Ukomavu
Ukomavu wa binadamu ni hali iliyokusudiwa ifikiwe na mtu kupitia ukuaji wake.
Sifa za mtu aliyekomaa
[hariri | hariri chanzo]1. Anayatambua mambo yalivyo. Anajitambua na kuwatambua wengine walivyo. Anatambua matukio pia katika sifa na kasoro. Anatambua yale anayoyaweza na yale asiyoyaweza. Hana wivu wala hofu. Anapima hali mbalimbali bila ya kufumba macho mbele ya mambo yasiyompendeza bali anatumia akili akabiliane nayo.
2. Anakubali hali ilivyo. Anajikubali na kuwakubali wengine walivyo. Akiona kasoro hachukii, bali kwanza anakubali hali ilivyo, halafu anajitahidi kuirekebisha iwezekanavyo. Hata akishindwa anakubali na kuvumilia. Vilevile anaweza kuyakubali mabadiliko na mambo mapya bila ya hofu, kwa kuwa anapima yote bila ya kufadhaika kwa kusema, “Itakuwaje?”
3. Anawajibika. Hangoji kuambiwa kila mara afanye nini na vipi, bali anaona mwenyewe anavyotakiwa kutenda, halafu anaamua kwa moyo ayatende. Ndiyo sifa kuu ya mtu aliyekomaa kweli: ana mwongozo wa maisha ndani mwake. Anazingatia pia kanuni za jamii na kusikiliza mashauri, lakini uamuzi wake unatoka ndani.
4 Anajiongoza kwa kuzingatia tunu alizojichagulia. Anaelekeza maisha yake upande fulani alivyoazimia. Katika kuamua la kufanya anafuata tunu hizo, si mkondo kama wanavyofanya kondoo.
5. Anahusiana vema na watu kwa sababu anawakubali, anawaheshimu na kuamini wanaweza kutenda mema. Anaelewa shida zao na kuwatimizia. Anawafanya wajisikie raha na kutokeza sifa zao. Mwenyewe anajisikia salama na kuwafanya washinde hofu zao na hivyo wakomae kwa urahisi zaidi.
6. Anafanikisha mipango. Ana mawazo ya kushangaza kwa kuwa mitazamo yake ni mipana na ya ndani zaidi. Mipango na miradi yake ni mingi, lakini haogopi kujaribu wala kushindwa, kwa kuwa anatambua mambo yalivyo na yanavyoweza kurekebishwa. Hivyo mara nyingi anafaulu kufanya mambo yawe alivyotaka. Mambo yaliyo magumu kwa wengine, kwake ni rahisi.
7. Anajiendeleza aishi kwa ukamilifu. Anatumia vizuri vipawa vyake vyote. Anafurahia mambo mbalimbali ya maisha na kufaidika nayo ili azidi kujiendeleza.
Pande mbalimbali za ukomavu wa mtu
[hariri | hariri chanzo]1. Wa maono: • anakubali maono yake bila ya kutawaliwa nayo; • anaweza kuyajulisha ili kusaidiwa; • anakabili magumu bila ya kuyaepa wala kuhangaika mno; • si mtu wa kujikinga kila mara.
2. Wa nafsi: • anasikiliza wengine, hatimaye anaamua mwenyewe bila ya wasiwasi mkubwa mno; • anaweza kubadili uamuzi wake akipata habari mpya; • anasema ukweli na kuchukua jukumu la uamuzi wake; • anapokea uamuzi wa wengine.
3. Wa jamii: • anaona wema wa wengine, asijifanye lengo la yote; • anafungamana vema na wengine; • ana marafiki wa kufaa; • hawategemei mno ndugu zake; • anafuata taratibu za jumuia; • analinganisha mahitaji yake na ya kikundi chake; • yuko tayari kutimiza sheria halali hata zisipompendeza • anafanya kazi hata ngumu kwa utulivu.
4. Wa maadili: • anapokea mawazo mazuri na kuyaishi; • anafuata malengo yake kwa sababu anayo ya kufaa; • anatimiza busara, haki, nguvu na kiasi; • yuko imara katika imani, tumaini na upendo.
5. Wa roho: • anafungamana vema na Mungu, malaika na watakatifu; • anamtegemea Mungu na kutimiza matakwa yake; • anaelewa wito wake, anauthamini na kudumu kwa hiari kuuitikia.
