Usiku wa roho
Usiku wa roho ni istilahi ya maisha ya kiroho iliyotumika hasa katika Kanisa Katoliki kwa kufuata mang'amuzi na mafundisho ya Yohane wa Msalaba. Kadiri yake, Mkristo aliyeendelea katika maadili na usikivu kwa vipaji vya Roho Mtakatifu anahitaji kupatwa na utakaso huo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuwa tayari kwa hatua ya muungano.
Haja ya kutakaswa roho na utangulizi wa hatua ya muungano
[hariri | hariri chanzo]“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa” (Yoh 15:1-2). “Katika mzabibu wa kawaida, tawi lenye machipukizi mengi linazaa kidogo, kwa sababu utomvu unapotewa na nguvu ukienea mno katika machipukizi yaliyozidi; ndiyo sababu mkulima anayakata. Kitu cha namna hiyo kinamtokea mtu ambaye ana msimamo mzuri na kuunganika na Mungu, lakini mapendo na maisha yake yanamwagika mno nje, kwa njia mbalimbali: hapo nguvu za maisha ya Kiroho zinapungua zisizae mema mengi zaidi. Kwa hiyo Bwana, kwa mfano wa mkulima, anawatakasa watumishi wema, mara nyingi anapogolea ndani mwao yasiyo na faida ili wazae zaidi; anawatakasa kwa muda mrefu kutosha, akiwatumia tabu na kuruhusu majaribu yanayowalazimisha kuyapinga kitakatifu kwa stahili nyingi, jambo ambalo linawaimarisha zaidi kwa ajili ya uadilifu. Bwana anawatia nguvu na kuwatakasa namna hiyo wale walio safi tayari, kwa kuwa hapa duniani hakuna aliye safi kutosha, kadiri ya maneno ya Mt. Yohane, ‘Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu’ (1Yoh 1:8)... Hivyo Bwana anawatakasa watumishi wake ili wazae zaidi, wastawi katika maadili na wazae matendo mema mengi zaidi kadiri walivyo safi” (Thoma wa Akwino).
Ndivyo alivyotakaswa Ayubu aliyesema, “Je, mtu hana wakati wake wa vita juu ya nchi?” (Ayu 7:1). Kwa maana hiyo mababu na walimu wa Kiroho walisema mara nyingi juu ya msalaba tunaopaswa kuubeba kila siku upande wa hisi na upande wa roho, ili polepole zitakaswe hata hisi ziitii kikamilifu roho, nayo imtii Mungu. Hayo yanafanyika hasa katika roho kutakaswa ili kuandaliwa iungane na Mungu.
Kasoro za walioendelea
[hariri | hariri chanzo]Inafaa tuzizingatie kwa sababu tatu: ili tuone haja na thamani ya msalaba unaotupasa kila siku; halafu tutofautishe tabu zisizo na maana tunazojipatia kipumbavu na zile zinazotutakasa; hatimaye tuelewe tutakavyohitaji kupitia toharani tusipofaidi vya kutosha misalaba ya maisha haya, kwa kuwa heri ya kumuona Mungu haiwezi kutolewa kwa mtu asiye safi kabisa.
Walioendelea, ambao wameshatakaswa hisi kwa kiasi kikubwa na wameanza kuishi Kiroho kwa kuzamia mafumbo ya imani, bado wana kasoro nyinginyingi, mfano wa kutu itakayokoma tu kwa kupatwa na moto unaotakasa. “Maana dhahabu hujaribiwa motoni, na watu wateule kalibuni mwa unyonge” (YbS 2:5).
Kwa namna fulani wanajitakia mitawanyiko ya mawazo wakati wa sala, utupu wa ndani kwa kujimwaga nje bure, mapendo ya kibinadamu mno kwa baadhi ya watu yanayosababisha kuwakosea wengine heshima, haki na upendo. Pengine wanatokeza tabia kali kwa kukosa subira. Wakidanganywa na shetani, baadhi wanatia maanani mno neema walizojaliwa, baadhi wanatumbukia ari chungu kwa jirani; hivyo bila kujitambua wanavimbika kwa kiburi katika mambo ya Kiroho na kujiamini, wanasogea mbali na usahili, unyenyekevu na usafi unaodaiwa na muungano wa dhati na Mungu. “Wanaweza wakawa wagumu kiasi kwamba kurudia uadilifu sahili na roho halisi ya ibada kuna shaka sana” (Yohane wa Msalaba). Basi, hatari zinazowakabili ni kubwa kuliko zile za mwanzoni.
Mbali ya kasoro hizo katika maisha ya ndani na uhusiano na Mungu, wanazo nyingine katika mafungamano na wakubwa wao, walio sawa nao na walio chini yao, ambazo zinadhuru upendo na haki na kuathiri utume na uongozi wao.
Kiburi upande wa maisha ya Kiroho na wa akili kinawafanya washikilie mno msimamo wao, namna yao ya kutazama, kuhisi na kutaka. Matokeo yake ni kijicho, uchu wa siri wa madaraka na hata kuongoza kwa mabavu (tabia yao isipoelekea kinyume, yaani kuruhusuruhusu mno na kuwa dhaifu mbele ya wanaowakosea wenzao). Vilevile mara nyingi hawana utayari na juhudi katika kutii, au wanatii kilaghai; wanakosa upendo kwa wivu, usengenyaji na mashindano.
Yanaweza yakazuka makosa mengi kati ya yale yanayovuruga zaidi roho. Undani wa akili na utashi umeathiriwa bado na kiburi, maoni na matakwa yao hata mwanga na matakwa ya Mungu visiweze kutawala bila kupingwa. Kasoro hizo kwa kudumu muda mrefu zinakomaa na kuharibu tabia isihusiane na Mungu kwa dhati. Matokeo ni magomvi na mafarakano mengi kati ya wale wanaotakiwa kushirikiana kwa wokovu wa watu.
Hayo yote yanadhihirisha haja ya “sabuni kali ya usiku wa roho, ambayo isipokuwepo usafi unaodaiwa kwa kuungana na Mungu utakosekana daima” (Yohane wa Msalaba). Hata baada ya kuvuka usiku wa hisi walioendelea ni washamba katika kutenda na kuhusiana na Mungu; wanamuelewa na kumzungumzia bila ukomavu. Ukamilifu tu, unaopatikana upande wa mafumbo, unaleta utu uzima ambapo roho inatenda makubwa, kwa sababu utendaji wake ni wa Kimungu kuliko wa kibinadamu.
Undani wa utashi unavyohitaji kutakaswa
[hariri | hariri chanzo]Yohane Tauler alisisitiza jambo hilo kutokana na umimi ambao haujitambui lakini unadumu ndani ya utashi na kusababisha tuseme na nafsi yetu bila utulivu wala faida, badala ya kusema na Mungu kwa amani na kwa kutiwa uhai. Umimi huo unasababisha tujifanye lengo la yote na kuhukumu jirani (kumbe tunajitetea mno); unajitokeza hasa katika majaribu, ambapo mara tunajitafutia nje msaada na faraja: lakini si hivyo tunavyomuona Mungu. Hatujajenga vya kutosha juu ya Kristo, ndiyo sababu nyumba yetu si imara. Tumejenga juu yetu, juu ya utashi wetu, na hiyo ni sawa na kujenga juu ya mchanga.
“Inambidi Mungu ajitwalie kabisa undani wa roho na kushika nafasi yote, jambo ambalo linawatokea tu marafiki wake halisi. Mwenyewe alitupelekea Mwanae pekee ili maisha matakatifu ya huyo Mungu-mtu, maadili yake makuu na kamili, mifano yake, mafundisho yake na mateso yake mengi yatuinue juu yetu wenyewe, tutoke kabisa umimi wetu na kuacha mwanga wetu mdogo hafifu uzame ndani ya nuru halisi… ‘Nuru yang’aa gizani, wala giza halikuipokea’ (Yoh 1:5). Nuru hiyo wanaipokea wale tu walio maskini wa roho na waliovua vizuri umimi wao na matakwa yao binafsi. Wengi walioshika ufukara miaka 40 hawajawahi kupokea hata mwali mdogo. Kwa njia ya hisi na akili wanajua vizuri yaliyosemwa juu ya nuru hiyo wasiionje kamwe kwa ndani; kwao ni ngeni na inabaki mbali nao. Hivyo umati mnyofu wa akina yahe walipomfuata Bwana wetu, Mafarisayo, wakuu wa makuhani na walimu wa sheria, wale wote wenye utakatifu wa kuonekana, walimpinga vikali na hatimaye wakamuua”. Hiyo inaonyesha unafikisha wapi undani huo wa umimi na kiburi unaotupofusha tusione makosa yetu. Mungu ndiye ukuu wa wanyenyekevu, na njia zake za juu hazieleweki kwa kiburi chetu. Basi ni muhimu nuru hai ya imani na vipaji ipenye undani wa akili yetu hadi mzizi wa utashi wetu.
Ili itokee hivyo haitoshi tujue na kusadiki maneno ya Injili, ni lazima tufyonze kwa dhati roho yake. La sivyo, chini ya sura ya Kikristo, pamoja na miundo na misamiati ya Kikristo, tutadumisha ndani mwetu kitu tofauti kinachokataa nuru ya uhai, kama ngome unapojificha umimi usiotaka kusalimu amri Mungu atutawale moja kwa moja. Ndiyo sababu wanaojiona wameendelea vya kutosha wasitambue kasoro zao, wako hatarini kuliko umati wa watu wanaoungama ukosefu wao na kudumisha uchaji wa Mungu. “Basi, wanangu wapenzi, mtumie utendaji wenu wote wa Kiroho na wa umbile ili hiyo nuru halisi ing’ae ndani mwenu mweze kuionja. Kwa namna hiyo mtaweza kuirudia asili yenu, inapong’aa nuru halisi. Ubinadamu utake usitake, mtamani na kuomba neema hiyo”. Hapa Yohane Tauler anatofautisha ujuzi wa kawaida wa imani na yale mang’amuzi ya upendo wa Mungu waliyowekewa marafiki wake, akialika wote wayatamani ili yarekebishe undani wa roho kwa kuiangaza na kuitoa nje ya ngome ilipojificha.
Kasoro hizo zote, ambazo kwa kiasi fulani zinadumu katika akili na utashi wa walioendelea, zinahitaji utakaso ambao Mungu tu anaweza kuufanya. “Mungu tu anaweza kutia umungu, kama vile moto tu unavyoweza kuwasha” (Thoma wa Akwino). Kutakaswa naye kutakuwa na mateso, kama kifo cha fumbo, yaani maangamizi ya umimi unaopinga neema hata vikali. Kiburi kinatakiwa kupigwa hadi kufa kiuachie nafasi unyenyekevu halisi. Hiyo nuru ya uhai iliyoongezeka duniani hadi ujio wa Mwokozi inatakiwa kuongezeka vilevile ndani ya kila mtu hadi aingie mbinguni.
Utakaso wa Kimungu wa roho ndio mapambano ya mwisho kati ya kiburi na unyenyekevu unaoendana na upendo. Pande hizo mbili zinaweza kuchorwa kama miti miwili: mmoja unatokana na asili na matokeo ya mizizi saba ya dhambi, unachanua maua ya laana na kuzaa matunda ya sumu. Kinyume chake, mti wa maadili na vipaji, mzizi wake ni unyenyekevu unaozidi kupenya ardhi ili kufyonza rutuba, matawi yake ya chini ni maadili ya kiutu na vipaji vinavyohusiana nayo, matawi yake ya juu ni imani, tumaini na upendo (ambao ndio wa juu na wenye kuzaa zaidi). Imani inahusiana na kipaji cha akili, na pia cha elimu ambacho kinakamilisha tumaini kikionyesha ubatili wa malimwengu na wa misaada ya binadamu kwa lengo la Kimungu, na hivyo kutufanya tutamani uzima wa milele kwa kumtegemea Mungu. Upendo unahusiana na kipaji cha hekima kinachosababisha hasa sala ya kumiminiwa inayoleta muungano na Mungu unaokuwa kama wa kudumu pamoja na kujiachilia kwake. Ili mti huo ustawi mpaka mwisho unahitajika ushindi wa moja kwa moja dhidi ya mabaki ya kiburi ambayo walioendelea wanayo upande wa akili na wa maisha ya Kiroho. Ndiyo sababu wanahitaji kutakaswa roho ambako, kwa msaada wenye nguvu wa Roho Mtakatifu, watekeleze kishujaa maadili ya Kimungu ili kushinda vishawishi dhidi yake.
