Kilimia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Picha ya Kilimia angani wakati nyotamkia inapita mwaka 2005

Kilimia (pia: thuria kutokana na Kar. "ثریا"; ing. - gir. Pleiades) ni fungunyota katika kundi la nyota la Thauri (ing. Taurus). Jina la kisayansi ni "M45" (katika orodha ya Messier).

Tabia za kiastronomia[hariri | hariri chanzo]

Kwa macho nyota sita hadi saba zaonekana vizuri sana na hadi 14 kwa jumla. Lakini kwa darubini kilimia ni fungunyota yenye nyota 1,200. Umbali wake na jua letu ni miaka ya nuru 410. Umri wake hukadiriwa kuwa miaka milioni 125.

Ishara ya mvua[hariri | hariri chanzo]

Fungunyota hii inaonekana vizuri kabisa kwa macho. Inaanza kuonekana angani masaa ya mwanzo wa usiku katika miezi kuanzia Oktoba. Hivyo kuonekana kwake imechukuliwa na wazee katika Afrika Mashariki kama kalenda ya kuandaa mashamba na kilimo kwa sababu mvua umekaribia. Hii ni sababu ya kupewa jina la "kilimia" kutokana na "kulima, kilimo".

Waswahili walitumia pia jina la kiarabu la "thuria" (ثریا).

Nafasi ya nyota kama ishara za kalenda zinapungua kwa sababu nyakati za kuonekana au kuzama hubadilika polepole baada ya karne kadhaa kutokana na mwendo wa mfumo wa jua letu angani.

Kilimia katika mapokeo ya tamaduni mbalimbali[hariri | hariri chanzo]

Kwa lugha nyingi kilimia huitwa kwa jina kama "nyota saba" kwa sababu ni takriban nyota 6 hadi saba zinazoonekana vizuri kwa macho. Mtu mwenye macho mazuri sana ataona hata 9 hadi 14.

Wazee wa Afrika ya Mashariki walikitazama na kuielewa kama ishara ya hali ya hewa hasa mvua wakatunga methali "Kilimia kikizama kwa jua huzuka kwa mvua, kikizama kwa mvua huzuka kwa jua"[1].

Kilimia ni pamoja na Orioni kati ya makundi ya nyota yanayotajwa mara kadhaa katika Biblia (Ayubu 9:9 na 38:31; Amosi 5:8).

Kuonekana kwao kulikuwa alama ya kalenda katika tamaduni nyingi kama kati ya Wakelti, Wagermanik, Waazteki na wengine.

Wagiriki wa Kale walikiita "Pleiadi" na kusimulia hadithi ya mabinti saba wazuri waliopelekwa angani na mungu Zeus ili kuwalinda dhidi ya tamaa za mvindaji Orion. Miaka 2500 iliyopita ilionekana Ugiriki jioni wakati wa Mei hivyo ilikuwa ishara ya kuanza mavuno. Kuzama wakati ule mwezi wa Novemba kulikuwa ishara ya kulima mashamba kabla ya baridi.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Kamusi ya methali za Kiswahili, Ahmed E. Ndalu, Kitula G. King'eiuk. 116, methali no. 778 & 779, East African Publishers, 1989 (kupitia google books, iliangaliwa Fenruari 2017
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kilimia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Astrowiki.PNG
Mradi wa Astronomia

Makala hii imewahi kukaguliwa na kuboreshwa kwenye warsha ya pamoja ya Jenga Wikipedia ya Kiswahili, Wikimedia Community User Group Tanzania na ASSAT. Imepewa hali ya ulinzi. Tunaomba mapendekezo yote ya usahihisho na nyongeza zipelekwe kwanza kwenye ukurasa wa majadiliano