Nenda kwa yaliyomo

Malezi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Darasa la wasichana wa Bamozai, Afghanistan.
Mwanafunzi darasani akipinga kuingizwa kwa siasa katika nyenzo za kusoma au walimu wanaotumia vibaya jukumu lao kufundisha wanafunzi, kinyume na malengo ya elimu ambayo hutafuta uhuru wa mawazo na kufikiria kwa kina.
Jan Steen (1672)

Malezi ni kazi maalumu ya muda mrefu ambayo binadamu anamsaidia mwingine kukabili maisha kwa jumla au sehemu yake mojawapo.

Ni kazi inayowapasa kwanza wazazi, ambao wanahitaji msaada wa ukoo, kabila, taifa, dini n.k.

Ni kazi inayohitaji moyo mkuu na ustahimilivu mkubwa.

Nchi za Afrika zilipojikomboa zilikazania elimu ili kupata mapema wataalamu kwa kazi na huduma za jamii.

Hasa siku hizi wengi wameona umuhimu wa kusoma ili kukabili maisha. Ila mara nyingi juhudi hizo hazilengi kujua ukweli, bali kufanikiwa katika kazi na uchumi, na zinaweka pembeni maadili yaliyokuwa muhimu katika malezi ya kimila.

Hayo yalikusudiwa kuwaandaa watoto na vijana kwa maisha, wawe washiriki wa ukoo na kabila ambao wamekomaa kiasi cha kuweza kuchukua majukumu yao.

Hata leo bila ya hayo ujuzi na ufundi vinaweza kuongezeka, lakini ukomavu haufikiwi.

Hivyo vijana wanachelewa kushika nafasi yao katika ujenzi wa jamii, k.mf. kwa njia ya ndoa.

Badala yake unaenea uhuni (uasherati, bangi, wizi n.k.).

Kwa kuwa ujana ni kipindi cha mabadiliko ya haraka pande zote, ni vigumu kuumudu sawasawa na kuwa na msimamo.

Hasa mijini kuna mchanganyiko wa watu (makabila, dini n.k.) pamoja na njia hasi za kuishi zinazotokana na ushindani mkubwa, utepetevu katika maadili na upotovu.

Katika hali hiyo dini ya ukoo si kinga tena: kijana mwenyewe anajichagulia aamini nini na aishi vipi badala ya kufuata tu mazoea ya nyumbani kama alivyofanya utotoni.

Anahitaji kusaidiwa ajibu maswali makuu ya maisha: “Mimi ni nani? Nimetoka wapi? Ninakwenda wapi? Nafikiriwa kuwa wa namna gani?”

Kumbe watu wazima wengi wanamsema badala ya kujihusisha naye katika matatizo yasiyoepukika ya umri wake.

Anahitaji kueleweka na kuthaminiwa, lakini akitafuta hayo anaitwa jeuri, mwenye kiburi n.k.

Hasa siku hizi kati ya wazee na vijana umbali ni mkubwa kutokana na mabadiliko ya nyakati (upande wa elimu, afya, uchumi, mawasiliano, tunu za maisha n.k.).

Vijana wanaonelea miundo asili ni mambo ya zamani, hata wakadharau utamaduni wa mababu kama kwamba mambo yake yote yamepitwa na wakati.

Kinyume chake wanapokea kwa urahisi mkubwa mawazo mengi ya kigeni kupitia vyombo vya upashanaji habari na mitindo mipya inayozuka mijini.

Halafu wanatumia muda mwingi kijiweni au katika burudani, kumbe ule wa kukaa na wazee ni mfupi mno: hilo ni pengo lisilozibika, kwa kuwa linawafanya wasifaidi mang’amuzi ya vizazi vilivyotangulia, kutegemezwa na mashauri wanayoyahitaji, kuungana na ndugu zao katika kukabili maisha.

Wanakuwa jamii tofauti, wageni kati ya watu wao! Maisha ya vijana kwa mtazamo wa sasa yanazidi kuwa tofauti na vijana wa zamani. Nyakati hizi kuna matatizo mengi yawapatayo vijana pamoja na wakati wa ubalehe, uzururaji mitaani, wizi, uvutaji bangi pamoja na kutumia aina nyingine za madawa ya kulevya.

Wazee wengi wanaona vijana wakiungana ni nafasi tu ya kujenga urafiki mbaya, si haja halisi ya nafsi na ya maisha.

Hivyo badala ya kuwasaidia kuchambua mambo wanazidisha hali ya kutoelewana nao.

Basi, hatuna budi kulea kwa kuoanisha ujuzi na ukomavu ili tupate watu tunaowahitaji: watu ambao ni huru kwa ndani na wanaweza kuwajibika kwa uadilifu.

Ili kijana azidi kukomaa kiutu anahitaji kusaidiwa ajifahamu ili kustawisha vipawa vyake na kupunguza kasoro zake.

Utu ndio msingi ambao juu yake yanajengwa maisha yote.

Mwenye matatizo nafsini mwake anasumbuka na kusumbua watu anaofungamana nao.

Basi, ni muhimu awahi kujirekebisha kama inavyobidi kuwahi ili kunyosha mti ukiwa bado mbichi.

Ni lazima aifanyie kazi nafsi yake kwa ustadi na bidii nyingi kuliko mkulima anavyoshughulikia shamba lake ili lizae sana.

Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Malezi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.