Tofauti na tabu za kawaida
[hariri | hariri chanzo]Bwana tu anaweza kuutakasa undani wa roho jinsi unavyohitaji. Basi, tufafanue utakaso huo tusije tukaingia hasara kwa kuuchanganya na tabu za nafsi na ukavu wa hisi. Kinachovitofautisha ni maendeleo katika kumjua na kumpenda Mungu. Tabu za nafsi hazitakasi zisipovumiliwa kwa upendo wa Mungu na kwa kujiachilia kwake. Vilevile tabu zinazotokana na utovu wa maadili (k.mf. hisi zisizoratibiwa) hazitakasi zisipopokewa kama aibisho la kufaa kwa kufidia makosa.
Giza ambamo roho inahisi imejikuta
[hariri | hariri chanzo]Kama vile utakaso wa Kimungu wa hisi unavyodhihirishwa na hali ya kunyimwa faraja za kihisi tulizoambatana nazo, ule wa roho unaonekana kuwa hasa kunyimwa mianga ya awali kuhusu mafumbo ya imani. Tuliyazoea hivi kwamba urahisi wa kuyafikiria katika sala ulitusahaulisha ukuu wake usio na mipaka na kutufanya tuyaone kibinadamu mno. Basi, ili atuinue juu Bwana anakuja kutubandua toka namna hiyo ya kuwaza na kusali. “Mungu anawaondolea hao walioendelea vipawa, mapendo na hisi, upande wa roho na wa hisi; anaacha akili gizani, utashi ukavuni, uwezo wa kukumbuka bila kumbukumbu maalumu, na mapendo ya mtu yakipotea katika mateso, uchungu na mafadhaiko. Ndani ya mtu hamna tena hisia wala mwonjo kuhusu mema ya Kiroho yaliyomvutia hapo awali” (Yohane wa Msalaba). Huzuni inayompata hapo si ile inayoweza ikatokana na ugonjwa wa nafsi, kuvunjwa moyo na kupambana na maisha. Ni tofauti hasa kwa sababu inaendana na hamu kubwa ya Mungu na ya ukamilifu, na utafutaji wa mfululizo wa yule ambaye peke yake anaweza kulisha na kuhuisha roho.
Hapo mtu anapaswa kusonga mbele “kama kipofu, kadiri ya imani tupu ambayo ni usiku wenye giza kwa vipawa vya umbile” (Mt. Yohane wa Msalaba). Hawezi tena kuambatana kwa urahisi na ubinadamu wa Yesu, ameondolewa kama mitume walivyoondolewa alipopaa mbinguni. Miezi ya nyuma urafiki wao ulistawi siku kwa siku, hata Yesu akawa uhai wao; kumbe kawaacha wasiweze kumuona wala kusikiliza maneno yake yenye faraja. Walijisikia wakiwa hasa mbele ya matatizo ya utume waliokabidhiwa kuufanya ulimwenguni kote, kati ya uovu na udanganyifu mkubwa. Walipaswa kukumbuka maneno ya Yesu: “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu” (Yoh 16:7). “Mitume waliambatana na ubinadamu wa Kristo bila kuinuka vya kutosha hadi upendo wa Kiroho kwa umungu wake, wala kuwa tayari kumpokea Roho Mtakatifu… ambaye watapelekewa ili awafariji na kuwaimarisha katika tabu zao” (Thoma wa Akwino). Hilo ondoleo la uwepo wazi wa Yesu kabla hawajageuzwa siku ya Pentekoste linasaidia kuelewa hali ya giza na ukiwa tunayoizungumzia, ambapo mtu anajiona ameingia usiku halisi wa roho kwa kuondolewa mianga kama jua linapotua magharibi.
Katika giza hilo ukuu wa Mungu unafunuliwa
[hariri | hariri chanzo]Je, katika giza hilo hakionekani chochote kile? Upande wa maumbile, jua likitoweka zinakuja kuonekana nyota zinazodhihirisha ukuu wa anga: hivyo usiku tunaona mbali kuliko mchana. Huo ni mfano wa ukweli mkubwa, kwamba roho inapoingia giza hilo haioni tena yaliyo jirani nayo, ila inazidi kuhisi ukuu na usafi usio na mipaka wa Mungu, unaopita wazo lolote tunaloweza kujitungia; kutokana na hisi hiyo inajiona wazi zaidi ilivyo nyonge.
Lakini, kabla hatujafurahia nyota za angani tunapaswa kuzoea kutembea usiku bila hofu na kushinda vishawishi vikali dhidi ya imani na tumaini. Kwa Yohane Maria Vianney teso kuu lilikuwa kujiona mbali na kipeo cha upadri, ambao katika giza la imani alizidi kutambua kilivyo kikuu, pamoja na haja za umati uliomkimbilia. Kadiri alivyoona mema mengi yaliyohitajiwa, alishindwa kuona na kufurahia yale aliyoyatenda. Teso lake kuu lilikuwa kuona dhambi na upotevu wa milele, kidogo kama Yesu kuhani na sadaka juu ya msalaba na Maria chini yake. Teso hilo linategemea kuzidi kupenya katika usiku wa imani wema mkuu wa Mungu (ambao unapuuzwa na kudharauliwa) na thamani ya uzima wa milele.
Ukuu na wema wa Mungu na unyonge wetu vinapingana kiasi cha kuangaziana ajabu. Hivyo Anjela wa Foligno aliandika, “Najiona sina jema wala adili lolote, nimejaa wingi wa vilema… rohoni mwangu naona kasoro tu… Ningependa kuwajulisha wengine kwa sauti kubwa uovu wangu… Mungu amejificha kwangu… Niwezeje kumtumainia?… Hata kama wenye hekima wote waliopo duniani na watakatifu wote wa mbinguni wangenijaza faraja zao, wasingenisaidia chochote kabla Mungu hajabadili undani wa roho yangu. Tabu hiyo ya ndani ni mbaya sana kuliko kifodini”. Baada ya hapo, akikumbuka mateso ya Kristo, alitamani tabu hiyo iongezeke kwa kuwa inatakasa na kufunua vilindi vya mateso hayo. Siku chache baadaye, akiwa njiani alisikia kwa ndani maneno yafuatayo, “Binti yangu, nakupenda kuliko yeyote wa bonde hili… Fransisko alinipenda sana nikamtendea mengi; lakini mtu angenipenda kuliko Fransisko ningemtendea mema mengi zaidi… Nampenda upeo yule anayenipenda bila uongo… Hakuna anayeweza kujisingizia, kwa kuwa wote wanaweza kupenda; Mungu anaomba upendo tu, kwa kuwa mwenyewe anapenda bila uongo, naye ndiye upendo wa roho”. Yesu msulubiwa akimuonyesha kidogo mateso yake akaongeza, “Tazama vema: je, ndani mwangu unakuta chochote kisicho upendo?”
Mfano mwingine wa usiku wa roho ni Paulo wa Msalaba aliyeandika, “Tabu ndogondogo za mwili au za roho ndiyo vidato vya kwanza vya ile ngazi ndefu takatifu inayopandwa na watu bora na wakarimu. Hao wanapanda hatua kwa hatua hadi kufikia kidato cha mwisho. Huko juu wanakuta uchungu safi kabisa, usiochanganyikana hata kidogo na faraja toka mbinguni wala duniani. Nao wakiwa waaminifu wasijitafutie faraja yoyote, watavuka toka huo uchungu safi hadi upendo safi wa Mungu usiochanganyikana na chochote kingine. Lakini wanaofikia hatua hiyo ni wachache sana… Wanajiona kana kwamba wameachwa na Mungu, kwamba yeye hawapendi tena, amewakasirikia… Nikiruhusiwa kusema hivi, kidogo ni kama adhabu ya kumkosa Mungu milele, ni teso ambalo uchungu wake hauna mfano. Lakini mtu akiwa mwaminifu anakusanya hazina isiyopimika! Dhoruba zinapita na kwenda zake, kumbe yeye anakaribia muungano halisi, mtamu na wa dhati na Yesu msulubiwa, ambaye anamgeuza ndani mwake na kumlinganisha naye”.
Hugo wa Mt. Viktori alifananisha roho kutakaswa na Mungu na mageuzo ya ukuni mbichi ulioshikwa na moto, “Ubichi unakauka, moshi unapungua, mwali mshindi unapamba… nao hatimaye unaushirikisha ukuni umbile lake, hata ukuni mzima unakuwa mkaa wenye kuwaka. Ndivyo upendo wa Mungu unavyokua polepole rohoni; mwanzoni hisia za moyoni zinapinga na kusababisha tabu nyingi na mafadhaiko: ni moshi mzito unaotakiwa kutawanywa. Halafu upendo wa Mungu unazidi kuwaka, mwali wake unakuwa mkali zaidi… na hatimaye unapenya roho nzima. Ukweli wa Mungu unapatikana na kumezwa katika sala ya kumiminiwa: roho iliyojikana inamtafuta Mungu tu. Kwa roho yeye ni yote katika yote, nayo roho inatulia katika upendo wake na kukuta humo furaha na amani”.
Yohane Tauler pia alieleza kwamba Roho Mtakatifu anauondolea undani wa roho yale yote yenye umimi na kiburi bado. Anaiacha tupu ili kuiponya, halafu anaijaza pamoja na kuiongezea zaidi na zaidi uwezo wa kupokea. “Hapo inaonekana njia isiyo na mtu, iko gizani na faraghani. Kwenye njia hiyo Mungu anajitwalia tena yale yote aliyowahi kuyatoa. Hapo mtu anaachwa peke yake kabisa hata kuonekana hajui tena chochote kumhusu Mungu. Anafikia hatua ya kufadhaika asijue tena kama aliwahi kushika njia nyofu… hiyo inamtia uchungu mkubwa kiasi kwamba ulimwengu huu mpana unaonekana naye mdogo mno. Hasikii tena chochote kumhusu Mungu wake, hajui tena chochote juu yake, na mengine yote kwake ni karaha. Ni kana kwamba amebanwa na kuta mbili, mbele yake kuna upanga na nyuma yake mkuki mkali. Basi aketi na kusema, ‘Nakusalimu, Mungu wangu, uchungu mkali uliojaa neema zote!’… Kwake inaonekana ni jaribu linalomtesa kuliko moto wa milele, kama huo ungewezekana duniani. Yale yote anayoweza akaambiwa katika hali hiyo hayamfariji kama asivyoweza kufarijiwa na jiwe. Tena, jambo asilopenda kabisa ni kusikia viumbe wakisema”.
Vinsenti wa Paulo kwa miaka minne alijaribiwa hivyo na kishawishi kikali cha mfululizo kuhusu imani hata akaandika maneno ya Nasadiki akayavaa juu ya moyo akayakandamiza mara kwa mara ili kuthibitisha kwamba hajakubali kishawishi hicho.
Baada ya kifo cha Mama Teresa maandishi yake yaliyotolewa hadharani[1] [2] yakafichua siri ya maisha yake ya ndani, yaani kwamba alipitia kwa karibu miaka 50 mfululizo katika hiyo hali ngumu ya usiku wa roho, bila ya hiyo kuweza kumzuia atabasamu muda wote.
Tukidhani utakaso huo wa Kimungu ni nje ya njia ya kawaida ya utakatifu, sababu ni kwamba hatufikirii vya kutosha utakaso wa dhati unaohitajika ili kupata mara uzima wa milele na kumuona Mungu moja kwa moja. Pengine tukisoma walimu wa Kiroho walivyoufafanua ni kwa udadisi, si kwa hamu nyofu ya utakatifu wetu. Tungekuwa nayo, tungeona maandishi yao yanavyotufaa.
