Tumaini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Waridi likitokeza tumaini katika kambi ya maangamizi ya Auschwitz.
Tumaini katika gereza la kukata tamaa, 1887, mchoro wa Evelyn De Morgan.
Maadili ya Kimungu

Tumaini ni hali ya nafsi yenye matarajio mema kuhusu mambo yajayo.

Katika dini tumaini linatokana hasa na imani katika wema wa Mwenyezi Mungu.

Katika Biblia[hariri | hariri chanzo]

Ukristo, ukimfuata Mtume Paulo, unaliorodhesha pamoja na imani na upendo kati ya maadili yanayodumu. “Hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu” (1Thes 1:3). “Sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu” (1Thes 5:8). “Sikuzote tukiwaombea, tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote, kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni” (Kol 1:3-5). “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo” (1Kor 13:13).

Hayo matatu yanaitwa maadili ya Kimungu kwa kuwa asili na lengo lake ni Mungu mwenyewe. Hatuwezi kujipatia hayo, bali tunamiminiwa naye kwa pamoja tuweze kumsadiki, kumtumaini na kumpenda inavyotupasa tuwe marafiki wake. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Ef 2:8). “Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana” (1Thes 4:9).

Imani inatuletea tumaini na upendo kwa sababu tukipokea ufunuo wa Mungu na kumjua alivyo mwema, tunamtamani na kumtegemea ili tumpate milele, na tunavutiwa kumrudishia upendo. Hivyo imani inachanua tumaini na kuzaa upendo: hapo ni hai na kutuokoa. “Katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo” (Gal 5:6).

Tumaini ndiyo msimamo wa utashi wa kumlenga Mungu kama heri yake ya milele, kwa kutegemea ukuu wa wema ambao ameahidi kutusaidia. Abrahamu “aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa” (Rom 4:18). “Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu” (Eb 10:23). “Nani aliyemtumainia Bwana akaaibika?” (YbS 2:10).

Hata hivyo, hatuwezi kujua kama tutafika mbinguni, ila tumaini linatupa hakika ya kwamba tunaelekea huko, na kwamba tukiendelea mpaka mwisho tutafika kweli. “Sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani ukombozi wa mwili wetu. Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena.” (Rom 8:23-24). “Mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mk 13:13).

Katika maisha ya kiroho[hariri | hariri chanzo]

Sawa na imani, adili la kumiminiwa la tumaini ni la lazima kwa wokovu na kwa ukamilifu wa Kikristo. Tena haitoshi tumtumainie Mungu kwa namna dhaifu na kwa kwikwi kama wengi wanavyofanya; bali tuyapende matakwa yake ambayo mara nyingi yana giza, pengine yanashangaza hata kutaka kuchukiza: tuyapende kwa utiifu wa kitoto na kusubiri msaada wa Mungu kwa tumaini imara, nyenyekevu na la kudumu.

Kasoro za kuepwa[hariri | hariri chanzo]

Ni lazima tuepe kasoro mbili zinazopingana: kujiamini kipumbavu na kukata tamaa. Inafaa tuzione kwanza ili tuelewe tumaini halisi ni nini na jinsi linavyoinuka juu ya hizo.

Kujiamini kuna namna mbili: ama mtu anategemea mno nguvu zake mwenyewe asiombe vya kutosha msaada wa Mungu wala kuzingatia neema inavyohitajika kwa tendo lolote la kuletea wokovu; ama mtu anatarajia kupewa na huruma ya Mungu jambo lisilowezekana kabisa, k.mf. msamaha pasipo toba halisi, au uzima wa milele pasipo juhudi.

Mara nyingi watu hao, wakipatwa na majaribu, wanatumbukia kosa lililo kinyume chake, yaani kukata tamaa, kana kwamba jema lililo gumu kupatikana, ambalo ndilo kusudio la tumaini, lingekuwa halifikiki. Kukata tamaa kunaweza kukazaa uzembe katika mambo ya Kiroho, unaotufanya tuione ngumu mno kazi ya kupata utakatifu na unaotuzuia tusijitahidi kuifanya. Hatimaye kuna hatari ya kukata tamaa kuhusu wokovu wenyewe.

