Mfumo wa jua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Jua letu na sayari zake.
Sayari nne kubwa ziliundwa hasa na gesi, nyingine ni sayari ndogo kama dunia yetu za mwamba.[1]

Mfumo wa jua (en:solar system) ni utaratibu wa jua letu, sayari na sayari kibete zinazolizunguka pamoja na miezi yao, asteroidi, meteoridi, kometi na vumbi ya angani, vyote vikishikwa na mvutano wa jua.

Utaalamu kuhusu mfumo wa jua hujadiliwa katika fani ya astronomia.

Muundo wa mfumo wa jua[hariri | hariri chanzo]

Karibu masi yote ni ya jua lenyewe, likiwa na asilimia 99.86 za masi ya mfumo wake. Kwa hiyo sayari zote kwa pamoja na asteroidi ni asilimia 0.14 tu.

Umbali kati ya jua na dunia yetu ni takriban kilomita milioni 150 mia hamsini. Umbali huu huitwa „kizio astronomia“ (en:astronomical unit AU). Sayari ya mbali ni Neptuni ambayo ina umbali wa vizio astronomia 30 thelathini kutoka jua. Magimba ya nje sana yanazunguka jua kwa umbali wa vizio astronomia 50 hamsini au zaidi.

Pamoja na sayari kuna idadi kubwa ya violwa vingine. Vingi ni vipande vidogo vya mwamba vinavyokusanyika katika kanda 3 zenye umbo la mwirino ambazo ni ukanda wa asteroidi, ukanda wa Kuiper na wingu la Oort.

Sayari hupatikana kwa vikundi viwili. Jua linazungukwa kwanza na sayari 4 nne za Utaridi, Zuhura, Dunia na Mirihi ambazo ni ndogo na ambazo ni sayari za mwamba kama dunia.

Baada ya njia mzingo wa Mirihi kuna pengo la umbali wa vizio astronomia zaidi ya tatu na nusu hadi Mshtarii. Katika pengo hili linazunguka ukanda wa asteroidi wenye violwa lakhi kadhaa pamoja na sayari kibete ya Ceres.

Nje ya ukanda wa asteroidi hufuata kundi la sayari za gesi ambazo ni kubwa kushinda sayari za ndani. Sehemu kubwa ya masi yake si mwamba bali gesi iliyoganda na kuwa imara kutokana na baridi kali.

Sayari za jua letu[hariri | hariri chanzo]

Kuna magimba 8 yanayozunguka jua letu na kuitwa sayari. Hadi Zohali (ing. Saturn) zinaonekana kwa macho na tangu zamani zilijulikana kwa majina yao. Sayari ya saba na nane ziligunduliwa tu tangu kupatikana kwa darubini. Hadi mwaka 2006 Pluto iliyopo nje ya Neptuni ilihesabiwa kuwa sayari, lakini tangu azimio la Umoja wa Wanastronomia Pluto inaitwa sasa „sayari kibete“ pamoja na nyingine, si sayari kamili tena.

Sayari ambazo zipo katika mfumo wa jua ni kama zifuatazo:

Namba zote zinazotaja sifa mbalimbali za sayari zinaonyesha kipimo kulingana na tabia za dunia yetu kuwa "1". Kuhusu majina ya sayari kadhaa kuna mkanganyiko katika kamusi na vitabu. Pale ambako jina au umbo tofauti la jina ni la kawaida linaonyeshwa katika mabano kama (jina). Majina yanayotumiwa katika vitabu kadhaa, hasa vya shule za msingi, bila kuwa na uhakika yanaonyeshwa katika mabano ya italiki pamoja na alama ya swali kama (? jina). [2]

* Utaridi ni jina la sayari ya kwanza kutokana na lugha ya Kiarabu na pia katika mapokeo ya Kiswahili tangu kale. Vitabu vingine hutumia neno "Zebaki" ambalo pia lina asili ya Kiarabu likimaanisha metali mojawapo; inaonekana limepatikana kama tafsiri ya jina la Kiingereza la sayari ya kwanza "Mercury" bila kujua historia ya majina ya sayari sita ya kwanza yaliyoingia katika Kiswahili kutoka lugha ya Kiarabu. [3]
** Zuhura - Ng'andu ni sayari ambalo kwa Kiswahili lina jina la Kibantu pamoja na jina lenye asili ya Kiarabu
*** Tazama makala ya Dunia kwa ajili ya namba halisi. Neno "ardhi" hutumika na waandishi kadhaa badala ya "dunia" wakitaka kutaja sayari ya tatu.
**** Tangu mwaka 2006 Pluto imeingizwa katika kundi la "sayari kibete" Katika vitabu vya shule ya msingi inatajwa mara nyingi kwa jina Utaridi - ambayo haiwezekani maana Pluto haikujulikana kabla ya mwaka 1931 lakini "Utaridi" ni jina linalopatikana tangu zamani kwa Kiswahili likimaanisha sayari ya kwanza.
Jina la sayari Kipenyo kwenye ikweta
kulingana na kipenyo cha dunia = 1
Masi Nusukipenyo ya mzingo wa kuzunguka jua Muda wa mzingo
(miaka)
Kuinama kwa mzingo wa kuzunguka jua
Pembenukta (°)
Muda wa siku ya sayari
(siku)
Miezi
Utaridi
[4]
0.382 0.06 0.387 0.241  7.00 58.6 0
Zuhura (Ng'andu)** 0.949 0.82 0.72 0.615  3.39 -243 0
Dunia (Ardhi)*** 1.00 1.00 1.00 1.00  0.00 1.00 1
Mirihi (Murihi, Meriki, Mars) 0.53 0.11 1.52 1.88  1.85 1.03 2
Mshtarii
[5]
11.2 318 5.20 11.86  1.31 0.414 63
Zohari (Zohali, pia Zuhali)
[6]
9.41 95 9.54 29.46  2.48 0.426 49
Uranus
[7]
3.98 14.6 19.22 84.01  0.77 -0.718 27
Neptun
[8]
3.81 17.2 30.06 164.8  1.77 0.671 13

Sayari za nyongeza?[hariri | hariri chanzo]

Katika miaka iliyopita wanaastronomia wamejadili uwezekano wa kuwepo kwa sayari za ziada katika umbali mkubwa. Imetambuliwa ya kwamba muundo wa mfumo wa jua ni kubwa kuliko wataalamu wa kale walifikiri.

Tangu kutambuliwa wa ukanda wa Kuiper ambamo Pluto ni sehemu tu inajulikana ya kwamba kuna magimba ya angani mengi yasiyoonekana kwa kirahisi kwa sababu yanapokea na kuakisia nuru kidogo sana kutoka jua.

Kuhusu magimba ya angani yaliyombali zaidi kuliko ukanda wa Kuiper hakuna uhakika bado, Lakini tangu mwaka 2012 vipimo vyipya vilisababisha kutokea kwa nadharia tele kuhusu sayari ya tisa katika umbali mkubwa sana ambyo haikutazamiwa bado.

Mwaka 2017 kiolwa cha anga kilitazamiwa kilichotoka nje ya mfumo wa jua letu. Kiolwa hiki kilichoitwa ʻOumuamua kilifika kwa njia isiyolingana na bapa la sayari za mfumo wa jua tena kwa kasi kubwa mno hivyo ilionekana si sehemu ya mfumo wetu.

Mfumo wa jiosentriki[hariri | hariri chanzo]

Ulikuwa mfumo wa sayari, jua, nyota na magimba mengine angani ambao zamani ulipendekeza kwamba vyote vinazunguka dunia, ambayo ndiyo ilichukuliwa kuwa kitovu cha ulimwengu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Hand, Eric (January 20, 2016).
  2. Linganisha ukurasa wa majadiliano:sayari
  3. kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina asilia, linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch [1]
  4. Inaitwa "Zebaki" katika kamusi kadhaa, kwa kosa la kutafsiri upya jina la Kiingereza limalomaanisha metali na pia sayari, tofauti na Kiswahili
  5. inaitwa kwa kosa "Sumbula" katika vitabu vichache; lakini Sumbula ni jina la nyota ya en:Spica
  6. Katika vitabu vichache inaitwa "Saratani" au "Satani" kwa kosa; Saratani ni jina la kundinyota ya Cancer; inaonekana kuna kosa kutokana matamshi ya kienyeshi ya jina "Saturn"
  7. Vitabu vichache vinatumia kwa kosa jina "Zohali" ambalo ni jina la sayari inayoitwa kwa Kiingereza "Saturn"
  8. Vitabu vichache vinatumia kwa kosa jina "Kausi" ambalo ni jina la kundinyota inayoitwa kwa Kiingereza "Sagittarius"
Science-symbol-2.svg Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mfumo wa jua kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.