Ukuaji wa binadamu
Ukuaji wa binadamu ni safari ya kutoka utotoni kuelekea utu uzima.
Unadai tujipokee tulivyo, pamoja na mema na mapungufu yetu, tukimshukuru Mungu kwamba anatupenda tulivyo.
Lakini ni lazima pia tupambane na mapungufu yetu ili kustawisha mema tuliyojaliwa na kufikia uhuru wa ndani.
Kukua kiutu kweli ni kuwajibika maishani kadiri ya mpango wa Mungu aliyetuumba.
Safari hiyo ina hatua mbalimbali, ambazo kila mojawapo ina kazi yake maalumu na ugumu wake.
Kazi hiyo ifanyike katika mazingira ya kufaa, la sivyo tutadumaa.
Kadiri ya Erikson kuna hatua nane zinazofuatana:
1. Mtoto mchanga (miaka 0-2) 2. Mtoto aliyeachishwa (2-4) 3. Chekechea (4-7) 4. Mwanafunzi wa shule ya msingi (7-13) 5. Kijana (13-20) 6. Mtu mzima (20-35) 7. Mtu wa makamo (35-60) 8. Mzee (60 n.k.)
Hatua za kwanza ni fupi lakini muhimu sana, kwa sababu mambo yanayotokea wakati huo yanaathiri maisha yote. Mtoto akisaidiwa vizuri atakuwa mtu ambaye anajisikia salama, anaona mazingira kwa utulivu, anajitawala, anajiamini, haogopi kuwajibika na kuanzisha mambo.
Katika hatua nne za kwanza mtu anahitaji kuziba mapengo yake, katika zile nne za mwisho anahitaji kustawi.
Katika kila hatua hana budi kufanya kazi fulani na kukabili ugumu maalumu ili kukua. Vilevile anahitaji kusaidiwa kufanya hivyo (ndiyo malezi).
Tunapitia hatua hizohizo kila tunapoingia maisha mapya (k.mf. shuleni).
Kujiamini na kuamini wengine
[hariri | hariri chanzo]Mtoto anapozaliwa anaanza kuishi katika ulimwengu tofauti na ule aliouzoea tumboni mwa mama. Yuko kwenye hewa na mwanga badala ya kuogelea katika majimaji. Anapaswa kupumua na kutafuta mahitaji yake mwenyewe, ingawa bado anamtegemea sana mama (kwa maziwa, upendo, usalama n.k.).
Ugumu wa kipindi hicho ni kwamba anataka kuwa naye daima, lakini wao ni watu wawili tofauti. Hivyo anapaswa kukubali ukweli huo na kuanza kujiamini. Anaanza kutambua kama anapendwa na kupokewa au la, naye anaanza kutofautisha watu wa kuwaamini na wale ambao asiwaamini.
Anahitaji upendo, usalama na chakula toka kwa mama.
Kujitawala na kuongozwa
[hariri | hariri chanzo]Mtoto wa miaka 2-4 anatembea, anasema, anacheza na kuvumbua vitu vingi, anaanza kujitambua na kutambua uhusiano wake na ndugu. Anaanza kutumia utashi ili kujitawala: miaka hiyo anasema mara nyingi, “hapana” na kugombana na mzazi.
Ugumu ni kufaulu kujitawala; akishindwa atakuwa daima na aibu na shaka, hasa akilaumiwa na kupewa adhabu kali mno.
Anahitaji kupokewa na kusaidiwa akuze mema anayoyafanya. Anahitaji pia unyofu na msimamo wa nidhamu kutoka kwa wazazi. Ikiwezekana wamueleze kwa ufupi lakini wazi sababu za kumkataza. Pengine anahitaji kuvumiliwa.
Kuanzisha mambo
[hariri | hariri chanzo]Mtoto wa miaka 4-7 anawaza sana kwa ubunifu. Ndio wakati wa kuuliza maswali mengi, “Kwa nini...?”. Anafyonza na kuiga lolote lile. Anaanza kutambua tofauti za jinsia, na mwenendo unaomfaa kama mtoto wa kiume au wa kike.
Ugumu ni kwamba asipojibiwa maswali atajisikia kutupwa. Hivyo ni rahisi kuwa atajisikia daima na hatia, hata asipofanya kosa.
Anahitaji kupokewa, kukubaliwa, kujibiwa.
Kutenda
[hariri | hariri chanzo]Mtoto wa miaka 7-13 anachukua majukumu ya kiadili. Kisha kutofautisha uadilifu na uovu, anachagua kutenda mema au mabaya. Anapanua mawazo, anafanya kazi za mikono, anatengeneza vitu. Pia anajenga uhusiano na wengine, anafanya kazi pamoja nao. Anahisi kuwa anaweza au hawezi. Ni umri mzuri wa kufundishwa dini na kuongozwa kiadili. Kwa kuwa ana mambo mengi ya kufanya, jinsia huwa imelala, kabla haijaamka katika ubalehe. Lakini hiyo inategemea mazingira na malezi.
Ugumu ni kwamba asiposaidiwa sawasawa atakuwa mnyonge daima, atajiona hawezi chochote, au walau si sawa na wengine. Hivyo mazingira yanaweza kumjenga au kumbomoa.
Anahitaji kutiwa moyo (anapenda ukweli na sifa) ajihisi anaweza kufanya kitu, atambue mahitaji ya wengine na kuwasaidia wayapate.
Kujipatia taswira-nafsi
[hariri | hariri chanzo]Umri wa miaka 13-20 ni kipindi cha mpito chenye mabadiliko mengi yanayoathiri mwendo mzima wa kijana ili atoke utoto na kuingia utu uzima. Msichana anabalehe mapema kuliko mvulana. Mvulana ana mwamko mkubwa kuliko msichana. Kuna mvuto mkubwa kati yao, hivyo wanahitaji kuongozwa na nidhamu safi (maadili ya unyago). Ni kipindi cha [[vurugu na cha hisi kali (kulia, kucheka n.k.). Akili inapanuka sana na kupenda nadharia; hivyo ni wakati wa kujipatia maarifa.
Ugumu ni kwamba hatambui mahitaji yake halisi (yuko wapi, naye ni nani?), anaogopa (je, atafaulu kuwa mtu mzima?), hajui kutumia hiari yake vizuri, anataka kuishi tofauti na maelekezo ya wazazi ili ajitegemee. Kutokana na hayo anayatilia shaka mafundisho ya dini (ukweli uko wapi?).
Anahitaji kujifahamu na kujipatia msimamo (taswira-nafsi) katika maisha, la sivyo atazama katika vurugu tupu.
Kufungamana na watu
[hariri | hariri chanzo]Kati ya miaka 20 na 35 kijana anakuwa mtu mzima na kuweza kufungamana kwa dhati na wengine kwa kupenda na kupendwa, na kwa kushirikishana yaliyo muhimu. Hiyo inatakiwa sio tu katika ndoa, bali hata utawani ili mtu aishi kulingana na umri wake.
Ugumu ni kutojifahamu na kuogopa kufahamika alivyo.
Anahitaji kuvumilia, kuheshimiana na watu pamoja na kujali mipaka katika kupendana.
Kuzaa matunda
[hariri | hariri chanzo]Kati ya miaka 35 na 60 mtu anapaswa kuzaa matunda, kuonyesha matokeo ya maisha yake, hasa kwa kulea wanaofuata na kwa kuwatunza waliotangulia.
Ndio ugumu wake; asipofanya hivyo mtu anabaki tasa.
Anahitaji kukubali uongozi na kujitolea zaidi na zaidi.
Kujumlisha maisha
[hariri | hariri chanzo]Baada ya miaka 60 mtu anatakiwa kukusanya vipande vya maisha yaliyopita na kuleta umoja katika nafsi yake.
Ugumu ni kwamba hataki kuzeeka, kumbe anapoelekea kifo sharti aendelee kuzaa matunda kwa kushirikisha hekima ambayo alijipatia na ambayo inatarajiwa kumuandaa kwa kifo.
Anahitaji kuyapokea maisha yalivyo sasa, pamoja na mipaka inayozidi kutokana na uzee (hadi ukongwe). Asiporidhika atakata tamaa, na kuanza kunung’unika, kulaumu na kupatwa na wasiwasi kila mara.