Nenda kwa yaliyomo

Elimuanga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Aina mbalimbali za darubini ni vyombo muhimu vya elimuanga.

Elimuanga (pia: astronomia, kutoka maneno ya Kigiriki ἄστρον astron "nyota" na νόμος nomos "sheria") ni elimu juu ya magimba ya ulimwengu kama vile nyota, sayari, miezi, vimondo, nyotamkia, galaksi kuhusu nyendo zao, nafasi, umbali, ukubwa na sheria zinazotawala tabia zake.

Elimuanga ni tofauti na unajimu ambayo si sayansi bali jaribio la kuona uhusiano kati ya nyota na tabia za wanadamu na pia kutabiri mambo yajayo. Hata hivyo vyanzo vya fani zote mbili zilikuwa karibu sana katika historia ya binadamu hadi kutokea kwa elimuanga ya kisayansi.

Chanzo na historia ya elimuanga

Elimu ya nyota nyakati za kale

Tangu zamani watu waliangalia nyota wakajifunza kuzitofautisha. Mabaharia na wasafiri wakati wa usiku waliweza kutumia nyota kama vielekezi safarini. Walitazama pia mabadiliko ya kurudia kati ya nyota zinazoonekana angani wakati wa usiku. Wakaona mabadiliko haya ya jinsi nyota zinavyoonekana yaweza kuwa uhusiano na nyakati za mvua, baridi na joto, mavuno na ustawi wa mimea katika mwendo wa mwaka. Kutazama nyota vile kulikuwa msaada wa kupanga vipindi vya mwaka na kuunda kalenda.

Watazamaji wa nyota walianza kutambua pia tofauti kati ya nyota mbalimbali, kwa mfano nyota zenye mahali palepale kila wakati na nyota chache za pekee zilizobadilisha mahali angani kwa utaratibu wa kurudia na hizi ziliitwa sayari, tena nyota nyingine zilizoonekana kwa muda tu zikibadilisha mahali pake angani zikaitwa vimondo.

Kwa karne nyingi wataalamu katika sehemu mbalimbali za dunia walihisi ya kwamba nyota hizo zilikuwa miungu iliyoonekana kwa mbali sana. Katika vitabu vya dini vya kale kuna majadiliano juu ya tabia zao; wakati mitholojia ya mataifa mengi iliona nyota kuwa miungu, Biblia ilifundisha ni taa zilizowekwa angani na Mungu pekee aliye mwumbaji wa ulimwengu.

Wataalamu wa kale katika nchi kama Uhindi au Ugiriki ya Kale walianza kutambua mwendo wa sayari na kuunda nadharia yuu ya uhusiano wa dunia, jua na sayari nyingine. Ndiyo chanzo cha imani ya kwamba nyota zinaweza kuwa na tabia fulani na athari juu ya maisha duniani na hasa kama mtu alizaliwa wakati nyota fulani ilionekana, basi tabia zilizoaminiwa kuwa za nyota ziliweza pia kuathiri maisha ya mtu huyo. Hapa kuna asili ya "kupiga falaki" na unajimu wa kisasa. Wakati uleule wataalamu hao walitazama nyota jinsi zilivyo, kuziorodhesha na kupiga hesabu za kalenda. Orodha ya kale iliyoendelea kutumiwa kwa zaidi ya miaka 1,000 ilikuwa ya Klaudio Ptolemaio kutoka Misri.

Kupanuka kwa elimu tangu kupatikana kwa darubini na kamera

Kwa macho matupu mtu mwenye afya ya macho anaweza kuona takriban nyota 6000 - 7000. Leo hii kuna zaidi za nyota 945,592,683 zilizoorodheshwa katika orodha za kimataifa.

Katika karne ya 17 darubini za kwanza zilibuniwa Ulaya. Hivyo utazamaji wa nyota uliboreshwa na magimba ya angani mengi yalianza kuonekana. Galileo Galilei aliweza kuona miezi ya Mshtarii mwaka 1609 iliyokuwa haijajulikana hadi siku ile.

Katika karne ya 19 kifaa cha kamera kilileta tena upanuzi wa elimu; upigaji picha uliwezesha uchunguzi wa picha za nyota wakati wowote. Kamera iliwezesha pia kuona nyota zisizoonekana kwa macho tu. Kuingiza mwanga kwenye kamera kwa masaa kunakusanya nuru hafifu na hivyo kuonyesha lakhi za nyota zisizoonekana kwa macho. Sehemu kubwa ya kazi ya wataalamu wa anga ilihama kutoka kwenye darubini kwenda deski ya mtafiti, siku hizi mbele ya kompyuta yenye data.

Mitambo mipya

Maendeleo ya tekinolojia yalileta mitambo mipya inayowezesha kupima mawimbi yasiyoonekana kwa macho kama vile

Magimba ya anga yanatoa kila aina ya mnururisho kwenye spektra.

Vipimo hivi vilipanusha tena elimu tuliyo nayo kuhusu muundo wa ulimwengu. Mnururisho wa mandharinyuma (ing. cosmic background radiation) ulitambuliwa uliothibitisha nadharia kuhusu umri wa ulimwengu tangu mlipuko mkuu.

Kuangalia nyota kwenye anga-nje

Tangu mwanzo wa usafiri wa anga-nje wataalamu wa anga walipata nafasi ya kuangalia na kupima nyota nje ya athira ya angahewa ya Dunia (inayopunguza kiasi cha nuru inayoonekana) na nje ya ugasumaku wake.

Tangu miaka ya 1970 satelaiti mbalimbali zilirishwa zinazobeba darubini za anga-nje. Utafiti wa nyota umepanuka hadi kupima miale ya eksirei na ya gamma inayozuiliwa na ugasumaku na angahewa. Maendeleo yamekuwa makubwa isipokuwa gharama zimekuwa pia kubwa za kuunda vifaa, kuvipeleka kwenye anga-nje halafu kuvitunza , hadi gharama za kupeleka watu huko juu kwa matengenezo. Kati ya darubini za anga-nje zilizokuwa mdhhuri sana ni Darubini ya Hubble.

Pamoja na uwezo wa kompyuta wa kushughulikia idadi kubwa za data darubini za anga-nje zmeleta vipimo na data za nyota mamilioni.(itaendelea)

Marejeo


Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Elimuanga kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.