Kimondo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Vimondo vinavyong'aa angani; picha imechukuliwa kwa muda wa dakika kadhaa na kuonyesha vimondo vilivyoonekana katika kipindi hicho. Nyota hazionekani tena kama nukta, bali kama mistari mifupi kutokana na mwendo wa dunia na anga katika muda wa kupigwa kwa picha.

Vimondo (pia: meteori au meteoridi) ni violwa vidogo vya angani vinavyozunguka jua. Vinaweza kuangukia duniani vikionekana kama moto angani.

Ukubwa

Ukubwa wa kimondo ni kuanzia punje ya mchanga hadi kufikia kipenyo cha mita kadhaa. Hivyo kimondo ni kidogo kuliko asteoridi na kikubwa kushinda vumbi la angani.

Kimondo hiki cha chuma kilipatikana China.

Kugonga angahewa ya dunia

Obiti ya kimondo unaweza kuingiliana na obiti ya dunia au sayari nyingine. Kimondo kikilikaribia kiolwa cha angani kikubwa zaidi kinavutwa nalo.

Kikikaribia mno dunia yetu kinaingia katika angahewa na kuanguka chini kwa kasi kubwa sana. Njiani kinapashwa moto kutokana na msuguano wa hewa dhidi yake. Kiasi cha joto kinatosha kuchoma kabisa kimondo kidogo hewani. Hii inaonekana kwa macho matupu kama mstari wa moto angani unaowaka kwa sekunde 1-2. Kama kimondo ni kikubwa zaidi ni sehemu zake za nje tu zinazochomwa na kiini kinagonga uso wa dunia.

Kati ya vimondo kumi vikubwa kabisa duniani ambavyo mabaki yake yanaonekana, kimojawapo ni Kimondo cha Mbozi nchini Tanzania.

Hatari za vimondo ?

Vimondo ni hatari kwa vyombo vya angani kwa sababu ya kasi yake kubwa. Hata punje ndogo yaweza kusababisha uharibifu mwingi.

Duniani kuna pia hatari fulani lakini si kubwa hali halisi. Katika miaka yote ya karne ya 20 kuna taarifa 21 pekee za nyumba kugongwa na kimondo.

Katika karne ya 20 kuna taarifa zifuatazo kuhusu watu walioathiriwa na vimondo:

Kasoko huko Arizona (Marekani) kutokana na mgongano wa kimondo

Mgongano na vimondo vikubwa

Mbali na hayo, kuna hatari moja kubwa kwa uhai wote duniani. Wataalamu huamini ya kwamba kila baada ya miaka elfu kadhaa hadi laki kadhaa kimondo kikubwa au zaidi asteroidi inaweza kugonga dunia. Nishati ya mgongano wa aina hii inaweza kuwa kubwa sana na kuleta uharibifu mwingi.

Tokeo la Tunguska tarehe 30 Juni 1908 katika pori la Siberia liliangusha miti milioni 60 kwenye eneo la kilomita za mraba 2000. Wataalamu walio wengi huamini ya kwamba lilisababishwa na kimondo. Kama lingetokea juu ya mji wa kisasa kungekuwa na vifo vingi sana.

Kuna pia kasoko kadhaa zilizosababishwa na vimondo. Vimondo vikubwa sana vilivyoweza kusababisha kasoko kubwa vinatokea kila baada ya miaka milioni kadhaa. Lakini vina hatari ya kuua kiasi kikubwa cha viumbe vyote katika nchi au hata katika dunia nzima.

Viungo vya Nje

Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kimondo kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.