Teresa wa Mtoto Yesu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Teresa mwaka 1895.

Teresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D. (Alençon, Ufaransa, 2 Januari 1873 - Lisieux, Ufaransa, 30 Septemba 1897) ni jina la kitawa la Thérèse Françoise Marie Martin, maarufu pia kama Teresa wa Lisieux, anayeheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu mwenye sifa za bikira na mwalimu wa Kanisa.

Akifurahia udogo wake, Teresa alijitokeza kama “mtaalamu wa elimu ya upendo” (Papa Yohane Paulo II), katika maandishi yake, hasa katika shajara alimosimulia kwa unyofu wa hali ya juu jinsi kwa neema alivyoelewa na kutekeleza Injili katika maisha yake yaliyofichika ndani ya monasteri ya Wakarmeli Peku.

Tangu mwaka 1927 ni msimamizi wa wamisionari wote (pamoja na Fransisko Saveri), na tangu mwaka 1944 wa Ufaransa (pamoja na Yoana wa Arc).

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 1 Oktoba[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Asili na utoto[hariri | hariri chanzo]

Teresa mwaka 1881 akiwa na umri wa miaka 8.

Teresa, mtoto wa tisa na wa mwisho wa Louis Martin na Marie-Azélie Guérin (Zélie), ambao wanaheshimiwa kama wenye heri tangu tarehe 19 Oktoba 2008 na kama watakatifu tangu tarehe 18 Oktoba 2015, alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 kwenye barabara Saint-Blaise 42, huko Alençon, mkoa wa Normandie (Ufaransa).

Walipokuwa vijana wazazi wake walitaka kuingia utawani, wasiweze. Baada ya kuoana, maisha yao yote yaliongozwa na imani na maadili ya Ukristo.

Teresa alipozaliwa, watoto 4 walikuwa wameshafariki, naye aliyumba sana kinafsi alipofiwa mama yake akiwa na umri wa miaka 4 tu. Hapo mjomba wake, Isidore Guerin, aliteuliwa kuwa mlezi msaidizi wa mabinti watano walioachwa na marehemu ambao wote wakawa masista baadaye. Hivyo, tarehe 15 Novemba 1877, Louis Martin alihamia Buissonnets, kitongoji cha Lisieux, awe jirani na shemeji yake mwenye famasia. Huko Teresa alijenga uhusiano mkubwa na binamu yake Maria.

Lakini uhusiano wa pekee hasa alikuwa nao kwa dada zake Paulina na Maria, akiwaona kama mama zake.

Teresa alisimulia alivyoponywa ugonjwa wa nafsi yake kwa kutokewa na Bikira Maria akimtabasamu. Baadaye alipokea komunyo ya kwanza na katika kuungana hivyo na Yesu alimfanya kiini cha maisha yake.

Wito[hariri | hariri chanzo]

Thérèse Martin alipokuwa na umri wa miaka 13 (Februari 1886).
Teresa muda mfupi kabla ya kusafiri kwenda Italia (1887).

Mwaka 1882, Paulina alipoingia monasteri ya Wakarmeli ya Lisieux, Teresa angetaka kumfuata, lakini hakuweza kutokana na umri wake mdogo. Zaidi tena alitaka kufanya hivyo Maria pia alipoingia monasteri hiyohiyo mwaka 1886.

Usiku wa Noeli iliyofuata, alishinda moja kwa moja huzuni yake iliyomfanya alielie daima. Alielewa anahitaji kumtafuta Mungu kwa ukomavu zaidi na kujipatia hivyo "elimu ya upendo" ambayo inajumlisha kweli zote za imani. Mwenyewe aliita neema hiyo “wongofu kamili”, na tangu hapo alianza “kupiga mbio kama jitu”.

Alipofikia umri wa miaka 14 Teresa alizidi kushikamana kwa imani na Yesu msulubiwa, akajitosa kwa “moyo wa kimama” kumuombea muuaji aliyeonekana kukabili adhabu ya kifo bila kutubu. “Nilitaka kwa gharama yoyote kumzuia asiende motoni milele… Nilikuwa na tumaini kubwa kabisa katika Huruma ya Yesu isiyo na mipaka”. Ndiyo mang’amuzi yake ya kwanza ya umama wa kiroho.

Teresa alianza kupigania wito wake dhidi ya upinzani wa watu mbalimbali waliotaka kuahirisha hatua ya kujiunga na utawa. Kwa ajili hiyo mnamo Novemba 1887 alisafiri hadi Roma akaombe ruhusa ya Papa Leo XIII, lakini alikataliwa kwa wema. Kitu hicho kilimsikitisha lakini bila kumhangaisha, kwa sababu alijua amefanya kila aliloweza ili kuitikia wito wake mapema.

Kuingia monasteri[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa kurudi Ufaransa, askofu wake alibadili msimamo na kumruhusu. Hivyo tarehe 9 Aprili 1888 msichana Teresa alingiia Karmeli “ili kuokoa roho za watu na kuombea mapadri”, akiwa na miaka 15 tu. Ile tisa iliyofuata ikawa na maendeleo ya kiroho ya kasi ajabu.

Wakati huohuo baba yake alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa akili uliomtia tabu na aibu sana. Huo ukawa sababu ya uchungu mwingi hata kwa binti yake mpendwa, ambaye lakini kwa njia hiyo alijaliwa kutazama uso wa Yesu katika mateso yake.

Kisha kuweka nadhiri[hariri | hariri chanzo]

Aliweka nadhiri zake za kwanza tarehe 8 Septemba 1890, ikawa arusi ya kiroho katika udogo: “Ilikuwa siku ya Maria Kuzaliwa. Lo, sikukuu nzuri kweli kwa kuolewa na Yesu! Bikira mtakatifu katika udogo wake kama mtoto mchanga ndiye aliyemtoa aliye Ua lake dogo kwa Yesu mdogo”.

Kwa Teresa, kuwa mtawa maana yake ilikuwa kuwa bibiarusi wa Yesu na mama wa roho za watu. Ndiyo maana siku hiyo aliandika sala iliyotokeza dira yote ya maisha yake, akimuomba Yesu, kama zawadi ya Upendo wake usio na mipaka, aweze kuwa mdogo kuliko wote, lakini hasa aliomba wokovu wa watu wote: “Leo kusiwe na roho yoyote ambayo ipotee milele”.

Mwaka 1893 aliteuliwa kuwa mlezi msaidizi wa wanovisi, kazi aliyofanya kwa bidii na ufanisi mkubwa. Baadaye kwa maandishi yake yaliyoenea upesi duniani kote akawa mlezi wa umati wa watu akiwaelekeza kufuata Heri Nane alizotangaza Yesu mlimani.

Mwaka 1894, baada ya ugonjwa wa muda mrefu, mzee Louis Martin alifariki, na binti yake mwingine, Selina, aliyekuwa anamtunza, aliweza kujiunga na monasteri hiyo. Kamera yake imetuachia picha halisi za Teresa.

Miaka ya mwisho[hariri | hariri chanzo]

Adolphe Roulland, mmoja wa mafrateri wawili ambao Teresa alikabidhiwa kuwaombea.

Muhimu sana ni “Majitoleo kwa Upendo wenye Huruma” ambayo aliyafanya katika sikukuu ya Utatu Mtakatifu ya mwaka 1895 na yalifungua kipindi cha mwisho cha maisha yake mafupi kilichojaa mateso katika muungano na yale ya Yesu.

Mwezi Aprili 1896, alipatwa na TB, ugonjwa uliokuja kumuua baada ya miezi 18. Mateso ya mwili yaliendana na yale ya ndani yanayojulikana kama "usiku wa roho" na ni jaribu kali la imani. Pamoja na Bikira Maria chini ya msalaba wa Mwanae, Teresa alifaulu kulishinda katika giza nene lilioenea ndani mwake. Alitambua kwamba alipaswa kupatwa na jaribu hilo kwa ajili ya wokovu wa wakana Mungu wote wa ulimwengu wa kisasa, ambao aliwaita “ndugu”.

Alizidi vilevile kutekeleza upendo wa kidugu: kwa masista wa jumuia yake, kwa wamisionari wawili aliokabidhiwa awaombee, kwa mapadri na kwa watu wote, hasa wale wa mbali zaidi, akawa kweli dada wa wote. Upendo wake wa kuvutia ulitokeza furaha ya dhati ambayo mwenyewe alifichua siri yake: “Ee Yesu, furaha yangu ni kukupenda wewe”.

Katika hali hiyo ya mateso, akitekeleza upendo wa hali ya juu katika mambo madogo ya maisha ya kila siku, Teresa alitimiza wito wake wa kuwa upendo katika moyo wa mama Kanisa.

Katika barua yake ya mwisho, aliandika hivi juu ya picha ya Mtoto Yesu iliyochorwa ndani ya Hostie takatifu: “Siwezi kumuogopa Mungu aliyejifanya mdogo hivi kwa ajili yangu! … Mimi nampenda! Kwa kuwa yeye ni Upendo na Huruma tu!”

“Mimi amenipa Huruma yake isiyo na mipaka, na ni katika kioo hicho kisichosemeka kwamba nazingatia sifa zake nyingine za Kimungu. Hizo zote zinaonekana kwangu zinang’aa kwa upendo. Hata Haki yake, labda kuliko sifa nyingine, inaonekana kwangu imevikwa Upendo”.

Ndani mwake yalitimia maneno aliyoyandika: “Watakatifu wote walielewa, na kwa namna ya pekee labda wale waliojaza ulimwengu kwa mwanga wa mafundisho ya Injili. Haikuwa katika sala kwamba Mt. Paulo, Mt. Augustino, Mt. Yohane wa Msalaba, Mt. Thoma wa Akwino, Fransisko, Dominiko na marafiki wa Mungu wengine wengi hivi walichota elimu ile ya ajabu ambayo iliteka akili bora?”

“Mimi nahitaji kufungua tu Injili takatifu ili ninuse mara manukato ya maisha ya Yesu, na hapo nijue njia ambayo nipige mbio juu yake; nami nakimbilia nafasi ya mwisho, si ile ya kwanza… Nahisi kwamba hata kama dhamiri yangu ingelemewa na makosa yote ya jinai yanayoweza kufanyika… kwa moyo uliovunjika kwa uchungu ningejitupa mikononi mwa Yesu Mwokozi wangu, kwa sababu najua anampenda mwana mpotevu”.

Tarehe 10 Julai 1897 udhaifu wa mwili ulimzuia asiendelee kuandika habari za maisha yake kama alivyoagizwa. Neno la mwisho aliloliandika katika sentensi isiyomalizika ni "upendo".

Alifariki tarehe 30 Septemba 1897, mnamo saa 19:20, huku akitazama sanamu ya Msulubiwa aliyoishika mikononi na kusema, “Mungu wangu, nakupenda!”. Maneno hayo yalikuwa muhtasari wa maisha yake.

“Yesu, nakupenda” ndiyo yanayotawala maandishi yake yote. Kwa njia hiyo alizama katika Utatu Mtakatifu. Katika mashairi yake aliandika, “Lo, unajua, Yesu Mungu, kuwa nakupenda / Roho wa Upendo ananiwasha kwa moto wake / Ni kwa kukupenda kwamba nampendeza Baba”.

Heshima baada ya kufa[hariri | hariri chanzo]

Basilika la Lisieux, lenye eneo la 4500 m2 na urefu wa mita 95, lililojengwa kwa heshima yake mwaka 1937.

