Parsek

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Paralaksi inasababisha nyota (njano) kuonekana mahali tofauti ikipimwa kutoka sehemu mbili tofauti za obiti ya Dunia


Parsek (en:parsec, kifupi cha parallax second, kutoka maneno paralaksi na sekunde) ni kipimo cha umbali kinachotumiwa katika astronomia kwa kutaja umbali kati ya nyota na violwa vingine vya angani. Kifupi chake ni pc.

Umbali wa parsek 1 ni sawa na miakanuru 3.26 au karibu kilomita trilioni 31 au mita 3.0857×1016.

Ufafanuzi wa parsec ni umbali kati ya Jua na gimba la angani linaoonekana kwa pembe la paralaksi la sekunde moja ya tao (en:arcsecond).

Msingi wa kipimo hiki ni hali ya paralaksi inayosababisha ya kwamba nyota inaonekana mahali tofauti kama inaangaliwa kutoka sehemu moja kwenye obiti ya Dunia ikizunguka Jua au kutoka sehemu nyingine kinyume chake. Tofauti hii ilhali umbali wa Jua-Dunia unajulikana inaruhusu kupiga hesabu ya trigonometria na kugundua umbali wa nyota iliyopimwa.

Kwa kutaja umbali mkubwa sana kuna pia vizio vya kiloparsek (kpc), megaparsek (Mpc) na gigaparsek (Gpc).

Wanaastronomia hupendelea kutaja umbali kwa parsek kuliko miakanuru.

Parsek na Kiloparsek

Umbali kati ya nyota jirani hutajwa kwa Parsek. Kama umbali unazidi parsek 1,000 kizio cha Kiloparsek kinatumiwa, kwa mfano kutaja umbali kati ya sehemu tofauti ya galaksi moja au ndani ya kundi la galaksi.

  • Parsek inalingana na takriban miakanuru 3.26
  • Nyota iliyo karibu zaidi na Jua letu ni Proxima Centauri, sehemu ya mfumo wa Alpha Centauri (Rijili Kantori) ina umbali wa parsek 1.30 (miakanuru 4.24)
  • Umbali wa fungunyota la Kilimia ni 130±10 pc (miakanuru 420±32.6)
  • Kitovu cha Njia Nyeupe (galaksi yetu) kina umbali wa kiloparsek 8 (miakanuru 26.000) kutoka Dunia; Njia Nyeupe huwa na kipenyo cha takriban 34 kpc (miakanuru 110.000)
  • Galaksi jirani ya Andromeda iko kwa umbali wa 780 kpc (miakanuru milioni 2.5) kutoka Dunia

Megaparsek na gigaparsek

Umbali wa milioni moja parsek huitwa Megaparsek (Mpc). Umbali kati ya galaksi au kati ya makundi ya galaksi hutajwa kwa megaparsek. Zaidi ya megaparsek 1,000 hutajwa kwa Gigaparsek (Gpc). Gigaparsek 1 inalingana na miakanuru bilioni 3.26

Mifano

  • Galaksi ya Andromeda iko takribani 0.78 Mpc (miakanuru 2.5) kutoka Dunia.
  • Kundi la galaksi lililo karibu (Virgo Cluster) lipo kwa umbali wa 16.5 Mpc (miakanuru 54) kutoka dunia [1]
  • Galaksi ya RXJ1242-11 iliyo na shimo jeusi kubwa kama Njia Nyeupe huwa na umbali wa takriban 200 Mpc (miakanuru milioni 650) kutoka Dunia
  • Upeo wa mwisho wa ulimwengu unaoweza kutazamiwa unakadiriwa kuwa na nusukipenyo cha 14.0 Gpc [2]

Tanbihi

  1. The ACS Virgo Cluster Survey. XIII. SBF Distance Catalog and the Three-dimensional Structure of the Virgo Cluster, tovuti ya Chuo kikuu cha Harvard, iliangaliwa julai 2017
  2. Misconceptions about the Big Bang, tovuti ya Scientific American March 2005, kupitia tovuti ya archive.org, ilitazamiwa Julai 2017