Nenda kwa yaliyomo

Antoni wa Padua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mt. Fransisko wa Asizi na mfuasi wake Mt. Antoni wa Padua katika mchoro wa Simone Martini.
Njozi ya Mt. Antoni wa Padua ilivyochorwa na Gaetano Lapis
Basilika la Mt. Antoni wa Padua

Antoni wa Padua (kwa jina la kiraia Fernando Martim de Bulhões e Taveira Azevedo; Lisbon, Ureno 15 Agosti 1195 - Padova, Italia 13 Juni 1231) alikuwa padri na mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo, maarufu hasa kwa mahubiri yake yaliyomstahilia heshima ya kutangazwa Mwalimu wa Kanisa.

Kwa vipawa vyake vya pekee upande wa akili, elimu, busara, kiasi, ari ya kitume na sala hasa, alichangia sana maendeleo ya shirika lake.

Ni mmojawapo kati ya watakatifu wanaoheshimiwa zaidi katika Kanisa Katoliki, pia kwa sababu ya miujiza mingi inayosemekana kupatikana kwa kukimbilia maombezi yake.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Juni[1].

Waamini wengi wanapenda picha zinazomuonyesha akiwa na maua meupe pe, yakimaanisha usafi wa moyo wake, na akimshika mtoto Yesu mikononi, kadiri ya tukio la ajabu lililosimuliwa na vyanzo mbalimbali.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Kabla ya kujiunga na Wafransisko[hariri | hariri chanzo]

Mtakatifu huyo aliishi katika kipindi cha mageuzi cha Karne za kati. Maisha yake yaliandikwa kwa mara ya kwanza (Vita prima au Assidua) na mtawa asiyejulikana mwaka 1232 kufuatana na taarifa za askofu wa Lisbon, Soeiro II Viegas (1210 - 1232).

Antoni alizaliwa na familia ya kisharifu karibu na kanisa kuu la Lisbon tarehe 15 Agosti 1195: huko alipata ubatizo kwa jina la Fernando halafu elimu.

Akiwa na miaka 15 alijiunga na shirika la Agostino wa Hippo kwanza katika monasteri ya Lisbon, halafu (1212) akahamia Coimbra ili kutulia zaidi. Katika mji huo maarufu kwa elimu alijitosa kusoma Biblia na mababu wa Kanisa, akijipatia ujuzi alioushirikisha baadaye kwa kufundisha na kuhubiri.

Huko Coimbra lilitokea jambo lililobadili kabisa maisha yake. Akiwa padri tayari, alihamia kwa Ndugu Wadogo (1220) kisha kuona masalia ya wafiadini 5 wa kwanza wa shirika hilo jipya yakitokea Moroko walipouawa na Waislamu. Ndipo alipojibadilishia jina kuwa Antoni.

Jaribio la umisionari[hariri | hariri chanzo]

Akitamani yeye pia kuwa mmisionari na kumfia Yesu, mwaka huohuo alikwenda Moroko pamoja na mwenzake mmoja, lakini baada ya kuugua huko miezi kadhaa alikubali kurudi Ureno.

Hata hivyo baharini meli yao ilipatwa na dhoruba iliyowatupa katika kisiwa cha Sicilia, ambapo walisikia kwamba mwezi Mei huko Assisi kutakuwa na mkutano mkuu wa shirika.

Miaka ya kwanza huko Italia[hariri | hariri chanzo]

Hivyo mwaka 1221 alikwenda huko kushiriki huo mkutano maarufu ulioitwa “wa mikeka”, na ndipo alipokutana na mwanzilishi, Fransisko wa Asizi, pamoja na kujua zaidi hali ya shirika, mipango yake ya kitume na mabishano kuhusu kanuni iliyokuwa inatungwa.

Akiwa mnyenyekevu sana, ingawa mwenye hekima na elimu kubwa, mkutano ulipokwisha alikuwa hajachaguliwa na mkuu yeyote wa kanda, mpaka ndugu Grasyano alipompeleka Montepaolo, karibu na Castrocaro, walipokuwepo watawa wengine 6, ili awasomee Misa. Aliishi huko mwaka mmoja akifanya kazi duni, pamoja na kusali na kujinyima.

Sanamu ya Antoni wa Padua.

Katikati ya mwaka 1222, watawa hao walikwenda Forlì kushiriki upadrisho. Askofu alipohitaji mhubiri atoe mawaidha kwa mapadri wapya, hakupatikana. Basi, mkubwa wake akamuagiza Antoni, ambaye akaja hivyo kujulikana kwa ubora wa mahubiri.