Mara baada ya kufa maandishi yake yalianza kusambaa kwa namna ya ajabu na kumvutia heshima ya wengi. Pia ilitokea miujiza kwa maombezi yake. Ni kama alivyosema, kuwa atamimina mvua ya mawaridi kutoka mbinguni, akitumia [[uzima wa milele] kutenda mema mengi duniani.

Papa Pius XI alimtangaza mwenye heri tarehe 29 Aprili 1923, tena mtakatifu tarehe 17 Mei 1925, na Papa Yohane Paulo II alimtangaza mwalimu wa Kanisa tarehe 19 Oktoba 1997 kutokana na mchango wake mkubwa katika teolojia ya Kiroho.

Njia yake ya kiroho[hariri | hariri chanzo]

“Njia ndogo ya tumaini na upendo”, njia ya "utoto wa kiroho” aliyoielekeza inafundisha kutimiza sharti la Yesu: “Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia katika ufalme wa mbinguni” (Math 18:3). Njia hiyo inatia moyo wa kujitoa kikamilifu kama kikafara kwa wokovu wa ulimwengu. Mwenyewe aliifuata hata akasema: “Kupenda ni kutoa yote, na kujitoa pia”. “Sijawahi kumnyima chochote Mungu mwema!”

Siri yake ni nguvu ya upendo, ambao Teresa alitambua ndio wito wake katika Kanisa: kuwa moyo wa Mwili wa Kristo ili kusaidia viungo vyake vyote kufanya kazi vizuri.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Ee Mungu wangu! Utatu mtakatifu! Natamani tu kukupenda na kukufanya upendwe...

Ili maisha yangu yaweze kuwa tendo moja tu la upendo kamili: Ninajitoa mhanga kama kitambiko cha kuteketezwa kabisa na upendo wako rahimu.

Nakusihi uniteketeze bila ya kukoma, ukiyaruhusu yale mawimbi ya upendo wako usiopimika, yanayojazana ndani yako, yafurike rohoni mwangu: hivyo nami niweze kuwa shahidi wa upendo wako, Mungu wangu!

Unijalie kifodini hicho baada ya kunitayarisha kutokea mbele yako, hatimaye unisababishe kufa: na roho yangu iruke moja kwa moja, bila ya kuchelewa popote pale, ifikie kukumbatiana milele na upendo wako rahimu.

Ee mpenzi wangu, mimi napenda, katika kila pigo la moyo wangu, kurudia upya, mara nyingi zisizohesabika, hili tendo langu la kujitoa kwako.

Mpaka hapo vivuli vitakapotoweka, nami nikaweza kukuambia milele, uso kwa uso, jinsi ninavyokupenda.


Ee Yesu, upendo wangu, hatimaye nimegundua wito wangu.

Wito wangu ni kupenda!

Ndiyo, nimeona nafasi yangu ndani ya Kanisa, na nafasi hiyo umenipatia wewe, Mungu wangu.

Katika moyo wa Kanisa, mama yangu, nitakuwa upendo: hivyo nitakuwa yote na hamu yangu itatimia.


Ee Bwana Yesu, mimi si tai, ila nina macho na moyo wake.

Ingawa ni mdogo, nathubutu kulikazia macho jua la upendo, na kutamani kurukia kwake.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Maandishi yake katika tafsiri ya Kiswahili na ya Kihaya[hariri | hariri chanzo]

  • THERESIA WA MTOTO YESU, Ua la Upendo, Maisha ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Aliyoyaandika Yeye Mwenyewe – tafsiri ya J. J. Rwechungura – ed. Paulines Publications Africa – Nairobi 1992 – ISBN 9966-21-021-0
  • THEREZA OW’OMWANA YEZU – Akamuli k’engonzi, Oburora bw’Omutakatifu Thereza Ow’omwana Yezu Obwo Yayehandikire Wenene – tafsiri ya J. J. Rwechungura – ed. Marianum Press Kisubi – Kisubi 1960

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Filamu juu yake[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]