Mambo yanayozuia ukomavu
[hariri | hariri chanzo]Binadamu anakusudiwa kukomaa, lakini hafanikiwi sikuzote. Tunawaona watu waliolemaa upande wa mwili, lakini wengi zaidi wamelemaa upande wa nafsi. Sababu ni kwamba mtu akikosa haja zake za msingi hawezi kustawi. Haja hizo zina nguvu sana, nazo zisipotimizwa zinamuacha mtu kilema.
Mambo yanayompata hata akalemaa kinafsi yanaelezwa na mviringo ufuatao usioelekea popote:
1. Hatimiziwi haja za nafsi, ambazo ni za msingi kama zile za mwili, hivyo zisipotimizwa yanaanza matatizo.
2. Hajisikii vizuri, hata kama ni mtoto au haelewi, kwa kuwa mtu akihisi hapendwi, hatakiwi, hayuko salama, basi anajisikia vibaya mpaka ndani.
3. Anapatwa na wasiwasi unaofanya nafsi isistawi, hata kama mwili unaendelea kukua. Ndiyo sababu anashindwa kushirikiana vizuri na watu au anajitenga nao kwa kuona hawampi anayoyahitaji.
4. Kutokana na hofu hashiriki vizuri katika mambo yote. Anatambua kwamba akibaki peke yake hapati nafasi ya kupendwa, lakini anashindwa kukabili hofu yake.
5. Matokeo yake ni kwamba anajihisi hastahili kutimiziwa haja zake. Hatimaye anaweza akajichukia kama kwamba ndiye anayesababisha watu wasimtimizie haja zake.
6. Anafadhaika asijue la kufanya mbele ya matatizo hayo. Anashindwa kupata jibu kuhusu haja zake kutimizwa kesho: ikiwa leo hapati anayoyahitaji hata kwa watu wenye wajibu kwake, je, atayapata lini?
7. Anafuata njia za kujikinga na hofu hizo kusudi asiendelee kufadhaika. Moja ya njia hizo ni kusukuma ndani kabisa mwa nafsi yake yale yasiyompendeza yasielee tena katika kumbukumbu; lakini kadiri mambo hayo yalivyoshindiliwa ndani yanamvuruga na kujitokeza kwa matendo na maneno yasiyotarajiwa. Njia nyingine ya kujikinga ni kutokubali hali halisi, yaani kukataa kukabili jambo la hatari au lisilopendeza. Njia nyingine ni kuhamisha dhihirisho la ono fulani (hasira, chuki n.k.) limlenge mtu tofauti na yule anayekusudiwa. Njia nyingine ni kuishi katika ndoto za mchana badala ya kuwazia hali halisi: mtu anajichorea akilini picha ya ulimwengu mwingine ambapo mambo yanakwenda anavyotaka, hata akaamini ndio wa kweli. Njia nyingine tena ni kujitafutia visingizio ili kutosikia aibu moyoni: mtu anaweza akafikia hatua ya kumshtaki mwenzake kwa kosa alilolifanya mwenyewe. Njia ya mwisho ni kudai kwamba wengine ndiyo wenye hali aliyonayo mwenyewe asiikubali.
8. Kwa kuwa njia hizo hazimtimizii haja zake, hazimsaidii ila zinamtuliza kijuujuu tu kwa muda, yaani zinafunika matatizo yake badala ya kuyatatua. Mtu amejikinga isivyofaa, basi shida inabaki palepale. Hivyo mviringo usioelekea popote umekamilika kwa kurudia namba moja: mtu anahitaji bado kupendwa, kukubaliwa, kuthaminiwa na kuwa salama. Nani atamsaidia?
Dalili za mtu asiyekomaa
[hariri | hariri chanzo]1. Anapurukusha tu na kulipua kazi mpaka asimamiwe.
2. Hatimizi vizuri wajibu wake kwa jumla, ni mtegezi.
3. Anachekacheka na kucheza wakati usiofaa.
4. Ana kiburi cha kitoto.
5. Hajui kujiheshimu wala kuwastahi wengine.
6. Ni mbishi, pia kwa makusudi, tena mlalamishi.
7. Hajui kulinda siri za nyumbani, ni mchongezi.
8. Hajali maonyo, anayachukua kimzaha.
9. Hakubali maoni ya wengine.
10. Si mnyofu wala hajui kujieleza wazi alivyo.
11. Anaogopa kutoa mawazo yake mbele ya watu.
12. Haamui kwa utashi imara.
13. Anafuata mkumbo.
14. Katika kuwapenda wenzake ana ubaguzi.
15. Anajipendekeza na kujipendea.
16. Anadai kubembelezwa na kufarijiwa.
17. Hana uvumilivu wala moyo mkuu.
18. Anatunza kinyongo.
19. Anakata tamaa kwa urahisi.