Nenda kwa yaliyomo

Uislamu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kaaba ni kibla ya Waislamu wote duniani wakati wa swala.

Uislamu (kwa Kiarabu: الإسلام al-islam) ni dini inayotokana na mafunzo ya Mtume Muhammad.

Wafuasi wa imani hiyo huitwa "Waislamu" na wanakadiriwa kuwa milioni 1,800 hivi. Hivyo ni dini ya pili duniani yenye wafuasi wengi baada ya Ukristo wenye wafuasi milioni 2,400.

Uislamu ni ile imani kuwa muumba ni mmoja tu kwa dhati na sifa zake. Nguzo nyingine za imani zinajengwa juu ya imani ya Mungu mmoja wa kweli, imani juu ya maisha baada ya kifo, imani juu ya Malaika wa Mungu, vitabu vyake na kudra na tafsiri ya vitendo ya imani hii ni: Sala, Zakah, Saumu na Hija.

Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya

Uislamu

Imani na ibada zake

Umoja wa Mungu
Manabii
Misahafu
Malaika
Uteule
Kiyama
Nguzo za Kiislamu
ShahadaSwalaSaumu
HijaZaka

Waislamu muhimu

Muhammad

Abu BakrAli
Ukoo wa Muhammad
Maswahaba wa Muhammad
Mitume na Manabii katika Uislamu

Maandiko na Sheria

Qur'anSunnahHadithi
Wasifu wa Muhammad
Sharia
Elimu ya Sheria za KiislamuKalam

Historia ya Uislamu

Historia
SunniShi'aKharijiyaRashidunUkhalifaMaimamu

Tamaduni za Kiislamu

ShuleMadrasa
TauhidiFalsafaMaadili
Sayansi
SanaaUjenziMiji
KalendaSikukuu
Wanawake
ViongoziSiasa
Uchumi
UmmaItikadi mpyaSufii

Tazama pia

Uislamu na dini nyingine
Hofu ya Uislamu

Imani na kitabu chake

Imani katika Uislamu ni kumwamini Mungu mmoja tu peke yake anayeitwa Allah, ambaye hajazaa wala hajazaliwa na hafanani na yeyote yule. Kitabu kitakatifu cha Waislam ni Qur'an ambayo inaaminiwa ilifunuliwa kwa Mtume Muhammad kutoka kwa Mwenyezi Mungu mbinguni kupitia malaika Jibrili; ni kawaida kusema Qurani "iliteremshwa" kwa Muhammad. Kwa imani hiyo, kabla yake walioteremshiwa kitabu ni Musa (Torati), Daudi (Zaburi) na Isa (Injili).

Pamoja na Qurani kuna mafundisho ya Sunna na Hadith ambayo ni maneno ya mtume Muhammad na masimulizi juu ya matendo yake ambayo pengine hutazamiwa kama mwongozo katika Uislamu.

Qurani inasisitiza kwamba Allah hana mshirika, hana baba wala mwana, hakuzaa wala hakuzaliwa, na hana mwanzo wala mwisho.

Pamoja na amri mbalimbali kuna mfumo wa sheria za kidini zinazoitwa kwa jumla "sharia"; inajumlisha maagizo kuhusu mambo mengi ya maisha ya kila siku, uchumi na siasa.

Historia ya chanzo cha Uislamu

Muhammad alizaliwa mnamo mwaka 570 BK kama mtoto wa mfanyabiashara mjini Maka uliopo kwenye Bara Arabu.

Kufuatana na mapokeo ya Kiislamu malaika Jibril alimtokea alipokuwa na umri wa miaka 40 yaani mnamo mwaka 610. Kutoka kwa malaika alipokea maneno ya Kurani na ufunuo huu uliendelea hadi mwisho wa maisha yake.

Mtume alitangaza yale aliyosikia kwa wafuasi wake na maneno haya yalianza kukusanywa tayari wakati wa maisha ya mtume. Baada ya kifo chake mwaka 632 khalifa wa tatu Uthman ibn Affan alikusanya muswada na kumbukumbu zote na kuziweka pamoja na kuwa kitabu kamili.