Wengi wanayumbayumba hivyo wasiweze kamwe kuelewa tumaini la Kikristo na kuliishi ipasavyo.

Mfumo halisi wa tumaini la Kikristo[hariri | hariri chanzo]

Adili hilo linazungumziwa kidogo kuliko imani na upendo, lakini ni muhimu. Likiwa adili la kumiminiwa na Mungu linapita maumbile, hivyo linapita hamu ya kimaumbile ya kupata heri na hata lile tumaini la kimaumbile kwa Mungu linaloweza kutokana na kuujua wema wake kwa akili tu.

Kwa tumaini la kumiminiwa tunalenga heri ipitayo maumbile, yaani kumpata Mungu milele, kumuona kama anavyojiona, na kumpenda kama anavyojipenda. Tena tunamlenga tukitegemea msaada aliotuahidia. Sababu ya kutumaini si juhudi zetu, bali ni Mungu anayetusaidia daima kadiri ya huruma yake, ahadi zake na uwezo wake mkuu. Sababu ya adili lolote la Kimungu haliwezi kamwe kuwa kiumbe, hata kikiwa bora, bali ni Mungu tu. Hivyo tunataka kumpata Mungu, lakini kwa ajili yake, kwa kuwa ndiye lengo kuu la tumaini ambalo tena linatakiwa kuhuishwa na upendo. Yaani kwa tumaini tunamtamani Mungu si kwa ajili yetu kama tunavyotamani chakula ili kuishi, bali kwa kujiweka chini yake. Kwa hiyo halina kasoro yoyote: ni adili la Kimungu, ingawa la chini kuliko upendo.

Ikiwa adili la kiutu la moyo mkuu ni zuri kwa sababu linatufanya tukusudie makuu, zuri zaidi ni tumaini linalotufanya tumlenge Mungu mwenyewe tuwe naye milele. Hasa kwa sababu halitutamanishi tu kiwango cha chini cha heri ipitayo maumbile, bali uzima wa milele pasipo kupanga kiwango chochote; kinyume chake linatufanya tumuelekee Mungu kwa kasi zaidi na zaidi kutokana na kumtamani zaidi na zaidi.

Hakika ya tumaini[hariri | hariri chanzo]

Thoma wa Akwino ametofautisha vizuri aina mbalimbali za hakika. Kwanza alikabili hoja ya kwamba hakuna anayeweza kuwa na hakika ya kuokoka asipojaliwa ufunuo wa pekee; na kwa kuwa huo ni wa nadra, tumaini la wengi linaonekana halina hakika. Tena ya kwamba kati ya wale wanaotumaini wengi watavunjika moyo na hatimaye kupotea. Akasisitiza kuwa tumaini lina hakika, ingawa tofauti na ile ya imani iliyomo akilini: hakika ya tumaini imo katika utashi na ina namna ya elekeo. Tumaini linaelekea kwa hakika lengo lake likishiriki hakika ya imani; kama vile tukipanda treni tuna hakika ya kuwa njiani na tunatumaini kufika salama, ingawa hatuna hakika ya kufika. Hakika ya tumaini si ya kufikia wokovu, bali ya kuuelekea kwa uongozi wa imani usiodanganya kadiri ya ahadi za Mungu “ambaye haagizi kamwe yasiyowezekana, bali anatuagiza tutende tunavyoweza, na tuombe tusiyoyaweza peke yetu” (Mtaguso wa Trento). Yatokanayo kwa utekelezaji ni mengi kuhusu sifa za tumaini ambazo zikue pamoja nalo.

Sifa za tumaini la Kikristo[hariri | hariri chanzo]

“Wote wanapaswa kuwa na tumaini imara kabisa kuhusu msaada wa Mungu. Watu wasipokataa neema zake, mwenyewe atatimiza kazi ya wokovu aliyoianzisha ndani mwetu, akisababisha ndani mwetu kutaka na kutenda. Lakini ‘anayejidhania kuwa amesimama aangalie asianguke’ (1Kor 10:12), na atimize wokovu wake ‘kwa kuogopa na kutetemeka’ (Fil 2:12) ‘katika tabu, katika kukesha, katika kufunga’ (2Kor 6:5)… Kadiri ya neno la mtume Paulo, ‘Kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi’ (Rom 8:13)”. Kulingana na mafundisho hayo ya Mtaguso wa Trento, tumaini la Kikristo lina sifa mbili: kufanya juhudi ili kutojiamini kipumbavu kwa kusubiri tuzo ya Mungu pasipo kufanya kazi; na kuwa imara lisishindikane, ili kutokata tamaa.

Linadaiwa bidii kwa sababu linalenga jema lililo gumu kupatikana; tunapaswa kujitahidi kwa unyenyekevu na kujikana ili tudumishe hamu hai ya uzima wa milele. Hamu hiyo inapozwa na uchu wa anasa na wa vyeo na ni ya nadra hata kwa Wakristo wema, ingawa hakuna la kutamaniwa kuliko muungano na Mungu. Halafu tunapaswa kujitahidi ili kustahili heri ya milele. Tunahitaji neema ili kulifikia lengo, lakini tunajaliwa neema ili tuifanyie kazi kwa bidii kubwa zaidi na zaidi, si kusudi tupumzike: “Mwenye kusaburi hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mk 13:13). “Hata mtu akishindana katika machezo, hapewi taji, asiposhindana kwa halali” (2Tim 2:5). Inatupasa tuondoe vizuio vya tabia mbovu, uzembe, kiburi, ugomvi, uchu wa madaraka, na tushike amri za Mungu vizuri zaidi na zaidi kadiri ya wito wetu. Tumaini hilo lenye bidii pamoja na kipaji cha uchaji vinatuepusha tusijiamini kipumbavu.

Kati ya matatizo yanayoweza yakazuka hadi kifo na hadi kuingia mbinguni, tumaini linatakiwa kuwa imara lisishindikane wala kupungua kamwe kwa vishawishi, majaribu au makosa. Halitakiwi kushindwa na vishawishi vinavyotokana na ulimwengu, mwili na shetani: “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” (Rom 8:31). “Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1Kor 10:13). Tumaini halitakiwi kupungua hata kwa majaribu ambayo Bwana anatutakasa na kutufanyiza kazi kwa wokovu wa watu. Sababu ya kutumaini ni mwenyewe aliye tayari daima kutusaidia. Abrahamu “aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa” (Rom 4:18), hadi akajiandaa kumchinja mwanae Isaka aliyeahidiwa atampatia uzao mkubwa. Lengo la Mungu kutakasa tumaini ni kuliondolea vurugu za umimi, si kutufanya tuache hamu ya wokovu wetu, jambo ambalo lingekuwa sawa na kujinyima kumpenda milele Mungu kuliko vyote. Kama tungeacha kutumaini kwa lengo la kupata upendo safi zaidi, papo hapo tungeacha upendo wenyewe. Hatimaye, tumaini halitakiwi kupungua hata mbele ya makosa tuliyotenda. “Msizingatie kamwe makosa yenu yaliyopita isipokuwa kwa mwali mwangavu wa huruma isiyo na mipaka, ili kumbukumbu yake isiwakatishe tamaa, bali iwafanye mtumainie thamani isiyo na mipaka ya stahili za Mwokozi” (Katerina wa Siena). “Watu wanaweza wakadhani kwamba nina tumaini kubwa kwa Bwana kwa sababu sijawahi kutenda dhambi. Mama yangu, ukweli ni kwamba kama ningekuwa nimetenda madhambi yote yanayowezekana ningekuwa na tumaini hilohilo, ningeona wingi huo wa makosa ni tone la maji tu lililotupwa katika tanuri yenye kuwaka” (Teresa wa Mtoto Yesu). Yaani sababu ya kutumaini si juhudi zetu wala usafi wetu, bali ni huruma ya Mungu inayotusaidia.

