Unyenyekevu
Unyenyekevu (kutoka kitenzi "kunyenyekea"; neno la Kiingereza "humility" linatokana na Kilatini humilitas, ambapo mzizi ni humus, udongo. Sababu ni kwamba unyenyekevu ni kuelekea chini.[1]) ni hali ya kujishusha mbele ya wengine, hasa wakubwa au wanaostahili heshima ya pekee, kama vile Mungu.
Lengo la kufanya hivyo ni kukubali ukweli, kinyume cha kinavyotaka kiburi, kinavyojitahidi kujikuza bila haki.
Kati ya kweli zinazomhusu binadamu kuna udogo wake kimaumbile na ukosefu wake kimaadili. Ndizo zinazomdai anyenyekee kama adili la msingi.
Katika Biblia
[hariri | hariri chanzo]Unyenyekevu unahimizwa katika Agano la Kale (Mith 3:34) na zaidi katika Agano Jipya kufutana na mfano wa Mwana wa Mungu ambaye alijishusha kabisa (Fil 2:1-17) akahimiza wanafunzi wake kumfuata hasa katika hilo ili hatimaye kutukuzwa pamoja naye. (Math 23:12).[2] Ni muhimu Wakristo wote wazingatie jinsi yeye, kama Bwana na mwalimu wao, alivyotekeleza unyenyekevu ili wafuate nyayo zake, na waone jinsi kujishusha kwake kulivyoendana na maadili ya hali ya juu.
Mtume Paulo akitaka kuhimiza unyenyekevu aliandika juu ya ukuu usio na mipaka wa Mwokozi ili tuelewe zaidi alivyojishusha: ni jambo la ajabu jinsi alivyounganisha hayo mawili, lakini kwa namna fulani muungano huo unatakiwa kupatikana katika ukamilifu wa Kikristo. “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu, ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba” (Fil 2:5-8).
Mwana pekee “hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho”. Ibilisi, ambaye ni kiumbe tu, alitaka kulingana na Mungu, akakataa kimatendo utawala wake: “nitafanana na yeye Aliye juu” (Isa 14:14). Hata alipomshawishi Eva alisema, “Mtakuwa kama Mungu” (Mwa 3:5). Lakini Yesu, anayesadikiwa kuwa Mungu kweli, alijishusha kabisa: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu… Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu” (Yoh 1:1,14). “Alijifanya kuwa hana utukufu”. Hakupoteza umungu wake, ila alitwaa umbile letu akaanza kuishi duniani katika hali duni. Umungu ndio ukamilifu usio na mipaka wa sifa zote, kumbe ubinadamu uko chini kuliko umbile la malaika yeyote, kwa kuwa hata yule wa mwisho ni roho tu. “Akatwaa namna ya mtumwa”, kwa kuwa binadamu, kiumbe cha Mungu, ni mtumishi wa Aliye Juu. Basi Mwana pekee wa Baba alitwaa umbile hilo ili katika Nafsi moja awe Mwana wa Mungu na Mwana wa Adamu, awe Mwana pekee aliyezaliwa tangu milele yote na mtoto mchanga pangoni, halafu mtu wa mateso aliyesulubiwa. “Akawa ana mfano wa wanadamu… akaonekana ana umbo kama mwanadamu”. Aliamua kufanana na wadogo wake katika yote, isipokuwa dhambi; tena aliamua kuzaliwa fukara, kuteswa na njaa, kuchoka na kuishiwa nguvu, sawa nasi na zaidi tena. “Alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba”. Mungu-Mtu alijishusha ilivyoandikwa, “Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekeza, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu” (YbS 3:18-20). Kitambulisho cha unyenyekevu ndicho utiifu unaopinga kiburi kinachotuelekeza kutimiza matakwa yetu, kutaka kujitokeza, kuongoza wengine bila kuongozwa na yeyote. Basi, ili atuponye kiburi chetu, Mwana pekee wa Mungu alijifanya mtiifu hata mauti ya msalaba.
