Anselm wa Canterbury

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Anselm

Anselm wa Canterbury (Aosta, leo nchini Italia, 1033 au 1034Canterbury, Uingereza, 21 Aprili 1109) alikuwa kati ya wanafalsafa na wanateolojia muhimu zaidi wa zama za kati za Ulaya.

Baada ya kujiunga na monasteri wa Wabenedikto wa Bec huko Ufaransa, alipopata sifa kama kiongozi wa kiroho na mlezi, kama mhubiri wa mrekebishaji wa umonaki, alichaguliwa (1093) kuwa askofu mkuu wa Canterbury (Uingereza).

Mwaka 1163 alitangazwa kuwa mtakatifu.

Mwaka 1720 alitangazwa na Papa Klementi XI kuwa Mwalimu wa Kanisa kutokana na ubora wa maandishi yake yaliyotangulia nyakati zijazo na kumfanya ajulikane kama mwanzilishi wa teolojia ya shule.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 21 Aprili.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Utoto na ujana[hariri | hariri chanzo]

Anselm alizaliwa mjini Aosta[1] au karibu nao [2] Aosta katika ufalme wa Burgundy (leo katika mkoa wa Valle d'Aosta, inapotumika lugha ya Kifaransa nchini Italia) mwaka 1033 au 1034.[1] Familia yake ilikuwa tajiri na ya kisharifu na upande wa mama ilihusiana na watawala wa Savoy[3].

Baba yake, Gundulf de Candia, mwenye asili ya Kilombardi, alikuwa mkali, tofauti na mama, Ermenberga wa Geneva.

Alipofikia umri wa miaka 15, Anselm alitamani kuingia monasteri, lakini hakuruhusiwa.[1] Jambo hilo lilimfanya augue; kisha kupona aliacha masomo na kuishi kistarehe tu. Wakati huo mama alifariki na baba alizidi kuwa mkali.

Alipofikia miaka 23, Anselm aliondoka nyumbani, akavuka milima ya Alps na kutangatanga katika Burgundy na Ufaransa.[2] Akivutiwa na sifa ya Lanfranko (priori wa Abasia ya Bec), alikwenda Normandia mwaka 1059.

Mwaka uliofuata, kisha kuishi kidogo huko Avranches, aliingia rasmi malezi ya kitawa kama mnovisi akiwa na miaka 27.

Kuanzia hapo kanuni ya Benedikto wa Nursia iliathiri kabisa mawazo na maisha yake.[4]

Miaka huko Bec hadi Canterbury[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1063, Lanfranko aliteuliwa abati wa Caen na Anselm priori wa Bec.[5] Anselm alishika nafasi hiyo kwa miaka 15 halafu akawa abati kutokana na kifo cha Herluin wa Bec, mwanzilishi wa abasia hiyo, kilichotokea mwaka 1078. Aliwekwa wakfu na askofu wa Evreux tarehe 22 Februari 1079.[6]

Chini ya Anselm, Bec ikawa kituo bora cha elimu Ulaya, ikivuta wanafunzi kutoka nchi mbalimbali,[7] ingawa masomo hayakuwa na nafasi ya kwanza katika umonaki.[8]

Akiwa Bec aliandika vitabu vya kwanza vya falsafa, Monologion (1076) na Proslogion (10771078). Hivyo vilifuatwa na Majadiliano kuhusu Ukweli, Hiari na Anguko la Ibilisi.

Wakati huo alijitahidi pia kulinda uhuru wa abasia dhidi ya mamlaka za nje.[9]

Mnara wa Mt. Nicholas kwenye abasia ya Bec.

Mara kadhaa Anselm alitembelea Uingereza ili kusimamia mali za abasia na kumuona Lanfranko, hadi huyo alipofariki mwaka 1089.[10] Kwa kuwa alithaminiwa na wenyeji wa huko, mwenyewe alichaguliwa kushika nafasi ya Lanfranko kama Askofu mkuu wa Canterbury.

Askofu mkuu wa Canterbury[hariri | hariri chanzo]

Kuanzia mwaka 1093 alipopata kuwa askofu mkuu, alishindana mara kadhaa na wafalme wa Uingereza Williamu II na Henri I ili kutetea uhuru wa Kanisa lisiingiliwe na serikali; kwa sababu hiyo mara mbili ilimpasa kwenda uhamishoni.

Hatimaye upatanisho kati ya mfalme na papa ulimwezesha kurudi Canterbury, alipofariki mwaka 1109.

Kitabu maarufu zaidi alichokiandika miaka hiyo ya mwisho kati ya Uingereza na Italia, kinaitwa Cur Deus homo (Kwa nini Mungu kuwa mtu?) na kimeathiri kwa miaka elfu mtazamo wa Kanisa la magharibi kuhusu fumbo la wokovu.

Anselm aliacha pia mkusanyo mkubwa wa Sala na wa Tafakuri, mbali na Barua nyingi, ambazo zinawezesha kuona mafungamano ya kirafiki aliyokuwa nayo kwa wanafunzi wake.

