Astronomia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Aina mbalimbali za darubini ni vyombo muhimu vya astronomia.

Astronomia (kutoka maneno ya Kigiriki ἄστρον astron "nyota" na νόμος nomos "sheria")[1] ni elimu juu ya magimba ya ulimwengu kama vile nyota, sayari, miezi, vimondo, nyotamkia, galaksi kuhusu nyendo zao, nafasi, umbali, ukubwa na sheria zinazotawala tabia zake.

Astronomia ni tofauti na unajimu ambayo si sayansi bali jaribio la kuona uhusiano kati ya nyota na tabia za wanadamu na pia kutabiri mambo yajayo. Hata hivyo vyanzo vya fani zote mbili zilikuwa karibu sana katika historia ya binadamu hadi kutokea kwa astronomia ya kisayansi.

Chanzo na historia ya astronomia

Elimu ya nyota nyakati za kale

Tangu zamani watu waliangalia nyota wakajifunza kuzitofautisha. Mabaharia na wasafiri wakati wa usiku waliweza kutumia nyota kama vielekezi safarini. Walitazama pia mabadiliko ya kurudia kati ya nyota zinazoonekana angani wakati wa usiku. Wakaona mabadiliko haya ya jinsi nyota zinavyoonekana yaweza kuwa uhusiano na nyakati za mvua, baridi na joto, mavuno na ustawi wa mimea katika mwendo wa mwaka. Kutazama nyota vile kulikuwa msaada wa kupanga vipindi vya mwaka na kuunda kalenda.

Watazamaji wa nyota walianza kutambua pia tofauti kati ya nyota mbalimbali, kwa mfano nyota zenye mahali palepale kila wakati na nyota chache za pekee zilizobadilisha mahali angani kwa utaratibu wa kurudia na hizi ziliitwa sayari, tena nyota nyingine zilizoonekana kwa muda tu zikibadilisha mahali pake angani zikaitwa vimondo.

Kwa karne nyingi wataalamu katika sehemu mbalimbali za dunia walihisi ya kwamba nyota hizo zilikuwa miungu iliyoonekana kwa mbali sana. Katika vitabu vya dini vya kale kuna majadiliano juu ya tabia zao; wakati mitholojia ya mataifa mengi iliona nyota kuwa miungu, Biblia ilifundisha ni taa zilizowekwa angani na Mungu pekee aliye mwumbaji wa ulimwengu.

Wataalamu wa kale katika nchi kama Uhindi au Ugiriki ya Kale walianza kutambua mwendo wa sayari na kuunda nadharia yuu ya uhusiano wa dunia, jua na sayari nyingine. Ndiyo chanzo cha imani ya kwamba nyota zinaweza kuwa na tabia fulani na athari juu ya maisha duniani na hasa kama mtu alizaliwa wakati nyota fulani ilionekana, basi tabia zilizoaminiwa kuwa za nyota ziliweza pia kuathiri maisha ya mtu huyo. Hapa kuna asili ya "kupiga falaki" na unajimu wa kisasa. Wakati uleule wataalamu hao walitazama nyota jinsi zilivyo, kuziorodhesha na kupiga hesabu za kalenda. Orodha ya kale iliyoendelea kutumiwa kwa zaidi ya miaka 1,000 ilikuwa ya Klaudio Ptolemaio kutoka Misri.

Kupanuka kwa elimu tangu kupatikana kwa darubini

Kwa macho matupu mtu mwenye afya ya macho anaweza kuona takriban nyota 6000 - 7000. Leo hii kuna zaidi za nyota 945,592,683 zilizoorodheshwa katika orodha za kimataifa.

Katika karne ya 17 darubini za kwanza zilibuniwa Ulaya. Hivyo utazamaji wa nyota uliboreshwa na magimba ya angani mengi yalianza kuonekana. Galileo Galilei aliweza kuona miezi ya Mshtarii mwaka 1609 iliyokuwa haijajulikana hadi siku ile.

Siku hizi wataalamu wameelewa tabia za nyota nyingi kuwa magimba kama jua letu wakati sayari kuwa magimba kama dunia yetu yanayozunguka jua letu katika mfumo wa jua. Wameelewa pia ya kwamba kuna mabilioni ya nyota zinazojumuika pamoja katika makundi makubwa yanayoitwa galaksi.

Vyombo vya utazamaji vilivyopatikana katika karne ya 20 vilionyesha magimba yasiyoonekana kwa macho kwa sababu hayana nuru ya kawaida bali yanafikisha kwetu mnururisho wa mawimbi ya redio tu.

(itaendelea)

Marejeo

  1. Awali makala iliitwa "Falaki"(kutoka Kiarabuعلم الفلك 'ilm al-falak "elimu ya mizingo ya magimba ya angani") lakini kwa kufuata ushauri wa Dr Noorali T Jiwaji, Open University of Tanzania, ilionekana ya kwamba wataalamu wa fani hii katika Tanzania walipatana kutumia neno "Astronomia".

Viungo vya nje

Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Astronomia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.