Uongozi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Niccolò Machiavelli ambaye, katika kitabu chabe maarufu The Prince, aliandika kama kiongozi hawezi kuogopwa na kupendwa kwa wakati mmoja, ni afadhali aogopwe kuliko kupendwa.

Uongozi ni mamlaka au karama ya kuwaonyesha watu njia kwa vitendo.

Kipimo cha uongozi ni jinsi gani kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.

Kiongozi bora hana muda wa kulalamika bali anatafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi au watu walio chini yake. Kiongozi wa kweli akiongea, watu husikiliza.

Maana ya uongozi[hariri | hariri chanzo]

Uongozi ni dhana, taaluma inayompa mhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaongozwa naye kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao.

Uongozi ni dhana, taaluma anayopewa mhusika katika kuwaongoza wale waliohitaji kusimamiwa au walioamuliwa kusimamiwa katika kufanikisha jambo fulani kwa maslahi ya wote au ya mtu mmoja mmoja.

Aina za uongozi[hariri | hariri chanzo]

i) Kuna njia nyingi za kuainisha uongozi lakini njia ya msingi ni kuangalia jinsi kiongozi alivyoingia madarakani na utaratibu wake wa kuongoza.[1]

ii) Katika viongozi wapo Wafalme, Marais, Mawaziri, Watemi, Machifu, Wakurugenzi, Viongozi wa dini[2] n.k.

iii) Viongozi hawa wote tunaweza kuwagawa katika mafungu yafuatayo kutokana na jinsi walivyoingia madarakani na namna wanavyoongoza kama ifuatavyo:

  • i. Wale wanaopata uongozi kwa kurithi.
  • ii. Wanaopata uongozi kwa kuchaguliwa.
  • iii. Wanaojitwalia mamlaka ya kuongoza kwa nguvu.
  • iv. Wanaoteuliwa na mamlaka za juu zaidi.

iv) Kiongozi anayeingia madarakani kwa mojawapo ya njia zilizotajwa hapa juu anaweza kutumia mtindo wake wa uongozi. Ipo mitindo mbalimbali ya uongozi:

  • i. Uongozi wa kimila
  • ii. Uongozi wa kidemokrasia.
  • iii. Uongozi wa kiimla ni mtindo wa kuongoza ambao kiongozi huongoza kwa amri bila kushirikisha watu wengine katika kufanya maamuzi. Mara nyingi uongozi wa aina hii haulengi katika kukidhi maslahi ya walio wengi, bali tu ya yule anayeongoza na wale wanaomlinda.
  • iv. Uongozi wa kidemokrasia ni ule wa kushirikisha watu katika kufanya maamuzi na utekelezaji wake. Kwa kawaida viongozi wa aina hii hulenga kukidhi mahitaji ya walengwa.

Viongozi wanaochaguliwa mara nyingi huwa wanapewa muda wa kuongoza, na wale viongozi wanaojiteua hujipatia wao wenyewe muda wa kuongoza au hata hapo watakapoamua kuachia madaraka.

Sifa za kiongozi bora[hariri | hariri chanzo]

i. Awe na ufahamu. Kiongozi ni lazima awe na ufahamu mkubwa juu ya taasisi anayoiongoza, malengo yake, mazingira na matatizo yake.

ii. Awe mwaminifu. Kila taasisi inalenga kufikia shabaha fulani. Ni wajibu wa kiongozi kuwaongoza wanataasisi ili wafikie malengo yao. Kwa hiyo kiongozi ni lazima aweze kubuni mikakati na mbinu zitakazoiwezesha taasisi anayoongoza kufikia malengo yake.

iii. Awe na maadili mema. Kiongozi ni lazima akubalike katika jamii na taasisi anayoiongoza. Ili akubalike hana budi kuzingatia maadili ya msingi ya jamii na taasisi yake. Mtu mwongo, mlevi, mvivu, asiye mwaminifu n.k. hawezi kuwa kiongozi mzuri.

iv. Amche Mungu.

v. Awe anakubalika na watu anaowaongoza.

vi. Awe anaongoza watu katika misingi bora ya uongozi bila kujali jinsia, rangi, dini wala kabila. Awathamini watu wa makundi yote.

vii. Awe anakubali kushauriwa ua kupokea ushauri kutoka kwa wengine.

viii. Awe na uwezo wa kujifunza kutoka kwa watu wengine waliofanikiwa.

ix. Awe na mawazo ya mbele ya kuona tatizo na kuonyesha baadhi ya njia za kulitatua, pamoja na kuona fursa

Marejeo[hariri | hariri chanzo]