Nenda kwa yaliyomo

Kamusi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kamusi za Kiswahili
Kamusi ya Kiswahili-Kiswahili (kamusi wahidiya)
Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza (kamusi thania)

Kamusi (kutoka neno la Kiarabu قاموس qamus) ni kitabu ambacho kinaorodhesha maneno ya lugha yaliyokusanywa kutoka kwa watumiaji wa lugha fulani, kwa mfano lugha ya Kiswahili.

Maneno hupangwa kwa mtindo wa alfabeti, hutoa maana, asili na ufafanuzi wa utumizi wa maneno na jinsi yanavyotumika au yanavyotamkwa.[1]

Aina za kamusi

Kuna aina mbalimbali za kamusi ambazo ni:

 1. Kamusi wahidiya yaani ya lugha moja ambako maneno yanapangwa na kuelezwa kwa lugha ileile (mfano: Kiswahili-Kiswahili)
 2. Kamusi thania yaani ya lugha mbili ambako maneno ya lugha moja yanaorodheshwa halafu maana huonyeshwa kwa lugha tofauti, mfani ni Kiswahili-Kiingereza, au Kiingereza-Kiswahili
 3. Kamusi elezo (ing. encyclopedia) inayolenga kukusanya maelezo ya mambo ambayo yanatajwa kwa maneno. Wikipedia ni kamusi elezo ya kwanza kwa Kiswahili.

Historia ya kamusi

Utungaji wa kamusi ulianza katika jamii zilizojua kusoma na kuandika. Kamusi ilihitajika ili imsaidie mtumiaji kufahamu maana za maneno. Kamusi zilianza kutungwa ili kukidhi haja ya kutaka kupata maana za maneno. Jamii isiyojua kusoma na kuandika hususani ile ambayo haikuingiliana na watu wa jamii nyingine yenye utamaduni tofauti, haikuhitaji kamusi kwani kila mwanajamii alifahamu msamiati wote uliohitajika kwa mawasiliano. Kwa hali hii ni dhahiri kuna haja ya kamusi iliyochochewa na kuongezeka kwa msamiati kutokana na kupanuka kwa matumizi ya lugha.

Matumizi ya lugha yalipanuka ili kutosheleza haja ya kueleza na kufafanua dhana mpya zilizotokana na kukua na kubuniwa kwa maarifa mapya yalijidhihirisha katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia. Utungwaji wa kamusi ulianza bila kuwa na misingi ya kuifanya kazi au msingi na kanuni za kutunga kamusi zilizuka na kubuniwa kadiri kamusi za aina mbalimbali zilivyotungwa.

Kamusi ya mwanzo kutungwa ilikuwa ya lugha mbili yaani kamusi ya thaniya na kisha kamusi ya lugha moja yaani kamusi walidiya. Matini ya mwanzo ambayo ni kamusi ya kwanza ilikuwa ya Kisumeri au Kiakadi. Hizi zilikuwa ni lugha za Mesopotamia katika nchi ya Iraki ya leo. Wasumeri waliokuwa wakiishi Mesopotamia ya kusini walikuwa watu waliostaarabika sana baina ya miaka 4000-2000 kabla ya kuzaliwa Kristo. Waligundua manta anuwai hesabu, hifadhi ya nyaraka pia waligundua namna ya kuandika. Maarifa yao yaliandikwa katika matofali ya mfinyanzi ambayo huandikwa yakiwa bado mabichi. Baada ya utawala wao kuangushwa na Waakadia wa Mesopotamia (Iraki) kaskazini yapata miaka 2350 KK, Kisumeri kiliendelea kutumiwa na Waakadi kama lugha ya elimu. Waakadi walijifunza Kisumeri ili waweze kusoma katika taasisi za Wasumeri zilizofundisha taaluma mbalimbali ili kuwasaidia wanafunzi wa lugha ya Kisumeri, misamiati ya Kisumeri uliorodheshwa pamoja na visawe vyake katika lugha ya Kiakadi [2].

Kigiriki ni mojawapo ya lugha za Kihindi-Kiulaya inayotumiwa hasa nchini Ugiriki. Maandishi yake yamejulikana tangu miaka 3500 iliyopita. Hakuna lugha nyingine duniani inayozungumzwa hadi leo yenye historia ndefu kuliko hiyo, isipokuwa Kichina. Alfabeti ya Kigiriki ilianzishwa wakati wa ustaarabu wa Ugiriki wa leo. Alfabeti hiyo ni alfabeti mama ya lugha za Ulaya, kwa sababu ni asili ya alfabeti ya Kilatini ambayo ni mwandiko unaotumiwa zaidi leo duniani. Wagiriki waliongeza alama za vokali (kama a-e-i-o-u) na kubadilisha mwendo wa mwandiko kutoka kulia kwenda kushoto jinsi ilivyo hadi sasa katika mwandiko wa Kiarabu na wa Kiebrania ambazo ni lugha za Kisemiti jinsi ilivyokuwa Kifinisia.

Utungaji wa kamusi ulichochewa na haja ya kutaka kufasili maneno magumu yaliyokuwa katika lugha. Pia kamusi za Kigiriki zilikuwa zinahusu misamiati ambayo ilikuwa ikipatikana kwenye vitabu vyenye taaluma mbalimbali za wakati huo na pia maneno ya lugha za kigeni kwa Kigiriki. Pia misamiati katika dini iliandikwa ili watumiaji wa lugha ya kigiriki waweze kuelewa maana zake.

Kamusi za Kiswahili

Tazama pia makala kuu: Kamusi za Kiswahili

Kamusi za kwanza za Kiswahili zinazojulikana zilitungwa na wamisionari Wakristo katika karne ya 19. Wa kwanza alikuwa Ludwig Krapf, mmisionari Mjerumani aliyefika Mombasa kwa niaba ya Misioni Anglikana; alikamilisha muswada mnamo 1848 akaendelea kuifanyia kazi baada ya kurudi Ujerumani ikachapishwa mwaka 1882. Hii ilikuwa kamusi thaniya iliyoorodhesha istilahi za Kiswahili pamoja na tafsiri na maelezo kwa Kiingereza. Krapf alitumia mwandiko wa Kilatini kwa kuandika Kiswahili, lugha iliyowahi kuandikwa kwa mwandiko wa Kiaarabu hadi wakati ule.

Mnamo mwaka 1870 Askofu Edward Steere alitoa "Mwongozo wa Kiswahili cha Zanzibar" alipoeleza sarufi ya Kiswahili pamoja na kurasa 180 za faharasa ya maneno ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza. Mwanafunzi wake alikuwa A.C. Madan aliyekamilisha kazi ya Steere na kutunga kamusi za Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza.

Mnamo 1891 padre Mkatoliki Charles Sacleux alitunga kamusi ya Kiswahili-Kifaransa inayosifiwa kwa kuonyesha vizuri asili ya maeneno yaani etimolojia.

Katika karne ya 20 serikali za kikoloni zilifanya jitihada za kusanifisha Kiswahili; pamoja na kamusi za Wajerumani Carl Gotthilf Büttner na Carl Velten ni hasa jitihada za Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili chini ya Frederick Johnson iliyopanua kazi ya Madan na kutoa kamusi iliyotumiwa Kenya na Tanganyika.

Baada ya uhuru kazi hiyo iliendelezwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye pia katika mabaraza ya kitaifa ya Kiswahili Tanzania, Zanzibar na Kenya. Taasisi hizo zote zimetoa kamusi zao.

Muundo wa kamusi

Kimuundo kamusi imegawanyika katika sehemu kuu tatu:

 1. Utangulizi
 2. Matini
 3. Sherehe/hitimisho

1. Utangulizi wa kamusi

Hii ni sehemu ya kwanza ya kamusi, sehemu hii hujumuisha muhtasari wa sarufi ya lugha yenyewe pamoja na maelezo ya namna ya kutumia kamusi pia huonesha vifupisho mbalimbali.

2. Matini ya kamusi

Hii ni sehemu yenye vidahizo vyote vya kamusi husika, kuanzia alfabeti a-z vidahizo vyote huorodheshwa hapa na kufafanuliwa.

3. Sherehe ya kamusi

Ni taarifa zinazoingia mwishoni mwa kamusi.

Faida za kamusi

 • Kamusi hutusaidia kujua msamiati mpya.
 • Kamusi hutusaidia kujua aina za maneno, kwa mfano kitenzi.
 • Kamusi hutusaidia hata kwa wale watu ambao hawajui lugha, k.mf. Kiswahili.
 • Kamusi huelezea zaidi kuhusu maneno. Kwa mfano: tembo - kisawe chake ni ndovu.
 • Kamusi hutusaidia kujua lugha ya kigeni, kwa mfano Kifaransa
 • Kamusi hutusaidia kusoma hata kwa wale wasiojua kusoma, kwa sababu kamusi huwa na michoro au picha.

Dhima ya picha katika kamusi

Michoro (au picha) katika kamusi ina faida zifuatazo:

 • humvutia mtumiaji
 • husaidia wale wasiojua kusoma
 • husaidia kuelewa kwa undani zaidi maana ya neno

Marejeo

 1. Masuko Christopher Saluhaya, 2013. ISBN 978 9987 9581 1 5.
 2. (MCArthur, 1986)

Tazama pia

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kamusi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.