Ndipo alipoanza kazi hiyo kwa kutembelea mahali mbalimbali pa Italia na Ufaransa, akifundisha maadili kama ilivyokuwa desturi ya shirika, lakini pia kuponda uzushi na kurudisha katika Kanisa Katoliki wengi walioliasi.

Kutokana na elimu yake alisisitiza umuhimu wa kuandaa ndugu wengine kwa kazi hiyo, lakini hakukubali kufanya hivyo mpaka aliporuhusiwa na Fransisko kufundisha teolojia huko Bologna (1223). Katika barua fupi aliyomuandikia, mwanzilishi huyo alimuita kwa heshima “askofu wangu” na kumwekea sharti la kutozimisha roho ya sala kwa masomo.

Akiwa wa kwanza, au mmojawapo kati ya wale wa kwanza, kufanya kazi hiyo, aliweka misingi ya teolojia ya Kifransisko, iliyofikia kilele chake katika mafundisho na maandishi ya Bonaventura wa Bagnoregio na Yohane Duns Scotus.

Miaka miwili Ufaransa[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na uwezo wake katika kuhubiri, aliagizwa pia (1224) kwenda kuzuia uenezi wa uzushi wa Wakatari huko Ufaransa alipobaki miaka 2. Wakati huo alichaguliwa kuwa mhudumu wa jumuia kadhaa.

Mkuu wa shirika Italia Kaskazini[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kushiriki mkutano mkuu wa mwaka 1227, mtumishi mkuu mpya alimchagua Antoni kuwa mtumishi wa kanda ya Italia Kaskazini. Kwa miaka 3 iliyofuata, pamoja na kutembelea konventi za eneo hilo kubwa kama kiongozi, aliendelea na kazi ya kuhubiri huko na huko, akiwa amejichagulia Padova kama makao yake.

Ndani ya shirika, baada ya kifo cha Fransisko, yalikuwa yamezuka mabishano makali kati ya walioshikilia wasia wa mwanzilishi na wale waliotaka shirika liweze kushindana na mashirika mengine. Yeye na Watumishi wengine kutoka kanda mbalimbali wakaona utatuzi unaweza kutokea kwa Papa tu.

Akipokea ombi lao, Papa Gregori IX (1227-1241) alitoa tamko rasmi la kwanza juu ya kanuni (1230), akitumia mamlaka yake ya Kipapa na hasa ujuzi wake wa nia ya Fransisko (akiwa ndiye aliyemsaidia kutunga kanuni alipokuwa bado kardinali, jina lake Ugolino).

Kuhusu wasia alitamka si sheria inayowabana Wafransisko wasiweze kufafanua kanuni yao wala kufafanuliwa na Kanisa, wala kuomba wala kupewa hati na fadhili za Papa. Sababu ya msingi ni kuwa Kanisa liko juu kuliko kanuni.

Kwa kukabili suala hilo kwa mtazamo wa sheria, Gregori IX alikata hamu ya mwanzilishi ya kuiona kanuni kama kituo cha kuanzia safari tu, si cha mwisho. Kwa namna hiyo aliwaingiza zaidi Ndugu Wadogo ndani ya kawaida ya Kanisa.

Upande wa ufukara kwa jumla alitetea msimamo wa mwanzilishi (kwa jinsi alivyomheshimu hata akamtangaza mtakatifu karibu bila kufuata taratibu za kesi), ila aliulegeza kiasi, kwa lengo la kufanikisha zaidi utume wa Ndugu Wadogo na hivyo kurekebisha Kanisa lililokuwa na hali mbaya kiroho.

Kwa ajili hiyo Gregori IX aliwapa pia hati na ruhusa nyingi za pekee dhidi ya mamlaka ya Maaskofu na maparoko. Hivyo njia ikawa wazi kuligeuza shirika la wadogo wanaohubiri toba kwa unyenyekevu chini ya padri yeyote, liwe shirika imara lililo chini ya Maaskofu kwa machache tu.

Mageuzi hayo, yaliyosababisha kwa muda mrefu upinzani mwingi wa Maaskofu na mapadri wanajimbo, yalichangiwa pia na ustawishaji wa elimu ndani ya shirika uliozidi kuwalinganisha Ndugu Wadogo na watawa wengine na kuongeza idadi ya mapadri kati yao.

Katika hayo yote, inasadikika kuwa Antoni alichangia kiasi chake.

Mwisho wa maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kusafiri sana, hatimaye Antoni alirudi Padova kumalizia maisha yake. Huko alihubiri kwa mara ya mwisho Kwaresima ya mwaka 1231 iliyo kilele cha kazi yake na iliyozingatia sana masuala ya jamii, akafariki ameishiwa nguvu tarehe 13 Juni 1231, akiwa na umri wa miaka 36 tu.

Heshima baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Alitangazwa mtakatifu na Papa Gregori IX mapema sana, tarehe 13 Mei 1232, na mwalimu wa Kanisa na Papa Pius XII mwaka 1946 kwa jina la Doctor Evangelicus (Mwalimu wa Kiinjili), kutokana na mafundisho yake kujaa roho na maneno ya Injili ya Yesu Kristo.

Mafundisho yake[hariri | hariri chanzo]

Antoni ametuachia mifululizo miwili ya hotuba juu ya masomo ya Biblia yalivyopangwa na liturujia, mmoja kwa ajili ya Jumapili, mwingine kwa ajili ya sikukuu za watakatifu. Humo anaelekeza kwa usahili na uzuri wa Kiinjili safari ya Kiroho ya kumfuata Yesu Kristo. Akitambua ubinadamu ulivyo, anahimiza mfululizo kupiga vita dhidi ya kiburi, uroho na uchafu ili kutekeleza maadili ya unyenyekevu na utiifu, ukarimu na ufukara, kiasi na usafi wa moyo.

Mada kuu ya mahubiri yake ni kwamba mtu wa sala tu anaweza kupiga hatua katika maisha ya Kiroho. Humo anafundisha juu ya sala kama uhusiano wa mapendo na Bwana unaohitaji hali ya kimya, si cha nje tu, bali hasa cha moyoni. Kwake inahitajika misimamo minne: kwanza, kuweka wazi moyo wetu kwa Mungu; pili, kutambua uwemo wake na kuongea naye kwa upendo; tatu, kumueleza shida zetu; nne, kumsifu na kumshukuru.

Katika mafundisho kama hayo inajitokeza tayari tabia maalumu mojawapo ya teolojia ya Kifransisko: kusisitiza upendo, ambao kutoka kwa Mungu unaenea rohoni upande wa utashi na unakuwa chemchemi ya ujuzi wa Kiroho unaopita ujuzi mwingine wowote. Kwa sababu ni kwa kupenda kwamba tunakuja kufahamu. “Upendo ndiyo roho ya imani na kuipa uhai; bila upendo, imani inakufa”.

Tabia nyingine ni kumpa Kristo nafasi yake kama kiini cha mpango wa Mungu na cha mambo yote. “Ukimhubiri Yesu, atalainisha mioyo migumu; ukimlilia atapunguza ukali wa vishawishi; ukimfikiria ataangaza uelewa wako; ukisoma habari zake atashibisha akili yako”.

Katika kuzingatia kwa mshangao unyenyekevu wa umwilisho na upendo wa mateso yake, Antoni kama Fransisko alitambua zaidi wajibu wa kumshukuru Mungu na kuheshimu kila mtu.

“Kristo, aliye uhai wako, ametundikwa mbele yako, uweze kuutazama msalaba kama kwamba ni kioo. Humo utaweza kujua majeraha yako yalivyokuwa ya kukufisha, kiasi kwamba Damu ya Mwana wa Mungu ilikuwa dawa pekee ya kukuponya. Ukitazama kwa makini zaidi utaweza kutambua ukuu wa hadhi yako kama mtu na wa thamani yako… Hakuna mahali ambapo mtu ataweza kuelewa vizuri zaidi ubora wake kuliko kwa kujitazama katika kioo cha msalaba”.

Mbele ya ustawi wa miji na biashara, uliofanya wengi wasijali mahitaji ya mafukara, alielekeza utajiri wa kweli, ule wa moyo wenye huruma: “Enyi matajiri, mwatendee kwa wemamaskini, mwapokee nyumbani mwenu: kesho wenyewe ndio watakawaowapokeeni katika maskani za milele palipo uzuri wa amani, hakika ya usalama na utulivu tajiri wa shibe ya milele”.

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • St. Anthony, Doctor of the Church, Franciscan Institute Publications, 1973, ISBN 9780819904584
  • Anthony of Padua, Sermones for the Easter Cycle, Franciscan Institute Publications, 1994, ISBN 9781576590416
  • Attwater, Donald; Attwater, John (1993), The Penguin Dictionary of Saints (toleo la 3rd), New York, New York: Penguin Books, ISBN 0-14-051312-4 {{citation}}: Unknown parameter |coauthors= ignored (|author= suggested) (help)
  • Silva, José Manuel Azevedo (2011), Câmara Municipal (mhr.), A criação da freguesia de Santo António dos Olivais: Visão Histórica e Perspectivas Actuais (PDF) (kwa Portuguese), Santo António dos Olivias (Coimbra), Portugal: Câmara Municipal de Santo António dos Olivais, ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2011-12-20, iliwekwa mnamo 5 Septemba 2011 {{citation}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)CS1 maint: unrecognized language (link)

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  1. Martyrologium Romanum