Athari ya Doppler

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Mawimbi yanayotoka na kiolwa chenye mwendo huonyesha athari ya Doppler
Badiliko la urefu wa mawimbi ya sauti kwa mfano wa gari linalopita

Athari ya Doppler ni badiliko ya marudio na masafa ya mawimbi kutokana na mwendo wa chanzo cha mawimbi au mwendo wa mtazamaji.

Inatokana na badiliko la kasi ya chanzo cha wimbi na mpokeaji wa wimbi, yaani mtazamaji wa wimbi, au kifaa cha kupimia mawimbi.

Inasababishwa na mabadiliko ya umbali kati ya chanzo cha wimbi na mpokeaji wa wimbi, yaani mtazamaji au kifaa cha kupimia mawimbi.

Jina latokana na mwanafizikia Mwaustria Christian Doppler aliyetambua mara ya kwanza ya kwamba mapimo ya marudio ya wimbi hutegemea kasi husianifu wa chanzo chake na mtazamaji. Alitaka kueleza kwa njia hiyo tofauti ya rangi kati ya sehemu mbili za nyota maradufu.

Mawimbi ya sauti[hariri | hariri chanzo]

Mfano wa kimsingi ni sauti ya gari linalopita. Mtazamaji atasikia sauti ya gari itakuwa tofauti wakati gari linamkaribia na pia atasikia sauti nyigine wakati imekwishampita na kwenda mbali naye. Wakati gari linakaribia kiimbo kinapanda na kusikika kuwa juu lakini wakati imepita na kuondoka kwenda mbali kiimbo kinashuka. Lakini ndani ya gari sauti inasikika ni ileile.

Kwa mtazamo wa fizikia sababu yake ni ya kwamba masafa ya mawimbi huwa mafupi wakati wa kukaribia na kuwa marefu wakati wa kwenda mbali.

Mawimbi ya nuru[hariri | hariri chanzo]

Kwenye nuru athari ya Doppler husababisha mabadiliko ya rangi kuelekea upande wa buluu kwenye spektra (huitwa msogeo buluu). Chanzo cha nuru kikikaribia msogeo buluu huwa kubwa zaidi. Kinyume chake kama chanzo cha nuru kinakuwa mbali tunaona msogeo mwekundu katika spektra yake na kisogezo hiki ni kikubwa kutegemeana na kasi yake.

Athari ya Doppler na giza la usiku[hariri | hariri chanzo]

Athari ya Doppler inaeleza giza la usiku. Tukitazama anga wakati wa usiku tungepaswa kuona mwanga maana kuna nyota nyingi mno. Kwa macho tunaona takriban nyota 6000 lakini kwa darubuni kubwa idadi ya nyota ni mabilioni kwa hiyo kila sehemu tunapotazama kuna nyota kadhaa ila tu hatuoni nuru yao. Sababu yake ni upanuzi wa ulimwengu tangu mlipuko mkuu. Nafasi yote ya anga-nje inazidi kupanuka. Kwa hiyo sehemu zote ziko katika mwendo wa kuwa mbali zaidi kati yao. Mwendo huu unaleta athari ya Doppler, yaani nuru kutoka vyanzo vya kwenda mbali inapata kisogezo chekundu; mnururisho katika anga unaelekea kuwa na mawimbi marefu zaidi. Nishati ya mawimbi imeshapoa. Sehemu kubwa sana ya nuru yote iliyowahi kutokea tangu chanzo cha ulimwengu haiko tena katika masafa ya nuru inayoonekana kwa hiyo haiwezi kuchangia kwenye mwangaza wa anga la usiku.