliki[hariri | hariri chanzo]

Kwa imani ya Kanisa Katoliki, hakuna wokovu bila upendo[2]. Adili hilo la Kimungu, lililo kuu kuliko yote[3] na linalotakiwa kuyaongoza na kuyahuisha mengine pia, halitakiwi kubaki lilivyo, bali kukua ndani mwetu hadi siku ya kufa.

Fundisho hilo linaweza, tena linapaswa kuangaza maisha ya Kiroho, kwa sababu ni msingi wa himizo lolote la kusonga mbele kwa unyenyekevu na moyo mkuu, kwa kutamani muungano wa dhati na Mungu, kwa kujitahidi kuupata pamoja na kuuomba. Basi, tuone kwanza kwa nini upendo unatakiwa kustawi daima, halafu jinsi unavyostawi.

Kwa nini upendo unatakiwa kustawi hadi kufa[hariri | hariri chanzo]

Hata katika kiwango kidogo upendo halisi (ambao tuliupokea kwa ubatizo na kurudishiwa pengine kwa upatanisho) unampenda tayari Mungu Mwokozi kuliko yote, na kwa ajili yake unampenda jirani kama mtu mwenyewe anavyojipenda. Kiwango hicho cha upendo uliomiminwa rohoni kinapita bila kifani pendo la kimaumbile tunaloweza kuwa nalo kwa Muumba na kwa watu; hakimbagui yeyote, kwa kuwa ubaguzi huo ungekuwa dhambi ya mauti inayofuta upendo. Lakini upendo huo wa wanaoanza uko mbali na ushindi dhidi ya umimi wowote. Unaendana bado na kujipendea ambako kunasababisha si dhambi ya mauti, bali dhambi nyepesi nyingi na hivyo kunazuia upendo usiweze kutenda na kupamba vizuri.

Ni wazi kuwa upendo huo unatakiwa kustawi: “Hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” (Fil 1:9). “Bwana awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu” (1Thes 3:12-13). “Mwenye haki na azidi kufanya haki, na mtakatifu azidi kutakaswa” (Ufu 22:11). “Njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu” (Mith 4:18). Hapa duniani Mkristo ni msafiri anayemuelekea Mungu na kumkaribia kwa vitendo vya upendo kamili zaidi na zaidi, kwa “hatua za upendo” (Gregori Mkuu). Upendo wake unaweza na kupaswa kustawi mfululizo, la sivyo badala ya kusafiri atasimama kabla hajafika. Lengo la njia ni kutembea, si kulala.

Kila mtu anayeelekea uzima wa milele anatakiwa kukua katika upendo ili azidi kumkaribia Mungu: si tu wanaoanza na wanaoendelea, bali hata waliokamilika. Tena hao wa mwisho wanapaswa kwenda kasi zaidi kadiri wanavyomkaribia na kuvutwa naye. Nguvu ya maisha yao ya Kiroho inaongezeka zaidi na zaidi, elekeo la roho yao linainuka zaidi na zaidi; kwao hakuna machweo: mwili tu unadhoofika kwa uzee.

Bwana alisema, “Mimi nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu” (Yoh 12:32). “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka” (Yoh 6:44). Mungu ndiye anayetufanya twende, anakotuvutia ni kwake: ndiye mwanzo na mwisho wa yote, ndiye wema mkuu unaovuta upendo kwa nguvu kadiri tunavyomkaribia. Ndiyo sababu katika maisha ya watakatifu, ustawi wa upendo miaka yao ya mwisho ni mkubwa sana; ingawa wanalemewa na uzee na udhaifu upande wa hisi (k.mf. kumbukumbu) wanang’amua ukweli wa maneno, “Ujana wako unarejezwa kama tai” (Zab 103:5). Maendeleo hayo ya kasi zaidi na zaidi yalikuwepo hasa katika bikira Maria, kwa kuwa ndani mwake hayakuzuiwa na chochote, tena yalikuwa ya haraka kadiri ilivyokuwa kubwa neema ya kwanza aliyojaliwa. Basi, upendo hautakiwi tu kustawi hadi kufa, bali kustawi zaidi na zaidi, kama vile kasi ya kitu kinachoanguka inavyozidi hadi kikafika ardhini.

