Galileo Galilei

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Uchoraji wa Galileo Galilei

Galileo Galilei (5 Februari 15648 Januari 1642) alikuwa mtaalamu wa fizikia, hisabati na astronomia kutoka nchini Italia.

Anakumbukwa kwa sababu aliweka misingi kwa mbinu mpya za sayansi zinazoendelea kutumiwa hadi leo. Akiwa mtaalamu wa kwanza aliyetumia darubini kwa kutazama nyota na sayari alipanusha ujuzi wa binadamu juu ya ulimwengu.

Ujana wake[hariri | hariri chanzo]

Baba yake alikuwa mfanyabiashara aliyejishughulisha pia na maswali ya hisabati.

Galileo alisomeshwa kwenye shule ya monasteri akaendelea kusoma tiba mjini Firenze lakini akaacha masomo hayo akachukua hisabati badala yake.

Kanuni za anguko[hariri | hariri chanzo]

Miaka 1589 - 1592 alipata nafasi ya profesa ya hisabati kwenye chuo kikuu cha Pisa. Hapa alifanya utafiti juu ya kanuni za anguko la magimba. Aliweza kuonyesha kwamba magimba yote huanguka kwa mkasi uleule yakianguka pasipo hewa kama ni makubwa au madogo. Kwa tamko hili alionekana kumpinga Aristoteles aliyepokewa na wataalamu na kanisa kama msingi wa utaalamu wote.

Astronomia na darubini[hariri | hariri chanzo]

Akahamia chuo kikuu cha Padua alipofanya kazi kati ya 1592 na 1610. Alisikia kuhusu chombo kipya cha darubini (kionambali) kilichobuniwa na Mholanzi Hans Lipperhey akaiiga na kujenga yake. Alikuwa mtu wa kwanza aliyetumia chombo hicho kwa kutazama mwezi, sayari na nyota. Aliona milima kwenye mwezi akawa mtu wa kwanza aliyeona miezi ya sayari Mshtarii. Vilevile aliweza kuangalia sayari Ng'andu (Zuhura/Venus) jinsi ilivyoonyesha awamu sawa na mwezi zilizoonekana kama mwezi mwandamu, nusu mwezi au mwezi mpevu. Aliona pia madoa ya jua.

Mwaka 1610 mtawala wa Toskana, Cosimo II kutoka nasaba ya Medici, aliyewahi kuwa mwanafunzi wake, alimkaribisha kuwa mwanahisabati mkuu na pia profesa huko Pisa.

Alipendwa na watu wengi, pia na kardinali Maffeo Barberini aliyeendelea baada ya kuwa Papa Urban VIII.

Kesi ya Kanisa dhidi yake[hariri | hariri chanzo]

Sanamu ya Galileo Galilei kwenye kaburi lake ndani ya Kanisa la Msalaba Mtakatifu mjini Firenze, Italia

Matokeo ya utafiti wa Galilei yalipinga hoja la awali lililofundishwa na wataalamu wa Ugiriki ya Kale na kukubaliwa katika Kanisa Katoliki. Kwa Galilei ilikuwa wazi ya kwamba dunia yetu si kitovu cha ulimwengu tena aliamini lilikuwa jua badala yake na kwamba Nikolaus Kopernikus pamoja na Johannes Kepler‎ waliwahi kusema ukweli. Hivyo Galilei alishtakiwa kuwa mafundisho yake yalipinga Biblia na imani.

Katika kesi alionywa asiseme maoni yake mapya ni ukweli badala yake alitakiwa kusema ni uwezekano tu. Sehemu ya vitabu vyake vilipigwa marufuku na mwenyewe aliambiwa kukaa ndani ya nyumba yake.

Mwaka 1992 Papa Yohane Paulo II alisema kuhusu kesi dhidi ya Galilei: « Kama wapinzani wake walio wengi, Galileo hakutofautisha mtazamo wa sayansi kuhusu mambo ya kimaumbile na fikra za kifalsafa juu ya maumbile ambazo kwa kawaida zinadaiwa nao. Ndiyo sababu alikataa pendekezo alilopewa la kuita 'dhana' mafundisho ya Kopernicus, hadi yathibitishwe moja kwa moja, ingawa hilo lilikuwa sharti la mbinu ya majaribio aliyoibuni mwenyewe kwa akili kubwa. [...] Kumbe, suala walilojiuliza wanateolojia wa wakati huo lilikuwa lile la ulinganifu wa mafundisho ya jua kuwa kiini cha ulimwengu na Maandiko Matakatifu. Hivyo sayansi mpya, kwa mbinu zake na uhuru wa ukufanya utafiti unaodaiwa nazo, ililazimisha wanateolojia kujiuliza juu ya vigezo vyao vya kufafanulia Maandiko. Wengi wao wakashindwa kufanya hivyo. Ajabu, Galileo, mwamini mnyofu, alijitokeza anaelewa kuliko wanateolojia waliompinga kuhusu jambo hilo. » (Yohane Paulo II kwa wanasayansi wa Akademia ya Kipapa ya Sayansi, 31 Oktoba 1992)

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Jua habari zaidi kuhusu Galileo Galilei kwa kutafuta kupitia mradi wa Wikipedia Sister
Wiktionary-logo.svg Uchambuzi wa kamusi kutoka Wikamusi
Wikibooks-logo.svg Vitabu kutoka Wikitabu
Wikiquote-logo.svg Dondoo kutoka Wikidondoa
Wikisource-logo.svg Matini za vyanzo kutoka Wikichanzo
Commons-logo.svg Picha na media kutoka Commons
Wikinews-logo.svg Habari kutoka Wikihabari
Wikiversity-logo-en.svg Vyanzo vya elimu kutoka Wikichuo

Maandiko ya Galileo[hariri | hariri chanzo]

Kuhusu Galileo[hariri | hariri chanzo]

Maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Galileo na Kanisa[hariri | hariri chanzo]


Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu: