Kundinyota

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Nyota za Orion angani
Baada kuunganisha nyota za Orion kwa kuwaza mistari kunajitokeza picha ya mvindaji
Orion kama mvindaji alivyowazwa huko Ulaya

Kundinyota (ing. star constellation) ni idadi ya nyota zinazoonekana angani kuwa kama kundi la pamoja.

Tangu zamani watu walitazama nyota kama nukta na kuwaza kuwa na mistari kati yao hivyo kuona picha. Kundinyota zinazojulikana sana ni kama vile Orion, Skorpio (nge), Andromeda, Msalaba wa Kusini.

Kujumlisha nyota hivi ilikuwa msaada kwa watu kukumbuka na kutambua nyota.

Hali halisi nyota hizi zinaonekana tu kama kundi lakini haziko mahali pamoja angani kwa sababu zinaweza kuwa mbali sana kutoka nyota nyingine inayoonekana kama sehemu ya kundinyota ileile.

Hivyo kundinyota ni tofauti na fungunyota (Kiing. star cluster) ambayo ni idadi kubwa ya nyota zilizopo karibu pamoja hali halisi. Ila tu kwa jicho tupu fungunyota inaonekana kama nyota moja tu au haionekani kutokana na umbali, zimetambuliwa kwa hadubini tu. Kilimia ni fungunyota ya pekee inayoweza kutambuliwa bila msaada wa mitambo na hivyo ni maarufu kama kundinyota pia.

Mfano wa Orion[hariri | hariri chanzo]

Picha za Orion katika makala hii zinaonyesha njia kutoka nyota angani hadi wazo la kundinyota. 1. Orion inaonekana vizuri kwa sababu kuna kwanza nyota tatu kama mstari. Juu yake upande wa kushoto kidogo ni nyota mbili zinazong'aa sana. Chini ya mstari wa nyota tatu kuna nyota mbili au tatu (inategemea ubora wa macho) za karibu sana. Halafu chini yake kuna tena nyota mbili za mbali kidogo zinazong'aa na kufanana zile mbili za juu. Kama giza inaongezeka ni tena nyota zaidi zinazoonekana.

2. Watu waliunganisha nyota kwa kuwaza mistari wakaanza kumwona mtu. Nyota tatu za katikati(δ, ε, ζ) ziliitwa ukanda, nyota mbili za kung'aa za juu (α, λ) zikawa mabega ya mtu na nyota mbili za chini (β,κ) miguu yake. Nyota mbili au tatu chini ya "ukanda" (ι, θ) zikatajwa kama silaha inayoaliki kwenye ukanda. Nyota nyingine hafifu zaidi zikaunganishwa katika picha hii: nyota za "π" 1,2,3 zikawa ama ngao au kando la nguo; λ kama kichwa.

3. Wasanii walichora picha kama ile ya juu upande wa kushoto (nyota kadhaa zilitiwa rangi katika makala hii kwa kuonekana vizuri zaidi si picha yenyewe). Hivyo katika mawazo ya watu wa kale katika tamaduni mbalimbali anga lilijaa mapepo au hasa miungu.

Kundinyota katika astronomia[hariri | hariri chanzo]

Kitaalamu kundinyota 88 zinakubaliwa kama msaada wa kutaja nyota. Sayansi ya astronomia inatumia kundinyota kama mbinu wa kupata ramani ya nyota jinsi zinavyoonekana angani. Majina ya nyota zinazoonekana hutajwa kufuatana na eneo la kundinyota zinapoonekana halafu kwa kuongeza herufi za kigiriki.

Mfano mashuhuri ni nyota iliyo karibu na jua letu katika anga la ulimwengu hutajwa kama "Alpha Centauri" maana ni nyota iliyohesabiwa kama nyota ya kwanza katika eneo la kundinyota Centaurus.

Wanaastronomia wanatumia zaidi mfumo wa digrii zinazolingana na utaratibu wa latitudo na longitudo hapa duniani wakitaka kutaja mahali kamili pa nyota. Lakini hadi leo kindinyota ni msaada wa kujua eti nyota fulani au nyotamkia inapatikana katika eneo gani. Hii ni sawa na kusema "mji fulani uko kaskazini-magharibi ya Afrika" kabla ya kutaja kikamilifu mahali pake kwa longitudo na latitudo.

Kundinyota na utabiri katika unajimu[hariri | hariri chanzo]

Kundinyota zimekuwa muhimu kwa ajili ya unajimu. Ni hasa kundinyota 12 za Zodiaki zinazodaiwa kuwa muhimu na kutawala tabia za watu kwenye horoskopi. Waswahili wa kale walirithi kundinyota hizi kutoka elimu ya Waarabu na kuziita buruji za falaki[1]Hata kama astronomia imeshatambua ya kwamba kundinyota hazipo hali halisi ni wazo tu tukitazama kutoka kwetu duniani; hali halisi hazipatikani angani bado unajimu inatangaza tofauti.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. J Knappert, fungu "In East Africa", makala AL-NUDJUM katika THE ENCYCLOPAEDIA OF ISLAM, LEIDEN BRILL 1997, VOLUME VIII NED — SAM, uk 105