Mlipuko mkuu

Mlipuko mkuu (au mlipuko asilia; kwa Kiingereza Big Bang) ni nadharia ya kisayansi kuhusu chanzo cha ulimwengu inayojaribu kueleza sababu ya kutokea kwa nyota, majarra na anga kwa jumla jinsi tunavyoviona leo.
Kutokea kwa ulimwengu
[hariri | hariri chanzo]Kufuatana na nadharia hiyo ulimwengu ulitokana na chanzo kidogo sana chenye joto na densiti kubwa, pasipo na nyota wala atomi wala umbo lolote. Hali hiyo inaelezwa ilikuwa ya pekee.
Takriban miaka bilioni 13.8 iliyopita [1] anga-nje lilianza kupanuka haraka na katika mchakato huo atomi ziliundika zilizoendelea kujenga mata tunavyoijua na kuwa nyota na majarra.
Ulimwengu unaendelea bado kupanuka na wakati huohuo kupoa. Nafasi ya ulimwengu inapanuka na katika mwendo huu halijoto inapungua.
Jina
[hariri | hariri chanzo]Jina la "Big Bang" lilibuniwa na mwanafizikia Fred Hoyle aliyepinga nadharia hiyo, lakini wengine walioitetea walipenda jina, hivyo likabaki. [2]
Athari ya Doppler na mlipuko mkuu
[hariri | hariri chanzo]Sababu za kubuni nadharia ya mlipuko mkuu ni kutafuta maelezo kwa vipimo vinavyopatikana kuhusu anga la ulimwengu.
Sababu muhimu zaidi ni mabadiliko ya nuru ya galaksi ambazo zinaonekana kuwa mbali sana. Nuru hiyo inasogea kwa upande wa nyekundu zaidi katika spektra yake. Huo msogeo wekundu (ing. redshift) wa nuru ya nyota za mbali huelezwa kwa athari ya Doppler. Maana yake ni kwamba, kama kitu kinakwenda mbali nasi, rangi yake huelekea kuwa nyekundu zaidi kwa sababu mwendo wake hupanua masafa ya mawimbi ya nuru. Nyekundu ina urefu mkubwa zaidi kati ya mawimbi ya nuru ya rangi zinazoonekana. Kadiri jinsi mwelekeo mwekundu unavyoongezeka vile, kitu kina mwendo wa kasi zaidi kuelekea mbali nasi.
Dalili nyingine ni mnururisho wa mandharinyuma (ing. cosmic background radiation) uliowahi kutabiriwa kinadharia na wanafizikia tangu miaka ya 1930. Uligunduliwa na kuthibitishwa kwa njia ya vipimo tangu mwaka 1964. Huo ni mnururisho dhaifu sana usio na asili katika nyota au galaksi yoyote; leo hii wanasayansi wengi wanaiona kama mabaki ya nishati ya mlipuko mkuu inayoendelea kujaza ulimwengu.
Kutokana na vipimo hivyo wanasayansi wengi kabisa wa fizikia na astronomia wanaona ya kuwa nadharia ya mlipuko asilia inaeleza vizuri zaidi vipimo vinavyopatikana kuhusu ulimwengu. [3]
Nadharia hiyo inaonekana kupatana na makadirio kuhusu viwango vya elementi vya kikemia vinavyogunduliwa katika anga la ulimwengu.
Awali kulikuwa na tofauti ya mawazo kama mlipuko mkuu ulikuwa chanzo kabisa cha ulimwengu au kama uliwengu mwingine ulikuwepo kabla yake, na labda mwendo wa kupanuka unaweza kurudishwa katika mwendo wa kukaza siku moja hadi mata yote kuwa mahali pamoja na kulipuka tena. [3]
Falsafa na dini
[hariri | hariri chanzo]Nadharia hiyo ina umuhimu pia kwa falsafa na dini, ambazo pia zinaeleza chanzo cha ulimwengu, k.mf. kwa kusema umeumbwa na Mungu.
Kuna wafuasi wa dini mbalimbali wanaopinga nadharia hiyo wakiona hailingani na imani yao.
Kinyume chake wako wengine wanaosema kuwa nadharia ya mlipuko mkuu inalingana vema na hoja ya uumbaji unaoendelea hata sasa kupitia sheria za maumbile zinazozidi kugunduliwa na sayansi.
Mwanzilishi mwenyewe wa nadharia hiyo alikuwa Georges Lemaitre (1894-1966), padre wa Kanisa Katoliki kutoka Ubelgiji. Ndiye aliyependekeza nadharia hiyo mwaka 1927, akifuatwa na wengine wengi zaidi na zaidi baada ya kupingwa sana kwa miaka mingi.
Kwa mtazamo wa padri huyo na Wakristo wengine kadhaa ni kwamba si lazima kusadiki masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji yanaeleza matukio kihistoria au kisayansi, bali yanadai msomaji akubali kuwa asili ya vitu vyote vilivyopo ni Muumba.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- 1 2 NASA. "Universe 101:Big Bang theory". Iliwekwa mnamo 2010-01-28.
{{cite web}}: Cite has empty unknown parameter:|coauthors=(help) - ↑ Sullivan, Walter (Agosti 22, 2001). "Fred Hoyle dies at 86; opposed 'Big Bang' but named it". New York Times. Iliwekwa mnamo 2010-01-28.
{{cite web}}: Cite has empty unknown parameter:|coauthors=(help)CS1 maint: date auto-translated (link) - 1 2 Chris LaRocco and Blair Rothstein. "The Big Bang: it sure was BIG!". Iliwekwa mnamo 2010-01-28.
{{cite web}}: Cite has empty unknown parameter:|coauthors=(help)
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- Singh, Simon (2005). Big Bang: the most important scientific discovery of all time and why you need to know about it. Harper Perennial. ISBN 9780007152520.
| Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mlipuko mkuu kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |