Nenda kwa yaliyomo

Ubuddha

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu kubwa ya Buddha kwenye kisiwa cha Lantau, Hong Kong, China).
Asilimia ya Wabuddha nchi kwa nchi, kadiri ya Pew Research Center, 2010.

Ubuddha ni mfumo wa kidini uliotokana na mafundisho ya Siddharta Gautama aliyejulikana kama Buddha.

Kuna wafuasi wengi, hasa katika Asia ya Kusini, Kusini-Mashariki na Mashariki. Makadirio ya idadi yao ni kati ya milioni 488-535 (7-8% ya watu wote duniani). Hivyo ni dini kubwa ya nne baada ya Ukristo, Uislamu na Uhindu.

Mafundisho yao yalianzishwa na Siddhartha Gautama aliyezaliwa mnamo mwaka 563 KK kufuatana na mapokeo; wataalamu wengine huona ya kwamba alizaliwa karne moja baadaye.

Wanahistoria wengi wa mwanzo wa karne ya 20 walitaja miaka 563 KK hadi 483 KK hivi,[1] lakini maoni ya siku hizi yanataja mwaka wa kufariki kati ya 486 KK na 483 KK au, hata kati ya 411 KK na 400 KK.[2][3]

Kadiri ya akiolojia, Buddha aliweza kuzaliwa huko Lumbini, (leo nchini Nepal)[4][5][4] au huko Kapilavastu, Piprahwa, Uttar Pradesh, India au tena Kapileswara, Orissa, India.[6][7][8][9][10]

Anaitwa pia "Buddha wa kihistoria" au "Buddha Shakyamuni" kwa sababu katika imani yao kuna mabuddha mbalimbali.

Neno "Buddha" si jina bali cheo cha heshima chenye maana ya "aliyeamka". Humo mna kiini cha imani ya Ubuddha kuwa binadamu huishi kwa kawaida bila ya kutambua hali yake mwenyewe, lakini akielewa mafundisho anakuja kuamka na kuona hali yake pamoja na njia inayopaswa kufuatwa.

Katika haya yote Wabuddha hufuata mfano wa Buddha Shakyamuni wakitegemea kufika kwenye hali ya kuamka.

Kati ya Wabuddha kuna mielekeo mbalimbali kama madhehebu. Yale yenye wafuasi wengi ni:

Maisha na mafundisho ya Gautama Buddha

[hariri | hariri chanzo]

Mtoto wa kifalme

[hariri | hariri chanzo]

Yeye alizaliwa na kupewa jina la Siddharta kutoka kwenye familia ya kifalme ya ukoo wa Shakyamuni yapata miaka 2500 iliyopita huko India ya kaskazini.

Mama wa Buddha alifariki angali yeye ni mtoto na tena alikuwa na shauku la kuwa mtoto atayemzaa si wa kawaida. Akiwa mjamzito, aliota ndoto ya tembo mweupe aliyehusunika na mtoto atakayejifungua.

Jambo hilo lilikuwa dalili ya kwamba mtoto atakayezaliwa atakuwa mtu mwenye bahati, tena maalum.

Mwona aliyetembelea jumba la kifalme ili kutoa utabiri wake kuhusu maajaliwa ya mtoto, kwa mujibu wa desturi na mila za siku zile, alitabiri kwamba mtoto huyo atakuja kuwa mkubwa na mtawala mahiri; ama ataiacha kasri ya baba yake na kuishi maisha ya upwekeni kutafuta shauri kuu kuhusu Maisha na Uhai.

Baba yake Siddharta aliyekuwa mtawala, alishtushwa mno na kauli juu ya mtoto wake kuja kuwa Mmistiya. Hivyo alijitahidi kila aliloweza kumficha mtoto kuhusu upande wa maisha wenye sura ya tabu na mahangaiko. Akijaribu kumsogezea na kumpa kila fahari ya maisha ili asahau sehemu ya nafsi yake yenye uwezekano wa kumfanya aghairi maisha ya anasa ili kwenda kuishi kimaskini kama wamistiya wengi wa zama zile walivyokuwa wakifanya, kutoka mijini na kwenda porini kuishi maisha duni na hali ya asili.

