Nenda kwa yaliyomo

Daudi (Biblia)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Daudi)
Daudi akimmaliza Goliathi katika mchoro wa Caravaggio.

Daudi (kwa Kiebrania דוד, Daud, kwa Kiarabu داوُد, Dāwūd; Bethlehemu, mnamo 1040 KK - Yerusalemu, 970 KK hivi) alikuwa mfalme wa pili wa Israeli ya Kale mnamo 1010 KK-970 KK. Alimfuata mfalme Sauli akafuatwa na Suleimani.

Mwana wa Yese, kama kijana alipelekwa kwenye jumba la mfalme Sauli alipopanda ngazi na kuwa kiongozi wa kijeshi.

Kati ya matendo yake yaliyokumbukwa zaidi ni ushindi juu ya Mfilisti Goliathi.

Pia Daudi alimuua mwanajeshi wake Uria na kumuoa mke wake Bathsheba: hivyo alifanya dhambi lakini Mungu alimtuma nabii wake Nathani kumlaumu. Daudi aliomba msamaha akasamehewa na Mungu. Pamoja na makosa yake, Daudi akabaki kielelezo cha mfalme wa Israeli, ambaye awe tofauti na watawala wengine wote kwa kuwa hasa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu bila ya kuyumba kwa kuelekea miungu mingine.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 29 Desemba[1].

Habari zake katika Vitabu vya Samweli[hariri | hariri chanzo]

1Sam 9:11-10:16 inasimulia Sauli alivyoteuliwa kuwa mfalme wa kwanza. Akitawala karibu miaka ishirini, alifanya makosa na kulaumiwa na Samweli, hata akakataliwa kabisa na Mungu kwa kutomtii kikamilifu (1Sam 15). Ingawa akaendelea kutawala kwa muda fulani, polepole alijitokeza kijana Daudi ambaye akaja kuanzisha ukoo wa kifalme wa milele.

1Sam 16-17 inaanza kutuletea mkusanyo wa hadithi juu ya Daudi ambazo zinampatia sifa aliyostahili, ingawa nyingine zinagongana: k.mf. kama aliingia katika utumishi wa Sauli kutokana na uhodari wake katika muziki au katika vita. Uhodari huo wote ukaendelea kusifiwa ila Daudi aliutumia kwa utukufu wa Mungu: ndiye aliyeingiza ala mbalimbali katika ibada na kutunga zaburi kadhaa, na ndiye aliyeeneza utawala wa Israeli kuliko yeyote.

Kadiri alivyozidi kupendwa na Mungu na watu, Sauli alimchukia kwa kijicho na kutaka kumuua (1Sam 18:6-16). Daudi alipolazimika kukimbia na kuunda kikosi chake akapata nafasi rahisi ya kumuua Sauli lakini alijizuia kwa kuheshimu krisma aliyopakwa awe mfalme (1Sam 24 na 26): hivyo ni mfano bora wa kujali wito wa Kimungu.

Baada ya kufanywa mfalme wa kabila lake (Yuda, yaani Kusini) na ya kupigana vita na mwana wa marehemu Sauli, Daudi akakubaliwa kuwa mfalme wa Israeli yote (yaani Kaskazini pia): pamoja na taarifa hiyo, 2Sam 5:1-12 inatuambia alivyoteka Yerusalemu uliokuwa bado mikononi mwa Wapagani akaifanya makao makuu ya kisiasa na ya kidini ya taifa lote la Mungu ili aunganishe Kaskazini na Kusini katika mji huo uliopo katikati. Kuanzia hapo Yerusalemu ukawa mji mtakatifu wa dini tatu zinazomuabudu Mungu wa Abrahamu.

2Sam 6 inasimulia sanduku la agano lilivyohamishiwa Yerusalemu kwa shangwe kubwa; hasa Daudi alicheza mbele ya Mungu kwa nguvu zake zote huku amevaa nguo ndogo ya kikuhani tu, bila ya kujijali kama mfalme.

Kwa unyenyekevu wake huo alimpendeza Mungu akapewa naye ahadi ya ajabu, yaani kwamba ufalme wake utadumu milele (2Sam 7). Utabiri huo wa nabii Nathani ukaja kuongoza tumaini la Waisraeli hasa walipodhulumiwa, k.mf. zamani za Yesu chini ya ukoloni wa Kirumi, ambapo wote walimtazamia mwana wa Daudi mwenye kurudisha ufalme wa Israeli.

Pamoja na hayo, kisha kupewa ahadi hiyo alikwenda mbele ya Mungu na kusali vizuri kama kawaida yake hata nje ya ibada: sala yake ya sifa na shukrani imejaa mshangao kwa ukuu wa Mungu na fadhili zake na kumalizika kwa ombi nyenyekevu.

Ingawa hakukubaliwa kumjengea Mungu hekalu la ajabu alivyokusudia, amekuwa mwalimu wa sala kwa nyakati zote: hata leo liturujia ya Uyahudi na ya Ukristo inategemea sana zaburi zake.

Matendo mengine tofauti yaliyoathiri sana maisha ya Daudi ni dhambi alizotenda kwa ajili ya mke wa Uria Mhiti, yaani uzinifu, unafiki, ulevyaji na uuaji wa askari huyo mwadilifu (2Sam 11). Basi, nabii Nathani akamuendea ili kumlaumu na kumtabiria adhabu mbalimbali, hasa kwamba upanga hautaondoka nyumbani kwake (2Sam 12:1-25).

Ikawa hivyo hasa kwa sababu ya Absalomu mwanae ambaye alimuua kaka yake (2Sam 13:22-37) na baada ya kusamehewa akafanya njama hata akamfukuza Daudi toka Yerusalemu (2Sam 14:28-15:29) akazini na masuria wake mahali pa wazi (2Sam 16:20-23). Hata hivyo Daudi akazidi kumpenda na alipoambiwa ameuawa akamlilia kwa namna ambayo iliwashangaza na kuwachukiza waliompigania: lakini yeye ambaye alijiombea na kupewa msamaha wa Mungu hakumchukia mwanae aliyehatarisha maisha yake (2Sam 18:19-20:8).

2Sam 24 pia inatuchorea sura yake ya kiroho: alipoadhibiwa na Mungu kwa tauni iliyoua Waisraeli wengi baada ya yeye kuhesabu askari wote alioweza kuwategemea vitani, basi kama mchungaji mwema aliomba adhabu imuangukie mwenyewe, lakini si kondoo zake wasio na kosa. Mfalme wa kumpendeza Mungu ni mchungaji wa watu wake; kadiri ya Injili, Yesu Kristo mwana wa Daudi anawajua kondoo zake mmojammoja kwa jina, naye amejitwisha adhabu ya makosa yao: ndiye mfalme na mchungaji bora.

Habari zake za mwisho[hariri | hariri chanzo]

Habari za mwisho za Daudi zinapatikana katika Kitabu cha Kwanza cha Wafalme 1-2 tunaposikia juu ya njama ya mtoto mwingine: Adoniya alitaka kutawala akajifanya mfalme huku Daudi mkongwe hana habari. Lakini Nathani akaingilia kati ili mwandamizi awe Solomoni, ambaye alipozaliwa na mke wa Uria alimhakikishia Daudi msamaha wa Mungu.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

(2Sam 7:18)[hariri | hariri chanzo]

"Mimi ni nani, Bwana Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa"?

(2Sam 24:17)[hariri | hariri chanzo]

"Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu"!

(1Nya 29:10-13)[hariri | hariri chanzo]

"Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako. Ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu".

Kitabu cha Zaburi[hariri | hariri chanzo]

Zaburi nyingi zinamtaja Daudi kama mwandishi au zimeandikwa kwa heshima yake.

Daudi katika Kurani[hariri | hariri chanzo]

Qurani inafundisha kwamba Dawd (داود) alikuwa mtume wa Allah aliyeteremshiwa kitabu cha "Zabur".

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Ufafanuzi wa Vitabu vya Samweli[hariri | hariri chanzo]

  • Auld, Graeme (2003). "1 & 2 Samuel". Katika James D. G. Dunn and John William Rogerson (mhr.). Eerdmans Commentary on the Bible. Eerdmans.
  • Bergen, David T. (1996). 1, 2 Samuel. B&H Publishing Group.
  • Gordon, Robert (1986). I & II Samuel, A Commentary. Paternoster Press.
  • Hertzberg, Hans Wilhelm (1964, trans. from German 2nd edition 1960). I & II Samuel, A Commentary. Westminster John Knox Press. {{cite book}}: Check date values in: |date= (help)
  • Tsumura, David Toshio (2007). The First book of Samuel. Eerdmans.

Ya jumla[hariri | hariri chanzo]

Marejeo mengine[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mtu wa Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Daudi (Biblia) kama habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.