Kwa njia moja au nyingine ni lazima tupitie urojorojo huo ili mateso, unyenyekevu na upendo wa Yesu kwetu visiwe havieleweki au kueleweka kinadharia tu; pasipo ujuzi wake hai hapana upendo kwa msalaba wala kwa utakatifu halisi. Kwa mfumo wake, neema inayotia utakatifu ikistawi inazidi kutufananisha na Mungu. Kadiri ilivyo ya Kikristo inazidi kutufananisha na Msulubiwa hadi tuingie mbinguni.
Tunapaswa pia kutambua tofauti za watu na za neema walizonazo, tusije tukawadai kuliko uwezo wao: tuhimize kwa wengine ushujaa wa mfululizo, kwa wengine hatua ndogondogo za kulisogelea lengo. Lakini kila mmoja anapaswa kujitoa sadaka afanane na Kristo.
Kinachosababisha roho kutakaswa hivyo
[hariri | hariri chanzo]Kisha kufafanua watumishi bora wa Mungu wanavyotakaswa roho, tueleze kiteolojia kinachosababisha hali hiyo, ambapo mambo ya Kiroho yanang’amuliwa katika giza na uchungu.
Mwanga wa kumimininiwa unaotakasa na moto wa kiroho
[hariri | hariri chanzo]Waadilifu wameandikwa, “Mungu amewajaribu, na kuwaona kuwa wamemstahili; kama dhahabu katika tanuru aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara” (Hek 3:5-6). Maandiko yanarudiarudia wazo hilo, “kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu” (Kumb 4:24) dhidi ya yale yanayomzuia asitawale rohoni. Nabii aliandika, “Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, nao umeishinda... amenifanya kuwa mtu wa pekee, na mgonjwa mchana kutwa” (Mao 1:13); ndivyo alivyoona vizuri makosa ya Israeli, haki ya Mungu na wema wake akamtolea dua nyingi kwa wokovu wa wakosefu.
“Kwa kuwa wewe unaiwasha taa yangu; Bwana Mungu wangu aniangazia giza langu” (Zab 18:28). Ndivyo Roho Mtakatifu anavyoangaza kama umeme roho anayotaka kuitakasa. Pengine anatuambia, “Je, unataka kutakaswa?” Tukikubali ataanza kazi ya dhati, akitupatia ukweli wa Kimungu ili kutuondolea umimi unaotudanganya bado mara nyingi. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yoh 8:31-32). Yaani, tukishika kimaisha neno la Kristo kwa kujirekebisha, polepole ukweli mkuu utatupenya na kutukomboa kutoka udanganyifu wa hatari zaidi, ule tunaojiambia. Hatuwezi kamwe kutamani vya kutosha mwanga huo unaotakasa; kumbe, mara nyingi tunaukwepa kwa kuogopa kukosolewa.
Yohane wa Msalaba aliufafanua hivi, “Usiku huo wenye giza ni Mungu kuiathiri roho ili kuitakasa na ujinga na kasoro za kawaida. Wanasala wanauita sala ya kumiminiwa na teolojia ya mafumbo, ambapo Mungu anaifundisha roho kwa siri na ukamilifu wa upendo, pasipo mchango wa mhusika, na hata pasipo huyo kuelewa hiyo sala ya kumiminiwa ni nini”. Baadaye akarudia mfano wa Hugo wa Mt. Viktori, “Mwanga wa Mungu unaoitakasa roho na kuiandaa kwa muungano kamili unafanana na moto unaotakasa ukuni kabla haujaugeuza ndani yake. Huo moto wa kimaumbile unaanza kukausha ukuni ukiondoa ubichi wake: halafu unautia rangi nyeusi na kuufanya utoe harufu mbaya na kuutolea takataka zote… Hatimaye unaanza kuuwasha kwa nje, na joto linaugeuza kuwa moto na linaufanya ung’ae kama moto wenyewe. Ndivyo ilivyo kwa moto wa Kimungu wa sala ya kumiminiwa. Kabla haujasababisha muungano na mageuzo ya roho ndani ya Mungu, ni lazima aiondolee vipingamizi vyote. Anaitolea takataka zote, anaifanya nyeusi… roho inaonekana mbaya, ya kuchukiza na kutopendeza kuliko awali. Basi utakaso huo unafanyika ili kuondoa vilema vyote ambavyo roho haijaviona kwa jinsi vilivyoshikamana nayo na kuwa kitu kimoja nayo; haikujua vipo wala haikudhani mabaya makubwa hivyo yamo ndani mwake. Hapo inadhani unyonge wake unamfanya Mungu aichukie”.
Matatizo hayo ya kufaa ni tohara halisi ya kabla ya kufa, ambapo mtu anatakaswa na moto wa Kiroho wa sala ya kumiminiwa na upendo. Ndiyo sababu “mtu anayetendewa hivyo duniani, ama anakwepa tohara ya ng’ambo ama anabaki toharani kidogo sana; saa moja ya mateso hayo katika maisha haya inafanya kazi bora kuliko saa nyingi za toharani” (Mt. Yohane wa Msalaba) kwa sababu hapa tunatakata kwa kustahili. Basi, kwa kuwa hali ya toharani ni adhabu ya kosa lililotakiwa kuepwa, njia ya kawaida ya utakatifu ni kutakaswa kabla ya kufa, ingawa wachache tu wanakwenda mbinguni wasipitie toharani. Watakatifu tu wanatimiza kikamilifu utaratibu wa maisha ya Kikristo.
Athari ya kipaji cha akili katika utakaso huo
[hariri | hariri chanzo]“Mtu anapokea namna mpya ya kutazama mambo, kwa kuwa mwanga wa neema ya Roho Mtakatifu ni tofauti na hisi, kama vile mambo ya Kimungu na yale ya kibinadamu… Hivyo basi polepole usiku huo wenye giza unambandua na namna yake ya kawaida ya kuelewa, ili umuinue kwenye namna ya Kimungu iliyo tofauti na wazo lolote la kibinadamu, kiasi kwamba anadhani kuwa anatembea nje yake mwenyewe”. Fundisho hilo la Yohane wa Msalaba linaangazwa na lile la Thoma wa Akwino kuhusu kipaji cha akili kusababisha upenyaji mpya na utakaso: “Kadiri mwanga wa akili ulivyo mkubwa unapenya undani wa jambo ili kuelewa mfumo na sifa zake. Basi, mwanga wa kimaumbile wa akili yetu (hata ukiwa mkubwa namna gani) uwezo wake una mipaka usiovukika. Kwa hiyo mtu anahitaji mwanga upitao maumbile ili kupenya mbali zaidi (kwa Mungu au katika vilindi vya roho), na mwanga huo upitao maumbile ambao binadamu anajaliwa unaitwa kipaji cha akili”. Ni wa juu kuliko mifuatano ya mawazo, ni chanzo cha ujuzi wa mara moja, sahili na wenye kupenya kama mwali wa jua.
Kipaji hicho kinadai iwepo kwanza imani iliyo hai kwa upendo, nacho kinaikamilisha hivi: imani hai inatufanya tushikilie mafumbo ya Mungu kwa sababu yamefunuliwa naye, lakini peke yake haiwezi kutufanya tupenye maana yake ya dhati. Upenyaji huo hautokani na masomo, bali na mwanga maalumu wa Roho Mtakatifu unaoshinda masomo kwenda juu na ndani, tena si kinadharia tu, bali kwa namna hai na kimaisha. Mwanga huo wenye kupenya tunaupokea kwa mikono miwili kwa kipaji cha akili. Hicho kwanza kinatuzuia tusichanganye maana halisi ya Neno la Mungu na ufafanuzi wake mdanganyifu; kinaonyesha mara ubatili wa hoja za kupinga kama noti mbaya inayoharibu ulinganifu wa noti zote: hapo tunatambua udanganyifu hata tusipoweza kuukanusha kiteolojia. Kipaji hichohicho kinatokeza umbali mkubwa uliopo kati ya mambo ya Kiroho na ishara zake, kati ya roho na mwili. Vilevile kinazuia tusichanganye faraja za kihisi na nderemo za Kiroho ambazo ni za juu na za hakika zaidi.
Kipaji hicho hakizuii tu udanganyifu, bali kinatufanya tupenye kwa namna hai kweli za dini zinazoeleweka (kama vile uwepo wa Mungu), na hasa mafumbo yapitayo uwezo wa akili: “Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu” (1Kor 2:10). Hapa duniani hakiwezi kuyaonyesha wazi, ila katika giza la imani kinaonyesha maana yake ya dhati iliyo vigumu kuieleza, ukuu wa Mungu, sifa zake, Ubaba wake kwa Neno na kwetu, ukombozi n.k.
Kipaji hicho kinatuongoza kuelewa na kutenda pia, kikitukumbusha umuhimu wa amri ya upendo, na thamani ya uzima wa milele tunaposhawishwa kukata tamaa. Kinatuzindua kuhusu mambo ya Kiroho, kinatuonyesha ukosefu wetu kuliko utafiti wowote wa dhamiri, kwa kutuangazia unyonge wetu pamoja na ukuu wa Mungu. Ndiyo sababu kinahusiana na heri ya wenye moyo safi, kwa kuwa kinatakasa akili yetu dhidi ya udanganyifu katika kuelewa na kutenda, na kinaibandua na picha za hisi.
“Hatumjui Mungu alivyo” (Thoma wa Akwino). Umungu haufikiwi na maumbile, kwa kuwa uko juu kuliko sifa zote zinazoweza kujulikana na kushirikiwa kimaumbile, juu ya uhai, umoja, ukweli, wema, ujuzi na upendo; unashirikishwa tu kwa namna ipitayo maumbile ya neema inayotia utakatifu. Duniani hatuwezi kuujua, ndiyo sababu wanasala waliuita giza kuu. “Siku moja roho yangu ilinyakuliwa, nikamuona Mungu katika uangavu mkubwa kuliko wowote niliowahi kujua… Nilimuona Mungu katika giza, na ni lazima liwe giza, kwa kuwa yuko juu mno kuliko roho, na lolote linaloweza kufikiriwa halilingani naye… Sioni kitu ila naona yote; hakika inapatikana katika giza. Kadiri giza lilivyo nene, wema unazidi yote. Ni fumbo lililofichika… Uweza, hekima na utashi wa Mungu, nilivyoviona vizuri ajabu siku nyingine, natambua ni kidogo kuliko hilo. Hilo ni kitu kizima, hivyo ni kama sehemu zake tu” (Anjela wa Foligno). Maana yake, sasa sioni kitu maalumu, ila naona sifa zote za Mungu zimeunganika vizuri ajabu katika ukuu wake unaozidi akili yangu.
Giza hilo ni Mungu ambaye “amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona” (1Tim 6:16). Mwanga unaotakasa wa kipaji cha akili unaonekana giza, kwa kuwa unatuingiza katika giza la juu la fumbo la Mungu, lililo kinyume cha giza la chini la mwili, tamaa, dhambi na udanganyifu.
Hivyo kipaji cha akili kinathibitisha hakika ipitayo maumbile inayotokana na imani, kikitufanya tupenye mafumbo na kukataa udanganyifu. Sala ya kumiminiwa iliyopo katika hiyo hali ya giza inatokana kwa mbali na imani hai na kwa jirani na kipaji cha akili; mara nyingi hata kile cha elimu kinachangia kwa kutuonyesha hasa unyonge wetu. Ukavu wa roho unaopatikana katika hali hiyo unaonyesha hakuna athari kubwa ya kipaji cha hekima kinachotuonjesha mambo ya Mungu kikituletea hivyo faraja na amani kubwa. Upenyaji wa kipaji cha akili ni tofauti na mwonjo huo. Ndiyo sababu anayezidi kupenya ukuu wa Mungu anajisikia mbali naye kutokana na unyonge wake; ila, kisha kutakaswa roho, ataonja kwa dhati uwemo wa Utatu rohoni mwake, ataujua kama kwa kuung’amua, jambo ambalo linaanza kidogo kabla ya usiku wa roho na litakamilika katika muungano unaotugeuza.
Giza la mwanga mkali
[hariri | hariri chanzo]Tueleze zaidi kwa nini mwanga wa kipaji cha akili unaonekana giza ili tutofautishe giza la juu na giza la chini, tukiinuka mfululizo ili kupenya lile la juu, yaani ile nuru anamokaa Mungu. Hapo usiku wa roho utaonekana ni uzima wa milele unaochipuka kwa uchungu ndani mwetu. Kwa ufupi, mwanga wa kumiminiwa unaotakasa unaonekana giza kwa sababu ya ukali wake na ukuu wa jambo unaloliangaza; nao unatutesa kwa sababu ya uchafu na udhaifu wetu, tunaoutambua zaidi kutokana na vishawishi vya wakati huo.
Matokeo ya mwanga mkali mno
[hariri | hariri chanzo]“Hekima ya Mungu inaonekana giza kwetu kwa kuwa inapita uwezo wa kimaumbile wa akili yetu, hivyo kadiri inavyodhihirika kwetu tunaiona kama giza” (Yohane wa Msalaba), kwa sababu tunazidi kuelewa umungu unavyopita mawazo yote tunayoweza kujitungia juu yake, k.mf. uhai, ukweli, wema, ujuzi, upendo wenyewe. Ndani yake una sifa hizo kwa namna bora hivi tusiweze kuufikia. “Jua likipambazuka na rangi nyekundu… au likitua na rangi nyeupenyeupe, tunasema ni dalili ya mvua. Teotimo, jua si jekundu, wala jeusi, wala jeupe, wala la kijivu wala la kijani. Nyota hiyo haipatwi kabisa na hali hizo wala mabadiliko ya rangi, kwa kuwa rangi yake pekee ni ule mwanga wake mkali na wa kudumu… Ila sisi tunasema vile kwa sababu ndivyo linavyoonekana kwetu kadiri ya hewa mbalimbali zilizopo kati yake na sisi, zinazofanya tulione namna tofauti. Ndivyo tunavyofikiri pia kumhusu Mungu: si kadiri alivyo, bali kadiri ya matendo yake ambayo tunamtazama… Ndani ya Mungu mna ukamilifu mmoja tu ambao ndani yake zimo sifa nyingine zote njema kwa namna bora kabisa tena kuu hata roho yetu isiweze kudhani kamwe” (Fransisko wa Sales).
Nuru hiyo isiyofikiwa ndiyo giza kuu kwetu; kama vile mwanga wa jua unavyopofusha macho ya ndege wa usiku asiyeweza kuvumilia hata mwanga dhaifu wa alfajiri. Aristotle aliwahi kusema kadiri mambo ya Kimungu yalivyo maangavu ni giza kwetu, kwa kuwa yako mbali zaidi na hisi zetu, k.mf. “jua lipo” ni tamko wazi kwetu kuliko “Mungu yupo”. Lakini kwa usahihi Mungu tu yupo kweli, ndiye Aliye: mwanga wa jua ukilinganishwa naye ni kivuli tu. Vilevile muda upitao ni wazi kwetu kuliko umilele usiopita wala kubadilika.
Hivyo mambo ya Mungu yanayotuelea (k.mf. uwepo wake) ni yale tunayoyapata katika kioo cha viumbe vinavyoonekana tukitumia mwanga dhaifu unaolingana na umbile letu. Kumbe ulinganifu wa dhati wa haki na huruma zisizo na mipaka pamoja na hiari kuu katika fumbo la uteule, ingawa ni mwangavu sana, kwetu ni giza nene. Ndiyo sababu mara nyingi wanaopitia usiku wa roho wanajaribiwa kuhusu fumbo hilo, wasiweze kuishia maelezo rahisi ya kibinadamu: wanahisi kwamba wangeyakubali wangeshuka badala ya kupanda. La kufanya ni kuruka kishawishi hicho kwa tendo kubwa la imani kuelekea giza la juu la umungu na vilindi vyake, ambamo ulinganifu huo unang’aa. Vilevile Utatu ulio mwanga wenyewe unaonekana giza kwetu. Ndiyo sababu Teresa wa Yesu alisema, “Kadiri mafumbo ya imani yalivyo ya giza, najisikia kuyaheshimu, kwa kuwa najua giza hilo linatokana na mwanga mkali mno kwa akili yangu finyu”. Mateso ya Yesu yaliyokuwa saa ya giza nene na ya kukwaza zaidi kwa mitume, ndiyo saa ya ushindi wake mkuu dhidi ya dhambi na shetani. “Mwali wa Kimungu wa sala ya kumiminiwa unapopenya roho, unaijaza uangavu, lakini kwa kuwa unapita umbile la roho, unaitia giza kwa maana unaiondolea hisi zake na mapendo yake ya kibinadamu ambavyo awali ilikuwa ikivitambua kwa mwanga wa kimaumbile… Hapo roho inaanza kupima vizuri zaidi sana yaliyo kweli na yaliyo uongo; inayaona mara na kuyaelewa wazi zaidi sana kuliko kabla haijaingia giza hilo” (Yohane wa Msalaba).
Matokeo ya mwanga juu ya macho mabovu
[hariri | hariri chanzo]Zaidi ya hayo, mwanga wa Kimungu unaomiminwa katika usiku wa roho unaitesa kutokana na uchafu ilio nao bado. “Mwanga unachukiza macho mabovu, ingawa unayapendeza yaliyo safi” (Augustino). Inatokea hivyo hasa mwanga huo ukitakiwa kushinda pingamizi la muda mrefu la mtu asiyependa kuangaziwa kasoro zake fulanifulani (k.mf. ari chungu au kujiridhia kwa siri) kwa kuwa anataka kuziona ni maadili anavyodanganywa na umimi na shetani. “Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa” (Yoh 3:20).
Mara nyingi mtu anateseka pia kwa kuwa anashindwa kuelewa sababu ya Mungu kumjaribu vile, kwa mfano wa hakimu asiye na huruma. Kwake ni vigumu kusadiki kimaisha wema wa Mungu: hata akiambiwa ukweli huo anauona ni nadharia tu, kumbe anajisikia haja ya kuung’amua kwa faraja kidogo. “Tabu hiyo ni kali sana kwa roho iliyo chafu bado, inapomiminiwa huo mwanga unaotakasa. Kwa kuwa usafi huo unaojiambatanisha na uchafu ili kuumaliza, unaionyesha vizuri roho ilivyo chafu na nyonge hata ikadhani Mungu anaiwinda kama adui yake” (Yohane wa Msalaba).
Hofu ya kukubali vishawishi
[hariri | hariri chanzo]Tabu hiyo ya ndani inazidishwa tena na hofu ya kukubali vishawishi vinavyojitokeza wakati huo dhidi ya imani, tumaini na upendo. Katika hali hiyo chungu, mtu anaona vizuri kwamba pengine amevipinga, lakini anahofia kuwa pengine amevikubali. Hofu hiyo inamfadhaisha kwa jinsi anavyompenda Bwana tayari, asitake kuchukiza ukuu wake wala kudharau wema wake. Ndiyo sababu, wakati kilele cha roho kina tendo la imani iliyoangazwa na kipaji cha akili, lililo tendo sahili la kuzamia mafumbo kwa ukavu na bila kujitambua, mtu anajiona kama ameachwa na Mungu. Anayejaribiwa hivyo ana mawimbi ya kwenda na kurudi kama roho za toharani ambazo, zikisukumwa na upendo zimuelekee Mungu, zinajisikia kurudishwa na unyonge wao. Katerina wa Genoa alisema hizo zina tabu kubwa ambayo haieleweki kwa yeyote duniani tena inaongezeka kadiri ya maendeleo ya utakaso, kwa kuwa ndani mwao hamu ya Mungu inakua; lakini hata furaha takatifu inakua kwa sababu zinazidi kujali matakwa ya Mungu kuliko tabu yao. Yeye anang’oa mzizi wowote wa umimi hata kusababisha rohoni “tendo la mwisho la upendo ambalo anamalizia kuitakasa”.
Kwa kawaida kiongozi wa Kiroho hawezi kumfariji mtu anayeteseka hivyo; akisema juu ya matokeo matukufu ya jaribu hilo, na juu ya nuru tamu atakayoikuta baada ya handaki hilo, mhusika haelewi kwa jinsi alivyozama katika mateso yake. Hawezi kufarijiwa kibinadamu ila kwa uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu na kwa matendo sahili ambayo huyo anasababisha ndani yake. “Roho zinazotembea mwangani zinaimba tenzi za mwanga; kumbe zinazotembea gizani zinaimba tenzi za giza. Tuache hizo na hizo vilevile ziimbe mpaka mwisho sehemu na maneno zilivyopangiwa na Mungu. Tusiweke chochote katika vile anavyojaza mwenyewe; tuache matone yote ya hiyo nyongo ya machungu ya Kimungu yatonetone hata kulevya… Roho tu anayetia uchungu, ndiye anayeweza kufariji. Maji hayo mbalimbali yanabubujika toka chemchemi moja” (Jean Pierre Caussade).
“Naua mimi, nahuisha mimi, nimejeruhi, tena naponya, wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu” (Kumb 32:39). “Wewe unayo mamlaka juu ya uhai na mauti, watelemsha mpaka malango ya kuzimu, na kuleta juu tena” (Hek 16:13). Ndiyo yanayotokea katika usiku wa roho, ulio kifo cha fumbo na unaoandaa kuingia undani wa muungano na Mungu. Aliyeondolewa umimi wote anafikia unyofu mkuu. Kinyago chochote kimeanguka; mtu hana tena chochote cha kwake, yuko tayari kumpata Mungu, walivyofanya mitume waliojieleza kuwa “kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote” (2Kor 6:10). Utupu anaouona ndani unamfanya amtamani zaidi Mungu.
Thibitisho
[hariri | hariri chanzo]Hayo yote yanaweza kuthibitishwa namna mbalimbali. Kwanza kwa dogma ya toharani.
Pili kwa maneno ya Yohane wa Msalaba: “Katika usiku wa roho Mungu anamuangaza na kumtakasa mtu kama anavyowaangaza malaika; lakini malaika mbinguni yuko tayari kupokea mwanga huo, kumbe mtu akiwa bado mchafu hawezi kuupokea pasipo uchungu, kama vile macho mabovu yanayopokea mwanga mkali mno”. Tukiupokea mwanga huo wa Mungu, kwa kawaida hatutambui kwamba anatuangaza, lakini tunaangaziwa neno fulani la Injili, na hiyo ni ishara ya kupokea neema ya mwanga.
Tatu kwa mfano wa usiku wa kawaida unaotusaidia kuelewa ule wa roho, ambapo tunaona mbali kuliko wakati wa mwanga uliotangulia; ni lazima tuondolewe mianga ya chini ili tuanze kuona ukuu wa anga la Kiroho. Mitume walipokosa kuuona tena ubinadamu wa Yesu walianza kuchungulia ukuu wa umungu wake, na siku ya Pentekoste wakaangazwa na kuimarishwa vizuri hivi hata Mt. Petro aliwahubiria waliokuwa hekaluni, “mlimwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake” (Mdo 3:15). Tena, kesho yake: “hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” (Mdo 4:12). Mahubiri ya namna hiyo yanatokana na kuzamia fumbo la Kristo. Ndivyo inavyotakiwa kuwa ili hotuba ziwe hai na za dhati; lakini hiyo haitokei kikamilifu kabla roho haijatakaswa. “Kabla mtu hajafikia huo ulinganifu wa juu, anatakiwa kuachana na wingi usiolingana wa aina mbili: ule wa wingi wa vitu vya nje… na ule wa wingi wa mawazo yanayofuatana; ni lazima afikie mtazamo sahili wa ukweli” (Thoma wa Akwino). Sadaka hiyo maradufu ya hisi na ya mifuatano ya mawazo inafanyika polepole katika sala, hata akili ifikie kupima yote Kiroho: “Mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu. Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo” (1Kor 2:15-16).
Yohane Tauler pia alieleza hayo kwa mtu, ambaye anajaribiwa na kujiona anasali bure, kwamba hata hivyo anatafutwa na Mungu na akimuitikia kwa unyenyekevu na tumaini kama mwanamke Mkananayo, “yatatokea yote unayoyataka na jinsi unavyotaka, kwa kuwa Bwana anasema, kadiri ulivyoachana na ya kwako, inakubidi uingie yaliyo yangu… Kadiri mtu anavyojikana na kutoka nje yake mwenyewe, ndivyo Mungu anavyoingia kweli ndani yake”. Neema hiyo ya kujikana ndio utekelezaji wa neno la Injili, “Amin, amin, nawaambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyohiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yoh 12:24). Heri kifo kinachofuatwa na ufufuko huo wa Kiroho!
Maelekezo kwa wakati huo mgumu
[hariri | hariri chanzo]Elekezo la jumla kwa uongozi wa wanaojaribiwa hivyo ni kwamba tuwatendee kwa huruma nyingi na tuwasaidie kupokea matakwa ya Mungu.
Elekezo la kwanza ni kwamba wakubali kwa moyo jaribu hilo kwa muda ule wote ambao atataka udumu, na waishi kwa kujiachilia mikononi mwake. Kadiri watakavyokubali utakaso huo, utawahi kwisha, kwa kuwa lengo alilokusudia Mungu litafikiwa mapema zaidi. Kama ule wa toharani, kwa kawaida utakuwa mfupi kadiri ulivyo mkali, isipokuwa kama mtu atatakiwa kuteseka kwa ajili ya wakosefu, mbali ya utakaso wake binafsi.
Kuhusu kujiachilia tuepe hatari mbili zinazopingana. Utulivu wa kupita kiasi unakanusha haja ya mchango wetu na kufikia hatua ya kudai eti! Tujinyime tumaini na hamu ya kuokoka. Kumbe hapo tunapaswa “kutarajia yasiyoweza kutarajiwa” (Rom 4:18). Kinyume cha kosa hilo ni lile la kuzidisha haja ya mchango wetu kwa kupunguza ile ya sala na kupuuzia nguvu ya dua zetu kwa jinsi Mungu anavyoongoza yote.
Tuongeze maelekezo matatu kuhusiana na maadili ya Kimungu ambayo tuyaishi hasa katika usiku wa roho, tamko la mtume linapotimia kwa namna ya pekee, “Haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani” (Rom 1:17). Usiku wa roho ni usiku wa imani kuhusu mafumbo yanayoonekana giza kadiri yalivyo ya juu kuliko hisi. “Imani inahusu yasiyoonekana” (Thoma wa Akwino). Tunayoyaona hayahitaji kushuhudiwa tuyasadiki.
Imani katika fumbo la msalaba
[hariri | hariri chanzo]Basi, katika jaribu hilo ni lazima tusadiki kwa uthabiti yale ambayo Mungu ametuambia kuhusu manufaa makubwa ya msalaba unaotakasa katika maisha ya Kanisa na katika yale ya Kiroho ya kila mtu. Ili imani hiyo isiwe ya nadharia tu tujisemee, Msalaba ni wa lazima na wa kufaa kwangu. Tusadiki kwamba ni vema kwetu kutakaswa kwa uchungu hivi, kwamba hiki ni kitambulisho kimojawapo cha watoto wa Mungu, tena kwamba utakaso huo wa dhati na mchungu unamtukuza Bwana. “Kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye” (Rom 8:17). Kama vile neema inayotia utakatifu ni kushiriki umungu na kufananishwa na Mungu, vilevile kadiri inavyotokana na Yesu Msulubiwa na inavyotufananisha naye inatuandaa kubeba msalaba kama yeye. Kwa maana hiyo inaongeza namna maalumu kwa neema inayotia utakatifu ya watu wa kwanza.
Hivyo tunakuja kufahamu fumbo la ukombozi kwa namna hai na ya dhati zaidi, kama kwa kuling’amua. Tunakuja kuelewa Wayahudi walivyodanganyika kumlilia Bwana, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani” (Math 27:40). Kinyume chake wangepaswa kumkiri kama akida alipomuona alivyokufa, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Mk 15:39). Siku ya Ijumaa Kuu ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na shetani ulikuwa mkubwa kuliko ule alioupata dhidi ya kifo kwa ufufuko wake.
Basi, msalaba ni kitambulisho cha Mkristo aliyelinganishwa na Mwokozi wake, na zifuatazo ni dalili za uteule: kuvumilia tabu kwa upendo wa Mungu; kupenda maadui bila kujali matusi na masingizio yao; kupenda mafukara, hasa ikiwa uchungu unasukuma kuwasaidia. Kwa hiyo, kwa mfano wa watakatifu, katika usiku wa roho tunapaswa kutazama mara nyingi mateso ya Yesu na kuomba mwanga wa kuelewa kwa dhati alivyojishusha na alivyozaa kwa njia hiyo matunda ya ukombozi yasiyohesabika.
Tumaini imara na sala ya kudumu
[hariri | hariri chanzo]Katika huo utakaso mchungu tunapaswa pia kutumaini yale yasiyotumainika kibinadamu na kuomba msaada wa Mungu bila kuchoka. Ndivyo alivyofanya Abrahamu alipojaribiwa kwa kudaiwa amchinje mwanae. Kama ilivyomtokea mwanamke Mkananayo, mwanzoni Mungu anaonekana hasikilizi; kumbe anataka kupima tunavyomtumainia; na wakati huohuo tukimuomba anatujalia neema ya kuzidi kusali, jambo ambalo linashuhudia tayari kuwa anataka kutusikiliza.
Tunapaswa kuomba watakatifu watuombee, hasa waliojaribiwa hivyo. Tunapaswa kusali inavyofundisha liturujia, inayozidi kudhihirisha ubora wake kwa wanaovumilia jaribu hilo. “Ee Bwana, nakuomba sana, uniokoe nafsi yangu. Bwana ni mwenye neema na haki, naam, Mungu wetu ni mwenye rehema” (Zab 116:4-5). “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu… Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji” (Zab 23:1,4). Tukisali hivyo, tumaini litatakasika na kuimarika ndani yetu; badala ya kujinyima hamu ya wokovu tunatakiwa kumtamani Mungu kwa usafi na nguvu zaidi na zaidi. Bila shaka hatupaswi kumlenga kwa faida yetu kwanza, kama tunavyotamani tunda linalohitajika kulindia uhai wetu, bali tutamani kumpata akiwa ni wema mkuu ili tumtukuze milele. Hivyo sababu ya upendo inainua ile ya tumaini bila kuiangamiza.
Upendo wa kulingana na matakwa ya Mungu
[hariri | hariri chanzo]Hatimaye katika jaribu hilo tunahitaji kupenywa na neno la Yesu, “Chakula changu ndicho hiki: niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yoh 4:34). Katika tabu na machungu ya roho tunapaswa kujilisha matakwa ya Mungu ili yatawale ya kwetu na umimi wote ukome moja kwa moja. Itatokea hivyo tukikubali kwa upendo wa Mungu tutende na kuteseka yale yote anayotaka kadiri tunavyoonyeshwa na utiifu, na matukio na mwanga wa ndani wa Roho Mtakatifu.
Hivyo wakati huo tuchimbe Heri Nane na kukariri maneno ya Mt. Paulo, “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?… Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni dhiki, au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?… Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rom 8:31,35,37-39).
Ni vema pia tumuombe Mungu upendo kwa msalaba, hamu ya kushiriki jinsi Mwanae alivyojishusha kadiri anavyotutakia. Tena tumuombe katika hamu hiyo tuone nguvu ya kuvumilia yoyote yanayoweza yakatokea, tuyavumilie kwa amani na hata kwa furaha ili kuinua moyo wetu na wa wale wanaotujia.
“Kabla utashi wetu haujakumbatia aibu na sadaka za kila aina, kazi ya Mungu haikamiliki rohoni au inafanyika kidogo tu. Kuvumilia tabu ni hatua fulani, lakini haitoshi. Kwa uvumilivu tunaweza tukafikia utakatifu, lakini njia pekee ya kuinuka juu yetu ni kuungana na kushiriki sadaka ya Yesu Kristo. Ndiyo nguvu yetu na chanzo cha ule uzima wa Kimungu unaojijenga juu ya magofu ya umimi wetu… Kuimarisha utashi wetu kuhusu karaha za umbile letu ni jambo linalopatikana tu kwa sala ya kudumu isiyochoka, kwa kutojiamini kabisa na kwa kumtumainia Mungu kadiri ya uweza wake usio na mipaka” (Maria wa Kutungwa Mimba). Hapo jaribu hilo gumu tutaliona kuwa jema, au walau tutasadiki linatufaa na kututakasa. “Msalaba una usalama. Msalaba una uzima. Msalaba unakulinda na maadui wote. Msalaba unakujaza utamu wa mbinguni. Msalaba una maadili yote. Msalaba una utakatifu kamili… Hakuna mtu mwenye kufahamu moyoni mwake mateso ya Yesu kama yule aliyepata kuteseka vilevile… Mateso yanayopatikana sasa hayafanani na utukufu wa siku za mbele” (Kumfuasa Yesu Kristo II,12:2,5,10).
Utakaso huo mchungu kwa kuondoa umimi na kiburi unafanya nafasi kubwa rohoni na kututia hamu ya Mungu iliyo kubwa zaidi na zaidi. “Kama vile mtu anavyoweza kukamilishwa na wema wa Mungu tu, vivyo hivyo wema huo hauwezi kutekeleza ukamilifu wake kwa nje kuliko kwa ubinadamu wetu. Huo unahitaji sana na unaweza sana kupokea mema, nao wema una ukarimu mkubwa na elekeo kubwa la kuzawadia. Hakuna kinachoufaa ufukara kuliko utajiri mkarimu, wala hakuna kinachoupendeza utajiri mkarimu kuliko ufukara wenye kuhitaji… Kadiri fukara anavyohitaji anatamani kupokea, kama vile utupu unavyotamani kujazwa. Basi ni mkutano mtamu na wa kutamaniwa ule unaofanyika kati ya utajiri na ufukara; hata karibu isingewezekana kusema upi unafurahi zaidi: kama ni wema tajiri unapoenea na kujishirikisha, au kama ni upungufu wenye kuhitaji unapopokea. Lakini Bwana wetu amesema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea’ (Mdo 20:35). Basi, wema wa Mungu unafurahia kutugawia neema kuliko sisi kuzipokea” (Fransisko wa Sales). Nafasi inayopatikana katika mtu aliyevuliwa umimi na kiburi inamwezesha kupokea zaidi na zaidi wingi wa upendo. Kwa maana hiyo “Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Mith 3:34; Yak 4:6; 1Pet 5:5), naye anawanyenyekesha ili kuwajaza.
Hayo yote yanathibitisha kwamba, “Upendo kwa Mungu unaunganisha, kwa kuwa unainua mapendo yetu kutoka mema mengi hadi wema mkuu; ndiyo sababu maadili yanayotokana na upendo yanafungamana. Kinyume chake kujipendea kunabomoa, kunatawanya na kupotosha mapendo yanayolenga viumbe vingi na vya kupita” (Thoma wa Akwino). Upendo wa Mungu unazidi kung’arisha ndani mwetu mwanga wa akili na ule wa neema, kumbe dhambi inachafua roho na kuiondolea uangavu huo wa Kimungu. Utakaso wa roho tuliouzungumzia unauondoa uchafu uliomo ndani mwa vipawa vyetu vya juu viweze kung’aa kwa mwanga wa kweli.
Matokeo ya roho kutakaswa hasa upande wa maadili ya Kimungu
[hariri | hariri chanzo]Kisha kueleza utakaso huo na uongozi unaohitajika, tuseme matokeo yake ni yapi ukivumiliwa kwa moyo. Ndiyo lengo la Mungu katika kuwatakasa watumishi wake, kwamba upande wa juu wa roho uinuliwe kuliko umbile lake na kuandaliwa uungane na Mungu, kama vile hisi zilivyohitaji kutiishwa chini ya roho. Kati ya matokeo hayo, mengine ni ya kubomoa, yaani kukomesha kasoro, na mengine ni ya kujenga, yaani kukamilisha maadili yaliyomo upande wa juu wa roho.
Matokeo ya kubomoa
[hariri | hariri chanzo]Matokeo hayo yanajitokeza kwa kuzidi kupunguza mitawanyiko ya mawazo, upumbavu wa roho, na haja ya kujimwaga nje na ya kufarajika. Polepole umimi unakwisha. Mtu hadanganyiki kama awali, kwa kuwa anazidi kuishi kadiri ya upande wa juu wa roho, ambamo adui hawezi kuingia ila Mungu tu. Bila shaka adui anazidisha vishawishi vyake, lakini mtu akikimbilia kiini chake mwenyewe anamokaa Mungu, adui hawezi kumdhuru wala kujua kinachotokea ndani mwake; sanasana anaweza kushuku, kwa sababu siri za moyo ziko nje ya uwezo wake. Utakaso huo unafuta kasoro nyingine nyingi: zile zinazohusu mafungamano na majukumu; ukali wa silika unaoelekeza kukosa subira; kiburi cha chinichini kinachosababisha vurugu na mashindano; pia kutojali shida (pengine kubwa) za jirani anayeomba msaada. Hapo mwenye jukumu la kusimamia wengine na kujitoa kwa ukarimu anaelewa kwa dhati maneno ya Yesu: “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya” (Yoh 10:11-12). Ili tufaidike na maneno hayo tumuombe Bwana atuzidishie ari halisi, ambayo ina subira na upole, si umimi, inachota uzima ndani ya Mungu ili kuushirikisha zaidi na zaidi.
Pengine yanatokea matakaso ya pamoja (k.mf. dhuluma) tunayopaswa kufaidika nayo. Hapo ushujaa wa maadili unakuwa wa lazima, maana tunajikuta katika haja yenye heri ya kugeuka watakatifu tusije tukapoteza roho yetu. Mara nyingi wanaoonekana wema katika hali ya amani, wanajitokeza dhaifu na waoga katika shida hizo kubwa, kumbe wengine wasiotarajiwa wanajitokeza bora. Lakini haiwezekani kamwe kuwa watakatifu pasipo kulingana na Kristo msulubiwa. Utakatifu halisi unadai utakaso uleule katika vipindi vya amani na vile vya vurugu. Watakatifu walioishi katika vipindi vitulivu vya maisha ya Kanisa walipatwa na majaribu ya Kiroho, ambayo wasingekuwa nayo wasingefikia usafi kamili alioutaka Mungu.
Hatimaye kuna majaribu mengine yanayotudai utashi mnyofu tu, k.mf. matukio ya pekee yakitulazimisha kusimama upande wa Mungu kwa sadaka kubwa. Mzee Simeoni alisema juu ya mtoto Yesu, “Huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa” (Lk 2:34). Yaani ilimbidi Yesu, aliyekuja kuokoa wote, asababishe wengine waangukie uasi kwa kukataa kumtambua kuwa ndiye Kristo. Hivyo yalifunuliwa mawazo ya siri ya Mafarisayo ambayo kwa kiasi fulani yangefichika kama wangeishi kabla yake. Kitu cha namna hiyo kinatokea waadilifu na waovu wanapofarakana k.mf. bikira Maria akitokea. Kama Blaise Pascal alivyosema, kuna mwanga wa kutosha kwa wanaotaka kuona, na giza la kutosha kwa wasiotaka. Matukio hayo yanathibitisha maelezo yetu kuhusu roho kutakaswa, kwa kuwa ziara za Bwana “ni za aina tofauti: za kufariji… za kukosoa… na pengine za kuhukumu” (Thoma wa Akwino). Huenda akatutembelea ili kutufariji, kama katika maono ya Lurdi, lakini tusipofaidika anaweza akatuadhibu, na tusipofaidika tena anaweza akatuhukumu.
Hayo yanaonyesha tunavyopaswa kujitahidi tufaidike na majaribu tunayoletewa na Bwana, hasa katika kipindi kirefu cha usiku wa roho tunachozungumzia. Tukikivumilia kwa moyo, kasoro nyingi zinazozuia ustawi wetu zitang'olewa moja kwa moja: hapo umimi utauachia nafasi upendo wenye ari.
Matokeo ya kujenga
[hariri | hariri chanzo]Matokeo hayo ni hasa ustawi wa kasi wa maadili yaliyomo upande wa juu wa roho (kwa namna ya pekee unyenyekevu, ibada na yale matatu ya Kimungu) ambayo yanatakaswa kikamilifu yaache kutegemea sababu za kibinadamu ambazo ni za ziada tu na zinafanya yatekelezwe kibinadamu mno. Kwa mfano, wengine wanahudhuria misa kila siku kwa sababu ni jambo jema, lakini pia kwa sababu ni desturi ya mazingira wanapoishi, kiasi kwamba kama desturi hiyo ingekoma, labda wangeacha kuhudhuria kila siku. Kumbe ni lazima maadili yatekelezwe zaidi na zaidi kwa upendo wa Mungu, mbali na sababu za chini. Hapo inazidi kujitokeza sababu hasa ya kila moja kati ya maadili matatu ya Kimungu: ukweli mkuu unaojifunua kama sababu ya imani, uweza usio na mipaka unaokuja kusaidia kama sababu ya tumaini, na wema mkuu unaopendeza mno kama sababu ya upendo.
Lakini kwanza kuna utakaso wa namna hiyo katika unyenyekevu. Ili kiburi chote kifukuzwe ni lazima Bwana alete uvuvio maalumu wa vipaji vya elimu na akili ambavyo anatuonyesha wazi unyonge wetu kiasi tusichoweza hata kudhani, na anatuangazia moyoni vificho vya kasoro za hatari. Ni kama mwali wa jua ambao ukipenya chumba chenye giza unaonyesha mavumbi yote ambayo yanaelea hewani lakini hayakuweza kutambulika kwanza. Kwa mwanga huo unaotakasa tunaona ndani mwetu rundu ya kasoro tusizokuwa tumezizingatia; tunaabika kiasi cha kutouvumilia.
Ndio utakaso wa ule unyenyekevu wa kununa tu ambao tunajiweka pembeni kwa sababu hatukubaliwi. Hapo unakuwa unyenyekevu halisi wa moyo unaopenda kuwa si kitu ili Mungu awe yote. Unainamia ukuu usio na mipaka wa Aliye Juu na yale yote ya kwake yaliyomo katika kila kiumbe. Hapo tunang’amua kwamba kwa nguvu zetu tu hatuwezi kutenda lolote la kustahili uzima wa milele. Tunaona ukweli wa fundisho la Kanisa kwamba hata mwanzo wa wokovu unategemea neema tu na kwamba inahitajika zawadi ya pekee ili kudumu mpaka mwisho. Tunakuja kuelewa kuwa neema, mbali na kuwezeshwa na ridhaa yetu, ndiyo inayosababisha ridhaa hiyo: “ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Fil 2:13). Katika kipindi hicho, mtu anapopambana na vishawishi vikali vya kukatisha tamaa, anahitaji kuusadiki huo uwezo wa Kimungu wa neema unaomuinua aliye dhaifu aweze kutekeleza amri na kugeuka.
Ndivyo unyenyekevu unavyostawi hatua kwa hatua hadi ushujaa. Unadai uvuvio maalumu wa Roho Mtakatifu na utakaso wa Kimungu tunaouzungumzia. Wenyewe upo katika njia ya kawaida ya kufikia utakatifu; ukamilifu wa Kikristo haupatikani bila unyenyekevu wa namna hiyo. Katika watakatifu wote tunaona unyenyekevu huo mkubwa unaotokana na kuzama katika kweli kuu zifuatazo: 1) Tumeumbwa na Mungu kutoka utovu wa vyote naye anatudumisha kwa hiari yake. 2) Pasipo msaada wa neema yake hatuwezi kutenda lolote la kustahili wokovu. Hapo wanafikia kutambua kuwa neema inatolewa bure na kutenda yenyewe, na kuwa bila neema hawawezi kusonga mbele ila kurudi nyuma tu. Unyenyekevu uliotakaswa hivyo unaimba utukufu wa Mungu kuliko nyota za angani.
Kuna utakaso wa namna hiyo kwa adili la ibada pia. Ni lazima iwepo ibada halisi, yaani utayari wa utashi katika kumtumikia Bwana, hata isipokuwepo ibada ya kihisi wala faraja za rohoni kwa miezi na miaka. Hapo uvuvio wa kipaji cha ibada unakuja kusaidia adili la ibada; unatufanya tudumu katika sala bila kujali ukavu mkubwa wa roho. Ibada hiyo ya dhati inazaa heri ya upole.
Utakaso wa imani
[hariri | hariri chanzo]Kama vile Bwana anavyowafundisha marafiki wake kuwa wapole na wanyenyekevu wa moyo, ndivyo pia anavyotakasa imani yao. Waamini wote wanayasadiki yaliyofunuliwa na Mungu, lakini wachache tu wanayaishi mafumbo yaliyoshikwa na imani. Sanasana wengi wanazingatia kweli zinazoeleweka (k.mf. uwepo wa Mungu na maongozi yake) na wanaishia upande wa nje na wa hisi wa ibada za Kikristo. Imani dhaifu haituwezeshi kuishi kweli mafumbo ya Utatu Mtakatifu, umwilisho, ukombozi, ekaristi na uwemo wa Roho Mtakatifu ndani mwetu. Tunaweza tukayataja kwa moyo wa ibada, lakini kwetu ni hafifu, si hai, na kweli zake ziko mbali kama nyota: hayajawa vya kutosha mwanga wa uzima, msingi wa machaguo yetu na vipimo vya kawaida vya mawazo yetu.
Halafu sababu ya kusadiki mafumbo hayo ni kuwa Mungu ameyafunua kwetu, lakini tunaishia mno kutegemea sababu nyingine zinazotusaidia: kwanza imani iliyoenea katika mazingira yetu; halafu uwiano kati ya dogma zipitazo akili na kweli zinazoeleweka; hatimaye mang’amuzi ya kazi ya Mungu ndani mwetu. Kama angetuondolea ghafla sababu hizo zote za ziada na katika ukavu wa roho wa miezi na miaka tusingesikia tena faraja yake ndani yetu wala kuona ulinganifu wa mafumbo yapitayo maumbile na kweli za kimaumbile, tendo la imani lingekuwa gumu. Ndivyo ilivyo hasa mwanga wa Mungu unaotakasa unapokuja kuyaangazia katika mafumbo hayo yale ambayo ni ya juu zaidi na yanaonekana kutolingana na akili, kama vile haki yake upande mmoja na uteule usiostahilika upande mwingine. Tena katika jaribu hilo shetani anajitahidi kutupotosha kwa kutuonyesha eti! Haki ya Mungu ni kali mno. Kana kwamba walaaniwa wanaomba msamaha wasiupate, wakati kwa kweli hawauombi kamwe. Vilevile adui anajitahidi kutuonyesha kuwa ugawaji wa neema haukubaliki wala haufai. Tena kuwa Mungu mwema mwenye uweza wote asingeruhusu mabaya yote yanayotukia ulimwenguni; shetani anayazidisha ili kuleta hoja mpya. Anafanya tusikie noti mbaya ili ivuruge ulinganifu bora wa mafumbo ya imani. Akitaka tusadiki hakuna kitu kisha kufa, anajitahidi kuthibitisha udanganyifu huo wa kutisha. “Siku hizi pazia nzito na nyeusi imefunika roho yangu maskini… Hakika moja tu imeonekana kunipata: kwamba mambo yote ya Kimungu hayapo… Hiyo imenipata nitake nisitake, kama aina ya hakika isiyopingika ambayo sina budi kuikubali… Ni kama kubomoka kwa imani yangu niliyoipenda sana, ambayo kwa muda mrefu iliongoza maisha yangu… Lakini pengine wazo likanijia: kwamba ningekubali minong’ono hiyo, ningetia shakani maneno ya Bwana wetu ambaye alikuwa mtakatifu mno asiweze kudanganya, na hapo nikasikia kama wajibu ulionidai niwe mwaminifu kwake kwa heshima ya kupendana kwetu, kwa kuwa tumetoleana nafsi zetu. Hapo nikaweza kusema, Bwana, nasadiki, nataka kusadiki, lakini zidisha imani yangu” (Fransiska wa Yesu).
Mtu anajikuta kati ya athari mbili zinazopingana: ile ya mwanga wa Mungu unaomtakasa kwa kurusha akili yake katika vilindi visivyodhanika vya mafumbo kama vile angetupwa baharini bila kujua kuogelea; na ile ya shetani anayejitahidi kupotosha athari ya mwanga huo. Inabaki sababu moja tu ya kusadiki, yaani kwamba Mungu amefunua hayo. Hapo ni lazima kuomba neema ya msaada inayosababisha tendo la imani, neema ya kushinda na kama kuruka kishawishi badala ya kukifikiria, neema ya kuambatana na ukweli wa Mungu uliojifunua, na mamlaka yake ya kujifunua, juu kuliko dhana zetu finyu kuhusu ukamilifu wake. Hapo mwanasala anapokea mwanga upitao maumbile wa kipaji cha akili ambao kwa kumfunulia roho ya Neno la Mungu, unamlazimisha kuvuka herufi zake na kawaida ya kumfikiria Mungu kibinadamu. Katika huo usiku wa roho, mtu yuko katika mshangao: mwanga ni mkali mno kwa macho yake dhaifu bado. Lakini atalitoka jaribu hilo akiwa na ujuzi wa juu na imara zaidi kuhusu kweli za imani, akipita maneno ya dogma asadiki kwa dhati na kuishi mfululizo mafumbo yanayotolewa katika matamko hayo. Polepole anapata kimbilio katika yule asiyebadilika, katika ukweli mkuu, katika Neno lisiloumbwa lenye kuleta ufunuo, linalojulisha k.mf. kwamba Mungu akiacha mabaya yoyote yatokee ni kwa ajili ya mema makubwa zaidi ambayo aliyaona nasi pia tutayaona milele; pengine tunayachungulia katika usiku wa roho.
Hapo imani inaondolewa takataka yote; haiishii tena kwenye sababu za ziada za kusadiki (ambazo kwa sasa zimetoweka) wala upande wa hisi wa mafumbo ya umwilisho, ukombozi na ekaristi, bali inapenya vilindi vya ufunuo. Ndivyo imani ya mitume ilivyotakaswa katika jaribu chungu la wakati wa mateso, ambapo Yesu, ambaye watatu kati yao walimtazama mtukufu mlimani, alionekana kudhalilishwa na kuangamizwa. Bila kujali hayo, walitakiwa kusadiki, kama bikira Maria aliyesimama imara katika imani, kuwa yeye ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili na kuwa atafufuka siku ya tatu. Hata baada ya Kupaa Bwana, walipoondolewa fursa ya kumuona Yesu mfufuka, walipaswa kuishi katika giza la imani ambayo tangu Pentekoste wakaja kuitangaza kwa hakika hadi kuifia. Watakatifu waliofuata walipitia majaribu ya aina hiyohiyo, k.mf. M.H. Henri Suso kwa miaka kumi.
Mwishoni mwa jaribu hilo, imani imezidishwa mara kadhaa. Ili kuona uangavu wa mafumbo ya Mungu, ni lazima akili iwe imetoa sadaka yake kwa kujinyima kufuata macho yake na kwa kupokea kwa unyenyekevu mwanga wa Mungu. Ndio uongofu wa tatu ambapo maadili ya Kimungu yanatekelezwa kwa namna bora kuliko awali. Bwana analima tena palepale lakini kwa ndani zaidi ili mbegu anayotia ardhini izae si kumi wala thelathini, bali hata sitini na mia (taz. Mk 4:8). Hapo mtu anaanza kumtazama Mungu kwa dhati zaidi, kwa namna ambayo inaelekea kuwa ya kudumu, na ni kama kuongea naye mfululizo. Hekima hiyo ndiyo “lulu nzuri” ambayo tuuze vyote ili kuinunua (Math 13:45).
Utakaso wa tumaini
[hariri | hariri chanzo]Baada ya matokeo ya utakaso wa imani, yanaanza kujitokeza yale ya utakaso wa tumaini. Anayesadiki kuwa jambo muhimu pekee ni utakatifu na wokovu, anaweza akajiuliza kama ataweza kudumu mpaka mwisho kati ya majaribu anamojikuta.
Tumaini ni adili la Kimungu ambalo tunamlenga Mungu kama heri yetu, tukitegemea huruma yake na uweza wake usio na mipaka unaotusaidia ili tumfikie. Shabaha kuu ya tumaini ni kumpata Mungu milele; sababu yake ni Mungu kusaidia, kama vile sababu ya imani ni Mungu kuwa ukweli mkuu unaojifunua.
Kila Mkristo mwema ana adili hilo la kumiminiwa pamoja na upendo; na anapoomba neema zinazohitajika kwa wokovu anamtumaini Mungu mwenyewe. Lakini mara nyingi tumaini linakosa ukuu wake, kwa maana tunatamani mno malimwengu kadhaa yanayoonekana kuufaa wokovu wetu, kumbe sivyo; pengine tunatamani mema ya kibinadamu yanayoweza yakatudhuru na kuzuia mema ya juu yanayotokana na sisi kujibandua na yote na kuwa wanyenyekevu. Hapo tumaini linapungukiwa msukumo lisiweze kuruka moja kwa moja kwa Mungu.
Tena mara nyingi lina takataka fulani upande wa sababu yake, kwa kuwa tunatumaini msaada wa Mungu, lakini pia tunategemea kupita kiasi sababu za chini zisizo na hakika; tunajiamini mno, pamoja na uwezo wetu, maadili yetu na misaada ya kibinadamu tunayoweza kuipata; vilevile tunakata tamaa tukishindwa au tukikosa misaada hiyo. Ikiwa Mungu, kusudi atakase tumaini letu, anatuondolea ghafla malimwengu tuliyoyatumainia pamoja na sababu hizo za chini zilizotutumainisha (k.mf. wema na misaada ya marafiki, himizo na heshima ya wakubwa); na wakati huohuo anatuonyesha udhaifu wetu kwa kiasi tusichodhani; tena akiacha yatokee maradhi, masingizio na upinzani mkali dhidi yetu: je, tutaendelea kutumaini, mbali na tumaini lolote la kibinadamu, kutokana na sababu moja tu, yaani kuwa Mungu anabaki daima msaidizi wetu asiyeshindwa, litokee lolote lile?
Ndio wakati wa kujisemea, “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi” (Mao 3:22). “Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili” (Zab 103:8). “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1Kor 10:13). Yeye haruhusu kamwe tujaribiwe kupita uwezo wetu unaotegemezwa na neema yake; anatusaidia daima tupate wokovu; hatuachi kamwe kwanza; anataka kutuinua toka maanguko yetu kila tunapomlilia. “Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa, bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye” (Isa 54:10). “Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, atanisitiri katika sitara ya hema yake, na kuniinua juu ya mwamba… Bwana, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, bali Bwana atanikaribisha kwake” (Zab 27:5,8-10).
Watakatifu walitumaini hivyo katika majaribu makuu. “Nilisema nguvu zangu zimenipotea, na tumaini langu kwa Bwana. Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, pakanga na nyongo… Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana na kumngojea kwa utulivu… Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake haupendi kuwatesa wanadamu, wala kuwahuzunisha” (Mao 3:18-19,26,31-33). Ndivyo Yohane Mbatizaji alivyotumaini gerezani, alipoyaona yale yote yanayopinga ujio wa ufalme wa Mungu alioutangaza. Ndivyo Mt. Yohane wa Msalaba alivyotumaini gerezani, yote yalipoonekana kuchangia maangamizi ya urekebisho wa Karmeli. Ndivyo Alfonso Maria wa Liguori alivyotumaini shirika lake lilipoonekana kukoma. Ndiyo sadaka ya Isaka ambayo Mungu anawaomba tena watumishi wake ili wafanye kazi waliyokabidhiwa si kama kazi yao, bali kama kazi yake ambaye anaweza kushinda mapingamizi yote na hakika atayashinda kama ameamua milele kazi hiyo ifanikiwe.
Hapo, juu ya sababu yoyote ya kutumaini, inazidi kujitokeza sababu halisi ya tumaini la Kikristo, yaani Mungu aliye tayari kusaidia kutokana na uweza wake na stahili za Yesu zisizo na mipaka. Hapo mtu anajisikia kurudia sala ya Esta, “Bwana wangu, wewe peke yako u mfalme wetu, unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila wewe, maana hatari yangu imo mikononi mwangu… Ee Mungu, uweza wako ni juu ya yote; isikie sauti yao wasio na tumaini, utuokoe mikononi mwao wafanyao maovu, uniokoe katika hofu yangu” (Est 4:17l,y). Hapo tumaini linageuka kujiachilia kikamilifu kwa Mungu kuhusu kazi yake duniani na kuhusu wokovu wa milele.
Vilevile tunaposaidia wagonjwa mahututi tunatakiwa kuwaombea tumaini hilo la kujiachilia kikamilifu, na kadiri utashi wao unavyolingana na matakwa ya Mungu yaliyokwishajulikana, uko tayari kujiachilia kwa yale yasiyojulikana bado. Hivyo mtu anajiinua juu ya giza la dunia, udanganyifu na dhambi, ajizamishe katika giza la maisha ya ndani ya Mungu na la upendo wake kwa kila mmojawetu. Hapo si kwa nadra mtu anajaribiwa kuhusu fumbo la uteule, kama vile Katerina wa Siena ambaye shetani alimuambia, “Malipizi hayo yanasaidia nini kama hujateuliwa? Kumbe kama umeteuliwa, utaokoka bila hayo”. Mtakatifu akamjibu, “Kama nimeteuliwa, juhudi zako za kunipoteza zinasaidia nini? Kumbe kama sijateuliwa, kwa nini unanishughulikia hivi?” Ni kwamba uteule, kama vile maongozi yote ya Mungu, unahusu si lengo tu, bali pia njia za kulifikia. Kama vile katika maisha ya kawaida hatupati mavuno tusipopanda mbegu, katika utaratibu wa neema wokovu haupatikani pasipo sala na maadili.
Mwishoni mwa utakaso huo wa tumaini, adili hilo limeondolewa umimi uliochanganyikana nalo, pamoja na hamu isiyoratibiwa ya faraja, nalo limekuwa imara zaidi katika usafi wake. Limekuwa hamu motomoto ya kumpata Mungu kuliko zawadi zake; hata hivyo yeye hajitokezi: ndipo yanapoanza kuonekana matokeo ya utakaso wa upendo.
Utakaso wa upendo
[hariri | hariri chanzo]Hasa katika adili hilo matakaso ya Kimungu yanafanana na yale ya toharani, mbali ya tofauti kubwa ya kwamba hayo ya pili hayaongezi upendo wala stahili. Kila Mkristo mwema anao upendo, ambao tunampenda Mungu kwa ajili yake mwenyewe; lakini tunampenda pia kwa sababu anatupatia faraja, tunahisi uwemo wake mwetu, na kazi tunazomfanyia zinafanikiwa na kutufurahisha. Vilevile tunampenda jirani kwa ajili ya Mungu, kwa kuwa anapendwa na Baba yetu sote; lakini tunampenda pia kwa kuwa anaitikia upendo wetu; kumbe asipoonyesha shukrani hatumpendi vya kutosha, ingawa tunapaswa kuwapenda maadui pia na kuwaombea wanaotudhulumu. Maana yake upendo wetu una takataka na hautawali vizuri uchungu au ukali kwa kukosewa adabu.
Hivyo, Bwana anapotaka mtu mwenye tumaini kubwa afikie upendo safi ambao ampende kweli kwa ajili yake mwenyewe kuliko kwa zawadi zake, anamnyima kwa miezi na miaka faraja yoyote ya Kiroho pamoja na hisi ya uwemo wake, ingawa anazidi kuungana naye na kumtendea kwa dhati. Anaonekana kumuacha kama Yesu alipolia msalabani, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” (Zab 22:1). Ni maneno ya Zaburi ya Kimasiya ambayo yanafuatwa na mengine ya tumaini kamili, kujiachilia na upendo, kama ilivyotokea moyoni mwa Yesu. Katika usiku huo wa roho, mtu anapojiona ameachwa na Mungu, anatimiza tendo kubwa la upendo kwa sababu moja tu tena safi, yaani kwamba Mungu mwenyewe ni wema usio na mipaka, bora mno kuliko neema zake zote, na kwamba ndiye aliyetangulia kutupenda. Hivyo, kwa mfano wa Mwanae msulubiwa, anapaswa kumrudishia upendo kwa upendo.
Teresa wa Mtoto Yesu alipitia saa hizo chungu mwishoni mwa maisha yake, alipoandika, “Mungu amependa niyakabili mateso mengi ya aina mbalimbali. Tangu niwepo duniani, nimepata kuteseka sana. Lakini ikiwa utotoni mwangu niliteseka kwa huzuni, sasa siteseki tena kwa jinsi hiyo, bali kwa furaha na amani. Sasa ninafurahi kweli kuteseka… Wakati ule wa furaha wa kipindi cha Pasaka, Yesu alinifahamisha kuwa kweli wapo watu wasio na imani; watu ambao kwa kutotumia vema neema, waliipoteza hiyo hazina ya thamani, iliyo asili ya furaha halisi pekee. Pia Yesu aliruhusu roho yangu ivamiwe na giza jeusi kabisa, hata wazo la mbingu, ambalo awali lilikuwa tamu kwangu, likawa linasababisha tu mahangaiko na mateso. Jaribu hilo limedumu si siku chache wala majuma machache, lisiondolewe mpaka saa iliyopangwa na Mungu mwenyewe, ambayo haijafika. Ningependa kuweza kueleza jinsi ninavyojisikia; lakini, lo! Ninakiri kwamba haiwezekani. Ingembidi mtu apite mwenyewe katika shimo hili la giza ili kuelewa weusi wa giza hili… Hata hivyo, Ee Bwana, huyu mwanao amefahamu mwanga wako wa Kimungu; naye sasa anawaombea hao ndugu zake msamaha. Maana yuko radhi kuula mkate huu wa huzuni, kadiri ya muda wewe utakaoutaka; wala hataki kusimama na kuacha meza hii iliyojaa uchungu ambapo maskini wakosefu watakula mpaka siku ile uliyoipanga. Je, hawezi kuomba kwa ajili yake na kwa niaba ya ndugu zake, akisema, ‘Utuonee huruma, Ee Bwana, maana sisi tu maskini wakosefu! Ee Bwana utuachilie twende zetu tumetakata! Uwajalie wale wote ambao hawajaangazwa na ule mwanga wa imani, siku moja nao wauone uking’aa…’ Moyo wangu unaochoshwa na giza linalouzunguka, ninapotaka kuufariji kwa kuikumbuka ile nchi angavu ninayoitamani, ndipo teso langu linapokuwa maradufu. Inaonekana kana kwamba hilo giza, likiazima sauti ya wakosefu, linanidhihaki likisema, ‘Unaota tu juu ya mwanga, na juu ya nchi ya kwenu yenye manukato mazuri sana; pia unaota kuwa utakaa milele na Muumba wa maajabu hayo yote; isitoshe unasadiki kuwa siku moja utaondoka kwenye ukungu huu unaokuzunguka! Basi, endelea, endelea kuota vile, hata kufurahia kifo, ambacho, ole wako, hakitakupatia yale unayotumaini, bali tu usiku wa giza nene zaidi, usiku wa kutokuwepo kitu chochote kile…’ Adui yangu anaponichokoza, ninajihami kijasiri. Nikifahamu kuwa haifai kukubali kupigana naye, namgeuzia mgongo nisikubali kumtazama usoni; bali ninamkimbilia Yesu wangu. Ninamuambia Yesu kuwa niko tayari kuimwaga damu yangu, hadi tone la mwisho, ili kuiungama imani yangu, kwamba kuna mbingu. Pia ninamuambia kuwa ninaridhika kutoionja duniani humu furaha ya hizo mbingu nzuri ili yeye awafungulie milele wale maskini wasioamini. Hivyo, licha ya kujaribiwa namna hii kwa kuondolewa faraja yangu yote, naweza kupaliza sauti nikisema, ‘Umenifurahisha, Bwana, kwa kazi yako; nitashangilia kwa ajili ya matendo ya mikono yako’ (Zab 92:4). Kwa maana je, iko furaha kubwa kuliko ile ya kuteseka kwa ajili ya upendo wako? Kadiri teso lilivyo la ndani zaidi, na lisivyoonekana na macho ya watu, ndivyo linavyokufurahisha zaidi, Ee Mungu wangu! Lakini, hata kama kweli wewe usingelijua hili teso langu, jambo lisilowezekana, ningefurahi kuteseka, ikiwa kwa kuteseka ningezuia au kufidia dhambi moja ya utovu wa imani… Hivyo basi, ninapoimba juu ya furaha ya mbingu na juu ya kuishi na Mungu milele, sisikii furaha hiyo moyoni, ila tu ninayaimba yale ninayotaka kuyasadiki. Ni kweli kwamba pengine mshale mdogo sana wa jua hutokeza na kuliangaza giza langu; katika kitambo hicho naacha kujaribiwa. Lakini baadaye kumbukumbu ya mwali ule, badala ya kunifurahisha, inasababisha giza langu kuwa hata nene zaidi. Mama mpendwa, nilikuwa sijapata kufahamu jinsi Bwana wetu alivyo mwema na mwenye huruma kweli; maana hakuniletea jaribu hilo kabla sijaweza kulikabili. Kwa kuwa nadhani lingenijia kidogo mapema, lingenitumbukiza katika hali ya kukata tamaa. Kumbe sasa linaniondolea kila kitu ambacho kingekuwa kiridhisho cha kimaumbile kwa hamu yangu ya mbingu”.
Ndio utakaso wa pamoja wa maadili ya Kimungu, ambao kwake uliendana na malipizi kwa ajili ya wakosefu. Humo matendo ya imani, tumaini na upendo ni kama yameunganika katika kujiachilia kikamilifu kwa matakwa ya Mungu kama Yesu msalabani, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46). “Kadiri mtu anavyoelewa ukuu wa Mungu na kuona anavyostahili kupendwa, anazidi kuwaka upendo kwake na kuona tabu ya kutoungana naye bado” (Teresa wa Yesu). Baada ya utakaso huo wa mwisho, upendo kwa Mungu na kwa jirani umeondolewa takataka yoyote kama dhahabu iliyojaribiwa kwa moto, tena umezidishwa.
Tukisifu upendo wa mke wa baharia asiyekoma kumfikiria mumewe, ambaye tangu miezi hana habari zake na huenda akafa, bali anazidi kumpenda na kuwalea wanae wampende kana kwamba yupo; basi, hatuwezi kuacha kushangaa usafi wa upendo wa bibi arusi wa Yesu Kristo ambao utamu wake unageuka nguvu ya kuungana naye katika jaribu lolote, kwa kuwa: “Upendo una nguvu kama mauti… maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, wala mito haiwezi kuuzamisha” (Wim 8:6-7). Msalabani upendo wa Bwana, anayewaunda wafuasi kwa mfano wake, ulikuwa na nguvu kuliko mauti ya roho, dhambi na shetani na kwa ufufuko ukashinda kifo kilicho tokeo la dhambi. Katika kutakaswa na Mungu, watakatifu wanaungana na Kristo katika mateso kabla hawajalinganishwa naye katika utukufu wa milele.
Mateso yanayoweza yakaendana na kutakaswa kwa roho
[hariri | hariri chanzo]Teresa wa Yesu aliposema juu ya utakaso huo hakubainisha vizuri mateso ambayo yanaendana nao mara nyingi lakini si kwa lazima: “Mungu wangu! Jinsi zilivyo kubwa tabu za nje na za ndani ambazo mtu anapaswa kuzivumilia kabla hajaingia makao ya saba! Kwa kweli ninapozifikiria naona kwamba angewahi kuzijua, udhaifu wake wa kibinadamu ungesita kuamua hata kama angeahidiwa faida gani… Kweli katika hali hizo inaonekana yote yamepotea. Ni masingizio ya watu tunaohusiana nao… Wale walioonekana marafiki wanasaliti, tena wanang’ata kwa ukali zaidi; jambo ambalo hakika linaumiza kwa dhati. Ukiwasikia eti! Mtu huyo anadanganyika kwa namna ya pekee. Eti! Yote yanayomtukia yanatoka kwa shetani. Eti! Atapotea kama fulani au fulani… Namfahamu mtu aliyefikia hatua ya kuhofia hatapata tena padri anayekubali kumuungamisha… Mbaya zaidi ni kwamba maneno hayo, badala ya kukoma mapema, yanadumu pengine maisha yote… Na jinsi ilivyo ndogo idadi ya wanaotetea ikilinganishwa na ile ya wanaoteta wanavyotaka. Mang’amuzi ni kwamba watu wako tayari kutoa vilevile sifa na lawama, hata mtu asijali tena hizo wala hizo. Baadaye anaimarika badala ya kukata tamaa akiona anasemwa, kwa kuwa ameng’amua faida yake. Anaona kana kwamba wanaomdhulumu hawamkosei Mungu, ila mwenyewe amewaruhusu kwa faida yake. Jambo hilo linaonekana naye wazi. Hapo kwa kawaida Bwana anamtumia maradhi makubwa… Halafu niseme nini kuhusu tabu za rohoni? Ingewezekana kutoa picha yake, zile za nje zingeonekana nyepesi sana!… Teso lingine linalowapata, hasa kama waliwahi kutenda makosa, ni kwamba wanadhani Mungu ameacha wadanganyike kutokana na dhambi zao. Ni kweli kwamba wakati wa kujaliwa fadhili hawawezi kuwa na wasiwasi kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayezitenda ndani mwao. Lakini tabu yao inaanza upya kwa kuwa fadhili hizo zinapita haraka, wakati kumbukumbu ya dhambi zao inabaki, tena wenyewe wanaona ndani mwao kasoro nyingi (nani hana?). Muungamishi akiwatuliza, tabu inapungua, halafu inarudi tena. Lakini kama padri mwenyewe ndiye anayezidisha wasiwasi wao, tabu inakuwa karibu haivumiliki, hasa kama wakati huo wamo katika ukavu ambamo tunadhani hatujawahi wala hatutawahi kuwaza lolote juu ya Mungu na ambamo tukisikia anazungumziwa ni kama kusikia juu ya mtu tuliyepata habari zake muda mrefu uliopita… Bwana anamruhusu shetani amshawishi na kumfanya aamini amelaaniwa na Mungu… Katika dhoruba hiyo hawezi kupata faraja yoyote… dawa pekee ni kutumainia huruma ya Mungu, naye isipotarajiwa kwa neno moja analomuambia mtu au kwa tukio moja linalotukia anamkomboa mara na mabaya yake yote”.
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Teresa, Mother et al., Mother Teresa: In My Own Words. Gramercy Books, 1997. ISBN 0-517-20169-0.
- ↑ Teresa, Mother & Kolodiejchuk, Brian, Mother Teresa: Come Be My Light, New York: Doubleday, 2007. ISBN 0-385-52037-9.
Vyanzo
[hariri | hariri chanzo]This article incorporates text from a publication now in the public domain: Herbermann, Charles, ed. (1913). "St. John of the Cross". Catholic Encyclopedia. Robert Appleton Company.
- Chong-Beng Gan, Peter (2015). Dialectics and the Sublime in Underhill's Mysticism. Springer.
- Kigezo:Cite magazine
- Schneiders, Sandra M. (2005). "John of the Cross". Katika Jones, Lindsay (mhr.). MacMillan Encyclopedia of religion. MacMillan.
- Underhill, Evelyn (1999). Mysticism. Oneworld Publications. ISBN 1-85168-196-5.
Marejeo mengine
[hariri | hariri chanzo]- May, Gerald G. (2004). The Dark Night of the Soul. A Psychiatrist Explores the Connection Between Darkness and Spiritual Growth. New York City: HarperCollins. ISBN 0-060-55423-1.
- McKee, Kaye P. (2006). When God Walks Away. A Companion to the Dark Night of the Soul. New York City: Crossroad Publishing Company. ISBN 0-824-52380-6.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Utenzi wa Yohane wa Msalaba
[hariri | hariri chanzo]Wikisource has original text related to this article: |
- Dark Night of the Soul verse translation of the poem.
- Text of Dark Night of the Soul from the Christian Classics Ethereal Library
- Original and Translation of Dark Night of the Soul From The Collected Works of St. John of the Cross
Ufafanuzi wake mwenyewe
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Usiku wa roho kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |