Mwakanuru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Miaka ya nuru)
Kuna nyota 33 ndani ya miaka 12.5 ya mwanga kutoka Jua

Mwakanuru (kwa Kiingereza: "Light year" [1]) ni kizio cha umbali kinachotumiwa katika fani ya astronomia. Ni kipimo cha umbali ambao mwanga umeusafiri kwa mwaka mmoja wa dunia yaani siku 365.25.[2].

Msingi wa kipimo hiki ni kasi ya nuru. Nuru inatembea takriban kilomita 300,000 kwa sekunde. Idadi kamili ni mita 299,792,458 kwa sekunde moja. Mwezi wa Dunia yetu una umbali na Dunia kama sekunde moja ya nuru au kilomita lakhi tatu na dunia.

Katika mwaka mmoja umbali huo unafika mita 9.461  × 1015.

Kipimo hiki kinahitajika kutaja umbali kati ya nyota za angani. Umbali huu umepimwa kuwa miakanuru mia, elfu au hata milioni kadhaa. Kutokana na ukubwa wa ulimwengu umbali katika anga-nje ni kubwa sana.

Hali halisi hatuoni nyota jinsi zilivyo "sasa" lakini jinsi zilivyokuwa wakati uliopita kutegemeana na umbali wao. Nyota jirani kabisa na jua letu inaitwa Alpha Centauri umbali wake ni 4.2 mwakanuru maana yake nuru yake inahitaji zaidi ya miaka minne hadi imefika kwetu. Kwa maana nyingine tunaiona nyota hii jinsi ilivyoonekana miaka minne iliyopita.

Tukiangalia nyota ambazo ziko mbali sana, nuru yake imesafiri miaka elfu kadhaa. Kwa darubini tunaona nyota ambazo nuru yake imeshapita miaka milioni kadhaa. Inawezekana kwamba nyota kadhaa tunazoona hazipo tena. Hasa tukizingatia nyota kubwa sana zilizo mbali uwezekano ni mkubwa kwamba zimelipuka tayari[3].

Vizio vingine katika astronomia[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wengi wa astronomia hupendelea kutumia kizio cha parsek kinacholingana na miakanuru 3.26; inafafanuliwa kama umbali ambako pande mbili za obiti ya Dunia yetu ya kulizunguka Jua zinaonekana kwa pembe ya sekunde ya tao 1. Kwa umbali ndani ya mfumo wa Jua kuna pia "kizio astronomia" (ing. astronomical unit) ambayo ni sawa na umbali wa wastani kati ya Dunia na Jua.

Angalia pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]