Nenda kwa yaliyomo

Siasa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mwanasiasa)
Kampeni za kisiasa nchini Italia.

Siasa ni njia ya kufanya maamuzi katika ngazi mbalimbali za jamii, kama vile mji, taifa, au hata dunia nzima (siasa ya kimataifa).

Sehemu muhimu ya siasa ni majadiliano kati ya watu mbalimbali wenye nguvu au mamlaka.

Katika demokrasia kila mtu ana kiasi fulani cha nguvu, kwa hiyo siasa ya demokrasia ina maana ya watu wote kuchangia maamuzi.

Hapa chini, mifumo mbalimbali ya kisiasa huelezwa kifupi:

Utawala wa Kifalme

ni mfumo wa uongozi unaompa mamlaka ya dola na ya serikali Mfalme. Katika mfumo huu madaraka hurithiwa na mtu wa familia ya kifalme.

Utawala wa Kiimla

ni mfumo wa uongozi unaotoa madaraka yasiyo na mipaka kwa kiongozi. Katika utawala huu watu binafsi hawana haki na uhuru katika maamuzi.

Utawala finyu

ni mfumo unaowapa wachache kati ya wengi nguvu za maamuzi katika dola na serikali. Nafasi ya wachache hawa hutokana na haiba na uwezo wao kiuchumi, kijamii, kijeshi au kutokana na mafanikio yao katika nyanja mbalimbali za maisha. Mfumo huu ni nadra sana siku za hivi karibuni. Pia waweza kuitwa utawala wa makabaila.

Utawala wa Umma

ni utawala unaotokana na jamii kuamua misingi ya kujiongoza, hivyo unatoa fursa ya madaraka kwa umma moja kwa moja au kutokana na kuwakilishwa. Mfumo huu wa utawala hujulikana kama demokrasia na umegawanyika katika sehemu zifuatazo:

Demokrasia Chama

ni aina ya demokrasia ya kura. Inashirikisha watu wote kuwa wanachama.

Demokrasia Baguzi

ni aina ya demokrasia inayojikita katika kulinda nguvu za kiuchumi zaidi.

Demokrasia Duni

ni aina ya demokrasia inayotokana na makundi ya watu na kisha kupitia makundi hayo watu kuunda serikali mfano: chama - serikali.

Demokrasia Endelevu

ni aina ya demokrasia inayotoa fursa ya usawa na kupinga matabaka katika jamii.

Demokrasia Shirikishi

katika aina hii ya demokrasia wachache hupewa dhamana na wengi katika uwakilishi wa jamii katika maamuzi.

Wachache huchaguliwa na wengi kwa njia ya demokrasia huru na haki kwa kufuata Katiba ya nchi hiyo. Mfano: Wabunge huwakilisha wananchi wao katika kuleta maendeleo na kuishauri serikali juu ya maendeleo ya nchi.