Alipofikia umri wa kuoa, baba yake alimpa mke ambaye alimzalia mjukuu mmoja. Hapo Siddharta alikuwa anatimiza miaka takribani ishirini na tisa.

Safari nne za Siddharta nje ya jumba la kifalme

[hariri | hariri chanzo]

Wakati ule Siddharta alitoka nje ya jumba la kifalme la baba yake kwa mara ya kwanza akiongozana na mtumishi wake mmoja mwadilifu.

Alishangaa sana alipomwona mtu aliyetembea kwa shida tu na uso ulikuwa na mafinyo. Akamwuliza mtumishi wake, "Kwa nini mtu huyu anatembea kwa shida na uso wake unaonyesha mafinyo?" Mtumishi akamjibu, "Huyu ni mzee. Watu wote watakuwa wazee siku mmoja. Ni hali ya kawaida". Siddharta, asiyewahi kumwona mzee kwa sababu baba yake hakuruhusu wazee katika mazingira ya mtoto wake, akashtuka akauliza: "Je, na mimi nitakuwa mzee na nitaonekana hivyo?". Mtumishi akamjibu, "Ndiyo, na wewe utazeeka kama kila mtu." Wakarudi kwao kimya.

Wakatoka nje tena. Safari ya pili wakamwona mgonjwa, na safari ya tatu wakaona maiti. Kila safari Siddharta alisikia ya kwamba hata yeye ataona mambo hayo maishani mwake. Yote yalimgusa sana akawa na wasiwasi kwa sababu pande hizo za maisha ziliwahi kufichwa mbele yake.

Katika safari ya nne walimwona mtawa wa Kihindu aliyeketi kando ya barabara. Siddharta alivutwa sana na fikra ya kwamba mtu huyO aliachana na mali na mambo yote kwa hiari yake na kufikia uhuru wa roho na hakuogopa tena kifo.

Hapo alikata shauri moyoni mwake kuondoka katika maisha ya kifalme na kutafuta maisha ya utawa.

Maisha ya mtawa

[hariri | hariri chanzo]

Siddharta aliondoka nje ya jumba la kifalme usiku mmoja bila ya kumwaga mtu yeyote, akajiunga na kundi la watawa na kufuata maisha yao.

Hatimaye, akiwa na wenzake alikutana nao katika harakati zake kutafuta kilele cha ufahamu, walikwenda kuishi kwenye misitu ya mbali na kudumu katika kutafakari na Milaya.

Miaka sita ilipita, iliyojaa maisha ya kujima na kila namna ya kuusonga mwili ili kutafuta taamuli. Hatimaye Siddharta mtawa alidhoofu na mwili wake kukonda kutokana na kufunga kwa siku mfululizo.

Siku moja akiwa mwenye kukata tamaa, akiwa kando ya mto, alipita mwanamke aliyebeba maziwa. Siddharta alimwomba yule mwanamke ampatie maziwa anywe, maana alikuwa mwenye kuhitaji. Basi yule mwanamke akampatia. Baada ya kunywa na kushukuru alijisikia ni mwenye utulivu akajisemea moyoni kwamba baada ya hapo ataketi chini ya mti na hatainuka tena mpaka atapotokewa na Taamuli.

Kutaalamiwa chini ya mti

[hariri | hariri chanzo]

Huo ukawa mwanzo mpya uliofuatiwa na baraka na neema. Kwani ni usiku uliofuatia alitokewa na Taamuli na Ufunuo. Katika imani ya Wabuddha akabadilika kuwa "Buddha" katika usiku huo yaani mtu aliyepokea ufunuo na ujuzi.

Baada ya hapo alikaa na kutafakari mambo yote aliyoyaona na kuangalia jinsi atakavyoweza kufundisha njia yenye kuleta wongofu. Kwani Taamuli yake ilifuatia kutambua Kweli Nne kuhusu maisha.

Baadaye alifundisha huko na huko India mashariki, kama vile Magadha na Kośala.[11][12]

Kweli Nne za Buddha

[hariri | hariri chanzo]

Kweli ya Kwanza ni kuwa Maisha ya duniani ni mateso kutoka kuzaliwa hadi kufa, hata kifo si mwisho kwani maisha ni mzunguko wa majira ya kufa na kuzaliwa tena na tena.

Kweli ya Pili ni kuwa asili ya masumbuko yote ni Ujinga, yaani kutokujua namna asilia na kanuni ya mambo na hali za maisha na jinsi yanavyosonga.

Kweli ya Tatu ni kwamba shida na masumbuko hutokana na kujishikiza kwa mwanadamu na mambo ya dunia hii pasipo uelewa wa lolote linalozidi milango ya fahamu na budi (Sehemu ya Akili yenye kuendesha fikra kutokana na milango ya fahamu).

Kweli ya Nne ni kwamba njia ya wongofu yaani namna ya kutoka katika matatizo hayo aliyoiita (Njia ya Nguzo Nane).

Njia ya Nguzo Nane

[hariri | hariri chanzo]

Ni gurudumu la nguzo nane ambazo humuongoza mwanadamu kuelekea kwenye Taamuli na hasa kufikia wongofu. Kufikia wongofu ni kuachana na mzunguko wa kufa na kuzaliwa unaosababishwa na matakwa yenye msingi wa Budi inayojengeka na kurudisha hali za kimaisha zenye kufanya mzunguko usiokoma wa masumbuko. Hivyo, njia hii iliyoitwa Dhammapada (Dhamma ni uadilifu na Pada ni njia) ndiyo pekee yenye kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye taabu na masumbuko ya ulimwengu. Nayo ina nguzo nane zifuatazo.

Moja ni Ono sahihi. Pili ni Dhamira sahihi. Tatu ni Kauli sahihi Nne ni Jitihada sahihi. Tano ni Tendo sahihi. Sita ni Isho sahihi. Saba ni Umakini sahihi. Nane ni Mkazo nia sahihi.

Milaya na Taamuli

[hariri | hariri chanzo]

Mkazo nia ni dhana ya kudumu katika kitendo cha akili yenye kuona pasipo kusogea ama kutangatanga juu ya jambo moja hadi lingine. Na hii ndio kigezo kikuu cha Siddhaharta Buddha katika kufundisha Milaya yenye kuongoza kwenye Taamuli.

Pia tazama

[hariri | hariri chanzo]

Vipassana.

  1. L. S. Cousins (1996), "The dating of the historical Buddha Archived 26 Februari 2011 at the Wayback Machine.: a review article", Journal of the Royal Asiatic Society (3)6(1): 57–63.
  2. See the consensus in the essays by leading scholars in The Date of the Historical Śākyamuni Buddha (2003) Edited by A. K. Narain. B. R. Publishing Corporation, New Delhi. ISBN 81-7646-353-1.
  3. "If, as is now almost universally accepted by informed Indological scholarship, a re-examination of early Buddhist historical material, ..., necessitates a redating of the Buddha's death to between 411 and 400 BCE...." —Paul Dundas, The Jains, 2nd edition, (Routledge, 2001), p. 24.
  4. 4.0 4.1 "Lumbini, the Birthplace of the Lord Buddha". UNESCO. Iliwekwa mnamo 26 Mei 2011.
  5. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-10-31. Iliwekwa mnamo 2015-01-21.
  6. "Kapilavastu". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2011-01-08. Iliwekwa mnamo 1 Machi 2011.
  7. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-06-03. Iliwekwa mnamo 2015-01-21.
  8. http://www.rediff.com/news/2002/sep/16spec.htm
  9. http://www.srilankaguardian.org/2008/03/buddha-born-in-orissa-scholars.html
  10. "Nakala iliyohifadhiwa" (PDF). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2012-03-18. Iliwekwa mnamo 2015-01-21.
  11. Warder, A.K. Indian Buddhism. 2000. p. 45
  12. Skilton, Andrew. A Concise History of Buddhism. 2004. p. 41

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]