Maadili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Maadili ni mafundisho yanayotolewa katika nafasi mbalimbali, hasa katika malezi, ili kuelekeza binadamu atende namna ambayo imjenge yeye na jamii nzima.

Maadili yanayohitajiwa na watu wote kimsingi ni yaleyale, lakini mazingira yanaweza kudai yatekelezwe kwa namna tofauti kiasi.

Pamoja na hayo, watu tangu zamani wametoa maadili namna maalumu kulingana na dini, utamaduni, falsafa n.k.

Mmomonyoko wa maadili[hariri | hariri chanzo]

Mmomonyoko wa maadili ni hali ya kukiukwa kwa maadili ya jamii fulani. Mmomonyoko wa maadili umesambaa kwa kasi sana, kwa vijana kuliko wazee, hiyo yote ni kwa sababu ya vyanzo vifuatavyo.

  1. Utandawazi: huo ni hali ya mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha kwa mwanadamu, kama vile siasa, uchumi n.k. ili kuwa na mfanano mmoja. Lakini mabadiliko hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili kwani vijana wamekuwa watu wa kujifananisha na maisha ya watu wa nchi nyingine, kwa mfano wanaiga namna ya mavazi. Mavazi mengi ya nyakati hizi ni mavazi ambayo yanaporomosha maadili.
  2. Teknolojia: usambaaji wa teknolojia na mawasiliano kurahisishwa kwa kupitia aina mbalimbali za mitandao ya kijamii kumekuwa ni changamoto kwa vijana. Wamekuwa wakitumia muda mwingi kwa kuperuzi mitandaoni na kufuatilia habari za wasanii ambazo haziwahusu kabisa. Lakini pia vijana wameweza kujiingiza kwenye vitendo vya ubakaji, kutokana na picha au video za ngono zinazooneshwa au kupakuliwa kwenye baadhi ya mitandao na kutazamwa na vijana, kwa hiyo teknolojia nayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha maadili ya vijana.
  3. Wazazi kutotimiza wajibu wao: wazazi wengi hawafuatilii watoto: huondoka nyumbani asubuhi na kurudi usiku ambapo huwakuta wamelala, lakini hawa watoto wanaweza wakashawishiwa kununua laptop na simujanja, ambapo huweza kuporomosha maadili yao hadi watakapokuwa wakubwa kwa sababu ni kama samaki ambaye hakukunjwa angali mbichi.
  4. Makundi ya rika: rika ni watu ambao wana umri mmoja au kukaribiana; mtu wa kundirika anaweza kuwa rafiki, jirani au hata mwanafunzi mwenzako. Makundi hayo kwa wakati huo inabidi yatazamwe kwa jicho la tatu, kwani huongelea zaidi mambo ya ngono, tofauti na zamani ambapo makundi hayo yalikuwa yanashauriana kuhusu upendo, usawa, haki na jinsi ya kujitegemea katika familia zao.

Njia zinazopendekezwa ili kutatua mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana ni kama vile:

  • kuelimisha juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii
  • kutoa elimu kwa wazazi juu ya namna bora ya malezi ya watoto
  • kuweka adhabu kwa watakaokiuka sheria au kutenda mambo yasio na maadili
  • kutoa hamasa kwa taasisi za dini juu ya msisitizo wa maadili na malezi ya watoto
  • kuhamasisha vijana kujiajiri ili kuepuka matumizi mabaya ya muda