Adili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sanamu ya adili (kwa Kigiriki ἀρετή) huko Efeso, Uturuki

Adili (kutoka neno la Kiarabu; kwa Kiingereza "virtue" kutoka Kilatini virtus, yaani nuguvu) ni uzoefu wa kutenda vema.

Katika falsafa[hariri | hariri chanzo]

Huko Ugiriki katika karne ya 5 K.K. wanafalsafa Plato na hasa Aristotle waliorodhesha maadili mengi yanayotegemea nne za msingi (maadili bawaba): busara, haki, nguvu na kiasi. Zaidi ya hayo, walionyesha kwamba haiwezekani kujipatia adili moja tu, bali uadilifu unadai mtu awe na maadili yote. Kwa mfano, haiwezekani kuwa mtu wa haki pasipo busara.

Katika Ukristo[hariri | hariri chanzo]

Katika Ukristo, juu ya maadili ya kiutu, mwamini anatakiwa kupokea maadili ya Kimungu yaliyoorodheshwa na mtume Paulo, yaani imani, tumaini na upendo ambayo yanaendana vilevile. Mtu anatakiwa kulenga ushujaa katika maadili yote.

Ushujaa wa maadili kwa jumla[hariri | hariri chanzo]

Ushujaa wa maadili, unaodaiwa na Kanisa ili kutangaza watumishi wa Mungu kuwa wenye heri mbinguni, unaanza katika utakaso wa Kimungu wa hisi yanapopatikana matendo ya kishujaa ya usafi wa moyo na ya subira. Matendo ya kishujaa yanapatikana zaidi katika utakaso wa Kimungu wa roho unaoingiza katika hatua ya muungano, na hasa baada ya jaribu hilo. Tukimuona mtu ametoka handaki hilo la kwanza, na zaidi hilo la pili, akiwa na ushujaa wa maadili, ni dalili ya kuwa amevuka vizuri asiache njia; au, kama alitenda makosa, ameinuliwa tena na neema ya Mungu na kuletwa hadi unyenyekevu mkubwa zaidi, kwa kutojiamini na kumtegemea yeye tu.ù

Sifa za adili la kishujaa[hariri | hariri chanzo]

“Adili la kawaida linamkamilisha binadamu kiutu, kumbe adili la kishujaa linampatia ukamilifu upitao utu. Shujaa akiogopa penye sababu za kuogopa, ni adili; asingeogopa katika nafasi za namna hiyo angekuwa shupavu tu. Lakini asipoogopa tena kitu kwa sababu anategemea msaada wa Mungu, adili hilo linapita utu, ni la Kimungu” (Thoma wa Akwino). Juu kuliko maadili ya raia mwema, mtakatifu huyo alifafanua maadili yanayotakasa: “Ni yale ya watu wanaoelekea kufanana na Mungu. Hapo busara inadharau malimwengu yote ipende zaidi kuzama ndani ya Mungu na kuelekeza mawazo yote kwake; kiasi kinaachana na madai ya mwili kadiri umbile linavyoweza kuvumilia; nguvu inamzuia mtu asiogope kifo wala ahera; hatimaye haki inamsukuma ashike moja kwa moja njia hiyo ya Kimungu tu”. Juu ya hayo tena yapo maadili ya roho iliyokwishatakata, yaani yale ya watakatifu wakuu hapa duniani na ya wenye heri mbinguni: “Hapo busara ni kama inahisi mambo ya Kimungu; kiasi hakijui tena tamaa za kidunia; nguvu inasahaulisha hofu yoyote; haki inafunga na Mungu agano agano la milele”. Akizungumzia Heri Nane alisema kuwa ndiyo matendo ya juu zaidi ya maadili na ya vipaji vya Roho Mtakatifu, na kuwa tuzo yake hapa duniani ni utangulizi fulani wa heri ya milele.

Mafundisho kuhusu adili la kishujaa yalijumlishwa hivi na Papa Benedikto XIV, “Masharti manne yanatakiwa kwa adili la kishujaa lililothibitishwa au lililodhihirika: 1) jambo linatakiwa kuwa gumu, la juu kuliko nguvu za kawaida za watu; 2) linatakiwa kutendwa mara, kama kwa urahisi; 3) tena kwa furaha takatifu; 4) si kwa nadra, bali kila inapopatikana nafasi”. Hivyo ushujaa wa maadili ni wa juu kuliko kawaida ya waadilifu. Unajitokeza mtu anapotimiza majukumu yote bila wasiwasi wala shuruti, hata katika nafasi ngumu zaidi.

Masharti hayo yaeleweke kuhusiana na mtu anayetekeleza adili la kishujaa: lililo gumu kwa mtoto wa miaka kumi ni lile lipitalo nguvu za kawaida za watoto wenye umri wake; vilevile lililo gumu kwa mzee ni tofauti na lililo gumu kwa mtu mwenye afya na nguvu. La pili, yaani utayari na urahisi, lieleweke upande wa juu wa roho, bila kukanusha ugumu upande wa chini, fumbo la Getsemane linavyothibitisha; ili sadaka ya kuteketezwa ikamilike ni lazima uwepo uchungu na ugumu mkubwa unaoshindwa mara na upendo wa kishujaa. Vilevile furaha takatifu, iliyo sharti la tatu, ni ile ya sadaka inayotupasa, nayo haizuii uchungu wala huzuni, bali pengine inaendana na hali ya kukaribia kulemewa ambayo inatolewa kitakatifu kwa Mungu; tena furaha ya kuteseka pamoja na Bwana inaongezeka pamoja na uchungu, ndiyo sababu ni dalili ya neema kubwa. Sharti la nne, yaani mazoea ya kutenda hivyo nafasi ikipatikana, linathibitisha zile zilizotangulia na linaonyesha adili la kishujaa lililokwishajaribiwa kweli.

Ushujaa wa maadili unadhihirika hasa katika kifodini, lakini hata nje ya hapo, k.mf. katika kusamehe na kupenda kwa namna ya ajabu wadhalimu. Ndivyo ilivyomtokea kwa namna ya pekee Yesu, hata kabla ya mateso yake, alivyoonyesha hasa kwa upendo wake usio na mipaka kwa ajili ya wote, upendo wa mchungaji aliyejiandaa kutoa uhai wake kwa ajili yetu.

Katika adili la kishujaa wastani adili ni wa juu kuliko katika adili la kawaida: sasa adili linatekelezwa pamoja na kipaji kinachohusiana nalo, na kwa kuwa linatumikia upendo tunakuta ndani yake mruko wa adili hilo la Kimungu. Halafu, kwa kuwa matendo ya kipaji yanategemea uvuvio wa Roho Mtakatifu, Mkristo shujaa anadumu mnyenyekevu kama mtoto wa Mungu anayemtazama daima Baba, tofauti na shujaa anayezingatia nguvu zake mwenyewe na kulenga makuu yatakayomtukuza, kuliko kumuacha Bwana atawale kwa dhati ndani mwake.

Ushujaa na ulinganifu wa maadili[hariri | hariri chanzo]

Ili tutofautishe uadilifu wa kishujaa, unaotokana na msaada mkubwa wa Mungu, na mambo yanayoonekana tu kufanana nao, tunapaswa kuzingatia masharti hayo manne lakini pia ulinganifu wa maadili. Busara, dreva wa maadili, inaongoza maadili ya kiutu, wakati upendo unaelekeza matendo ya maadili yote kwa Mungu na kuyafanya yastahili. Ndiyo sababu maadili yote, yakiunganika katika busara na upendo, yanakua pamoja kama vidole vitano vya mkono uleule mmoja, au kama viungo mbalimbali vya mwili mmoja. Fundisho hilo ni la msingi ili kubainisha maadili ya kishujaa, kwa sababu kutekeleza kwa pamoja maadili yanayoonekana kupingana kuna ugumu wa pekee, kwa kuwa silika ya kila mmojawetu inaelekea adili moja au lingine. Maadili ya kujipatia na ya kumiminiwa yanatakiwa kukamilisha maelekeo mema ya umbile letu na kupinga kasoro zinazoliharibu. Tunapaswa kupiga kinanda bila kutokeza noti zisizolingana na nyingine, tusichanganye upole na woga, wala moyo mkuu na kiburi.

Basi, tunaona umuhimu wa ulinganifu wa maadili, na ugumu wa kuyatekeleza yote karibu kwa wakati mmoja ili kudumisha ulinganifu wa maisha maadilifu. Litokanalo ni kwamba adili lolote halina kiwango cha ushujaa ikiwa mengine hayapo katika kiwango hichohicho walau katika utayari wa roho kuyatekelezwa nafasi ikidai hivyo. Si busara kutamka haraka kuwa mtumishi wa Mungu ana ushujaa wa adili fulani halafu kufasiri kwamba kwa sababu hiyo anayo mengine pia kwa kiwango hicho; ili tuweze kusema adili mojawapo ni la kishujaa, ni lazima tuwe tumeshapima ukuu wa mengine. Ingawa maadili, hasa ya Kimungu, yanakua pamoja, fulani anaweza kuelekea kiumbile au kimazoea adili moja au lingine; tena kuna watumishi wa Mungu ambao, kwa ajili ya utume maalumu, wanapokea neema za msaada zinazowafanya watekeleze adili moja kuliko mengine.

Mungu tu, anayeunganisha ndani mwake sifa zote kamili, anaweza kuwajalia watumishi wake waunganishe vilevile maadili yote katika mwenendo wao. Ulinganifu wa ajabu wa maadili ulionekana hasa ndani ya Bwana wakati wa mateso, ambapo tunaona upendo wa kishujaa kwa Mungu na huruma isiyopimika kwa watesi pamoja na upendo mkuu kwa ukweli na haki; unyenyekevu wa dhati na moyo mkuu wa ajabu; nguvu ya kishujaa katika kujishusha na upole mkuu. Hivyo ubinadamu wa Mwokozi ni kioo safi ambamo sifa za Mungu zinarudisha mwanga wake.

Ulinganifu wa maadili ndio unaotofautisha mashahidi wa kweli na watu waliovumilia mateso kwa kiburi na ushupavu katika kushikilia udanganyifu. Mashahidi wa kweli tu wanaunganisha nguvu na upole unaowafanya wawaombee watesi wao kama alivyofanya Mwokozi. Hasa ndani mwao tunakuta masharti manne ya uadilifu wa kishujaa tuliyoyafafanua. Humo tunaona kazi maalumu ya Mungu anayetegemeza watumishi wake asiache kuwajalia neema za pekee katika nafasi ngumu zaidi.

Tusisitize kuwa ushujaa wa watoto unapimwa kulingana na nguvu za kawaida za watoto waadilifu wa umri uleule. Ikiwa watu wazima kadhaa uadilifu wao ni mdogo, wapo watoto ambao uadilifu wao ni mkubwa. “Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu; kwa sababu yao wanaoshindana nawe” (Zab 8:2). Yesu aliwakumbusha maneno hayo makuhani na waandishi waliochukizwa na watoto kushangilia, “Hosana, Mwana wa Daudi!” (Math 21:15). Ikiwa pengine imani ya watoto ni kielelezo kwa watu wazima, ni vilevile kuhusu tumaini lao na upendo wao. Tukisoma matendo ya kishujaa ya watoto wenye umri wa miaka kumi na miwili au chini ya hapo, na maneno mazuri ajabu ambayo baadhi yao waliyatamka kabla hawajafa, tunakuta hekima ambayo katika usahili na unyenyekevu wake ni ya juu kuliko elimu changamano ya kibinadamu. Ni kipaji cha hekima katika kiwango cha juu, kulingana na upendo wa hao watoto ambao ni wakubwa kwa ushuhuda wa kishujaa waliomtolea Mungu. Katika usafi wa mtoto aliyebatizwa Roho Mtakatifu hahitaji kutakasa mengi kabla hajamshirikisha mianga yake na nguvu zake. Bila shaka mna madonda ya dhambi asili ambayo baada ya ubatizo ni kama makovu yanayoelekea kupona; lakini hayana sumu inayotokana na makosa yaliyorudiwarudiwa kwa hiari. Mtoto akiwa mwaminifu kwa neema katika kutimiza wajibu wa umri wake, Roho Mtakatifu anamsamehe matakaso yale machungu ambayo kwa waliotenda dhambi ni ya lazima kadiri walivyopotea. Hapo mtoto anainuka hata juu.