Nenda kwa yaliyomo

Serikali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nembo ya Taifa la Tanzania

Serikali (kutoka Kiajemi سرکاری, serkari, mamlaka) ni watu na taasisi ndani ya jamii hasa dola vyenye mamlaka ya kutawala na kufanya maazimio kwa wote katika eneo fulani.

Serikali inatunza na kutekeleza sheria, kanuni na miongozo na kuendesha shughuli muhimu za umma.

Shabaha kuu ya serikali ni kutunza amani na usalama wa raia katika jamii.

Mifumo mbalimbali ya serikali[hariri | hariri chanzo]

Serikali ya shirikisho au serikali kuu[hariri | hariri chanzo]

Kuna serikali za ngazi mbalimbali kwa mfano kwenye taifa, jimbo, mji na kijiji. Taratibu hutofautiana kati ya nchi na nchi. Katika mfumo wa shirikisho mamlaka ya serikali hugawiwa kwa kusudi kwenye ngazi mbalimbali hasa za taifa na jimbo.

Kinyume chake ni itikadi ya serikali kuu inayoweka mamlaka yote katika ngazi ya serikali kuu inayoweza kuamua kukabidhi sehemu ya madaraka yake kwa maeneo na vitengo vya kiutawala.

Serikali ya mtu mmoja au ya watu wengi[hariri | hariri chanzo]

Kati ya tofauti za kwanza katika mifumo ya serikali ni swali kama mtawala wa juu awe na madaraka yote au kama anapaswa kupewa mamlaka kwa muda tu tena kwa pamoja na watu wengine.

Udikteta na Ufalme mwenye mamlaka yote ni mifano ya serikali ya mtu mmoja asiyebanwa na mamlaka mengine.

Mahali pengi mfumo wa demokrasia umefaulu zaidi unaounda utawala juu ya uchaguzi wa raia wengi au wote na kukabidhi mamlaka kwa muda tu.

Hata hapa kuna tofauti kama katiba inampa mkuu wa serikali mamlaka mengi sana (kwa mfano mfumo wa Serikali ya kiraisi) au kama inagawa mamlaka zaidi kati ya watendaji na bunge (Serikali ya kibunge).

Tofauti kati ya jamhuri na serikali ya kifalme siku hizi si kubwa sana kwa sababu karibu wafalme wote hukubali Ufalme wa Kikatiba wakifuata katiba ya nchi.

Serikali katika mfumo wa mihimili ya utawala[hariri | hariri chanzo]

Zamani serikali ilikuwa jina kwa mamlaka yote ya dola. Siku hizi nadharia ya mgawanyo wa madaraka inaangaliwa zaidi.

Katika mfumo wa mgawanyo wa madaraka mamlaka hugawiwa kati ya mihimili mitatu ya utawala:

  • serikali au mamlaka ya utendaji inayotekeleza sheria
  • bunge au mamlaka ya kutunga sheria
  • mahakama au mamlaka ya kuamulia sheria