Ukristo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Sanamu ya Kristo mkombozi huko Rio de Janeiro (Brazil) ni sanamu ya Yesu kubwa kuliko zote zilizopata kutengenezwa.


Ukristo (kutoka neno la Kigiriki Χριστός, Khristos, ambalo linatafsiri lile la Kiebrania מָשִׁיחַ, Māšîăḥ, linalomaanisha "Mpakwamafuta" [1] ni dini inayomwamini Mungu pekee[2] kama alivyofunuliwa na Yesu Kristo, mwanzilishi wake, katika karne ya 1.

Dini hiyo, iliyotokana na ile ya Wayahudi, inalenga kuenea kwa binadamu wote, na kwa sasa ni kuu kuliko zote duniani, ikiwa na wafuasi 2,200,000,000 (33.39% kati ya watu 7.174 bilioni).[3]

Kitabu chake kitakatifu kinajulikana kama Biblia. Ndani yake inategemea hasa Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.

Kati ya madhehebu mengi sana ya Ukristo, karibu yote yanamkiri kuwa kwa pamoja Mungu kweli na mtu kweli: katika umoja na nafsi yake ya Kimungu zinapatikana sasa hali zote mbili.

Yote yanamkiri kuwa Mwokozi wa watu wote, na kuwa ndiye atakayerudi mwishoni mwa dunia kwa hukumu ya wote, ingawa maelezo kuhusu jambo hilo yanatofautiana.

Tena yote yanamchukua kama kielelezo cha utakatifu ambacho kiwaongoze katika maadili yao maalumu, kuanzia unyenyekevu na upole hadi upendo unaowaenea wote, bila kumbagua yeyote, hata adui.

Asili[hariri | hariri chanzo]

Chimbuko la Ukristo ni kuwepo kwa mtu aliyezaliwa takriban miaka 2000 iliyopita huko Mashariki ya Kati, katika kijiji cha Bethlehemu kilichopo hadi hivi leo kwenye mipaka ya Palestina; alikuwa akiitwa Yesu wa Nazareti au mwana wa Yosefu mchonga samani; mama yake akifahamika kwa jina la Bikira Maria.

Kwa kumuita pia Kristo, wafuasi wake walikiri kwamba ndiye aliyetimiza utabiri wa manabii wa kale, kama unavyopatikana katika vitabu vya Biblia ya Kiebrania na Deuterokanoni.

Masiya Yesu[hariri | hariri chanzo]

Ukristo ni matokeo ya utume wa Yesu, uliopokewa na waliomwamini kuwa ndiye Masiya, yaani mkombozi aliyetimiliza ahadi za Mungu kwa uzao wa Abrahamu.

Utabiri wa kuja kwake ulianzia katika bustani la Edeni pale Mungu alipomwambia mwanamke "uzao wako utamponda kichwa" nyoka, yaani shetani (Mwa 3:15).

Musa, mwanaharakati aliyewakomboa watu wa Israeli kutoka utumwani Misri takribani miaka 1250 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, ndiye nabii wa kwanza kutabiri wazi ujio wa Masiya au Kristo (Kumb 18:15-22, hususan mstari 18: "Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zenu; na nitatia neno langu kinywani mwake na atasema nao yote niliyomwamuru."

Kuja kwake kulitimia katika Agano Jipya, ambalo ni ukamilifu wa yote yaliyotabiriwa katika Agano la Kale. Kwani Musa alitumwa kuanzisha Agano la Kale kama maandalizi ya Agano Jipya, akikabidhi mifumo mingi ya nje na ndani kwa watawala na waamuzi waliomfuatia watakaoshikilia Agano la kusubiri Masiya wakishirikiana na manabii na makuhani.

Yesu alizaliwa miaka kama 1800 baada ya Abrahamu. Vitabu vya Injili vinaeleza matukio na mafundisho ya Yesu ambayo ndiyo mwongozo wa imani hiyo. Maisha na kazi ya Yesu yameibua mambo mengi katika historia. Ndiyo sababu kalenda iliyoenea duniani huhesabu miaka kutoka ujio wake; huu ni mchango mmojawapo wa Ukristo katika ustaarabu.

Mafundisho ya msingi ya Yesu[hariri | hariri chanzo]

Hotuba ya Mlimani kadiri ya Carl Heinrich Bloch. Hotuba ya Mlimani inachukuliwa na Wakristo kuwa utimilifu wa Torati iliyotolewa na Musa katika Mlima Sinai.

Yesu alifanya ishara za kustaajabisha, au miujiza. Matokeo ni kwamba, watu wengi wakamwamini.

Nikodemu, mshiriki mmojawapo wa baraza la Sanhedrini, ambayo ilikuwa pia mahakama kuu ya Wayahudi, alivutiwa na kutaka kujua zaidi kuhusu siri ya miujiza hiyo na ujumbe kutoka kwa Mungu; kwani yeye alihamasika kuona ishara zile kutoka kwa Mungu.

Yesu akamjibu kwamba hakika mtu hawezi kuingia ufalme wa Mungu asipozaliwa mara ya pili kwa maji na Roho Mtakatifu.

Pia akajieleza kuwa mpatanishi wa ulimwengu wa dhambi na Mungu na kwamba kila anayemgeukia kwa imani hatapotea, bali atarithi uzima wa milele: alisema mwenyewe ni mfano wa nyoka wa shaba aliyetengenezwa na Musa. (Yoh 2:23-3:21; Hes 21:9).

Akiwa kando ya Ziwa la Galilaya, Yesu alikuta umati wa watu umekusanyika. Basi akapanda mashua na kuenda mbali kidogo na ufuoni, akaanza kuwafundisha kuhusu Ufalme wa mbinguni kupitia mfululizo wa mifano.

Mmojawapo ni huu ufuatao: "Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali ambayo mtu anaipanda. Ingawa ni mbegu ndogo sana inakua na kuwa mti wa mboga mkubwa kuliko yote. Inakua mti ambao ndege wanauendea, wakipata makao katika matawi yake". (Math 13:1-52; Mk 4:1-34; Lk 8:4-18; Zab 78:2; Isa 6:9,10).

Kanisa siku za mwanzo[hariri | hariri chanzo]

Jumuia ya Wakristo inaitwa Kanisa, yaani "mkusanyiko" kama lilivyotajwa na Yesu mwenyewe hasa katika Injili ya Mathayo 16:18:

Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu, nitalijenga kanisa langu. Wala milango ya kuzimu haitalishinda.

Yesu aliita wengine 11 pamoja na Petro kuunda kundi la mitume wake. Idadi yao ilipangwa kwa kusudi la kudokeza kwamba ndiyo mwanzo mpya wa taifa la Mungu, kama vile watoto 12 wa Yakobo Israeli walivyokuwa mwanzo wa taifa lake la kale.

Yesu aliwapa hao Thenashara mamlaka ile aliyopewa na Mungu Baba ili kuokoa watu.

Ujio wa Roho Mtakatifu

Mara baada ya Yesu kwenda zake katika tukio linalotajwa kupaa kwake mbinguni, wafuasi wake wakarudi Yerusalemu, yapata mwendo wa sabato, na walipoingia huko, wakapanda ghorofani walipokuwa wakikaa Mtume Petro na wenzake. Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwapo wote mahali pamoja. Ukaja upepo toka juu kama upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukatokea na ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia. (Mdo 1:12-14, 2:1-4).

Hii ilifuatiwa na Petro na wenzake kuanza kuhubiri ufufuko wa Bwana Yesu na hatimaye kugusa watu 3,000 waliokubali kubatizwa siku hiyo. (Mdo 2: 37-40).

Ustawi wa jumuia ya kwanza ya wafuasi wa Kristo

Watu walipokuwa wakidumu katika fundisho la mitume, sala, kumega mkate na katika ushirika, wengi wakaona ishara zao nyingi basi nao wakauza mali zao, na vitu walivyokuwanavyo, na kugawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja.

Basi, siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakila pamoja na kushiriki kwa moyo mweupe.

Hivyo ndivyo jumuia ilivyozaliwa na kufahamika kama Kanisa. (Mdo 2:42-47).

Kukutanika na kushiriki mafumbo makuu, kushukuru na kusifu, pamoja na uwepo wa vipaji na karama za Roho Mtakatifu, hufanya Kanisa liwe hai.

Uenezi wa Kanisa Ujumbe wa Yesu ulienea haraka toka Yerusalemu hata Lida, Yafa, Kaisaria, Samaria, Damasko n.k. na kuanzisha jumuia nyingi.

Nazo jumuia kwa bidii za waamini wa mwanzo zikafika Foinike, Kipro, Antiokia, ambako waliitwa Wakristo kwa mara ya kwanza, kutokana na waamini wa mataifa mengine kuwazidi wale wenye asili ya Kiyahudi (Mdo 11:1-23).

Imani na desturi za mikusanyiko hiyo zenye asili ya Kiyahudi zilitapakaa na hivyo kuanza kusuguana na mapokeo ya jamii mbalimbali zilipopenya. Hii inatokana na ukweli kwamba watu wengi wa siku zile tayari walikuwa na imani zao walizokuwa wakizitunza.

Basi ukaja wakati ambao Wakristo wakaanza kukosoana kuhusu dhamiri zao na huduma. Ndiyo asili ya nyaraka mbalimbali ambazo zinaunda sehemu muhimu wa Agano Jipya.

Teolojia ya Nyaraka za Mtume Paulo[hariri | hariri chanzo]

Mtume Paulo akiandika waraka.

Paulo, maarufu kama mtume wa mataifa, aliandika hivi:

Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaotawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri; ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kutawala dunia hii hawaijui hata moja; maana kama wangalijua, wasingalimsulubisha Bwana wa utukufu; lakini, kama ilivyoandikwa:

Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.

Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho, maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuaye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua yaliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu, Maana,

Ni nani aliyefahamu nia ya Bwana, amwelimishe?

Lakini sisi tunayo nia ya Kristo. (1Kor 2:6-16).

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. (1 Wakorintho 12:12-13).

Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. (1 Wakorintho 12:28-31).

Lakini labda mtu atasema, 'Wafufuliwaje wafu?' Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu! uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu na mwili wake. Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya Jua, na fahari nyingine ya Mwezi, na fahari nyingine ya Nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota. Kadhalika na ufufuo wa wafu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutoharibika; hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu; hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa Roho.

Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko. Ndivyo ilivyoandikwa: mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa Roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama ilivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni. Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.

Angalieni, nawaambia ninyi siri: Hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo ndipo litakapokuwa lile neno lililioandikwa:

Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, ewe mauti, uchungu wako?

Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni Torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo! (1 Wakorintho 15:35-57).

Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kutimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na hila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure. Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote. Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami. (Wafilipi 2:12-18).

Mafarakano makuu kati ya Wakristo[hariri | hariri chanzo]

Matawi ya Ukristo yalivyotokea katika historia ya Kanisa. Upande wa juu ndio Kanisa la Magharibi, upande wa chini Makanisa ya Mashariki. Unene wa mistari haulingani na ukubwa wa madhehebu husika.

Ukristo ulizidi kupokea watu wa kila aina, hivi kwamba waamini wenye asili ya Kiyahudi walizidi kuwa asilimia ndogo hasa kufikia mwisho wa karne ya 1.

Ukristo ulienea hasa ndani ya mipaka ya Dola la Roma na kupokea yaliyo mema kutoka umataduni hasa wa Wagiriki (mashariki) na Walatini (magharibi), bila kukwamishwa na dhuluma za serikali zilizodumu kwa kwikwi miaka karibu 250 (64-313).

Hata nje ya dola hilo, Ukristo ulikabiliana na dhuluma, kama vile Mesopotamia na Uajemi, ambapo ulidumisha zaidi sura asili ya Kisemiti.

Tofauti hizo za utamaduni, pamoja na utaifa, zilichangia sana mafarakano.

Katika historia ndefu ya Ukristo, yalitokea mafarakano mengi, waamini wa Yesu wakizidi kutofautiana. Makundi makubwa zaidi ni: Kanisa Katoliki, Makanisa ya Waorthodoksi na ya Waorthodoksi wa Mashariki na madhehebu ya Uprotestanti.

Wakatoliki[hariri | hariri chanzo]

Zaidi ya nusu ya Wakristo wote wanashikamana katika imani na sakramenti chini ya maaskofu wenye ushirika kamili na yule wa Roma, ambaye kwa kawaida anaitwa Papa.

Kati yao umoja unazingatiwa sana kama sifa ya kwanza ya Kanisa inayotambulisha wanafunzi wa Yesu.

Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Wakristo wengi walioishi upande wa mashariki wa Dola la Kirumi na ng'ambo ya mipaka yake ya mashariki walitengana na Wakatoliki hasa katika karne V (Waorthodoksi wa Mashariki) na karne XI (Waorthodoksi).

Hata hivyo msimamo wao wa imani si tofauti sana, kwa kuwa wanachanga mapokeo ya awali ya Kanisa la Mitume na la Mababu.

Waprotestanti[hariri | hariri chanzo]

Utitiri wa madhehebu ya Waprotestanti ndio wenye tofauti kubwa zaidi kati yao wenyewe na kati yao na Wakristo waliotajwa kwanza.

Hiyo ilitokana na msimamo wa msingi wa urekebisho wa Kiprotestanti wa kutaka kila mmoja aweze kutafsiri Biblia alivyoielewa, bila kutegemea mapokeo wala mamlaka rasmi ya Kanisa, ila msaada wa Roho Mtakatifu.

Tangu mwaka 1907 tapo la Wapentekoste limeenea duniani kote (linakadiriwa kuwa na waumini milioni karibu 300) na kuathiri hata madhehebu yote ya zamani (ambapo mara nyingi waumini wa aina hiyo wanaitwa "Wakarismatiki").

Kanisa leo[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na historia ya Kanisa kuwa na mchanganyiko wa mazuri na mabaya, wengine wanahisi kuwa halina maana sana.

Hali hii inajionyesha hasa pale ambapo waamini wengi wameacha kwenda kanisani isipokuwa siku ya Krismasi na Pasaka au kwenye harusi na misiba.

Pia kutokana na mgawanyiko wa madhehebu, kumekuwa na mkanganyiko kuhusu kazi ya Kanisa la leo.

Wakatoliki, Waorthodoksi, Waorthodoksi wa Mashariki, Waanglikana, Wamethodisti, Walutheri na wengineo wanafuatilia desturi kama walivyozipokea. Mtiririko wa ibada zao huandikwa na hujulikana kama Liturujia.

Madhehebu mengine, hasa yale ya Kipentekoste, huwa na ibada ambazo hazijaandikwa kitabuni: kiongozi wa ibada wa siku hiyo huja na madondoo yake na mtiririko wa ibada huenda kama "Roho" atakavyoongoza siku hiyo. Kwa sababu hiyo husema kwamba hawafuati desturi au mapokeo. Ukiangalia zaidi utaona kuwa ibada zao pia huwa na mtindo na mtiririko fulani, kama vile kuimba mapambio ya harakaharaka wakiwa wanapiga makofi, kucheza na kurukaruka. Mapambio hayo hufuatiliwa na mengine ya taratibu wakiinua mikono kuabudu. Inawezekana kusema hao nao wana utaratibu au liturugia yao ingawa haijaandikwa kwenye vitabu.

Upande mwingine wanakanisa wanajaribu kuonyesha jitihada zao katika jamii, ikiwa ni pamoja na kuleta amani na maendeleo na kutoa misaada ya kijamii. Kuna uwezekano kwa madhehebu kadhaa kubadilisha mkazo wao kuutoa kwenye imani tu na kuuweka kwenye huduma za jamii au elimu: hii inafanya yaonekane kama moja ya mashirika ya hisani.

Binadamu wa karne ya 21 wanahitaji jibu litakalosaidia kuwakwamua kutoka matatizo yao. Wenye dini mbalimbali, hususan Wakristo, wanadai kujua ufumbuzi wa matatizo makuu ya binadamu, ingawa wachache tu wameweza kuonyesha dhahiri matatizo yaliyotatuliwa kabisa kwa dini. Wakati mwingine wanadini wenyewe wamekuwa chanzo cha matatizo badala ya kuyatatua.

Jibu linaweza kupatikana katika maneno ya Yesu mwenyewe, aliposema kwamba wafuasi wake ni chumvi ya dunia, ambayo ilete ladha katika maisha ya watu, lakini kama chumvi hiyo inapoteza ladha yake, haifai kitu, isipokuwa kutupwa na kukanyagwa kwa dharau. Hivyo changamoto ya Wakristo ni kufuata vema mafundisho ya imani yao ili kukidhi hitaji la nyakati hizi la kuishi kwa amani, furaha na upendo duniani kote .

Mfanano na dini nyingine[hariri | hariri chanzo]

Ukristo na dini nyingine zinahusiana kwa kiasi tofauti, kadiri ya mazingira asili, historia, mafundisho kuhusu imani na maadili, desturi, ibada n.k.

Ukristo na Uyahudi[hariri | hariri chanzo]

Ni wazi kuwa Ukristo unahusiana zaidi na dini ya Uyahudi, kwa sababu unatokana nayo na kutumia vitabu vyake vitakatifu (Tanakh na pengine Deuterokanoni pia). Haiwezekani kumuelewa Yesu kwa kumweka nje ya mazingira ya Kiyahudi.

Dini hizo mbili zilitengana moja kwa moja miaka 50 hivi baada ya Yesu kuaga dunia. Ni kwamba Wayahudi wa shule ya Jabneh (mwaka 80 hivi B.K.) waliamua kuwatenga kama wazushi wananchi wenzao waliomuamini Yesu Kristo, hasa baada ya kuona hawakusaidia vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni Warumi vilivyosababisha maangamizi ya Hekalu la pili na mji wa Yerusalemu mwaka 70 B.K.

Tangu hapo Wakristo hawakushiriki tena ibada pamoja na Wayahudi, wakazidi kuzingatia sakramenti ya Kumega Mkate katika Siku ya Bwana (Jumapili, siku inaposadikika Yesu alifufuka) badala ya Sabato (Jumamosi, siku ya pumziko ya Wayahudi). Kabla ya hapo Wakristo wa Kiyahudi walikuwa wanashika siku zote mbili.

Ukristo na Ubuddha[hariri | hariri chanzo]

Hakuna uhusiano wa kihistoria kati ya Yesu na Ubuddha. Hata hivyo mambo kadhaa yanafanana.

Yesu alifundisha kuhusu nidhamu mbili zinazompelekea mtu kuwa mwadilifu na hatimaye kuurithi utukufu wa kiroho ambao karama yake ni uzima wa milele: hizo ni kumpenda Mungu kwa moyo wako wote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote, na jirani yeyote kama unavyojipenda mwenyewe.

Buddha alifundisha hali ya kutodhuru viumbe hai wowote, tena kuwa na moyo mkuu wa mapenzi kwa vitu vyote. Hii ni miongozo inayolenga mtu atambue tabu anazodumisha yeye mwenyewe, kwa matendo yake na upeo ulio na mipaka, katika maisha yake ya kila siku.

Baada ya hili, mafundisho ya Kristo yanatofautiana katika kuchukulia hali hii. Kwa mujibu wa Kristo, dhambi, matendo yenye kukosea kanuni za kiroho na hata za kimaumbile, hufutwa na toba; wakati katika mafundisho ya Buddha, makosa yote yanatokana na kutokuwa makini. Hivyo, kwa mujibu wa Buddha, njia pekee ya kumkomboa mtu na shida zake ni kufuata mwongozo wa Nguzo Nane ambazo humweka katika hali ya kuweza kuamka kiroho wakati utulivu wa kimwili na wa kiakili unapofikiwa. Haya ndiyo yanayofanya Ubuddha kuwa ni njia inayojali sana nidhamu ya mtu kimatendo, wakati Ukristo hufuata sana moyo wenye kukiri makosa, na kutafuta uadilifu wa kweli wa kiroho. Huu ni uzuri wa pekee kutoka kwenye mafundisho ya Yesu: Tubuni kwa kuwa saa ya ukombozi ni sasa...

Jingine lenye tofauti ni kuwa Kristo hufundisha kuhusu Upendo kwamba ni Mungu, kwa kuwa Upendo una maana kuliko elimu yote ya binadamu, nao ndio unaounganisha na kutunza vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Hilo hutambulika kupitia Kristo ambaye hujidhihirisha kwa yule mwenye kumpokea Roho wa Mungu. Upande wa Buddha, hukanusha nafsi na pia Mungu, akisema: Ni Buddha mwenye ufahamu wa milele, tena hana nafsi isipokuwa Utupu; na ni wenye furaha isiyo kifani izidiyo yote yenye kufanyika ulimwenguni, yaani Nirvana; kila mtu ni Buddha aliyesahau asili yake ya ndani kabisa.

Ukristo na Uislamu[hariri | hariri chanzo]

Ukristo na Uislamu vinafanana zaidi kwa sababu Muhammad alifahamu Wayahudi na Wakristo wengi katika nchi yake na katika safari zake. Dini hizo tatu zinajulikana kwa kushika imani katika Mungu Pekee, muumba wa vitu vyote, na kwa kumchukua Abrahamu kama kielelezo cha imani na rafiki wa Mungu.

Mafundisho ya msingi ya Uislamu ni unyenyekevu kwa Mola mmoja aitwaye Allah , mwingi wa rehema na mwingi wa fadhila; nguzo ya Uislamu ni kumuabudu. Katika Uislamu, unyenyekevu wa mtu katika kumcha Mola kwa ibada na swala humpa kukirimika na kuhifadhika kwa Mola wake mwenye fadhila, ambaye atamtunuku haki yake. Naye mnyenyekevu kwa Mola ataishi kuona utukufu mwingi wa Mola wenye kutajwa katika Kurani kwa majina 99 ya Allah. Kati ya sifa na utukufu huo ulio na majina mengi, baadhi yake ni Al Rahman (kwa Kiarabu, "Mwenye rehema"), Al Nur ("Mwenye nuru") n.k. Hayo hufanana na neno la Nuru ya Bwana, rehema na ukombozi kuwa utukufu wa Mbingu katika mwongozo wa Kikristo.

Pia Uislamu unafundisha udugu miongoni mwa Waislamu yaani mzizi wa neno linalotumika sana katika Kurani: Waly (Wala, Wilayat, Mawla, Awla) katika kueleza jinsi Mwislamu apasavyo kuishi karibu na mwenzake. Nalo husisitiza upendo na kulindana kwa heri na pia kuepushana na shari. Hilo linafanana na upendo ambao katika Ukristo ndio adili kuu kuliko yote:

Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo... mimi si kitu kabisa. (1 Wakorintho 13:1-11).

Lakini katika Ukristo upendo hauna mipaka wala masharti. Unatakiwa kuenea kwa maadui pia na kusamehe kila mara kufuatana na mfano wa Baba wa Mbinguni.

Mwislamu kadiri ya wingi wa unyenyekevu na usafi wa moyo wake huakisi sifa za Mola wake. Uislamu hufundisha kuhusu vita vya ndani ambavyo muumini hupigana na nafsi yake yenye matamanio ya chini, ambayo huzaa chuki, dhuluma, wivu na maovu mengine ili kuishinda kwa utukufu wa Mola na kudumisha dini (mwongozo) yake katika ngazi zote za maisha.

Kabla yake Yesu alihimiza wote wafuate mfano wake wa upole na unyenyekevu wa moyo, akitoa kielelezo katika Heri Nane za hotuba ya mlimani. Tofauti ya msingi ni kuwa kwa mujibu wa Kristo, ni kwa neema ya imani katika Neno la Uzima kwamba mtu hukombolewa kutoka matamanio yake ya kibinadamu, mbali ya kwamba anapaswa kujitahidi asije akapotewa na neema hiyo na kurudia utumwa wa dhambi.

Ni imani ya Wakristo na ya Waislamu kwamba Yesu atarudi duniani kwa utukufu, ingawa jambo hilo wanalitafsiri kwa namna tofauti.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. Neno "Mkristo" (Χριστιανός) lilitumika mara ya kwanza kuhusiana na wafuasi wa Yesu katika mji wa Antiokia [Mdo 11:26] mwaka 44 BK. Wenyewe walikuwa wanajiita "ndugu", "waamini", "wateule", "watakatifu". Katika mazingira ya Kisemiti waliendelea na bado wanaendelea kuitwa "Manasara", yaani "Wanazareti" kutokana na jina la kijiji alikokulia Yesu. Kumbukumbu ya kwanza ya mwandishi ya neno "Ukristo" (Χριστιανισμός) ni katika barua za Ignas wa Antiokia, mwaka 100 hivi. See Elwell/Comfort. Tyndale Bible Dictionary, pp. 266, 828.
 2. Taz. Catholic Encyclopedia (article "Monotheism"); William F. Albright, From the Stone Age to Christianity; H. Richard Niebuhr; About.com, Monotheistic Religion resources; Kirsch, God Against the Gods; Woodhead, An Introduction to Christianity; The Columbia Electronic Encyclopedia Monotheism; The New Dictionary of Cultural Literacy, monotheism; New Dictionary of Theology, Paul, pp. 496–99; Meconi. "Pagan Monotheism in Late Antiquity". p. 111f.
 3. Taz. Hinnells, The Routledge Companion to the Study of Religion, p. 441. Zoll, Rachel (December 19, 2011). "Study: Christian population shifts from Europe". Associated Press. Retrieved 25 February 2012. 33.39% of 7.174 billion world population (under the section "People and Society") "World". CIA world facts. "The List: The World's Fastest-Growing Religions". foreignpolicy.com. March 2007. Retrieved 2010-01-04. "Major Religions Ranked by Size". Adherents.com. Retrieved 2009-05-05. ANALYSIS (2011-12-19). "Global Christianity". Pewforum.org. Retrieved 2012-08-17.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 • Albright, William F. From the Stone Age to Christianity.
 • Alexander, T. Desmond. New Dictionary of Biblical Theology.
 • Bahnsen, Greg. A Reformed Confession Regarding Hermeneutics (article 6).
 • Ball, Bryan; Johnsson, William (ed.). The Essential Jesus. Pacific Press (2002). ISBN 0-8163-1929-4.
 • Barrett, David; Kurian, Tom and others. (ed.). World Christian Encyclopedia. Oxford University Press (2001).
 • Barry, John F. One Faith, One Lord: A Study of Basic Catholic Belief. William H. Sadlier (2001). ISBN 0-8215-2207-8
 • Benton, John. Is Christianity True? Darlington, Eng.: Evangelical Press (1988). ISBN 0-85234-260-8
 • Bettenson, Henry (ed.). Documents of the Christian Church. Oxford University Press (1943).
 • Bokenkotter, Thomas. A Concise History of the Catholic Church . Doubleday (2004). ISBN 0-385-50584-1
 • Bruce, F.F. The Canon of Scripture.
 • Chambers, Mortimer; Crew, Herlihy, Rabb, Woloch. The Western Experience. Volume II: The Early Modern Period. Alfred A. Knopf (1974). ISBN 0-394-31734-3.
 • Coffey, John. Persecution and Toleration in Protestant England 1558–1689. Pearson Education (2000).
 • Cross, F. L.; Livingstone, E. A. (ed.). The Oxford Dictionary of the Christian Church. Oxford University Press (1997). ISBN 0-19-211655-X.
 • Deppermann, Klaus. Melchior Hoffman: Social Unrest and Apocalyptic Vision in the Age of Reformation. ISBN 0-567-08654-2.
 • Dilasser, Maurice. The Symbols of the Church. Collegeville, MN: Liturgical Press (1999). ISBN 0-8146-2538-X
 • Duffy, Eamon. Saints and Sinners, a History of the Popes. Yale University Press (1997). ISBN 0-300-07332-1
 • Elwell, Walter A.; Comfort, Philip Wesley. Tyndale Bible Dictionary, Tyndale House Publishers (2001). ISBN 0-8423-7089-7.
 • Esler, Philip F. The Early Christian World. Routledge (2004).
 • Farrar, F.W. Mercy and Judgment. A Few Last Words On Christian Eschatology With Reference to Dr. Pusey's, "What Is Of Faith?". Macmillan, London/New York (1904).
 • Ferguson, Sinclair; Wright, David, eds. New Dictionary of Theology. consulting ed. Packer, James. Leicester: Inter-Varsity Press (1988). ISBN 0-85110-636-6
 • Foutz, Scott. Martin Luther and Scripture Martin Luther and Scripture.
 • Fowler, Jeaneane D. World Religions: An Introduction for Students, Sussex Academic Press (1997). ISBN 1-898723-48-6.
 • Fuller, Reginald H. The Foundations of New Testament Christology Scribners (1965). ISBN 0-684-15532-X.
 • Froehle, Bryan; Gautier, Mary, Global Catholicism, Portrait of a World Church, Orbis books; Center for Applied Research in the Apostolate, Georgetown University (2003) ISBN=1-57075-375-X
 • Funk, Robert. The Acts of Jesus: What Did Jesus Really Do?. Polebridge Press (1998). ISBN 0-06-062978-9.
 • Glenny, W. Edward. Typology: A Summary Of The Present Evangelical Discussion.
 • Gonzalez, Justo L. The Story of Christianity: The Early Church to the Dawn of the Reformation, Harper Collins Publishers, New York (1984).
 • Hanegraaff, Hank. Resurrection: The Capstone in the Arch of Christianity. Thomas Nelson (2000). ISBN 0-8499-1643-7.
 • Harnack, Adolf von. History of Dogma (1894).
 • Hickman, Hoyt L. and others. Handbook of the Christian Year. Abingdon Press (1986). ISBN 0-687-16575-X
 • Hinnells, John R. The Routledge Companion to the Study of Religion (2005).
 • Hitchcock, Susan Tyler. Geography of Religion. National Geographic Society (2004) ISBN 0-7922-7313-3
 • Kelly, J.N.D. Early Christian Doctrines.
 • Kelly, J.N.D. The Athanasian Creed. Harper & Row, New York (1964).
 • Kirsch, Jonathan. God Against the Gods.
 • Kreeft, Peter. Catholic Christianity. Ignatius Press (2001) ISBN 0-89870-798-6
 • Letham, Robert. The Holy Trinity in Scripture, History, Theology, and Worship. P & R Publishing (2005). ISBN 0-87552-000-6.
 • Lorenzen, Thorwald. Resurrection, Discipleship, Justice: Affirming the Resurrection Jesus Christ Today. Smyth & Helwys (2003). ISBN 1-57312-399-4.
 • McLaughlin, R. Emmet, Caspar Schwenckfeld, reluctant radical: his life to 1540, New Haven: Yale University Press (1986). ISBN 0-300-03367-2.
 • MacCulloch, Diarmaid, The Reformation: A History. Viking Adult (2004).
 • MacCulloch, Diarmaid, A History of Christianity: The First Three Thousand Years. London, Allen Lane. 2009. ISBN 978-0-7139-9869-6
 • Marber, Peter. Money Changes Everything: How Global Prosperity Is Reshaping Our Needs, Values and Lifestyles. FT Press (2003). ISBN 0-13-065480-9
 • Marthaler, Berard. Introducing the Catechism of the Catholic Church, Traditional Themes and Contemporary Issues. Paulist Press (1994). ISBN 0-8091-3495-0
 • Mathison, Keith. The Shape of Sola Scriptura (2001).
 • McClintock, John, Cyclopaedia of Biblical, Theological, and Ecclesiastical Literature. Harper &Brothers, original from Harvard University (1889)
 • McGrath, Alister E. Christianity: An Introduction. Blackwell Publishing (2006). ISBN 1-4051-0899-1.
 • McGrath, Alister E. Historical Theology.
 • McManners, John. Oxford Illustrated History of Christianity. Oxford University Press (1990). ISBN 0-19-822928-3.
 • Meconi, David Vincent. "Pagan Monotheism in Late Antiquity", in: Journal of Early Christian Studies.
 • Metzger, Bruce M., Michael Coogan (ed.). Oxford Companion to the Bible. Oxford University Press (1993). ISBN 0-19-504645-5.
 • Mullin, Robert Bruce. A short world history of Christianity. Westminster John Knox Press (2008).
 • Norman, Edward. The Roman Catholic Church, An Illustrated History. University of California (2007) ISBN 978-0-520-25251-6
 • Olson, Roger E., The Mosaic of Christian Belief. InterVarsity Press (2002). ISBN 978-0-8308-2695-7.
 • Orlandis, Jose, A Short History of the Catholic Church. Scepter Publishers (1993) ISBN 1-85182-125-2
 • Ott, Ludwig. Grundriß der Dogmatik. Herder, Freiburg (1965).
 • Otten, Herman J. Baal or God? Liberalism or Christianity, Fantasy vs. Truth: Beliefs and Practices of the Churches of the World Today.... Second ed. New Haven, Mo.: Lutheran News, 1988.
 • Pelikan, Jaroslav; Hotchkiss, Valerie (ed.) Creeds and Confessions of Faith in the Christian Tradition. Yale University Press (2003). ISBN 0-300-09389-6.
 • Putnam, Robert D. Democracies in Flux: The Evolution of Social Capital in Contemporary Society. Oxford University Press (2002).
 • Riley-Smith, Jonathan. The Oxford History of the Crusades. New York: Oxford University Press, (1999).
 • Robinson, George. Essential Judaism: A Complete Guide to Beliefs, Customs and Rituals. New York: Pocket Books (2000).
 • Schama, Simon . A History of Britain. Hyperion (2000). ISBN 0-7868-6675-6.
 • Servetus, Michael. Restoration of Christianity. Lewiston, New York: Edwin Mellen Press (2007).
 • Simon, Edith. Great Ages of Man: The Reformation. Time-Life Books (1966). ISBN 0-662-27820-8.
 • Smith, J.Z. (1998).
 • Spitz, Lewis. The Protestant Reformation. Concordia Publishing House (2003). ISBN 0-570-03320-9.
 • Sproul, R.C. Knowing Scripture.
 • Spurgeon, Charles. A Defense of Calvinism.
 • Sykes, Stephen; Booty, John; Knight, Jonathan. The Study of Anglicanism. Augsburg Fortress Publishers (1998). ISBN 0-8006-3151-X.
 • Ustorf, Werner. "A missiological postscript", in: McLeod, Hugh; Ustorf, Werner (ed.). The Decline of Christendom in Western Europe, 1750–2000. Cambridge University Press (2003).
 • Walsh, Chad. Campus Gods on Trial. Rev. and enl. ed. New York: Macmillan Co., 1962, t.p. 1964. xiv, [4], 154 p.
 • Woodhead, Linda. An Introduction to Christianity.

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

 • Gill, Robin (2001). The Cambridge companion to Christian ethics. Cambridge, UK: Cambridge University Press. ISBN 0-521-77918-9. 
 • Gunton, Colin E. (1997). The Cambridge companion to Christian doctrine. Cambridge, UK: Cambridge University Press. ISBN 0-521-47695-X. 
 • MacCulloch, Diarmaid. Christianity: The First Three Thousand Years (Viking; 2010) 1,161 pages; survey by leading historian
 • MacMullen, Ramsay (2006). Voting About God in Early Church Councils. New Haven, CT: Yale University Press. ISBN 0-300-11596-2. 
 • Padgett, Alan G.; Sally Bruyneel (2003). Introducing Christianity. Maryknoll, N.Y.: Orbis Books. ISBN 1-57075-395-4. 
 • Price, Matthew Arlen; Collins, Michael (1999). The story of Christianity. New York: Dorling Kindersley. ISBN 0-7513-0467-0. 
 • Ratzinger, Joseph (2004). Introduction To Christianity (Communio Books). San Francisco: Ignatius Press. ISBN 1-58617-029-5. 
 • Roper, J.C., Bp. (1923), et al.. Faith in God, in series, Layman's Library of Practical Religion, Church of England in Canada, vol. 2. Toronto, Ont.: Musson Book Co. N.B.: The series statement is given in the more extended form which appears on the book's front cover.
 • Tucker, Karen; Wainwright, Geoffrey (2006). The Oxford history of Christian worship. Oxford [Oxfordshire]: Oxford University Press. ISBN 0-19-513886-4. 
 • Wagner, Richard (2004). Christianity for Dummies. For Dummies. ISBN 0-7645-4482-9. 
 • Webb, Jeffrey B. (2004). The Complete Idiot's Guide to Christianity. Indianapolis, Ind: Alpha Books. ISBN 1-59257-176-X. 
 • Woodhead, Linda (2004). Christianity: a very short introduction. Oxford [Oxfordshire]: Oxford University Press. ISBN 0-19-280322-0. 

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]