Ikiwa ni hivyo, upendo unastawi vipi ndani mwetu? Kwa kuwa hata katika kiwango cha chini unampenda tayari Mungu na majirani wote, hauwezi kuenea zaidi: lakini unaweza kuongezewa nguvu na kutia mizizi ndani ya utashi wetu zaidi na zaidi. Upendo hauongezeki kwa wingi kama nafaka, bali unakua kwa ubora, kwa kuongezewa nguvu katika utashi, ukizidi kuuelekezea mema yapitayo maumbile na kuuepusha na maovu. Mfano wake ni elimu ya msomi ambayo haipati daima taarifa mpya, ila inazidi kuzichimba na kuwa na hakika nazo; vivyo hivyo upendo unastawi ndani mwetu, ukitufanya tuwapende kwa namna kamili na safi zaidi na zaidi Mungu kwa ajili yake mwenyewe na jirani kwa ajili ya Mungu. Tukielewa hayo, tutaona haja ya kutakaswa kila uchafu ili kudhihirisha jinsi maadili makuu yanavyolenga ukweli na wema wa Mungu. Basi, upendo kama joto, unastawi kwa ubora, kwa kupata nguvu zaidi na zaidi; na hiyo inafanyika kwa namna tatu: kwa stahili, kwa sala na kwa sakramenti.

Ustawi wa upendo kwa njia ya stahili zetu[hariri | hariri chanzo]

Tendo linalotokana na upendo (au adili lolote linalohuishwa nao) linastahili tuzo lipitalo maumbile, hasa ustawi wa upendo wenyewe. Stahili hazisababishi ustawi huo, kwa kuwa upendo si adili la kujipatia, bali la kumiminiwa. Mungu tu anaweza kuutia ndani mwetu (kwa sababu ni kushiriki uzima wake wa ndani), naye tu anaweza kuustawisha: “Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye… ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu” (1Kor 3:6-9). Yeye “atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu” (2Kor 9:10). Ingawa matendo ya upendo hayawezi kusababisha ustawi wa adili hilo, yanauchangia kwa namna mbili, yaani kwa kuustahili na kwa kutuandaa tuupokee.

Stahili ni haki ya kupata tuzo; hailisababishi ila inalipata. Mwadilifu akitenda mema yapitayo maumbile anastahili upendo wake ustawi. Bwana kabla hajampa tuzo la mbinguni anampa lile la kukua katika upendo wake. Wazushi walioitwa Watulivu walidharau tuzo wakijidai eti! Hawajitafutii faida. Kumbe kadiri mtu alivyo na upendo, anatamani tuzo hilo: kumpenda Mungu kwa nguvu na usafi mkubwa zaidi na zaidi, jambo lisilotenganika na ustawi wa maadili mengine ya kumiminiwa na wa vipaji vya Roho Mtakatifu.

Matendo ya upendo (na ya maadili yanayohuishwa nao) hayastahili tu ustawi huo, bali pia yanaandaa kuupokea, kama kwa kufungua na kupanua akili na utashi ili uzima wa Mungu uweze kuvipenya zaidi, na kwa kuvitakasa uviinue juu zaidi. Hiyo ni kweli hasa kwa matendo motomoto ya upendo. Tendo moja la namna hiyo linaathiri pengine maisha yote ya baadaye na kustahili ustawi mkubwa wa upendo, likituandaa kuupokea. Ni kama kuinuliwa hadi ghorofa ya juu, tunapopewa mtazamo mpya wa mambo ya Mungu na kuvutiwa nayo zaidi. Tunaongezewa talanta, yaani Roho Mtakatifu anakuwemo ndani mwetu kwa namna mpya inayotenda zaidi.

Kwa kawaida yeye anamsukuma mtu kulingana na kiwango cha maadili na vipaji alichonacho au kulingana na usikivu wake. Kama angemsukuma atende kwa upungufu, angekuwa amempa bure kiwango kikubwa cha maadili na vipaji. Basi, mwadilifu asipozuia kazi ya Mungu, atapokea neema kubwa zaidi na zaidi apande mbio kwake.

Wanateolojia kadhaa wamefundisha kuwa Mungu anatukuzwa na tendo moja la upendo la talanta kumi kuliko anavyotukuzwa na vitendo kumi vya upendo vya talanta mojamoja; vilevile mwadilifu kamili mmoja anampendeza kuliko wengine wengi wanaobaki katika wastani. Ubora ni muhimu kuliko wingi. Ndiyo sababu ukamilifu wa Maria unapita ule wa watakatifu wote, kama vile almasi moja ilivyo na thamani kuliko vito vingine vingi.

Basi, upendo unatakiwa kustawi kwa njia ya stahili zetu hadi siku ya kufa. Pamoja nao utakua pia utayari wetu wa kupokea ongezeko lingine. Moyo unapanuka zaidi na zaidi na ujazo wake wa Kimungu unaongezeka: “mioyo yetu imekunjuliwa… Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa… nanyi pia mkunjuliwe mioyo” (2Kor 6:11,13).

Mara nyingi tunasahau tuko safarini kuelekea uzima wa milele, na tunajaribu kustarehe katika maisha haya kana kwamba yangedumu moja kwa moja. Mfano wake ni maabiria wa treni bora ambamo wanakula na kulala kama hotelini hata wakasahau wako safarini; pengine wakiangalia dirishani wanaona mandhari ikibadilika haraka na baadhi ya wenzao wakiteremka: hapo wanajisemea kuwa wao pia watawahi kufikia mwisho wa safari. Shida ni kwamba, ingawa tunaona wengi kufa, hatupati hakika ya ndani kuwa siku fulani itakuwa zamu yetu.

Basi, tunatakiwa kuishi kwa kukazia macho mwisho wa safari, kusudi tusipoteze tena muda tuliojaliwa, bali tuujaze iwezekanavyo matendo ya kustahili uzima wa milele.

Ustawi wa upendo kwa njia ya sala[hariri | hariri chanzo]

Ustawi wa upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji) unapatikana si kwa njia ya stahili tu, bali kwa sala pia, kama Kanisa linavyoomba, “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani, tumaini na upendo” (Jumapili ya 30 ya mwaka).

Tukumbuke tofauti iliyopo kati ya kuomba na kustahili: asiye na neema inayotia utakatifu hawezi kustahili (kwa kuwa neema hiyo ndiyo asili ya stahili yoyote ipitayo maumbile); lakini kwa neema ya msaada anaweza kujiombea (k.mf. neema ya uongofu) na akiomba kwa unyenyekevu, imani na udumifu, atapata. Stahili inahusu haki ya Mungu; kumbe sala inaelekea huruma ya Mungu ambayo mara nyingi inanyanyua walioanguka na kusikiliza ombi lao lisilostahili chochote. Mtu duni kuliko wote, aliyetumbukia vilindi asimoweza kustahili tena, anaweza kulilia huruma ya Mungu: “Kilindi chapigia kelele kilindi” (Zab 42:7), yaani kilindi cha unyonge kinalilia kile cha huruma. Mkosefu akisihi kwa moyo wote anasikilizwa, roho yake inainuliwa, na Mungu anatukuzwa. Nguvu ya sala haitegemei tu neema inayotia utakatifu iliyo ya lazima ili kustahili.

Tukishaongoka, tunaweza kustawishiwa uzima wa neema kwa stahili na kwa sala pia. Hiyo ikiwa na unyenyekevu, imani na udumifu, inatupatia ustawi wa maadili ya Kimungu tunaoomba katika maombi matatu ya kwanza ya Baba Yetu. Sala ya mwadilifu, anayependa kutafakari polepole na kujilisha kwa undani maombi hayo (hata kusimama pengine nusu saa kuzamia mojawapo kwa upendo), inastahili pamoja na kuomba neema: inampa haki ya kustawishiwa upendo ulioisababisha, na kwa nguvu ya ombi inapata kuliko inavyostahili. Tena, ikiwa motomoto kweli, inapata mara. Hapo tunaweza kuona matunda ya sala na jinsi inavyomvuta Mungu ajitoe kwetu kwa dhati, nasi tujitoe kwake. Hapo moyo unazidi kutanuka upokee neema kwa wingi zaidi; roho inajitenga na malimwengu na kumtamani zaidi Mungu, ambaye ndani yake inakuta yale yote yanayostahili kupendwa, tena kwa ngazi ya juu. Hakutatosha kamwe kuyaishi hayo katika sala ya moyo, k.mf. katika kimya kikubwa cha usiku, ambapo mtu yuko peke yake na Muumba na Mwokozi wake. Hapo anang’amua kuwa Mungu ni mwema kupita kiasi, na sala ni mwanzo wa uzima wa milele.

Kwa kusali mwadilifu anaweza kupata neema kadhaa asizoweza kustahili, hasa ile ya kudumu mpaka mwisho. Hawezi kustahili zawadi hiyo kwa sababu ni kudumu kwa hali ya neema iliyo chanzo kisichostahilika cha stahili. Lakini kifo chema kinapatikana kwa sala nyenyekevu, yenye imani, ya kila siku. Kanisa linatualika kukariri kwa bidii, “Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina”. Vivyo hivyo tunaweza kumuomba Mungu neema ya kumjua kwa ndani zaidi na zaidi, yaani ya kuzama katika sala, ambayo matokeo yake ni kuungana naye kwa namna imara na yenye matunda mengi zaidi: “Neno moja nimelitaka kwa Bwana, nalo ndilo nitakalolitafuta: nikae nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa Bwana na kutafakari hekaluni mwake” (Zab 27:4), yaani nione kila siku vizuri zaidi jinsi wema wake usivyo na mipaka kwa wale ambao wanamtafuta na kumpata.

Ustawi wa upendo kwa njia ya sakramenti[hariri | hariri chanzo]

Hatimaye upendo (pamoja na maadili mengine na vipaji) unastawi ndani mwetu kwa njia ya sakramenti, hasa ekaristi. Stahili na sala za mwadilifu zinapata zawadi za Mungu kulingana na imani na upendo alivyonavyo; kumbe sakramenti zinaleta neema kwa nguvu zake zenyewe katika wale wasioweka kizuio. Kwa kuwa ziliwekwa ili kutugawia stahili za Mwokozi, zenyewe zinasababisha neema bila kutegemea sala na stahili za yule anayeziadhimisha wala za yule anayezipokea. Padri mwovu, na hata mtu asiye Mkristo, anaweza kubatiza mradi awe na nia ya kufanya Kanisa linavyofanya.

Hata hivyo sakramenti zinaleta neema kwa kiasi tofauti kulingana na juhudi za yule anayezipokea. “Kila mmoja anapokea uadilifu kadiri Roho Mtakatifu anavyomtakia kulingana na utayari wake” (Mtaguso wa Trento). Moto unawaka wenyewe, lakini sisi tunafaidi joto lake kadiri tunavyoukaribia. Vivyo hivyo tunafaidika na sakramenti kadiri imani yetu ilivyo hai na utashi wetu ulivyo motomoto. Kwa msingi huo Mkristo anapoondolewa dhambi anapata neema kadiri ya majuto yake. “Nguvu ya majuto ya mwenye kuungama ni kubwa, sawa au pungufu kuliko kiwango cha neema alichokipoteza; hapo anapata tena neema kwa kiwango kikubwa, sawa au pungufu kuliko awali” (Mt. Thoma wa Akwino). Kwa mfano, aliyekuwa na talanta tano kabla hajazipoteza kwa dhambi ya mauti, akiwa na majuto kama ya talanta mbili, anapata tena neema, lakini kwa kiasi kidogo kuliko awali. Kinyume chake, kwa majuto makubwa anaweza kuipata kwa kiwango kikubwa zaidi. Hilo ni muhimu kwa wale wanaoanguka wakati wa kupanda mlima; wanaweza kuinuka kwa bidii na kuendelea na safari yao kuanzia pale walipoanguka. Lakini wakiinuka kwa kuchelewa na bila bidii wanajikuta chini, badala ya kuendelea tu kupanda.

Kwa msingi huohuo komunyo moja yenye bidii inafaa kuliko nyingi vuguvugu. Kadiri tunavyomkaribia Yesu ekaristi kwa imani hai, tumaini imara na upendo motomoto tunafaidi neema za mwanga, upendo na ushujaa za kututosha hata tukashirikisha wengine. Kinyume chake, tunda la komunyo ni dogo tukikaribia meza takatifu kwa namna ambayo inatosha tu tusikufuru. Hayo yatufikirishe tuking’amua kuwa hatuendelei kweli baada ya kukomunika kila siku kwa miaka kadhaa (ingawa ni kweli pia kwamba mtu akiendelea, anazidi kufahamu unyonge wake kadiri anavyokuja kujua ukuu wa Mungu). Tuwe na bidii za kutosha itutokee kama kwa watakatifu: kwamba kila komunyo iwe na upendo mkubwa na matunda mengi kuliko ile iliyotangulia. Kumbe mara nyingi uzembe na uvuguvugu vinazuia ustawi huo: kwa kuambatana na dhambi nyepesi fulani, tunda la komunyo linazidi kupungua, kama kasi ya jiwe lililorushwa hewani wima ambayo inazidi kupungua mpaka jiwe likaanguka tena ardhini.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]