Anselm anakumbukwa si tu kama mwanateolojia, bali pia kama mwanafalsafa, hasa kwa utafiti wake kuhusu unum argumentum, yaani hoja kuu inayojitegemea na kujitosheleza katika kuthibitisha uwepo wa Mungu na sifa zake.

Imani na akili[hariri | hariri chanzo]

Mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuchimba nadharia, Anselm alitafuta, kwa kufuata nyayo za Plato na Agostino wa Hippo, namna ya kukutanisha imani na akili.

Aliona akili ya binadamu ni chombo muhimu cha utafiti wa teolojia. Bila shaka, alidai kwanza imani, akisema "nasadiki ili nielewe, na nisiposadiki kwanza sitaweza kuelewa.

Hivyo, Anselm alirithi kutoka kwa Agostino kauli credo ut intelligam, intelligo ut credam (yaani "nasadiki ili nielewe, naelewa ili nisadiki").

Utafiti wa ukweli unategemea imani, lakini hiyo peke yake haitoshi, inadai pia aina mbalimbali za uthibitisho wa akili. Katika hilo akili, sawa na imani yenyewe, ana mwongozo wa hakika katika mwanga wa Mungu ambao usipokuwepo akili haiwezi kabisa kupenya fumbo la Mungu.

Kwa maneno mengine, akili haitoi matamko, bali inasaidia kuelewa imani.

Anselm ni kati ya wataalamu wa kwanza waliounganisha falsafa na teolojia, kadiri ya neno fides quaerens intellectum (yaani "imani inadai akili"), litakalokuwa msingi wa teolojia ya shule.

Sala zake[hariri | hariri chanzo]

Bwana, wewe ni Mungu wangu, wewe ni Bwana wangu lakini mimi sijakuona.

Wewe umeniumba na kuniumba upya, umenijalia mema yangu yote, lakini mimi sijakufahamu.

Nimeumbwa ili nikuone lakini sijafanya hilo ambalo kwa ajili yake nimeumbwa…

Unifundishe kukutafuta na ujionyeshe ninapokutafuta: siwezi kukutafuta usiponifundisha, wala kukuona usipojionyesha.

Nikutafute kwa kukutamani na nikutamani kwa kukutafuta, nikuone kwa kukupenda na nikupende kwa kukuona.


Nakuomba, Bwana, unijalie nionje kwa upendo yale ninayoyaonja kwa ujuzi; unijalie nijue kwa upendo ninayoyajua kwa akili.

Nakuwia kuliko uhai wangu wote, lakini sina zaidi, tena peke yangu siwezi kukurudishia uhai huo kikamilifu.

Univute kwako, Bwana, katika utimilifu wa upendo.

Mimi mzima ni wako kwa uumbaji; unifanye wako kwa upendo pia. Bwana, moyo wangu uko mbele yako.

Najaribu, lakini peke yangu siwezi kitu; fanya nisichoweza.

Unikaribishe katika chumba cha ndani cha upendo wako.

Naomba, natafuta, napiga hodi.

Wewe uliyenijalia kuomba, unijalie nipate; uliyenijalia kutafuta, unijalie nione; uliyenifundisha kupiga hodi, unifungulie.

References[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 Walsh, Michael, ed. Butler's Lives of the Saints. (HarperCollins Publishers: New York, 1991), pp. 117
  2. 2.0 2.1 Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 9.
  3. R. Southern. St. Anselm: Portrait in a Landscape. (Cambridge University Press: 1992), pp. 8. http://books.google.com/books?hl=en&lr=&id=lxf-LvQvvwIC&oi=fnd&pg=PR15&dq=anselm+of+canterbury+r-southern&ots=e6-_fZ6v0B&sig=3rOwM0tvC4VVInlSWl099J0dyjE#PPA8,M1
  4. R. Southern. St. Anselm: Portrait in a Landscape. (Cambride University Press: 1992), pp. 32. http://books.google.com/books?hl=en&lr=&id=lxf-LvQvvwIC&oi=fnd&pg=PR15&dq=anselm+of+canterbury+r-southern&ots=e6-_fZ6v0B&sig=3rOwM0tvC4VVInlSWl099J0dyjE#PPA8,M1
  5. Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 10.
  6. Vaughn, Sally. "St Anselm of Canterbury: the philosopher-saint as politician." Journal of Medieval History. 1 (1975), 279–306: 282.
  7. Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 15.
  8. Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 13.
  9. Vaughn, Sally. "St Anselm of Canterbury: the philosopher-saint as politician." Journal of Medieval History. 1 (1975), 279–306: 281.
  10. Charlesworth, M. J., trans. and ed. St. Anselm's Proslogion. (University of Notre Dame Press: Notre Dame, 2003), pp. 16.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Christian cross.svg Makala hii kuhusu Mkristo huyu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Anselm wa Canterbury kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.