Sayari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Sayari za mfumo wa jua letu; ukubwa unaonyesha uhusiano halisi kati ya sayari lakini umbali kati ya sayari hauonyeshwi

Sayari ni gimba la angani kubwa linalozunguka jua na kung'aa kutokana na nuru ya jua iliyoakisiwa, tofauti na nyota na jua zinazong'aa pekee yake.

Katika sayari viumbe mbalimbali vinapatikana, lakini dunia tu ina viumbe hai.

Sayari za jua letu[hariri | hariri chanzo]

Jua letu lina sayari nane ambazo ni Utaridi (Mercurius), Zuhura (pia: Ng'andu; Venus), Dunia yetu (Earth), Mirihi (Mars), Mshtarii (Jupiter), Zohali (Saturnus), Uranus na Neptun. Toka mwaka 1930 hadi Agosti 2006 Pluto ilikuwa ikitambulika kama sayari hivyo kufanya idadi ya sayari zinazojulikana kuwa tisa. Hata hivyo chama chenye mamlaka ya masuala ya sayari na nyota, International Astronomical Union kimetangaza rasmi kuwa Pluto sio sayari na kuiita sayari kibeti.

Sayari tano za Utaridi, Zuhura, Meriki, Mshtarii na Zohari [1] huonekana kwa macho kama nyota angani. Lakini tangu zamani zilitambuliwa kuwa tofauti kwa sababu hazikai mahali palepale kama nyota ya kawaida bali huhamahama angani. Kutokana na tabia hii zimetazamiwa mara nyingi kuwa na nguvu za pekee au hata kuwa miungu. Unajimu imetumia mwendo wa sayari zinazoonekana kwa macho kama msingi muhimu wa makadirio yao.

Sayari nyingine katika mfumo wa jua zimetambuliwa tangu kutokea kwa astronomia ya kisayansi kwa darubini. Hizi ni Uranus na Neptun. Katika lugha ya Kiswahili sayari zinazoonekana kwa macho huwa na majina ya asili ya Kiarabu isipokuwa Zuhura ina jina la Kibantu la Ng'andu pamoja na jina la asili ya Kiarabu. Majina mengine ni ya asili ya Kilatini.

Jumla ya jua, sayari zote 8 pamoja na miezi yao, sayari kibete, vimondo, nyotamkia na asteroidi inaitwa mfumo wa jua.

Aina za sayari[hariri | hariri chanzo]

Sayari za jua letu hutofautiana kwa ukubwa na muundo. Mshtarii (Jupiter) ni sayari kuwba na masi yake ni mara 318 masi ya dunia yetu. Sayari ndogo ni Utaridi na masi yake ni takriban nusu ya dunia.

Kutokana na umbali tunatofautisha "sayari za ndani" kuanzia Utaridi (Mercurius) hadi ukanda wa asteroidi, halafu "sayari za nje" kuanzia Mshtarii (Jupiter) hadi Uranus.

Muundo wa sayari ni tofauti; kuna vikundi kulingana na mata inayojenga sayari:

  • Sayari za mwamba: sayari hizi zina muundo unaofanana na dunia yetu; asilimia kubwa ya masi ni mwamba. Hizi ni sayari za ndani za mfumo wa jua letu. Zote ni ndogo kuliko sayari za nje.
  • Sayari jitu za gesi: sayari hizi kama Mshtarii (Jupiter) na Zohali (Saturnus) ni kubwa na zimefanywa na hidrojeni na heli. Masi ya Mshtarii ni mara 318 ile ya dunia, Zohali mara 95. Ilhali sayari hizi ni baridi kutokana na umbali mkubwa na jua, hidrojeni inatokea kwa kiasi kikubwa katika hali mango na kwenye sehemu za ndani hidrojeni ina tabia kama metali kutokana na shindikizo kubwa.
  • Sayari jitu za barafu: hizi ni Uranus na Neptun. Ni kubwa kuliko dunia, lakini si kama sayari jitu za gesi; Uranus huwa na masi 14 za dunia, Neptun na masi 17 za dunia. Ganda la nje ni mchanganyiko wa hidrojeni na methani, na sehemu za ndani ni barafu ya maji na methani.

Sayari nje ya mfumo wa jua letu[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wa astronomia wamegundua sayari za nje (ing. exoplanets) yaani sayari zilizopo nje ya mfumo wa jua letu zinazozunguka nyota mbalimbali. Kutokana na umbali mkubwa na matatizo ya utazamaji kwa muda mrefu hapakuwa na uhakika kama nyota kuwa na sayari ni jambo la kawaida angani au kama sayari ni chache tu. Hadi Novemba 2015 kuwepo kwa sayari 1983 kumethebitishwa na kati ya hizi mifumo ya sayari 491 imetambuliwa ambako ni zaidi ya sayari 1 zinapatikana.[2]

Nyingi kati ya hao zilikuwa na ukubwa kufanana na Mshtarii au kubwa zaidi. Lakini sayari ndogo zaidi zimetambuliwa pia. [3]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1].
    Menginevyo kuhusu mchangayiko wa majina ya sayari anagalia ukurasa wa majadiliano.
  2. Kamusi ya sayari za nje kwenye intaneti, ilizatamiwa 19 Novemba 2015
  3. Schneider, Jean (10 Septemba 2011). Interactive Extra-solar Planets Catalog. The Extrasolar Planets Encyclopaedia. Iliwekwa mnamo 2012-01-30.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Mfumo wa jua na sayari zake
Jua - Utaridi - Zuhura - Dunia (Mwezi) - Mirihi - Mshtarii - Zohali - Uranus - Neptun
Sun - Mercury - Venus - Earth (Moon) - Mars - Jupiter - Saturn - Uranus - Neptune
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Sayari kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.