Johannes Kepler

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kepler mwaka 1610.
Sanamu ya Tycho Brahe na Johannes Kepler mjini Prague.

Johannes Kepler (27 Desemba 157115 Novemba 1630) alikuwa mtaalamu wa astronomia, hisabati, theolojia na muziki kutoka nchini Ujerumani.

Amekuwa maarafu hasa kwa sababu alitambua kanuni za mwendo wa sayari zikilizunguka Jua.

Kazi yake

Astronomiae pars optica

Alianza masomo yake kwenye chuo kikuu cha Tuebingen katika fani ya theolojia akilenga kuwa mchungaji. Pamoja na theolojia alisoma pia hisabati halafu akafuata mwito wa kuwa mwalimu wa hisabati kwenye chuo cha Kiprotestanti mjini Graz (Austria). Baadaye aliitiwa Praha (leo nchini Ucheki) kama msaidizi wa Tycho Brahe aliyekuwa mwanahisabati rasmi wa Kaisari Rudolph II. Baadaye Kepler alipewa wajibu huu.

Kepler alitambua ya kwamba makadirio ya Nikolaus Kopernikus yalionyesha hali halisi, maana yake sayari pamoja na dunia zinazunguka jua. Hadi wakati ule wataalamu waliamini ya kwamba dunia yetu iko katikati ya ulimwengu na jua pamoja na sayari zinazunguka dunia.

Kanuni za mwendo wa sayari

  1. Kanuni ya kwanza inasema sayari inatembea njia yenye umbo la duaradufu, si duara kamili, ikizungukia jua. Kabla ya Kepler wanaastronomia waliona njia ya sayari ni duara kamili.
  2. Kanuni ya pili inasema ya kwamba sayari inaongeza mwendo ikikaribia Jua, lakini inapunguza mwendo ikienda mbali na Jua.
  3. Kanuni ya tatu inaeleza ya kwamba sayari iliyo karibu na Jua ina kasi kubwa kuliko sayari ambayo ipo mbali.

Kwa kanuni zake aliweza kutabiri mahali pa sayari angani vizuri kushinda wataalamu wote waliomtangulia.

Sala yake

“Kwako wewe, ambaye kwa mwanga wa uasilia unachochea ndani mwetu hamu ya neema yako ili tuweze kufurahia utukufu wako, kwako natoa shukrani, Bwana wangu na Mungu wangu, kwa sababu umenifanya kuonja furaha na raha katika vile vyote ulivyoviumba, katika vile vyote vilivyo kazi ya mikono yako azizi. Tazama, ee Bwana, nimemaliza kazi hii iliyokuwa wito wangu. Ili kuifanya nimetumia ile nguvu ya akili uliyonijalia wewe. Nimewaonyesha binadamu ukuu wa kazi yako, au walau sehemu ile ya ukuu wako usio na mipaka ambayo akili yako imeweza kuelewa.”[1]

Tanbihi

  1. Mwishoni mwa kitabu Harmonices mundi, 1618.

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons