Dhambi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Dhambi ni kosa la kiumbe mwenye hiari dhidi ya uadilifu unaompasa.

Inaweza kufanyika kwa mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu.

Maadili yanamuelekeza binadamu katika kutambua dhambi ni zipi pamoja na madhara yake.

Kwa kawaida dini zinahusianisha kosa hilo na Mungu aliye asili ya uadilifu, kwa kuwa ndiye aliyeumba viumbe vyote na kuvielekeza maishani.

Akiwapa baadhi ya viumbehai akili na utashi, papo hapo Mungu amewapa wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika utaratibu wa nafsi yao na wa ulimwengu wote.

Katika dini zinazofundisha kwamba Mungu alitoa ufunuo wake hata kwa njia ipitayo maumbile, ni dhambi kwenda kinyume cha ufunuo huo, kwa mfano unavyopatikana katika vitabu vitakatifu vya dini husika, kama vile Biblia kwa Wayahudi na Wakristo na Kurani kwa Waislamu.

Kutokana na uenezi wa dhambi kuanzia dhambi ya asili, linajitokeza suala la wokovu, ambalo linaweza kutazamwa zaidi kama neema, lakini kwa kawaida linadai toba ya mkosefu.