Kanisa Katoliki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Wakatoliki)
Rukia: urambazaji, tafuta
Papa Fransisko akiendesha Misa ya kuanzia rasmi huduma yake kama askofu wa Roma na mkuu wa Kanisa Katoliki duniani kote, tarehe 19 Machi 2013.
Hii ni sehemu ya mfululizo kuhusu
Kanisa Katoliki
StPetersBasilicaEarlyMorning.jpg
Imani

Umoja wa Mungu
Utatu (Baba, Mwana, Roho Mtakatifu)
Umwilisho Maisha ya Yesu
Msalaba Ufufuko Kupaa
Historia ya Wokovu Ufunuo
Biblia Mapokeo Ualimu Dogma
Neema Dhambi Wokovu Sakramenti
Watakatifu Bikira Maria

Muundo

Papa: Fransisko
Urika wa maaskofu Mitaguso mikuu
Kundi la Makardinali
Kanisa la Kilatini
Makanisa Katoliki ya Mashariki

Historia

Historia Ukristo
Ukatoliki Mlolongo wa Kitume
Sifa nne za Kanisa Utetezi Ekumeni
Maisha ya kiroho Amri Kumi Utawa
Sala Falsafa Teolojia
Muziki Sanaa Sayansi

Ibada

Liturujia Mwaka wa Kanisa
Ekaristi Liturujia ya Vipindi

Mapokeo ya liturujia

Liturujia ya Kilatini (Roma Trento Milano Toledo Braga Lyon Canterbury)
Liturujia ya Armenia Liturujia ya Misri
Liturujia ya Ugiriki Liturujia ya Antiokia
Liturujia ya Mesopotamia

Kanisa Katoliki ni jina linalotumika hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa urika wa maaskofu juu yake lote.

Ndilo kubwa kabisa kati ya madhehebu yote ya dini hiyo, likikusanya nusu ya wafuasi wote wa Yesu.

Hata hivyo, Wakristo wa madhehebu mengine wanaokubali kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli wanatafsiri tofauti sehemu inayokiri Kanisa la kweli kutambulishwa na sifa nne, ya tatu ikiwa kwamba ni katoliki: "Tunasadiki Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume".

Kanisa Katoliki, likiwa na miaka karibu elfu mbili, ni kati ya miundo ya zamani zaidi iliyopo duniani na imechangia kwa kiasi kikubwa ustaarabu wa Magharibi, ingawa tangu mwishoni mwa Karne za Kati athari yake inazidi kupungua, ilivyo wazi leo hasa katika masuala yanayohusu jinsia na uzazi.

Imani ya Kanisa hilo inatokana na ufunuo wa Mungu ulivyotolewa kwa Israeli na ulivyokamilishwa na Yesu ambaye alimtambulisha kama Baba na alilianzisha kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetumwa naye juu ya Mitume wake siku ya Pentekoste mwaka 30 (au 33) BK.

Ni imani inayoungamwa katika ubatizo, sakramenti ya kwanza na mlango wa sakramenti nyingine sita: kwamba Mungu ni mmoja tu katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Imani hiyo inatakiwa kutekelezwa katika maadili maalumu yanayotegemea hasa upendo ambao ndio adili kuu na uhai wa mengine yote.

Kutokana na juhudi za kutekeleza matendo ya huruma kwa yeyote mwenye shida, Kanisa Katoliki linatoa huduma za elimu na afya kuliko taasisi nyingine yoyote duniani kote.

Kama vielelezo vya utakatifu ambao waamini wote wanaitiwa, Kanisa linapendekeza watu wa Agano la Kale na wa Agano Jipya, hasa Bikira Maria, lakini pia wale waliojitokeza zaidi katika historia yake kama watakatifu.

Baadhi yao wana wafuasi wengi wanaounda familia za kiroho, mara nyingi kama mashirika ya kitawa yenye karama mbalimbali.

Maana ya jina[hariri | hariri chanzo]

Neno "katoliki" linatokana na kivumishi cha Kigiriki καθολικός (katholikòs), lenye maana ya «kamili, kadiri ya utimilifu», kinyume cha «vipandevipande».

Tunalikuta kwa mara ya kwanza katika maandishi ya Ignas wa Antiokia kwa Wakristo wa Smirna mwanzoni mwa karne II: «Alipo Yesu Kristo ndipo lilipo Kanisa Katoliki» (Ad Smyrnaeos, 8).

Ndivyo alivyolitofautisha na makundi madogomadogo yaliyokuwa yameanza kujitenga nalo.

Imani yake kuhusu fumbo lake kama ushirika[hariri | hariri chanzo]

Kanisa hilo linaamini kuwa ndani yake linadumu moja kwa moja Kanisa pekee lililoanzishwa na Yesu Kristo ambalo wanaunganishwa nalo wale wote wanaobatizwa katika madhehebu yoyote.

Tofauti kati yao ni kwamba baadhi (Wakatoliki) wana ushirika kamili nalo, wakati wengine (hasa Waorthodoksi, Waorthodoksi wa Mashariki na Waprotestanti) wana ushirika nalo kwa viwango mbalimbali, kadiri wanavyokubali mafundisho, sakramenti na uongozi wake.

Hatimaye, Kanisa hilo linaamini kuwa wale wote wasiobatizwa wanaitwa na Mungu kufanya hivyo na kujiunga nalo ili wafikie wokovu ulioletwa na Yesu Kristo.

Uenezi wake[hariri | hariri chanzo]

Asilimia ya Wakatoliki waliobatizwa kati ya wakazi wa kila nchi.

Kati ya madhehebu ya Kikristo, Kanisa Katoliki linakusanya waamini 1,290,000,000, yaani nusu ya wafuasi wote wa Yesu, na 17.7 % ya binadamu wote, likiwa na asilimia kubwa ya waamini kati ya wananchi wa Amerika (63.7%) na Ulaya (39.9%).

Hata hivyo Wakatoliki kwa muda mrefu sasa wanaongezeka hasa katika mabara ya Afrika na Asia.


Miundo yake[hariri | hariri chanzo]

Kanisa Katoliki linaishi katika majimbo 2,989, ambayo kwa kawaida yanaongozwa na Maaskofu (kwa jumla wako 5,173) wakisaidiwa na mapadri (415,348) na mashemasi, ambao baadhi yao wanajiandaa kupata upadrisho na zaidi ya 43,000 ni wa kudumu.

Kati ya majimbo hayo, mengi yanafuata taratibu za Kanisa la Kilatini, ila kuna mengine yanayofuata taratibu za Makanisa Katoliki ya Mashariki. Ni kwamba, tukitaka kutumia maneno kikamilifu tunapaswa kujua kwamba Kanisa la Kiroma si lile lote lililo chini ya Papa, bali lile tu linalofuata mapokeo ya Roma kuanzia ibada zake zinazotegemea lugha ya Kilatini. Kumbe yapo mengine (kama Kanisa Katoliki la Kiethiopia) ambayo hukubali pia uongozi wa Papa ila hufuata mapokeo ya Kiorthodoksi.

Asili ya makanisa hayo ni katika majaribio ya kuunganisha tena Makanisa ya Kiorthodoksi na lile la Roma; kwa kawaida majaribio hayo hayakufaulu, ila yalivuta maaskofu na Wakristo wachache. Maaskofu hao pengine walipewa na Papa cheo cha Patriarki (wa Aleksandria, wa Antiokia n.k.) kwa kushindana na Mapatriarki wa Makanisa ya kale. Lakini zipo nchi kadhaa ambako Wakristo wengi wa mapokeo ya Kiorthodoksi hufuata uongozi wa Papa kama kule Lebanon, Iraq na wengi kidogo katika nchi ya Ukraina.

Katika nchi kadhaa Makanisa mbalimbali ya Kikatoliki yanaishi kandokando, kwa mfano Misri kuna Kanisa Katoliki la Wakopti, Kanisa Katoliki la Kimelkiti, Kanisa Katoliki la Armenia, Kanisa Katoliki la Wakaldayo na la Kilatini. Mapadri (lakini si maaskofu) Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, ya Kigiriki, ya Kiarmenia na ya Kikaldayo wanaweza kuwa na ndoa na huendesha Misa katika taratibu zao za kale; kumbe mapadri Walatini hawawezi kuwa na ndoa na hufuata liturujia ya Roma.

Wote hao hukubali uongozi wa Papa bila kushindana, yaani wengine wanahudumia Wakatoliki wa mapokeo ya Kikopti, wengine wale wa mapokeo ya Kigiriki, wengine wale wa mapokeo ya Kiarmenia, wengine wale wa mapokeo ya Kikaldayo na wengine wale wa mapokeo ya Kiroma, hasa wahamiaji kutoka nchi nyingine.

Majimbo yote yanagawanyika katika parokia zinazoongozwa na padri anayeitwa paroko.

Kati ya waamini, ambao wengi kabisa kati yao ni wale wa kawaida wanaoitwa walei, wana nafasi ya pekee wamonaki na watawa wengine ambao wanaishi kwa mitindo mbalimbali iliyostawi katika historia ya Kanisa ili kumfuata Yesu kwa karibu zaidi katika useja mtakatifu, ufukara na utiifu, kadiri ya karama maalumu. Masista ni 693.575 hivi na mabruda zaidi ya 55,000.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Catechism of the Catholic Church. Libreria Editrice Vaticana (1994). Iliwekwa mnamo 1 May 2011.
  • Bunson, Matthew (2008). Our Sunday Visitor's Catholic Almanac. Our Sunday Visitor Publishing. ISBN 1-59276-441-X.
  • Gale Group. (2002) New Catholic Encyclopedia, 15 vol, with annual supplements; highly detailed coverage
  • Papa Yohane Paulo II, (2006) He Gave Them the Law of Life as Their Inheritance, in:Man and Woman He created Them. A Theology of the Body, transl. M. Waldstein, Boston: Pauline Books and Media, pp. 617–663 ISBN 0-8198-7421-3
  • Smith, Janet, ed. (1993) Why "Humanae Vitae" Was Right, San Francisco: Ignatius Press.
  • Smith, Janet (1991) "Humanae Vitae", a Generation Later, Washington D.C.: Catholic University of America Press,
  • Stewart, Cynthia. (2008) The Catholic Church: A Brief Popular History 337 pages
  • Vatican, Central Statistics Office (2011). Annuario Pontificio (Pontifical Yearbook). Libreria Editrice Vaticana. ISBN 978-88-209-7908-9.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
ChristianitySymbol.PNG Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kanisa Katoliki kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.