Ujumbe uliohubiriwa na Muhammad huko Maka ulipata wasikilizaji wachache, lakini viongozi wengi wa Kikuraishi, waliokuwa kabila kubwa Maka, waliwaona kama hatari kwa Maka na mwaka 622 Waislamu walipaswa kutoka Maka wakahamia Yathrib mji wa jirani uliojulikana baadaye kama Madina.

Uhamisho huu unaitwa hijra na tangu khalifa wa pili Umar ibn al-Khattab huhesabiwa kuwa ni chanzo cha kalenda ya Kiislamu.

Mjini Yathrib mtume aliendelea kuwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi. Alifanya mapatano na watu wa Yathrib iliyoitwa baadaye "madinat an-nabi"" ikajulikana kwa kifupi kama Madina.

Kutoka Madina mtume alianza kushambulia misafara ya watu wa Maka akawashinda mara kadhaa. Wakati huohuo aliwafukuza Wayahudi wa Yathrib.

Mwaka 628 viongozi wa Maka walilazimishwa kufanya mapatano na Waislamu na mwaka 630 jeshi la Waislamu liliingia mjini Maka.

Mtume alipoaga dunia mwaka 632 sehemu kubwa ya Bara Arabu ilikuwa chini ya Uislamu tayari.

Mafunzo ya Uislamu

Uislamu unawafunza wafuasi wake mambo mengi yanayohusiana na maisha, ikiwa yale yanayohusu ibada kama Sala, Zakat, Saumu na Hija; ambazo pamoja na kauli ya Shahada ("Nakiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mtume wake") huitwa nguzo za Uislamu au yale yanayohusu maingiliano baina ya wanadamu, yakiwa maingiliano ya kijamii kama ndoa na talaka na ujirani mwema, au ya kiuchumi kama biashara, au ya kisiasa kama kawaida za kumchagua kiongozi wa dola, au ya uhusiano baina ya mataifa mbali mbali ulimwenguni.

Waislamu wanatazama Uislamu kuwa mfumo kamili wa maisha ya binadamu, kiimani, kimaisha, kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Ibada katika Uislamu

Ibada katika Uislamu ni vile vitendo ambavyo Muislamu anamfanyia Mwenyezi Mungu peke yake, kwani ibada yoyote haitakikani iwe na ushirikina ndani yake, na wakati itakapokuweko aina yoyote ya shirki basi ibada ile inakuwa haina maana wala thawabu wala ujira wowote, ni kazi ya bure.

Kwa hiyo, kila Muislamu anatakikana wakati anapofanya ibada yake afanye kwa ajili ya Mola wake aliyemuumba akampa kila aina ya neema na kumtukuza kuliko viumbe vingine vyovyote, kwa kumpa akili, fahamu na elimu.

Kuna matendo kadhaa ambazo zinaitwa "Nguzo za Uislamu". Kwa kawaida ni tano zinazofundishwa katika madhehebu ya Wasunni jinsi inavyoonyeshwa hapo chini.

Washia hawahesabu shahada kati ya nguzo tano wakiona shahada pamoja na imani ya Kiislamu ni msingi kwa nguzo tano halafu wanaongeza "wilayat" yaani kukubali uongozi wa Maimamu kama nguzo ya tano .

  1. Shahada: (Kiarabu: الشهادة) Nguzo ya kwanza katika Uislamu hujumuisha kutoa kauli mbili: Hakuna Mola apasaye Kuabudiwa ila Allah na Muhammad ni Mtume wake. Kauli hizo hutolewa pale mwanadamu anapoingia Uislamu.
  2. Salat: (Kiarabu: صلاة‎) ni sala inayofuata utaratibu maalumu mara tano kila siku: Asubuhi, mchana, alasiri, jioni na usiku. Kabla ya kuingia katika ibada hii Mwislamu anapaswa kufanya wudhu ambayo ni tendo la kutakasa mwili kwa maji au -kama hakuna- kwa kutumia vumbi badala yake. Salat ina maneno yake na pia namna ya kusimama au kujinama. Salat hii ni tofauti na dua (دعاء) au sala ya kuomba kwa hiari.
  3. Zakat: (Kiarabu: زكاة‎‎) Nguzo ya tatu ya Uislamu nayo ni ibada inayomuelekeza Mwislamu kuwaangalia Waislamu wenzake kwa hali na mali, na kushughulikia mahitaji yao ya maisha, kwa kutoa fungu la mali yake asilimia 2.5 kila mwaka kwa mwenye uwezo na kuwapa wale walio maskini na wasiojiweza ili nao waweze kuishi vizuri.
  4. Funga/Saumu: (Kiarabu: صوم) Wakati wa mwezi Ramadani kila Mwislamu anapaswa kufunga chakula na kinywaji chote kuanzia asubuhi hadi jioni. Watoto na wagonjwa hawapaswi kutekeleza wajibu huu. Waislamu wanaona maana ya ibada hii kumkurubisha Mwislamu na Mola wake na kumfanya amche na kumuogopa zaidi, kwani saumu humsaidia Mwislamu kufahamu shida na taabu ambazo wale wasiokuwa na uwezo wanazipata wakiwa na njaa na hawana cha kukila, na kwa hivyo, huingiwa na huruma na kuwa na moyo wa kutaka kuwasaidia na kuwaondoshea shida hizo.
  5. Hajj (Kiarabu: الحجّ alhajj): Kila Mwislamu mwenye uwezo anatakiwa kwenda hijja Maka mara moja katika maisha yake wakati wa mwezi Dhul-Hija. Nguzo hii inawapa fursa Waislamu ulimwenguni kukutana na wenzao na kujua hali zao na kupata nafasi ya kuomba maghfira na msamaha kwa madhambi yao katika mkutano mkubwa kabisa wa wanadamu ulimwenguni.

Maingiliano katika Uislamu

Uislamu umeweka kawaida mbali mbali katika maisha wakati watu wanataka kuweka uhusiano fulani baina yao ili mambo yaende vizuri na uhusiano uzidi kuwa mwema baina yao. Katika maingiliano yaliyowekewa kawaida na nidhamu katika Uislamu ni mambo yanayohusu:

  1. Nikaha au ndoa baina ya Waislamu
  2. Biashara na mambo yanayohusu uchumi
  3. Uhusiano wa kijamii baina ya watu katika mtaa au kijiji au mji au nchi
  4. Uhusiano wa kimataifa baina ya madola mbali mbali, yakiwa ya kiislamu au yasiyokuwa ya kiislamu.

Vikundi na madhehebu

Kuna mielekeo mikubwa miwili ndani ya Uislamu ambayo ni vikundi vya Wasunni 85-90% na Washia 10-15%.

Kundi kubwa ni Wasunni waliopata jina kutokana na Sunna ("kawaida") ya mtume; takriban asilimia 85-90 ya Waislamu wote huhesabiwa humo. Kati yao kuna madhehebu 4 ambao ni Hanafi, Maliki, Hanbali na Shafii. Tofauti katika mafundisho si kubwa, zinahusu hasa sharia na fikh.

Kundi dogo zaidi ni Washia ambao wamegawanyika kati yao katika vikundi vingi. Washia walijitenga na Wasunni baada ya makhalifa wanne wa kwanza kuhusu swali ni nani anayefaa kuongoza Waislamu. Washia ni wale waliosisitiza sharti awe mtu kutoka ukoo wa Muhammad kupitia binti yake Fatima. Vikundi vya Washia vinatofautiana juu ya viongozi hawa. Jumuiya kubwa ya Washia ni Ithnashara walio wengi huko Uajemi, Irak na Lebanoni.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.