Mpito wa Zuhura

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Mahali pa Dunia, Jua na Zuhura wakati wa mpito wa Zuhura
Mpito wa Zuhura kwenye mwaka 2004
Msitari ya mpito wa Zuhura jinsi ilivyoonekana mwaka 1769 kwa mtazamaji huko Tahiti (nyekundu) na Vardø - Norwei (buluu). Kwa mtazamaji wa Tahiti Zuhura ilikuwa na njia fupi na kupita jua haraka zaidi. Tofauti kati ya vipimo mbalimbali iliruhusu kukadiria umbali wa Zuhura.

Mpito wa Zuhura mbele ya jua (ing. transit of Venus) unatokea wakati sayari Zuhura (Venus) inapita katika mstari baina ya jua na dunia.

Hii inalingana na kupatwa kwa jua kisehemu. Ilhali Zuhura iko mbali inaonekana ndogo na kufunika sehemu ndogo ya jua tu kwa mtazamaji kwenye dunia.

Sayari ya Zuhura wakati huu inaonekana kama duara ndogo nyeusi inayopita polepole kwenye jua. Kwa kawaida mpito mmoja hudumu masaa kadhaa.

Mpito uliopita ulitokea mwaka 2012, kabla ya hapo 2004. Mipito ijayo itatokea Disemba 2117 na Disemba 2125. Mpito wa mwaka 2012 ilirekodiwa ilitazamiwa kwenye intaneti.[1]

Mipito ya Zuhura inarudia kwa kufuata mfumo wa jozi ya mipito 2 kwa tofauti ya miaka 8; jozi hizi zina tofauti za miaka 121.5 na miaka 105.5. Baada ya miaka 243 yote inarudia.

Mtaalamu wa kwanza aliyetabiri mpito wa Zuhura kwa mwaka 1639 alikuwa Johannes Kepler lakini alifariki kabla ya tukio hivyo hakuona mwenyewe. Utabiri wake ulithebitishwa miaka 8 baadaye na Waingereza Jeremia Horrocks na William Crabtree wakati wa mpito wa pili tarehe 4 Disemba 1639.

Edmond Halley alitambua mwaka 1715 ya kwamba upimaji wa mpito wa Zuhura unaweza kuleta data za kuelewa umbali kati ya jua na dunia. Kutokana na makadirio yake jozi ya mipito iliyofuata kwenye miaka 1761 na 1769 iliangaliwa na wanaastronomia wengi waliojiandaa na kusafiri kwenda maeneo tofauti ya dunia ili kupata vipimo vyenye nyuzi tofauti kati ya mtazamaji na jua. Safari mashuhuri ya nahodha na mpelelezi James Cook ilikuwa na lengo kuu kuwapeleka wanaastronomia hadi visiwa vya Tahiti kwa kutazama na kupima mpito huu.


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. {http://www.exploratorium.edu/venus/ Webcast of the transit of Venus], tovuti ya exploratorium.edu. iliangaliwa Aprili 2017