Nenda kwa yaliyomo

Petro Krisologo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Petro Krisologo katika mavazi ya askofu mkuu.
Kanisa kuu la Imola (Italia).

Petro Krisologo (Forum Cornelii, leo Imola, Italia, 380 hivi - Imola, 450 hivi) alikuwa askofu mkuu wa Ravenna (wakati huo mji mkuu wa mwisho wa Dola la Roma la Magharibi, leo katika mkoa wa Emilia-Romagna huko Italia Kaskazini) aliyevutia umati wa watu kwenye imani kwa mafundisho yake yaliyo bora kwa hekima na ufasaha wa lugha[1].

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1729 Papa Benedikto XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Julai[2].

Habari za maisha yake ni chache, tena si za hakika. Alichoandika Agnus, mwanahistoria wa Ravenna, mwaka 840 hivi, si cha kuaminika sana.

Alizaliwa huko Forum Cornelii, leo Imola, Italia, mwaka 380 hivi.

Alivyosimulia mwenyewe, alipewa ubatizo, malezi ya kidunia na ya kiroho na hatimaye daraja takatifu ya ushemasi na Korneli, askofu wa Imola.

Papa Sixtus III (au Papa Selestini I) alimteua kuwa askofu wa Ravenna mwaka 433. Chini yake Kanisa la mji huo lilipewa baadhi ya haki za jimbo kuu kwa sababu ya kuwepo ikulu ya Dola. Hasa lilipata sifa kutokana na uchungaji wake wenye ari pande zote, unaoshuhudiwa na hotuba zake nyingi.

Hotuba ya kwanza jimboni aliitoa mbele ya Gala Plasidia, binti wa Kaisari Theodosi I, ambaye baadaye akawa mtawala kwa niaba ya mwanae Kaisari Valentiniani III.[3].

Akishirikiana na malkia huyo mwenye imani, alihamasisha ujenzi wa makanisa mazuri ajabu, hivi kwamba alipofariki yeye Ravenna, ambayo miongo michache ya nyuma ilikuwa kijiji kwenye madimbwi, iliweza kushindana na Konstantinopoli kwa mabasilika, vikanisa na monasteri, mbali na majumba.[4]

Ni kati ya wachungaji bora wa wakati ule, akitekeleza mwenyewe kipeo cha askofu alichokichora hivi: “Kuwa ndani ya Kristo mtumishi huru wa wote”

Uadilifu na ari yake vilimvutia waamini wengi waliomuita Krisologo (kutoka Kigiriki, "Neno la dhahabu") kwa sababu ya mvuto wa kiroho na ufasaha wa mahubiri yake.

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]

Tuna hotuba 183 za Petro, hasa za kufafanulia Biblia na za kumsifu Bikira Maria na Yohane Mbatizaji.

Petro alifafanua vizuri hasa fumbo la umwilisho na Kanuni ya Imani ya Mitume, akipinga uzushi wa Ario na ule wa Eutike. Alimuandikia huyo mwaka 449 ili akubali maamuzi ya Papa Leo I: “… kwa sababu mwenye heri Petro, ambaye anaishi na kuongoza akiwa katika ukulu wake mwenyewe, anawapa ukweli kuhusu imani wale wanaoutafuta”.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Maandishi yake

[hariri | hariri chanzo]
  1. https://www.santiebeati.it/dettaglio/28450
  2. Martyrologium Romanum
  3. Guido Pettinati, I Santi canonizzati del giorno, Edizioni Segno, Udine, Vol. VII, 1991, p. 333-336
  4. San Pietro Crisologo Omelie per la vita quotidiana, Città Nuova Edizioni, Roma. 1990 Introduzione p. 9.
  • Otto Bardenhewer, Patrology, tr. Shanan, pp. 526 ff.
  • Dapper, Der hl. Petrus von Ravenna Chrysologus, Posen, 1871
  • Looshorn, Der hl. Petrus Chrysologus und seine Schriflen in Zeitschrift f. kathol. Theol., III (1879), pp. 238 ff.
  • Wayman, Zu Petrus Chrysologus in "Philologus", LV (1896), pp. 464 ff.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]