Nenda kwa yaliyomo

Ufufuko wa Yesu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Piero della Francesca Ufufuko huko Sansepolcro (Italia).
Mfululizo wa kurasa juu ya Yesu
Yesu
Yesu Kristo na Ukristo

Umwilisho  • Utoto wa Yesu  • Ubatizo
Arusi ya Kana • Utume wa Yesu • Mifano ya Yesu  • Miujiza ya Yesu
Kugeuka sura • Karamu ya mwisho • Msalaba wa Yesu  • Maneno saba
Kifo cha Yesu  • Ufufuko wa Yesu
Kupaa mbinguni  • Ujio wa pili
Injili  • Majina ya Yesu katika Agano Jipya  • Yesu kadiri ya historia  • Tarehe za maisha ya Yesu • Kristolojia

Mazingira ya Yesu

Wayahudi • Kiaramu • Bikira Maria • Yosefu (mume wa Maria) • Familia takatifu • Ukoo wa Yesu • Ndugu wa Yesu • Yohane Mbatizaji

Mitazamo juu ya Yesu

Mitazamo katika Agano Jipya · Mitazamo ya Kikristo • Mitazamo ya Kiyahudi • Mitazamo ya Kiislamu • Yesu katika sanaa

Ufufuko wa Yesu ndio tukio kuu lililotangazwa daima na Kanisa lake lote kuhusu mwanzilishi wake, Yesu Kristo, kuanzia ushuhuda wa Mitume wa Yesu na maandiko ya Agano Jipya, hususan Injili, hadi leo.

Kadiri ya imani hiyo, siku ya tatu baada ya kuuawa msalabani Ijumaa kuu, Yesu alifufuka mtukufu akiacha kaburi lake na vitambaa vyote vilivyotumika kumzikia.

Tangu Jumapili hiyo na kwa muda wa siku arubaini (kadiri ya Matendo ya Mitume 1:3), yeye aliendelea kuwatokea mara kadhaa wanafunzi wake, hadi alipoonekana nao akipaa mbinguni huku akiwabariki.

Tukio hilo linaadhimishwa kila mwaka kwenye Pasaka ya Kikristo na kila wiki kwenye Dominika.

Kwa Wakristo, ufufuko wa Yesu ndiyo sababu na kielelezo cha ufufuko wa waadilifu wote siku ya kiyama.

Mahali na tarehe

[hariri | hariri chanzo]
Sehemu ya kikanisa kilichomo ndani ya Kanisa la Kaburi na Ufufuo wa Yesu mjini Yerusalemu, ambalo kadiri ya mapokeo ya Ukristo limejengwa palipokuwa na pango alimozikwa Yesu Kristo. Upande wa kulia panaonekana mahali alipolazwa.

Kadiri ya Injili, kaburi la Yesu lilikuwa karibu na Golgotha-Kalivari, nje kidogo ya ngome ya Yerusalemu.

Injili hazitaji tarehe wala mwaka wa tukio hilo. Wataalamu wengi, kwa kulinganisha habari zake na za vyanzo vingine vya historia ya Dola la Roma na vya dini ya Uyahudi, wanakadiria siku hiyo kuwa tarehe 9 Aprili mwaka 30.

Habari katika Injili ya Marko

[hariri | hariri chanzo]

16:1 Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka. 2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza; 3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi? 4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.

5 Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu. 6 Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka. 7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia. 8Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa.

9 Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. 10 Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. 11 Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki.

12 Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. 13 Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.

14 Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. 15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. 16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. 17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; 18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

19 Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. 20 Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.

Maelezo ya teolojia

[hariri | hariri chanzo]

Yesu alipokufa, nafsi yake ya Kimungu iliendelea kushikamana na roho na mwili vilivyotengana: kwa hiyo mwili wake uliozikwa haukuweza kuoza kaburini; roho yake ilishukia kuzimu kuwatoa waadilifu waliomtangulia awaingize pamoja naye mbinguni. “Mwili wake aliuawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri” (1Pet 3:19). “Roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu” (Mdo 2:31).

Siku ya tatu roho ya Yesu ilirudi mwilini mwake na kudhihirisha utukufu wa ufufuko. Tangu mwanzo Wakristo wanakiri kwa ufupi “ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko” (1Kor 15:4).

Ufufuko wa Yesu siku ya Jumapili ulishuhudiwa na malaika waliowaambia wanawake waliofika kaburini: “Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka” (Lk 24:5-6). Halafu Maria Magdalena, Petro na Mitume wenzake, hata watu zaidi ya mia tano walimuona na kumsikia, walimgusa na kula pamoja naye.

Yesu hakurudia maisha ya duniani: tofauti na watu aliowafufua warudie maisha haya, Yesu mfufuka ameshaingia utukufu wa milele: “amekwenda zake mbinguni” (1Pet 3:22), “hafi tena” (Rom 6:9), ana “funguo za mauti, na za kuzimu” (Ufu 1:18).

Ufufuko wa Yesu ni muhimu kwetu pia, kwa sababu kwa njia yake tu tunatiwa uzima: sasa rohoni kwa kuondolewa dhambi, na siku ya mwisho mwilini pia kwa kufufuliwa. Mwenyewe alisema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele” (Yoh 11:25-26). “Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu” (1Kor 15:20-21). “Alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuka ili tupate kuhesabiwa haki” (Rom 4:25).

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ufufuko wa Yesu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.