Nenda kwa yaliyomo

Paralaksi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mfano wa paralaksi: kutegemeana na mahali pa mtazamaji kiolwa kinachotazamiwa kitaonekana mbele ya sehemu ya buluu au ya nyekundu ya mandharinyuma yake

Paralaksi (ing. parallax, kutoka gir. παράλλαξις parallaxis "badiliko" ) inaonyesha badiliko la mahali dhahiri pa kiolwa (kitu kinachotazamwa) kwa mtazamaji anayebadilika mahali pake.

Hali halisi kiolwa kipo palepale lakini kutegemeana na mahali pa mtazamaji kitaonekana mahali tofauti kulingana na mandharinyuma yaani kulinganisha na vitu vilivyopo nyuma yake.

Paralaksi katika maisha ya kila siku

[hariri | hariri chanzo]

Tunaweza kupata mfano mmoja kwa njia ya jaribio: tukitandaza mkono na kunyosha kidole gumba na kukitazama mara kwa jicho la kulia mara kwa jicho la kushoto tutaona vitu vilivyo katika mandharinyuma yake vitaonekana vitasogea kidogo kila unapobadili jicho.

Maana tukilenga mkono kwenye kitu fulani kama vile mti wa mbali, tutaona kidole kikisogea mara kushoto mara kulia wa mti tukikitazama kwa jicho moja tu. Katika mfano huu kidole gumba ni kiolwa kinachotazamiwa na mti unachukua nafasi ya mandharinyuma yake. Mtazamaji ni jicho moja la kushoto au la kulia. Umbali baina ya macho yetu mawili ni badiliko la mahali pa mtazamaji.

Paralaksi hutokea kila wakati lakini katika mazingira ya kawaida tumeshaizoea hadi kutoitambua. Ila paralaksi kutokana na kutazama dunia kwa macho miwili inatuwezesha kuhisi umbali.

Paralaksi kwa ufafanuzi wa jiometria

[hariri | hariri chanzo]

Hisabati ya paralaksi inatumia kanuni za trigonometria (jiometria ya pembetatu). Tunahitaji kwanza nukta mbili kwenye mstari wa msingi tunazoweza kulinganisha na vipeo A na B vya pembetatu. Kipeo C ni ni nukta ya tatu au kiolwa kinachotazamiwa. Tukijua umbali kati ya A na B pamoja na pembe kati ya mistari inayounganisha A, B na C tunaweza kukadiria umbali wa C, yaani urefu wa pande AC ya pembetatu.

Katika mfano wa kidole gumba mbele ya macho umbali wa msingi AB ni umbali kati ya macho. Kwa urefu wa wastani wa mkono kidole (=nukta ya tatu) utakuwa na pembe ya takriban nyuzi 6.

Paralaksi itakuwa kubwa zaidi kadri mstari wa msingi ni mrefu na nukta ya tatu (kiolwa kinachotazamwa) iko karibu. Vilevile kinyume: kama nukta ya tatu iko mbali na mstari wa msingi si kubwa basi paralaksi huwa ndogo.

Paralaksi inasababisha nyota (njano) kuonekana mahali tofauti ikipimwa kutoka sehemu mbili tofauti za obiti ya Dunia

Matumizi ya paralaksi kwa kukadiria umbali wa kiolwa

[hariri | hariri chanzo]

Kama umbali kati ya nukta za mstari wa msingi unajulikana na kwa kufahamu au kupima pembe ya nukta ya tatu inawezekana kukadiria umbali wake kwa kutumia hesabu ya trigonometria.

Mbinu hii unatumiwa katika fokasi ya kamera au vifaa vya kupima ardhi na hasa katika astronomia.

Paralaksi katika astronomia

[hariri | hariri chanzo]
Namna ya kupima paralaksi ya nyota

Upimaji wa paralaksi ni msingi wa kujua umbali kutoka Dunia hadi sayari na nyota.

Paralaksi inatambuliwa kirahisi kwa Mwezi kwa sababu uko karibu nasi kuliko violwa vingine vya angani. Mwezi unaonekana mbele ya nyota tofauti ukiangaliwa kutoka sehemu za mbali za Dunia kwa mfano kutoka Afrika Kusini na Ulaya. Hii ni pia sababu ya kwamba kupatwa kwa Jua kunaonekana kuwa wa aina tofauti kutoka sehemu mbalimbali za Dunia. Kwa mfano kama Jua linapatwa kiasi tu pale tulipo tukio hilohilo linaweza kuonekana kama kupatwa kamili kwenye sehemu kusini au kaskazini zaidi kutoka kwetu.

Paralaksi ya sayari kama Zuhura itakuwa ndogo zaidi kwa sababu sayari hii iko mbali zaidi kuliko Mwezi hivyo tofauti mbele za nyota za mandharinyuma ni kiasi tu ikitazamwa kutoka sehemu tofauti za Dunia. Mpito wa Zuhura mbele ya uso wa Jua ulileta nafasi ya kupima paralaksi linganifu na ukingo wa Jua na hivyo kuwa msingi kwa makadirio ya kwanza kwa ajili ya kujua kizio astronomia. Hapa kipenyo cha Dunia kinachojulikana kilikuwa ni kipimo cha mstari wa msingi.

Kwa kupima umbali wa nyota nusukipenyo cha obiti ya Dunia ni mstari wa msingi. Paralaksi ni pembe kati ya mstari wa nusukipenyo hii na nyota inayotazamwa. Kama paralaksi hii inalingana na sekunde moja ya tao yaani sehemu ya 1/3600 ya nyuzi moja basi umbali wake ni kilomita bilioni 31 au miakanuru 3.26. Umbali huu huitwa pia kama parsek moja na hiki ni kiwango kinachotumiwa mara nyingi na wanaastronomia kutaja umbali wa nyota za mbali.

Paralaksi ya nyota ni ndogo hivyo haikutambuliwa kwa muda mrefu. Mjerumani Friedrich Wilhelm Bessel alifaulu mara ya kwanza kupima mabadiliko ya nyota 61 Cygni kwenye mwaka 1838 kwa kulinganisha vipimo mbalimbali alivyofanya kila baada ya nusu mwaka. Alifikia 0.31" na kiwango kinachofikiwa leo kwa vifaa bora ni 0.29" kinacholingana na miakanuru 11.

Kwa nyota za mbali zaidi ni vigumu zaidi kupata vipimo kamili. Chombo cha angani Hipparcos (High Precision Parallax Collecting Satellite) cha taasisi ya ESA kilichorushwa kwenye anga ya nje mwaka 1989 kiliweza kuleta vipimo vipya kwa nyota 118,000. Tangu mwaka 2013 chombo cha Gaia kinaendelea na vipimo vya bilioni 1 ya nyota.

  • Hirshfeld, Alan w. (2001). Parallax: The Race to Measure the Cosmos. New York: W. H. Freeman. ISBN 0-7167-3711-6. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help)
  • Whipple, Fred L. (2007). Earth Moon and Planets. Read Books. ISBN 1-4067-6413-2. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help).
  • Zeilik, Michael A.; Gregory, Stephan A. (1998). Introductory Astronomy & Astrophysics (tol. la 4th). Saunders College Publishing. ISBN 0-03-006228-4. {{cite book}}: Invalid |ref=harv (help).

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]