Nenda kwa yaliyomo

Benedikto wa Nursia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Benedikto wa Nursia alivyochorwa na Beato Angelico.
Benedikto wa Nursia alivyochorwa na Giovanni Bellini.

Benedikto wa Nursia (480-547) alikuwa mmonaki wa Italia aliyeandika kanuni ya utawa iliyoenea katika monasteri nyingi za Kanisa la Kilatini na hata nje yake. Wanaoifuata wanaitwa Wabenedikto[1].

Anaheshimiwa tangu zamani kama mtakatifu abati.

Wabenedikto wanaadhimisha sikukuu yake tarehe aliyofariki dunia, lakini kalenda ya Kanisa la Roma inaiadhimisha tarehe 11 Julai[2] tangu Papa Paulo VI alipomtangaza msimamizi mkuu wa Ulaya tarehe 24 Oktoba 1964. Waorthodoksi wanamuadhimisha tarehe 14 Machi.

Benedikto da Nursia, ndugu pacha wa Mtakatifu Skolastika, alizaliwa tarehe 12 Septemba 480, katika familia tajiri ya Roma. Baba yake, Eutropius Anicius, alikuwa kapteni mkuu wa Warumi katika eneo la Nursia, wakati mama yake alikuwa Claudia Abondantia Reguardati, malkia mdogo wa kijiji hicho.

Aliishi miaka ya utoto kijijini Nursia, akiathiriwa na wahamiaji kutoka Dola la Roma Mashariki ambao katika karne III walikimbia dhuluma wakashika maisha ya kiroho katika mapango waliyojichimbia mwambani kandokando ya kanisa dogo.

Alipofikia umri wa miaka 12 hivi mapacha walitumwa Roma kwa masomo, lakini walichukizwa na anasa za jiji hilo, alivyosimulia Papa Gregori I katika kitabu cha pili cha Majadiliano. Hivyo akaacha masomo, nyumba na mali ili avae kanzu ya kimonaki akampendeze Mungu tu.

Alipofikia miaka 17 alitawa kwenye bonde la mto Aniene karibu na Eufide (leo Affile), halafu alielekea Subiaco, alipokutana na mmonaki wa monasteri ya jirani ambayo abati yake Adeodatus alimvika kitawa akamuonyesha pango kwenye mlima Taleo.

Huko aliishi miaka 3 kama mkaapweke hadi Pasaka ya mwaka 500. Halafu akakubali kuongoza wamonaki wengine karibu na Vicovaro, lakini, baada ya kunusurika kuuawa kwa sumu, akarudi Subiaco, alipobaki karibu miaka 30, akihubiri neno la Mungu na kupokea wanafunzi wengi zaidi na zaidi, hata akawa anaongoza monasteri 13, kila mojawapoi kiwa na wamonaki 12 na abati.

Karibu na mwaka 529 baada ya upinzani mkali wa padri jirani aliyejaribu kumuua na kupotosha wafuasi wake, aliamua kuhama akaelekea Cassino ambapo, juu ya mlima alianzisha monasteri ya Montecassino juu ya mabaki ya mahekalu ya Wapagani.

Huko Montecassino Benedikto alitunga kanuni yake mwaka 540 hivi. Akifaidika na zile zilizotangulia, hasa Regula Magistri iliyoandikwa na mmonaki asiyejulikana, lakini pia ya Basili Mkuu, Yohane Kasiano, Pakomi na Sesari, aliunganisha nidhamu na heshima kwa mtawa na vipawa vyake, ili kuunda shule ya utumishi wa Bwana ambapo kauli-mbiu ni ora et labora ("sali na kufanya kazi").

Hadi kifo chake aliishi Montecassino, akitembelewa na waamini na watu maarufu kama Totila mfalme wa Ostrogoti. Alifariki tarehe 21 Machi 547, siku arubaini hivi baada ya Skolastica ambaye akazikwa pamoja naye katika kaburi moja.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Baba, utupe hekima tukutambue, akili tukuelewe, bidii tukutafute, subira tukungojee, macho tukuzingatie, moyo tukutafakari na maisha tukutangaze kwa uwezo wa Roho wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Picha mbalimbali

[hariri | hariri chanzo]

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  • A. GRUEN, O.S.B., Benedikto wa Nursia, Ujumbe Wake Leo –tafsiri ya A. Nyirenda, O.S.B. – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1993 – ISBN 9976-67-071-0
  • M. REGINA GUBERNA, O.S.B., Baba Benedikto – tafsiri ya D. Weis, O.S.B. – ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1983
  • Mtakatifu Sholastika – tafsiri ya Masista wa Chipole –ed. Benedictine Publications Ndanda Peramiho – Peramiho 1985 – ISBN 9976-63-080-8

Marejeo mengine

[hariri | hariri chanzo]
  • Gardner, Edmund G. (editor) (1911. Reprinted 2010). The Dialogues of Saint Gregory the Great. Merchantville, NJ: Evolution Publishing. ISBN 9781889758947. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-06-07. Iliwekwa mnamo 2012-04-06. {{cite book}}: |first= has generic name (help); Check date values in: |year= (help); Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)
  • "The Life of St Benedict," by St. Gregory the Great, Rockford, IL: TAN Books and Publishers, ISBN 0-89555-512-3

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.