Nenda kwa yaliyomo

Haki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Maadili bawaba
Haki.
Haki ilivyoonyeshwa na Luca Giordano.
Bibi Haki, kielelezo cha adili hili, amechorwa kama mungu wa kike akiwa na vifaa vitatu: upanga, mizani na kitambaa machoni.[1]

Haki (kwa Kiingereza: justice, kutoka neno la Kilatini: justitia ambalo mzizi wake ni jus, haki, unaopatikana katika justus, mwenye kujali haki) ndiyo utaratibu unaotakiwa katika mafungamano yoyote kwa kuwa ni adili la msingi la utu linalotufanya tumpatie mwingine anachostahili..

Kwa Kigiriki inaitwa dikaiosyne, kutokana na neno asili dike yaani anayeelekeza na kwa hiyo pia mwongozo, utaratibu. Tofauti na nomos, yaani sheria inayoongoza wanyama pia, dike inahitajiwa na binadamu ili kuishi kwa utaratibu. Ni kinyume cha bie, ukatili, nguvu inayoangamiza. Dikaios (mwenye kujali haki), ni mtu anayemtendea kila mmoja haki yake. Dikaia zoe ni maisha ya kiutu yanayopingana na hybris (kiburi) na ushenzi.

Maana ya haki inatofautiana kwa kila utamaduni. Katika maana ya kwanza kabisa ambayo ilitafsiriwa na mwanafalsafa wa Ugiriki, Plato kwenye kazi yake Jamhuri[2]. Kutokana na historia dhana mbalimbali zimegunduliwa.

Katika dini

[hariri | hariri chanzo]

Katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu, haki, pamoja na huruma, ni sifa ya Mwenyezi Mungu[3]. Kadiri ya Biblia, Torati ilitolewa naye ili kuwashirikisha Waisraeli haki yake.

Katika Kanisa Katoliki

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya maadili bawaba manne, lile la haki mara nyingi halizingatiwi vya kutosha na wale wanaofuata maisha ya Kiroho: wanajali aina mbalimbali za kiasi, mpango wa busara katika maisha, na upendo kwa jirani, lakini pengine wanapuuzia madai kadhaa ya haki. Kumbe tukitekeleza aina zake mbalimbali, tutaunda utashi wetu kwa namna bora. Kwa kuwa adili la haki limo ndani ya utashi ili kuukomboa na umimi, kama vile busara imo ndani ya akili ili kuizuia isipime mambo kijuujuu, na kama vile nguvu na kiasi vimo katika hisi ili kuzikinga na hofu na tamaa zisizoratibiwa.

Utashi ukikosa maadili yanayotarajiwa kuwemo ndani yake una upungufu mkubwa; kinyume chake, ukiwa nayo una nguvu mara kumi zaidi. Humo zinatakiwa kupatikana aina nne za haki, na juu yake maadili ya ibada, tumaini na upendo. Ndivyo utashi na tabia vinavyoundwa ili Mkristo aonekane na kuwa kweli mwenye akili nyofu na hasa mtoto wa Mungu. Basi, tutasema juu ya aina mbalimbali za haki tunazozivunja namna nyingi tunaposahau kimatendo kwamba hatutakiwi kuwatendea wengine tusivyopenda kutendewa. Mara nyingi tunafikiria tu haki katika mabadilishano (aina ya chini inayoratibu mabadilishano), bila kuzingatia vya kutosha haki katika ugawaji (inayoratibu kazi ya viongozi ya kugawa faida na mizigo kulingana na stahili, hitaji na umuhimu wa kila mtu) na hasa aina ya juu ya haki inayolenga moja kwa moja ustawi wa jamii nzima kwa kutunga na kutekeleza sheria na maagizo mengine (ndiyo haki ya kisheria). Juu tena upo usawa, ambao unazingatia si maneno tu ya sheria, bali roho yake, tena si ya sheria za nchi tu, bali ya zile zote zinazoratibu mwenendo wa Mkristo. Tungezingatia aina hizo nne za haki zinazotupasa, tungekwepa mashindano mengi kati ya watu binafsi, matabaka na makundi mbalimbali yanayotakiwa kufanya kazi ileile moja chini ya Mungu.

Haki katika mabadilishano, haki katika ugawaji na maisha ya Kiroho

[hariri | hariri chanzo]

Tunatambua majukumu yetu kuhusu haki tukifikiria kasoro za kuepwa, kwa sababu uchungu unaotupata tukikosewa haki unatufanya tung’amue thamani yake. Basi, matendo dhidi ya haki katika mabadilishano ni uuaji, wizi, dhuluma, riba ipitayo kiasi, masingizio, shuhuda za uongo mahakamani, lakini pia matusi ya hasira, dharau, shutuma na lawama zisizo na msingi, masengenyo, minong’ono ya kutia shaka juu ya wengine, porojo zinazopunguza heshima wanazostahili, na usahaulifu wa kwamba jirani anahitaji sifa njema ili atende mema (kiasi kwamba waliokamilika wanapaswa kujitetea, si kwa ajili yao, bali kusudi waweze kuwatendea mema wengine). Ni ushujaa bandia kumcheka asiyeweza kujitetea au asiyekuwepo. Tukivunja haki katika mabadilishano kwa namna yoyote kati ya hizo, tunapaswa kurudisha au kufidia madhara tuliyosababisha.

Kasoro inayopingana na haki katika ugawaji ni ubaguzi. Ni halali kumpa mmoja kuliko mwingine, ila ni dhambi kufanya hivyo kwa kumnyima huyo wa pili kitu anachokistahili, k.mf. tukijali utajiri wa watu hata kuwanyima maskini heshima au misaada ya Kiroho wanayohitaji. Dhambi hiyo ni kubwa katika mambo ya roho kuliko katika malimwengu. Tuangalie upande huo tusije tukawakosea marafiki wa Mungu aliojichagulia kati ya watu duni. Pengine tunawakosea haki watumishi wake wavumilivu tukijua watastahimili yote wasilalamike. Kumbe ni wajibu, tuzo na furaha kuuhisi utakatifu unaotupitia karibu chini ya sura nyenyekevu.

Haki ya kisheria, usawa na kuunda tabia

[hariri | hariri chanzo]

Juu kuliko haki katika mabadilishano na katika ugawaji, ipo haki ya kisheria (au ya kijamii) ambayo haihusu tu haki za watu binafsi bali ustawi wa jamii (yaani nchi, Kanisa na makundi yaliyomo ndani yake); inaelekeza kujifunza na kushika kikamilifu sheria za jamii husika. Kwa Mkatoliki ni kujifunza pia miongozo ya Papa kuhusu masuala ya kisasa. Kutofanya hivyo ni kosa linaloleta madhara makubwa kwa wote. Haki ya kijamii inatufanya tuhisi na kujali ustawi wa jamii ikituondolea ubinafsi na kutuelekeza tujitahidi kwa faida ya wote, tukijikana na kujinyima muda, starehe na maridhisho kadiri inavyohitajika. Kwa kuwa jamii inatupatia mengi, tunapaswa kujitolea kwa ajili yake. La sivyo tunainyonya badala ya kuichangia iendelee. Kila jamii ina wanyonyaji wake ambao, kama baadhi ya vijidudu na vijimea, wanaweza wakasababisha hata kifo chake. Ili tushinde kilema hicho tunapaswa kutimiza wajibu wa kisheria, kujitolea kwa ustawi wa jamii, bila kusahau ulivyo muhimu kuliko ule wa binafsi. Upande huo, kupenda sheria za utawa na za Kanisa ni adili kubwa linalokinga dhidi ya vurugu nyingi. Kwa msingi huo mashirika ya kitawa yanastawi katika sala na utume; lakini kanuni ikipuuzwa, sala na utume vinadumaa. Ndiyo sababu Mungu alitokeza mara kadhaa watakatifu waliofufua juhudi za mwanzoni.

Hatimaye, juu ya haki ya kijamii upo usawa (kwa Kigiriki “epi dikaion” = juu ya haki) ambao hauzingatii tu maneno ya sheria, bali hasa lengo la yule aliyeitunga. Kwa kuwa unazingatia roho ya sheria, hauitafsiri vikali mno bali kwa akili ya juu, kwa namna ya pekee katika nafasi maalumu ambapo haifai kuitekeleza ilivyoandikwa isije ikatimia mithali ya Kilatini inayosema, “summum jus summa injuria” (= ukali wa sheria ni utovu mkubwa wa haki). Mtungasheria anazingatia yanayotokea kawaida, ingawa sheria anayoitunga haitaweza kutekelezwa na mtu fulani katika nafasi za pekee, ngumu na chungu. Kwa mfano, kitu kilichowekezwa kinatakiwa kurudishwa kwa mmiliki, lakini haifai tumrudishie tukijua atakitumia vibaya (kama vile silaha katika hasira). Usawa, unaotukinga na Ufarisayo, ndio aina ya haki iliyo bora na inayolingana zaidi na hekima. Haudharau sheria, ila unapima utekelezaji wake mmojawapo kwa kulenga juu kuliko maneno ya sheria, kwenye mahitaji halisi ya jamii na heshima anayostahili binadamu. Jambo hilo muhimu linakuja kueleweka tu baada ya kuishi miaka mingi. Basi, usawa unafanana na upendo ambao uko juu zaidi tena.

Haki na upendo

[hariri | hariri chanzo]

Kisha kujua ukuu wa haki na aina zake, tunaweza kuona wazi zaidi uhusiano wake na upendo unaotakiwa kuihuisha kutoka juu. Maadili hayo mawili yanaratibu mafungamano ya watu, ila yanatofautiana kwa kuwa haki inatudai tumpe kila mmoja anachostahili na tumuache atumie haki yake. Kumbe kwa upendo tunampenda Mungu kuliko yote, na kwa ajili yake tunampenda jirani kama nafsi yetu. Hivyo haki inamtazama jirani kama mtu mwingine, wakati upendo unamtazama kama mimi mwingine. Adili la haki linaheshimu stahili za mtu, kumbe upendo unatoa zaidi, kutokana na kumpenda Mungu na mtoto wake. Hivyo tunaelewa kwamba “amani ni tunda la haki si moja kwa moja, ila kwa sababu haki inaondoa vinavyozuia amani. Lakini amani ni moja kwa moja tunda la upendo, kwa kuwa upendo unazaa amani kwa umbile lake. Hii ni kwa sababu upendo ni nguvu inayounganisha; na amani ndiyo muungano wa mioyo na matakwa” (Thoma wa Akwino).

Maadili yanayotegemea haki katika maisha ya Kikristo

[hariri | hariri chanzo]

Haki inayohuishwa na upendo inafuatana na maadili mengine ya kufanana nayo. Mojawapo ni bora kuliko haki yenyewe, yaani adili la ibada ambalo linampatia Mungu heshima inayotakiwa kwa ndani na nje, utiifu, sala na sadaka ya kuabudu, ya kufidia, ya kudua, ya kushukuru; pia linatukumbusha tuwaheshimu watakatifu na kwa namna ya pekee Mama wa Mungu. Hilo lifuatane na toba ili kufidia makosa dhidi ya Mungu. Haki inategemeza pia heshima ya kitoto kwa wazazi na nchi, heshima kwa watu kulingana na stahili, umri na cheo chao, utiifu kwa wakubwa, shukrani kwa misaada, uangalifu wa kuadhibu kwa haki inapofaa (pamoja na kutumia huruma), hatimaye usemakweli katika maneno na mwenendo. Inatukumbusha kuwa urafiki una haki na wajibu wa namna yake, ingawa hauwezi kudai kitu mahakamani. Pia, kuna wajibu wa upendevu, unaopingana na ulaghai na mabishano ya bure vilevile. Hatimaye kuna wajibu wa ukarimu, unaokwepa kwa pamoja uroho na ubadhirifu.

Hayo yote ni muhimu, lakini hata wanaofuata maisha ya Kiroho hawayafikirii vya kutosha, hivyo wanajipendea kuliko kuwajali wenzao. Pengine kwa kisingizio cha upendo, ari chungu inavunja upendo na haki kwa kuhukumu bila msingi, kusengenya na kutia shaka juu ya jirani. Kinyume chake, tungeyatimiza kwa bidii tuliyoyazungumzia, utashi ungenyoshwa na kuimarishwa na kuandaliwa uishi kwa maadili ya juu zaidi, yaani tumaini na upendo, yanayotakiwa kutuunganisha na Mungu na kudumisha muungano huo katika nafasi mbalimbali za maisha, hasa zile ngumu na zisizotarajiwa. Kuwa Wakristo hata katika matendo madogo, ndiyo heri halisi ya wanaomfuata Yesu.

Adili la haki, ambalo ni la pili kati ya maadili bawaba, ni bora kuliko nguvu na kiasi, hata kuliko ubikira. Ukuu wake unajitokeza hasa katika tamko la Yesu alipolizungumzia katika maana ya juu ambamo yote tuliyoyasema yamo, tena kwa namna bora iwezekanavyo: “Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa” (Math 5:6).

Haki ya kishujaa

[hariri | hariri chanzo]

Ili tupate picha ya haki kamili tukumbuke adili hilo halikatazi tu wizi na utapeli, bali pia uongo wowote, unafiki, ulaghai, kuvunja siri, kuwakosea watu heshima kwa masingizio, masengenyo na vitendo, kuwahukumu bila msingi na kuwacheka kwa dharau. Mara nyingi haki yetu ina dosari tunapoitekeleza walau kiasi kwa faida yetu, k.mf. tukilipa madeni ili kukwepa pia gharama ya kesi, au tukisema ukweli kwa kuzingatia usumbufu unaoweza ukatokana na uongo. Hapo inahitaji kutakaswa kama maadili mengine yote. Haki kamili inahitajiwa na wale wanaolenga muungano wa dhati na Mungu, kwa kuwa wanatakiwa wasiwe na kosa lolote dhidi ya wenzao bali watimize wajibu wowote wa haki na upendo kwao. “Uishindanie kweli hata kufa, naye Bwana atakupigania wewe. Usiwe mwepesi wa kunena, mlegevu wa kutenda, msahaulifu. Usiwe kama simba nyumbani mwako, mwenye kutuhumu watumishi wako. Mkono wako usinyoshwe kupokea, ukarudishwa wakati wa kulipa” (YbS 4:28-31).

Mtu aliyefikia hatua ya muungano anatakiwa kutimiza kishujaa aina zote za haki, zikiwa ni pamoja na usawa. Ashike kikamilifu sheria zote za Mungu na za kibinadamu, za Kanisa na za nchi. Akipaswa kugawa mema au mizigo, afanye hivyo kadiri ya stahili za kila mmoja, asijali undugu wala urafiki. Aepe dhara lolote kwa yeyote. Haki ya kishujaa inadhihirika hasa pale ambapo ni vigumu kuipatanisha na mapendo ya dhati: kwa mfano jaji anapotakiwa kumhukumu mwanae mwenye makosa; au mkubwa anapotakiwa kumtuma mwanae mpenzi wa Kiroho mahali pa mbali na pa hatari.

  1. Luban, Law's Blindfold, 23.
  2. Plato, Republic trans. Robin Waterfield (Oxford: Oxford University Press, 1984).
  3. "Righteousness and justice [as] the foundation of [His] throne;...." (Psalms 89:14)
  • Clive Barnett, The Priority of Injustice: Locating Democracy in Critical Theory (Athens, GA: University of Georgia Press, 2017), ISBN 978-0-8203-5152-0
  • Brian Barry, Theories of Justice (Berkeley: University of California Press, 1989)
  • Harry Brighouse, Justice (Cambridge: Polity Press, 2004)
  • Anthony Duff & David Garland eds, A Reader on Punishment (Oxford: Oxford University Press, 1994)
  • Colin Farrelly, An Introduction to Contemporary Political Theory (London: Sage, 2004)
  • Barzilai Gad, Communities and Law: Politics and Cultures of Legal Identities (Ann Arbor: University of Michigan Press, 2003)
  • David Gauthier, Morals By Agreement (Oxford: Clarendon Press, 1986)
  • Robert E. Goodin & Philip Pettit eds, Contemporary Political Philosophy: An anthology (2nd edition, Malden, Massachusetts: Blackwell, 2006), Part III
  • Serge Guinchard, La justice et ses institutions (Judicial institutions), Dalloz editor, 12 edition, 2013
  • Eric Heinze, The Concept of Injustice (Routledge, 2013)
  • Ted Honderich, Punishment: The supposed justifications (London: Hutchinson & Co., 1969)
  • James Konow (2003) "Which Is the Fairest One of All? A Positive Analysis of Justice Theories", Journal of Economic Literature, 41(4)pp. 1188–1239
  • Will Kymlicka, Contemporary Political Philosophy: An introduction (2nd edition, Oxford: Oxford University Press, 2002)
  • Nicola Lacey, State Punishment (London: Routledge, 1988)
  • John Stuart Mill, Utilitarianism in On Liberty and Other Essays ed. John Gray (Oxford: Oxford University Press, 1991)
  • Robert Nozick, Anarchy, State, and Utopia (Oxford: Blackwell, 1974)
  • Amartya Sen (2011). The Idea of Justice. Cambridge: Belknap Press of Harvard University Press. ISBN 978-0-674-06047-0.
  • Marek Piechowiak, Plato's Conception of Justice and the Question of Human Dignity (2nd edition, revised and extended, Berlin: Peter Lang Academic Publishers, 2021), ISBN 978-3-631-84524-0.
  • C.L. Ten, Crime, Guilt, and Punishment: A philosophical introduction (Oxford: Clarendon Press, 1987)
  • Plato, Republic trans. Robin Waterfield (Oxford: Oxford University Press, 1994)
  • John Rawls, A Theory of Justice (revised edition, Oxford: Oxford University Press, 1999)
  • David Schmidtz, Elements of Justice (New York: Columbia University Press, 2006)
  • Peter Singer ed., A Companion to Ethics (Oxford: Blackwell, 1993), Part IV
  • Reinhold Zippelius, Rechtsphilosophie, §§ 11–22 (6th edition, Munich: C.H. Beck, 2011), ISBN 978-3-406-61191-9

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
Wikimedia Commons ina media kuhusu:

Justice history travel guide kutoka Wikisafiri