Utiifu unafanya matendo yastahili, hivi kwamba mateso yenyewe, ingawa yanaonekana kuwa ya bure, yanaweza kuzaa tele. Hilo ni mojawapo kati ya maajabu ya Mwokozi: kutukuza uchungu kwa njia ya utiifu na upendo. Utiifu usipokataa kifo wala aibu ni wa kishujaa. Basi, kifo cha Neno aliyefanyika mwili kilikuwa cha aibu kuliko vyote, ilivyotabiriwa, “Tumhukumu auawe mauti ya aibu” (Hek 2:20). Msalaba ulitazamwa na Warumi na Wayahudi kama adhabu ya aibu na ya kutisha waliyowekewa watumwa n.k. “Aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu” (Kumb 21:23). “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti” (Gal 3:13). Ndiyo sababu msalaba “kwa Wayahudi ni kikwazo” (1Kor 1:23): ni lazima wasadiki kuwa mti wa laana umekuwa chombo cha wokovu; na kuwa aliyepigiliwa misumari juu yake, hakulaaniwa na Mungu, bali alikusudiwa awe chemchemi ya neema zote, apendwe na kuabudiwa. “Kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri… Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu… Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake” (Eb 11:26; 12:2; 13:13).
Hayo yote yalifumbika tayari katika Bwana kuzaliwa “kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu” (Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli): “Ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari… Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja - katika gombo la chuo nimeandikiwa - niyafanye mapenzi yako, Mungu” (Eb 10:5,7). Liturujia ya Noeli inatukumbusha mfululizo mfano huo, ikikaza unyenyekevu wa kuzaliwa kwake unavyopingana na ukuu wa Mwokozi. Bikira Maria alimzaa “mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni” (Lk 2:7). Neno aliyefanyika mwili hakupata nafasi: tusilisahau hilo hasa tunapoikosa sisi pia.
Upande mmoja Yesu anatuambia tujishushe tusiweze kamwe kujinyenyekeza mno; upande mwingine anatuambia, “Ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Math 5:48). Kuna watu wanaodhani kukosa unyenyekevu wakitamani muungano na Mungu ambao wanajisikia hawaustahili. Shida ipo hasa tunapopaswa kuchambua ndani mwetu unyenyekevu halisi na ule bandia, k.mf. tukitakiwa kushika msimamo dhidi ya wengine; pengine mwanzoni mwa mabishano tunasema kwa kutetea ukweli tu, lakini baadaye tunakuja kujibu kwa kiburi na utovu wa subira kutokana na umimi wetu kuchukizwa. Watu wanyofu wanatatua tatizo hilo kwa kutekeleza Biblia kuhusu muungano wa hayo mawili yanayoonekana kupingana: “Yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni” (Math 18:4). “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake” (1Pet 5:6). “Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza” (Yak 4:10).
Muungano huo wa unyenyekevu wa dhati na wa ukuu upitao maumbile unajitokeza hasa kwa watakatifu. Mtume Paulo aliandika, “Mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu” (1Kor 15:8-9). “Wao ni wahudumu wa Kristo? Nanena kiwazimu, mimi ni zaidi: katika tabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi” (2Kor 11:23). Alitaja hata “maono na mafunuo ya Bwana” (2Kor 12:1) aliyojaliwa, lakini mwishoni akasema, “Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu” (2Kor 12:7-10).
Thoma wa Akwino alifafanua hivi, “Kama vile upendo ulivyo mzizi wa uadilifu, kiburi ndiyo asili ya kila dhambi. Ni hamu isiyoratibiwa ya ukuu unaolengwa pasipo kufanywa njia ya kumtukuza Mungu. Ndivyo tunavyosogea mbali naye: ndiyo asili ya kosa lolote, na ndiyo sababu Mungu anawapinga wenye kiburi. Basi, kwa kuwa ndani ya waadilifu umo wema unaoweza ukawafanya wapatwe na kiburi, pengine Mungu anaacha wateule wake wapatwe na ugonjwa fulani, kasoro fulani, hata dhambi ya mauti ambayo iwazuie wasitakabari, iwaaibishe kweli na kuwafanya watambue kuwa kwa nguvu zao hawawezi kusimama wala kudumu hasa. Kwa namna ya pekee mtakatifu Paulo mtume angeweza kupatwa na kiburi kwa mambo mengi: alikuwa ‘ni chombo kiteule’ cha kuenezea imani kwa mataifa (Mdo 9:15); ‘alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu… akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene’ (2Kor 12:2,4); aliteseka sana kwa ajili ya Kristo, mara nyingi alitupwa gerezani akapigwa mijeledi; alikuwa na moyo safi kwa kujaliwa ‘kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu’ (1Kor 7:25); alifanya ‘kazi kupita wao wote’ (1Kor 15:10), alivyosema mwenyewe; na kwa namna ya pekee alikuwa na ujuzi wa mambo ya Mungu mkubwa hivi hata uweze kumtia kiburi. Ndiyo sababu Bwana alimpa dawa ya kiburi. Ili ukuu wa maono aliyojaliwa usimfanye apatwe na kiburi, alitiwa mwiba mwilini, ugonjwa uletao aibu na kusulubu mwili ili kuponya roho… Jinsi mkosefu anavyopaswa kutetemeka, mtume mkubwa kama huyo, chombo kiteule, asipojiamini! Mara tatu alimsihi kwa nguvu Bwana amuondolee mwiba huo; mara tatu, yaani mara nyingi na kwa udumifu. Hapo akasikia maneno yafuatayo: ‘Neema yangu yakutosha’, yenyewe itakukinga na dhambi. Uweza wa Mungu unaoonekana wazi katika udhaifu, ambao ni nafasi ya kutekeleza maadili ya unyenyekevu, subira na kujikana. Mtu akifahamu udhaifu wake anakuwa macho zaidi katika mashindano, na kwa hayo anaimarika. Basi, alisema mtakatifu Paulo, ‘nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi’, kwa sababu hivyo ninakuwa mnyenyekevu zaidi, na kupaswa kushindana ‘ili uweza wa Kristo ukae juu yangu’ na kuzaa matunda yake”.
Kinachowezesha kuoanisha unyenyekevu na moyo mkuu ni kwamba, “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7). “Kuhusu kujitathmini, daima mtu anatakiwa kuwa kama aliyefunga safari na kulenga makubwa zaidi, ‘Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la!’ (Fil 3:12)… Na daima mtu anatakiwa kujitahidi kufikia ukamilifu, ‘Nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele’ (Fil 3:13)” (Thoma wa Akwino).
Basi, kwa watakatifu unyenyekevu na moyo mkuu vinapatana: wanalenga makuu kupitia majaribu na aibu. Hata hivyo inabaki tofauti isiyopimika kati yao na Mwokozi ambaye hawezi kutenda dhambi bali ana ukuu wa kifalme. Kwa kiasi chake, ndivyo ilivyo kwa bikira Maria anayesadiki na Wakristo wengi kuwa alikingiwa dhambi yoyote. Katika wimbo wake anajitokeza kwa pamoja mnyenyekevu na mkuu ajabu: “Ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa; kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu… amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza” (Lk 1:48-49,52). Kitu hicho kinatokea tena katika maisha ya Kanisa ambapo yanatimia daima maneno yafuatayo: “Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Lk 14:11; 18:14). Katika dhuluma, Kanisa linaonekana kushindwa, kumbe linashinda; kwa unyenyekevu linalenga daima makuu mawili: utukufu wa Mungu na wokovu wa watu. Kitu cha namna hiyo kinatakiwa kumtokea kila Mkristo, hasa mtawa. Anapaswa kuwa mnyenyekevu kama mzizi uliofichika ardhini, na kulenga daima makuu, yaani imani hai zaidi, tumaini imara zaidi, upendo motomoto zaidi, muungano na Mungu ulio wa dhati na safi zaidi kila siku. Hivyo yanakuja kuoana yale yanayoonekana kupingana, kama mzizi mrefu wa mti (unaomaanisha unyenyekevu) unavyopenya zaidi na zaidi ardhini, maadamu tawi la juu (linalomaanisha upendo) linazidi kuelekea mbinguni. Polepole uzima wa Yesu unadhihirika “katika miili yetu ipatikanayo na mauti” (2Kor 4:11). Hakuna unyenyekevu halisi mbali na ule anaotujalia tukimuomba kwa moyo tufanane naye na tukikubali kufuata njia inayotufikisha huko.
Katika Kanisa Katoliki
[hariri | hariri chanzo]Agostino wa Hippo alisisitiza umuhimu wa adili hilo katika kusoma na kufundisha Biblia, akitumia mifano ya Mtume Paulo katika 1Kor 4:7 na wa Towashi Mwethiopia katika Mdo 8 (De Doctrina Christiana, prooem. 4-8). Kwa kuwa msomaji na mwalimu vilevile wanapaswa kukumbuka Biblia ni Neno la Mungu, si mali yao, la sivyo watashindwa kuielewa. (De Doctrina Christiana, 2.41.62).[3]
Bernardo wa Clairvaux alifafanua unyenyekevu kuwa: "Adili ambalo mtu, akijifahamu alivyo kweli, anajishusha. Yesu Kristo ndiyo ufafanuzi bora wa unyenyekevu."[4]
Kwa kumfuata Thoma wa Akwino, Wakatoliki wanahusianisha unyenyekevu na adili bawaba la kiasi[4][5], kwa sababu hilo linazuia maelekeo yote yasiyoratibiwa.[4]
Tunapozungumzia maadili ya kiutu yanayohusiana zaidi na maisha ya kuungana na Mungu, tunapaswa kuzingatia unyenyekevu unavyotakiwa kuwa. Tukimfuata Yesu kama kielelezo, umuhimu wa adili hilo na umbile lake vinaonyesha wazi umbali uliopo kati ya maadili yanayofundishwa na wanafalsafa na yale ya Injili. Katika mapokeo yote ya Kikristo unyenyekevu umetazamwa kuwa msingi wa maisha ya Kiroho, ambao unatakiwa kuchimbwa kwa kina kadiri jengo linavyokusudiwa kwenda juu. Unyenyekevu unaangamiza aina zote za kiburi, lakini tendo lake maalumu na kuu si hilo, kwa kuwa Bwana Yesu na bikira Maria hawakupaswa kupinga kiburi ndani mwao, lakini waliutimiza unyenyekevu na bado wanautimiza kwa namna bora. Basi, tendo hilo la kumnyenyekea kwanza Mungu, halafu jirani ni lipi?
Unyenyekevu kwa Mungu
[hariri | hariri chanzo]Tendo maalumu la unyenyekevu ni kuinama, kujishusha mbele ya Mungu na mbele ya yale yote yaliyo ya Mungu ndani ya kiumbe chochote. Kumnyenyekea ni kutambua kimatendo, si kinadharia tu, udogo wetu ulio wazi hata mbali na makosa; baada ya dhambi ni kutambua unyonge wetu pia.
Unyenyekevu unaungana na utiifu na ibada, ila unatofautiana navyo. Utiifu unahusu mamlaka ya Mungu na amri zake; ibada inahusu ukuu wake na heshima tunayopaswa kumpatia; kumbe unyenyekevu unakiri udogo na unyonge wetu kwa kutuinamisha ardhini na hivyo kuutukuza ukuu wa Mungu, kama malaika Mikaeli (kwa Kiyahudi, “Nani kama Mungu?”). Anayeishi Kiroho anajisikia furaha takatifu anapojishusha ili kukiri kwa matendo kuwa Mungu peke yake ni mkuu na kuwa ukuu wowote wa kibinadamu ni uongo mtupu ukilinganishwa na wa kwake.
Msingi wa unyenyekevu huo ni ukweli, hasa kwamba umbali kati ya Muumba na kiumbe hauna kiasi. Sisi ni wanyenyekevu kadiri tunavyotambua umbali huo usiopimika hata tukiwa juu namna gani. Kadiri tunavyopanda kwa Mungu, ukweli huo unazidi kuwa wazi kwetu. Hivyo aliyepanda juu zaidi ni mnyenyekevu zaidi kwa sababu ana mwanga mkubwa zaidi: bikira Maria ni mnyenyekevu kuliko watakatifu wote, tena Yesu ni mnyenyekevu kuliko Mama yake.
Tunaona unyenyekevu unavyolingana na maadili ya Kimungu tukizingatia kweli zake za msingi ambazo wanafalsafa wa kale hawakuzijua. Kwanza, uumbaji kutoka utovu wa vyote, ulio msingi wa unyenyekevu kadiri ya akili nyofu kwa kuwa unaweza kujulikana kwa juhudi za umbile letu. Pili, fumbo la neema na la haja ya msaada wa Mungu ili kutenda hata tendo dogo la kuletea wokovu; fumbo hilo linapita uwezo wa akili na kujulikana na imani tu.
Yatokanayo ni mambo manne kumhusu Muumba, kuhusu maongozi yake na kuhusu wema wake ambao ni chemchemi ya neema tena unaondolea dhambi.
Kwanza, kumhusu Muumba tunapaswa kukiri si kinadharia tu, bali kimatendo kuwa sisi peke yetu si kitu: “Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako. Kila binadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili” (Zab 39:5). “Nawe una nini usichokipokea?” (1Kor 4:7). Tumeumbwa kutoka utovu wa vyote kwa hiari ya Mungu, ambaye asingetudumisha tungetoweka mara. Tena, baada ya kuumbwa, ingawa tuko wengi zaidi, hakuna ongezeko lolote la ukweli, la ukamilifu, la hekima na la upendo, kwa kuwa tangu milele sifa hizo za Mungu ni kamili pasipo mipaka. Basi, tukijilinganisha na Mungu, sisi hatuko. Tungetoa yaliyo ya Mungu katika matendo yetu bora kisingebaki chochote, kwa sababu si kwamba sehemu yake moja inatoka kwetu na sehemu nyingine kwa Mungu, bali tendo lote ni la Mungu kama asili ya kwanza, halafu lote ni la kwetu kama asili ya pili.
Pili, pasipo Mungu mratibu mkuu, pasipo maongozi yake yanayoendesha vyote, maisha yetu hayana dira. Tunapaswa kupokea toka kwake maongozi ya jumla ya amri zake ili kufikia uzima wa milele, na maongozi maalumu ambayo amemchagulia kila mmojawetu tangu milele na ambayo tunaonyeshwa na wakubwa wetu wanaomwakilisha, na mashauri tunayopaswa kuomba, na matukio na uvuvio wa Roho Mtakatifu. Tunapaswa kukubali nafasi aliyotupangia, hata ikiwa duni. Unyenyekevu huo una faida kwetu na kwa wengine pia. Mwokozi alikubali kwa unyenyekevu usio na kifani kushika nafasi ya mwisho, hata wakamuona Baraba kuwa bora kuliko yeye, akapokea aibu ya msalaba. Kwa hiyo katika jengo la Mungu amekuwa jiwe kuu la msingi. Ndio unyenyekevu halisi ambao unazaa ajabu na kutangaza utukufu wa Mungu hata palipofichika. Basi, tupokee maongozi maalumu anayotuelekeza, hata yakidai tujitoe sadaka ya kuteketezwa: “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; hushusha chini, tena huinua juu” (1Sam 2:6-7).
Halafu, tatu, katika maongozi hayo hatuwezi kupiga hatua hata ndogo wala kutenda lolote la kuletea wokovu tusipopewa neema za msaada. Tukiri kwa furaha, “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu watoka kwa Mungu” (2Kor 3:5). “Hawezi mtu kusema, ‘Yesu ni Bwana’, isipokuwa katika Roho Mtakatifu” (1Kor 12:3). Hasa tunahitaji neema ili kudumu waaminifu mpaka mwisho; tunapaswa kujiombea neema hiyo kwa unyenyekevu.
Nne, unyenyekevu huo, unaotakiwa kuwemo ndani ya waadilifu wote, ulikuwa sifa ya watu wa kwanza katika utakatifu asili. Lakini baada ya dhambi tunapaswa kukiri kimatendo unyonge wetu pia: umimi, moyo finyu, ugeugeu, hasira, ndoto za mchana, usahaulifu wa mambo muhimu, kiburi, tamaa, hata kutojali utukufu wa Mungu na wokovu wa watu. Unyonge huo ni mbaya kuliko utovu wa vyote, kwa kuwa unafuja roho zetu na kuzifanya zichukize. “Unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu… Nimekutenda dhambi wewe peke yako, na kufanya maovu mbele za macho yako” (Zab 51:2-4). “Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri” (Zab 19:12).
Unyenyekevu huo haupingani na moyo mkuu, bali unaunganika nao na kukua pamoja nao kama vidole vya mkono mmoja: hatuwezi kuwa na unyenyekevu wa dhati pasipo moyo mkuu. Mkristo anatakiwa kulenga makuu yanayostahili heshima kubwa, ingawa anaona heshima si kitu; ayalenge kwa unyenyekevu na, ikiwa lazima, kwa kudhalilishwa. Azoee kukariri, “Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, bali ulitukuze jina lako” (Zab 115:1). Asiye na moyo anakataa kufanya yale ambayo anaweza na kupaswa kuyafanya, na asipotimiza wajibu mkubwa anatenda dhambi ya mauti. Kinyume chake unyenyekevu unamuinamisha mtu mbele ya Aliye Juu, ashike nafasi yake halisi ili Mungu atende ndani yake pasipo kizuio. Mnyenyekevu anajitia mikononi mwa Mungu na, ikiwa Bwana anatenda makuu kwa njia yake, hajitukuzi kuliko shoka likitumiwa na mtemakuni, wala kinubi kikichezwa na mwanamuziki bora.
Unyenyekevu kwa jirani
[hariri | hariri chanzo]“Kila mmoja anapaswa kutambua kwamba katika yale yaliyo ya kwake tu, yeye ni duni kuliko yeyote katika yale aliyojaliwa na Mungu” (Thoma wa Akwino). Kwa kuwa kila mtu peke yake si kitu, aliyonayo ya kwake tu ni unyonge wa makosa yake; basi akiri kimatendo kuwa hayo ni duni kuliko yale yote ambayo mwingine yeyote amejaliwa na Mungu upande wa umbile na upande wa Kiroho.
“Mtu mnyenyekevu kweli anajiona duni kuliko wengine, si kwa matendo ya nje, bali kwa kuwa anaogopa kutenda kwa kiburi kilichofichika hata mema anayoyatenda” (Thoma wa Akwino). “Mfikirie kwamba wapo watu ambao pasipo kuonekana ni bora kuliko nyinyi, hata mkionekana waadilifu kuliko wao” (Augustino). Tukariri, ‘Hakuna dhambi iliyotendwa na mwingine nisiyoweza kuitenda mimi pia kwa udhaifu wangu: kama sijaitenda ni kwa sababu Mungu kwa huruma yake hajaacha itokee’. Tumtukuze na kumuomba, “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu” (Zab 51:10); “Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka” (Mao 5:21).
Kwa kuwa upendo wake ndio asili ya mema yote, watakatifu wanajiambia, “Mtu huyu angejaliwa neema nilizozipata mimi, labda angekuwa mwaminifu kuliko mimi; na kama Mungu angeacha nitende makosa aliyoacha ayatende huyu, sasa ningekuwa mahali pake”. Ndio msingi wa unyenyekevu ambao kiburi chochote kivunjike juu yake. Unyenyekevu wa watakatifu unazidi kuwa wa dhati kadiri wanavyozidi kujua udhaifu wao mbele ya ukuu na wema wa Mungu. Tuulenge mfululizo unyenyekevu wao, lakini tusitumie maneno yao kabla hatujaamini ukweli wake; ungekuwa unyenyekevu bandia tu unaofanana na ule halisi kama kipande cha kioo na almasi.
Unyenyekevu kwa jirani si kuogopa watu wala kukosa moyo. Kuogopa watu ni kuogopa hukumu na hasira za waovu: hofu hiyo inasogeza mbali na Mungu. Utovu wa moyo unakwepa kazi ya lazima, na kuelekea mambo ya chini badala ya makuu yanayotupasa. Kumbe, unyenyekevu unatuinamisha mbele ya Mungu na mbele ya yaliyo yake katika jirani. Mnyenyekevu hauinamii kamwe uwezo wa waovu, tofauti na mwenye uchu wa madaraka, anayejishusha kupita kiasi ili afikie matamanio yake.
Unyenyekevu haukwepi makuu; kinyume chake unaimarisha moyo mkuu uyalenge hata kwa njia duni. Bwana ametuonyesha vizuri ajabu maadili hayo mawili yanavyotegemezana akisema (Math 20:28), “… kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia” (ndio unyenyekevu) “na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (ndiyo ari ya moyo mkuu). Mwokozi asingeweza kulenga mambo makuu zaidi wala kuyalenga kwa unyenyekevu mkubwa zaidi: alipania kutupatia uzima wa milele, lakini kupitia aibu na mateso ya msalaba. Maadili hayo yanayoonekana kupingana, yanaunganika ndani ya watakatifu pia ambao, kadiri walivyo wanyenyekevu, wana nguvu, wasijali binadamu hata wakitishwa namna gani.
Kiutekelezaji, ili tuufikie unyenyekevu kamili (ambao, tusipokuwa nao, hatuwezi kuwa na upendo kamili) tunapaswa kusimama vema kuhusu sifa na lawama. Kwanza, kuhusu sifa, tusijisifu kamwe, la sivyo tutajichafua tu; wanajisifu wale wanaodhani hawasifiwi vya kutosha na wengine. Halafu tusijitafutie sifa, la sivyo tutakuwa kiroja na kupoteza stahili za matendo mema. Hatimaye tusifurahie sifa tukizipata, la sivyo tutapoteza walau ua la stahili hizo.
Lakini ni lazima tupande juu zaidi kwa kusimama vema kuhusu lawama. Tunapaswa kupokea kwa subira lawama tunazostahili, hasa zikitoka kwa wakubwa wenye haki na wajibu wa kuzitoa: tukikunja uso tutapoteza faida ya maonyo hayo. Pengine tunapaswa kupokea kwa subira hata lawama ambazo hatustahili au kidogo tu. Hatimaye, kwa mfano wa watakatifu, inafaa tujiombee upendo kwa dharau.
Anselm wa Canterbury aliorodhesha vizuri vidato vya unyenyekevu: 1) kujua kwamba tunastahili dharau katika mengi; 2) kufurahia kuwa hivyo; 3) kukiri kuwa hivyo; 4) kutaka jirani asadiki hivyo; 5) kupokea kwa subira kusemwa hivyo; 6) kukubali kutendwa kama mtu anayestahili dharau; 7) kupenda kutendwa hivyo. Vidato vya mwisho vinadai kwanza sala ya kumiminiwa kuhusu unyenyekevu wa Bwana, aliyesulubiwa kwa ajili yetu, na hamu kubwa ya kufanana naye. Ni vema tulenge ukamilifu huo, lakini si wengi wanaoufikia; kabla ya hapo tuna nafasi nyingi za kukumbuka maneno ambayo Yesu ametuhimiza tumuige iwezekanavyo, “Mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu, na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu, na awe mtumwa wenu…” (Math 20:26-27).
Unyenyekevu wa kishujaa
[hariri | hariri chanzo]Unyenyekevu ni wa kishujaa unapofikia ngazi za juu zilizofafanuliwa na Anselm wa Canterbury, yaani si tu kutambua tunastahili dharau pande fulanifulani, bali kutaka watu wasadiki hivyo, kuvumilia waseme hivyo, kupokea dharau zao na hatimaye kupenda tutendwe hivyo, ili tulingane na Bwana aliyechagua kupatwa na aibu kuu za mateso kwa wokovu wetu.
Unyenyekevu huo unadhihirishwa na utaratibu mkubwa wa kudumu: “Kila mtu atatambulikana kwa uso wake; mwenye ufahamu atajulikana kwa sura yake popote umkutapo, nazo nguo za mtu, na finyo la kutoa meno, na mwendo wake, huonyesha mara alivyo yeye mwenyewe” (YbS 19:29-30). Uso mtulivu, mnyenyekevu, usiocheka mno, pamoja na mwendo mzito, mnyofu, usio na unafiki, vinashuhudia kuwa mtu anajisikia daima mbele ya Mungu na kuongea naye kwa ndani. Hivyo aliye mnyenyekevu na mtaratibu kweli anasema juu ya Mungu hata kwa mwenendo wake na kwa kimya chake.
Unyenyekevu wa kishujaa unaendana na kiasi hichohicho cha upole. Kwa njia ya adili hilo mtu anafikia kujitawala kikamilifu, hata kushinda ubaya kwa wema badala ya kuupinga kwa hasira. Ngazi za juu za upole ni kutofadhaishwa na matusi, kufurahia kitakatifu matokeo bora yanayotokana nayo, na hatimaye kumhurumia mtukanaji kwa matokeo mabaya yanayoweza kumpata. Ndivyo Yesu alivyolia juu ya Yerusalemu kwa kuwa ulikosa shukrani; alisikitikia maangamizi ya mji huo kuliko kifo kikatili kitakachompata.
Ndani ya mtu aliyekamilika unyenyekevu na upole vinaendana na maadili ya nguvu na moyo mkuu ambayo yanaonekana kuwa kinyume chake, kumbe yanakamilishana navyo.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Humble" from Merriam-Webster, m-w.com
- ↑ Humility, The Protestant theological and ecclesiastical encyclopedia, Herzog et al (Editors), Vol 2, 1860, pp 598-599
- ↑ Woo, B. Hoon (2013). "Augustine's Hermeneutics and Homiletics in De doctrina christiana". Journal of Christian Philosophy. 17: 99–103.
- ↑ 4.0 4.1 4.2 Catholic Encyclopedia, "Humilty", newadvent.org
- ↑ Humility, The Catholic encyclopedia, Herbermann et al. (Editors), Vol 7, 1910, pp 543-544
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Humility: The Beauty of Holiness, by Andrew Murray.
- Al-Munajjid, Sheikh Muhammad Saleh. Islam Q&A Website. "Different kinds of humility".
- Sister Huda. 19 November 1998. About.com Website."Humility" Ilihifadhiwa 7 Oktoba 2008 kwenye Wayback Machine., Islam.about.com. Retrieved April 5, 2006.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Catholic Encyclopedia, newadvent.org
- Judaism's take on humility (Chabad.org)
- World scripture: Quotes from religious texts about humility, unification.net
- I'm glad that I'm a nobody: A positive psychology of humility Ilihifadhiwa 4 Januari 2007 kwenye Wayback Machine., meaning.ca
- Catholic Encyclopedia, newadvent.org
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |