Nenda kwa yaliyomo

Shule

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Shule ya msingi ya Holy Child, Himo, Makuyuni (Monduli) - Tanzania.
Shule ya msingi vijijini nchini Zambia.

Shule (kutoka Kijerumani: Schule; nchini Tanzania na Kenya, huko Zanzibar huitwa skuli kutoka Kiingereza "school") ni taasisi inayoongozwa na mfumo maalumu ambayo watu hufunzwa habari za elimu. Pia ni jina la majengo yake.

Leo hii katika nchi nyingi watoto na vijana wanatakiwa waende shule kujifunza mambo ya msingi ambayo watayahitaji kwa maisha yao ya baadaye.

Mambo hayo ni masomo. Kila somo lina fahamu zake tofauti katika kufundisha. Kwa mfano: kuandika, kusoma, na kuhesabu namba (hisabati).

Shule ni mahali ambapo watu hujifunza mambo mengi ambayo huwasaidia katika kuyakabili maisha hata kupata elimu juu ya jambo fulani. Elimu hiyo ndiyo itakayomsaidia kutatua jambo hilo.

Watu wengi husema kwamba elimu haina mwisho, wakimaanisha kuwa elimu inaweza kutolewa kwa watu wote bila kujali kama ni watoto, vijana, watu wazima hata wazee.

Pia unaweza ukasema kwamba elimu ni ufunguo wa maisha ukimaanisha kuwa elimu ndiyo kila kitu kwenye maisha ya mwanadamu kwa kuwa huwezi kutatua tatizo fulani bila kupata elimu juu ya tatizo hilo.

Watu wanaopatikana shuleni ni wa aina tatu: wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wanaotunza majengo na vifaa.

Katika nchi nyingi masomo ya shule hupangwa kwa ngazi kufuatana na umri wa wanafunzi:

  1. Shule ya chekechea au vidudu au watoto wadogo chini ya umri wa miaka 6
  2. Shule ya msingi kuanzia umri wa miaka 6 kwa muda usiopungua 4 hadi 8
  3. Shule ya sekondari (huitwa pia "Shule ya upili") inayofuata baada ya shule ya msingi inawafunza wanafunzi hadi umri wa miaka 17, 18 au zaidi. Kwenye ngazi ya sekondari kuna mikondo mbalimbali inayoweka uzito kwa maeneo tofautitofauti ya elimu kadiri ya vipaji na uwezo wa wanafunzi.

Ngazi ya juu inayopatikana katika mfumo huu ni mtihani unaoandaa kwa kuingia katika ngazi ya juu ya elimu kwenye vyuo na Chuo Kikuu.

Kwa kawaida, mbali ya shule zinazoendeshwa na serikali, zipo nyingi zinazoendeshwa na dini na taasisi za binafsi.

Pamoja na hayo kuna shule zinazowalenga watu wazima au watu ambao hawakuendelea moja kwa moja katika elimu yao.

Nchi kadhaa huweka mkazo kwa shule ya ufundi inayolenga kuwapa wanafunzi wake elimu nzuri katika fani fulani ya biashara au ufundi.

Upatikanaji wa shule ni sehemu muhimu ya miundombinu wa kila nchi.

Makala hii kuhusu mambo ya elimu bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shule kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.