Nenda kwa yaliyomo

Sayari-nje

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Idadi ya Sayari za Nje, kufuatana na mwaka wa kugunduliwa hadi Septemba 2014.

Sayari-nje au Sayari ya nje (kwa Kiingereza "exoplanet", au "extrasolar planet") ni sayari inayozunguka nyota isiyo Jua letu. Iko nje ya mfumo wetu wa Jua.

Mnamo Aprili 2019 zaidi ya sayari-nje 4000 zinazozunguka nyota mbalimbali zimetambuliwa tayari. [1][2][3]

NASA - NPM-CalTek - M. Russo & A. Santaguida 2022

Wasiwasi kuhusu sayari-nje

[hariri | hariri chanzo]

Kwa muda mrefu sayari zilizoko nje ya mfumo wa Jua letu hazikujulikana. Wataalamu walitofautiana kama magimba ya namna hiyo yapo au la.

Giordano Bruno aliwaza mnamo karne ya 16 ya kwamba katika anga kuna dunia nyingi zilizo sawa na Dunia yetu.[4] Isaac Newton alifikiri pia ya kwamba sayari zinaweza kuwepo nje ya mfumo wetu. Lakini haikuwezekana kuthibitisha nadharia hizo hadi miaka ya 1990, hivyo idadi kubwa ya wanaastronomia bado walihangaika kama sayari-nje ziko au la.

Matatizo makuu ya kuthibitisha kuwepo kwa sayari-nje ni:

  • sayari ni ndogo sana zikilinganishwa na nyota
  • sayari haiwaki, yaani haina nuru yenyewe, isipokuwa inaweza kuakisi nuru ya nyota

Ugunduzi wa sayari-nje za kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1992 watafiti Aleksander Wolszczan na Dale Frail waliofanya kazi ya astronomia ya redio walitangaza kugunduliwa kwa sayari mbili zinazozunguka nyota tutusi (pulsar) PSR 1257+12.[5] Sayari hizo hazikuweza kutazamwa lakini kuwepo kwake kulikadiriwa kwa saabu watafiti walipima mabadiliko ya mwendo wa nyota yaliyoweza kuelezwa tu kutokana na masi ya karibu inayobadilisha mwendo wa kawaida. Miaka michache baadaye taarifa hii ilithibitishwa na wagunduzi wengine.

Wataalamu wa astronomia waliendelea kugundua sayari-nje zinazozunguka nyota mbalimbali. Kutokana na umbali mkubwa na matatizo ya utazamaji hakukuwa na hakika kwa muda mrefu kama sayari-nje ni jambo la kawaida angani au kama sayari ni chache tu.

Mbinu wa kutambua mpito wa sayari

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuboreshwa kwa vifaa, vipimo vya mabadiliko ya mng'aro vimeonyesha mipito ya sayari, maana wakati wa kupita kwa sayari kati ya nyota fulani na mtazamaji duniani, sayari inafunika sehemu ya nyota yake na hivyo mng'aro wake unapungua. Kiasi cha mabadiliko ya mng'aro kinaruhusu kukadiria umbali wa sayari na nyota yake na ukubwa wake. Sayari-nje nyingi zimetambuliwa kwa kutumia mbinu hii.

Kutokana na maendeleo ya darubini, tangu mwaka 2004 imewezekana kutambua moja kwa moja sayari-nje kadhaa lakini idadi yake hadi sasa ni ndogo kwa sababu ugunduzi ni mgumu.

Nyingi kati ya hizo zilikuwa na ukubwa wa kufanana na Mshtarii au zaidi. Mabadiliko ya mng'aro wakati wa mpito wa sayari mbele ya nyota ni madogo sana, hivyo si rahisi kuthibitisha mpito wa sayari ndogo inayosababisha mabadiliko madogo mno. Hata hivyo sayari ndogo zaidi kwa ukubwa kama Dunia zimetambuliwa pia.

Sizes of Kepler Planet Candidates – based on 2,740 candidates orbiting 2,036 stars as of 4 Novemba 2013 (2013 -11-04) (NASA).

Hadi tarehe 1 Aprili 2017 jumla ya sayari-nje 3,607 zilikuwa zimeshaorodheshwa katika "Extrasolar Planets Encyclopaedia"[6]

Siku hizi wataalamu wanaona idadi ya sayari ni kubwa sana. Maana mbinu ia kupima mpito wa sayari mbele ya nyota yake inaleta matokeo kwa sehemu ya nyota tu. Inatuonyesha matokeo kama bapa la mfumo wa nyota (ekliptiki yake) inalingana na mtazamo wetu kwa nyota husika; kama ekliptiki ya nyota imeinama mno kulingana na mtazamo wetu, hatuwezi kuona mpito wa sayari kutoka Dunia, hivyo hatuoni mabadiliko ya mng'aro.

  1. "Exoplanet Archive Planet Counts". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-12-12. Iliwekwa mnamo 2017-04-25.
  2. Johnson, Michele; Harrington, J.D. (Februari 26, 2014). "NASA's Kepler Mission Announces a Planet Bonanza, 715 New Worlds". NASA. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-03-01. Iliwekwa mnamo Februari 26, 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "The Habitable Exoplanets Catalog - Planetary Habitability Laboratory @ UPR Arecibo".
  4. Eli Maor (2013), uk 198
  5. Wolszczan, A.; Frail, D. A. (1992). "A planetary system around the millisecond pulsar PSR1257 + 12". Nature. 355 (6356): 145–147. Bibcode:1992Natur.355..145W. doi:10.1038/355145a0.
  6. Orodha ya Exoplanets, inataja " 3608 planets / 2702 planetary systems / 610 multiple planet systems", iliangaliwa Aprili 2017

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
  • Eli Maor (1987). "Chapter 24: The New Cosmology". To Infinity and Beyond: A Cultural History of the Infinite. Springer 2013 kupitia google books hapa