Nenda kwa yaliyomo

Niccolo Machiavelli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Niccolò Machiavelli)
Taswira ya Macchiavelli ilivyochorwa na Santi di Tito

Niccolo Machiavelli (kwa Kiitalia: Niccolò di Bernardo dei Macchiavelli) (3 Mei 146921 Juni 1527) alikuwa mwanasiasa, mwandishi na mwanafalsafa nchini Italia.

Machiavelli anajulikana duniani kwa maandishi yake ambamo alieleza siasa kama mbinu ya kutafuta na kutetea utawala bila kujali maadili au tofauti kati ya mema na mabaya.

Machiavelli alizaliwa mjini Firenze akaendelea kuishi huko.

Alijiunga na utumishi wa serikali ya jamhuri ya Firenze wakati watemi wa ukoo wa Medici walipofukuzwa mjini. Akawa katibu wa serikali na balozi wake katika safari mbalimbali za kutembelea watawala wa nje.

Maandishi

[hariri | hariri chanzo]

Kitabu chake ambacho kimekuwa maarufu kinaitwa "Il Principe" (tamka: il prin-chi-pe) au "Mtawala". Humo alieleza masharti ya utawala kwa kiongozi wa kisiasa.

Sanamu ya Niccolo Machiavelli katika Jumba la Uffizi, Firenze.

Aliandika ya kwamba kuna vipindi vigumu katika maisha ya mataifa na madola ambapo anahitajika kiongozi wa kisiasa atakayeshika utawala na kutengeneza upya misingi ya dola. Katika utekelezaji wa kazi hiyo anapaswa kushinda kwa namna yoyote akiondoa vizuizi na kila upinzani. Hatakiwi kubanwa na masharti wala sheria za maadili.

Machiavelli aliandika ya kwamba ni afadhali kama mtawala anapendwa na kuhofiwa na wananchi kwa wakati uleule. Ila, kama anapaswa kuchagua kati ya kupendwa au kuhofiwa kwa sababu haiwezekani kuwa na pande zote mbili wakati mmoja, ni heri akihofiwa.

Pia ni ushauri wa Machiavelli kwamba matendo ya kinyama yatekelezwe haraka na vikali kwa sababu yatasahauliwa; lakini mema yatolewe polepole na kidogokidogo ili yakumbukwe kwa muda mrefu. Mtawala anatakiwa kutetea kanuni za mema mbele ya watu hata kama yeye mwenyewe atatenda kinyume chake lakini ikiwezekana kwa siri.

Haya yote yanatakiwa machoni pa Machiavelli kwa shabaha ya juu ambayo ni heri ya umma. Utawala wa kiongozi mmoja uwe kipindi tu na shabaha iwe jamhuri inayofuata sheria zake. Ila tu katika vipindi vya matatizo uongozi mkali unapaswa kuwepo.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Niccolo Machiavelli kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.