Mtu wa kwanza alitoka wapi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Sura ya Homo sapiens wa zamani (kushoto) na ya Homo neanderthalensis (kulia) zinavyoonyeshwa huko Neanderthal Museum.

Mtu wa kwanza alitoka wapi ni swali ambalo wengi wanajiuliza. Kwa namna ya pekee wanafunzi wa shule ambao wanafundishwa katika historia kuwa mtu wa kwanza alitokana na kiumbehai mwenye asili moja na sokwe. Kumbe katika dini zao wanafundishwa kwamba mtu aliumbwa na Mungu. Hivyo wanajiuliza, lipi sahihi kuhusu hilo?

Wapo wengi wanaodhani kwamba ni lazima kuchagua moja katika ya hayo mawili: ama kwamba mtu ametokana na kiumbehai aliyetangulia ama kwamba Mungu alimuumba mtu wa kwanza kama tulivyo sisi leo.

Kwa namna hiyo wapo wanasayansi wanaopinga imani na wapo wahubiri wa dini wanaopinga sayansi.

Kumbe si lazima kuona upinzani kati ya imani na sayansi kwa sababu kila moja inakabili masuala yake kwa namna yake. Yaani sayansi inachunguza ulimwengu na vyote vilivyomo kwa vipimo na utafiti wa kitaalamu, wakati imani inapokea ufunuo wa Mungu.

Sayansi imechunguza viumbehai waliopo duniani sasa na mabaki ya wale waliokuwepo zamani. Hasa baada ya kugundua DNA imeweza kuona uhusiano kati ya hao viumbehai mbalimbali. Hivyo imethibitisha kwamba mwili wa binadamu na ule wa sokwe imetokana na kiumbehai wa zamani (miaka milioni 5 au zaidi iliyopita) katika mlolongo wa mageuko ya spishi.

Lakini sayansi haiwezi kusema kitu juu ya roho, kwa sababu si mata, hivyo haipimiki. Zaidi sana haiwezi kusema lolote juu ya Mungu na kazi yake, kwa sababu si wa ulimwengu huu.

Upande mwingine, wanaomuamini kama muumba wa vitu vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana, si lazima wasadiki kwamba aliviumba vyote kama vilivyo sasa. La sivyo wangeshindwa kueleza kwa nini watu wa leo wametofuatiana hivi, wakati wanaaminika wote kuwa watoto wa Adamu na Eva. Mabadiliko yalitokea kadiri ya maisha na mazingira, na bado yanazidi kutokea: kwa mfano leo watoto wanakuwa warefu zaidi.

Jambo la msingi kwa imani ni kwamba vyote asili yake ni Mungu tu aliyeviumba kwa hiari yake. Hata leo anazidi kuumba watu na viumbe vingine, lakini anatumia wazazi wao, hawaumbi moja kwa moja. Kwamba Mungu anatumia wazazi kuumba watoto, maana yake si kwamba ameacha kuwa muumba, kwa sababu ndiye aliyeumba wazazi na ndiye anayewawezesha kuzaa anavyotaka.

Ni vilevile kuhusu mtu wa kwanza: hata kama Mungu alitumia kiumbehai aliyetangulia katika kumuumba Adamu anabaki muumba wake kwa sababu hata kiumbe huyo alikuwa kazi yake kama ulimwengu wote ulivyo kadiri ya imani.