Matunda mazuri ajabu ya tumaini hai lililothibitishwa na majaribu[hariri | hariri chanzo]

Baada ya majaribu kadhaa, tumaini likiwa limeimarika linashinda kizuio chochote: “Tunasimama ndani yake (neema); na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na tufurahi katika dhiki pia; tukijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:2-5). “Mtume Paulo ametuonyesha kwanza ukuu wa tumaini kwa njia ya ukuu wa jambo linalotarajiwa, halafu nguvu, ari ya tumaini. Kwa kuwa anayetumaini sana jambo fulani, kwa ajili hiyo yuko radhi kuvumilia matatizo na machungu. Basi, ishara ya kuwa tunamtumainia Kristo kwa uimara ni kwamba hatufurahii tu wazo la utukufu ujao, bali pia tabu na majaribu tunayopaswa kuvumilia. ‘Imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi’ (Mdo 14:22). Mtume Yakobo alisema, ‘Hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi’ (Yak 1:2-3). Kwa kuwa anayevumilia majaribu anakuwa bora, amefaulu. Katika kitabu cha Hekima (3:4-6) imeandikwa kuhusu waadilifu, ‘Hata ikiwa - waonavyo watu - wanaadhibiwa, hata hivyo taraja lao limejaa kutokufa, wakiisha kustahimili kurudiwa kidogo watapokea wingi wa mema. Kwa kuwa Mungu amewajaribu, na kuwaona kuwa wamemstahili; kama dhahabu katika tanuru aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara’. Hivyo jaribu linakuza tumaini, na tumaini halidanganyi kamwe, kwa sababu Mungu hawaachi wanaomtumainia: ‘Nani aliyemtumainia Bwana akaaibika?’ (YbS 2:10). Ni wazi kuwa Mungu hatakataa kujitoa kwa wale anaowapenda, ambao ameshawapa Mwanae… amewaandalia mema ya milele wale wanaompenda kuliko vyote” (Thoma wa Akwino).

Katika majaribu makubwa, tutarajie yasiyotarajika, tukimpenda Mungu kwa ajili yake mwenyewe. Hapo upendo unastawi na kuwa safi, nao unahuisha tumaini badala ya kulifuta. Majaribu hayo yanafaa kulitakasa kutoka umimi wa kutaka kujipatia ukamilifu ambao ni “wetu”. Mama fulani aliyetaka “kupata utakatifu”, baadaye akatokeza hamu yake kwa namna isiyo ya binafsi hivyo, akisema, “Bwana, ufalme wako uzidi kufika ndani mwangu”. Hapo alifurahi kutoheshimiwa na watu, akitamani tu kuungana na Bwana. Tumaini linastawi kwa kutakaswa. “Nakushukuru kwa moyo, Bwana wangu, kwa kuwa mambo hayaendi ninavyotaka mimi, bali unavyotaka wewe: afadhali yaende unavyotaka wewe, kwa sababu hakuna shaka ya kwamba unavyotaka wewe ni vema kuliko ninavyotaka mimi” (Filipo Neri). Kwa wanaompenda Mungu, yote yanachangia ustawi wao, hata kusumbuka, kushindwa na kupingwa: hizo zote ni nafasi za kuinua moyo kwa Mungu kwa imani na tumaini. “Hata kama mtu hajisikii kuwa na tumaini hilo kwa Mungu, asiache kulitekeleza. Kutojiamini sisi na nguvu zetu kuendane na unyenyekevu na imani, ambavyo vinajaliwa kumtumainia Mungu. Kadiri tusivyo na raha tunapaswa kumtumainia yule ambaye anaona hali yetu na anaweza kutusaidia! Hakuna anayemtumainia Mungu pasipo kuchuma matunda ya tumaini lake. Mtu aendelee kutulia na kumtumainia yule anayeweza kustawisha kilichopandwa. Hatutakiwi kuacha kazi, lakini katika kuifanya tumtumainie Mungu tu kuhusu ufanisi wake” (Fransisko wa Sales).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Averill, James R. Rules of hope. Springer-Verlag, 1990.
  • Miceli, Maria and Cristiano Castelfranchi. "Hope: The Power of Wish and Possibility" in Theory Psychology. April 2010 vol. 20 no. 2 251–276.
  • Kierkegaard, Søren A. The Sickness Unto Death. Princeton University Press, 1995.
  • Snyder, C. R. Handbook of hope: theory, measures, & applications. Academic [Press], 2000.
  • Stout, Larry. Ideal Leadership: Time for a Change. Destiny Image, 2006

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: