Myeyungano wa kinyuklia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Jua linazalisha nishati yake kwa njia ya myeyungano nyuklia wa viini vya hidrojeni kuwa heli. Jua linayeyunganisha tani milioni 610 za hidrojeni katika kila sekunde kuwa tani milioni 606 za heli. Halijoto ya sentigredi milioni inahitajika kwa myeyungano.
Myeyungano wa hidrojeni - deuteri-triti (D-T) unaachisha nishati
Myeyungano D-T kuwa heli

Myeyungano wa kinyuklia (ing. Nuclear fusion, pia Uyeyunganishaji wa kinuklia[1]) ni mchakato ambamo viini 2 au zaidi vya atomu vyepesi zaidi vinaungana kuwa kiini kimoja kizito.

Masi ya kiini cha atomu kinachotokea ni ndogo kuliko jumla ya viini viwili vilivyoshiriki mle. Tofauti ya masi inabadilishwa kuwa nishati. Einstein alionyesha nishati inayotokana na badiliko hili katika fomula yake ya E=mc2|E=mc2. Hivyo myeyungano wa kinyuklia inazalisha kiasi kikubwa cha nishati.[2].

Myeyungano wa kinyuklia unatokea ndani ya nyota kama Jua letu. Katika kitovu cha Jua shinikizo kubwa ya masi yake linasababisha kutokea kwa mamilioni ya nyuzijoto.

Katika Jua letu atomi za hidrojeni zinayeyunganishwa katika mazingira ya shinikizo na joto kuu kuwa heli. Nishati inayopatikana hapa mi chanzo cha joto na nuru ya Jua. Kadri hidrojeni inapungua ndani ya nyota heli itayeyunganishwa

Myeyungano hauwezi kutokea na elementi zote. Kadri elementi za kuyeyunganiwa ni nzito zaidi mchakato huwa vigumu kutendeka na hukomea hadi chuma (Fe).

Kuanzia uzito wa chuma myeyungano unahitaji nishati zaidi kuliko kuzalisha. Elementi nzito kuliko chuma zinatokea tu katika milipuko ya nyota nova na supanova penye joto na shinikizo kubwa mno katika milipuko hii.

Mara nyota inapoishiwa elementi nyepesi kuliko chuma sehemu yake ya ndani inajikaza kuwa nyota kibete nyeupe ilhali sehemu za nje zinarushwa nje kwenye anga kama mawingu ya gesi ya ioni. Mabaki ya nyota yataendelea kupoa na mchakato wa myeyungano unakwisha polepole: nyota "inakufa". [3]

Kama masi yake ni kubwa, angalau mara kumi ya Jua letu, mlipuko na kutokea kwa nyota ya nova inaweza kutokea.

Kuna majaribio ya kibinadamu ya kuiga mchakato huu katika mitambo lakini hadi sasa haikuwezakana bado kufikia teknolojia inayoruhusu kuzalisha umeme kwa njia hii.

Hapa duniani ni vigumu kupata myeyungano kwa sababu viini vya atomu huwa na chaji chanja na chanja - chanja huwingana. Hapa nguvu kubwa inahitajika kushinda kizuizi hiki kama vile joto na shinikizo kali ndani ya Jua. Hadi sasa imekuwa vigumu kujenga mitambo inayoweza kuzalisha na kutunza joto ya nyuzi mamilioni pamoja shinikizo inayohitajika kuanzisha na kudumisha myeyungano wa nyuklia.

Lakini inawezakana kusababisha myeyungano wa kinyuklia kwa matumizi ya silaha katika bomu la hidrojeni. Katika bomu ya hidrojeni mlipuko wa bomu atomia ndogo (yaani nishati ya mwatuko nyuklia) unatumiwa ili kugonganisha viini vya atomu na kuanzisha myeyungano.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Uyeyunganishaji wa kinuklia" ni pendekezo la kamusi ya KSBFK, "myeyungano wa kinyuklia" ni pendekezo la KAST
  2. FusEdWeb | Fusion Education
  3. "Progress in Fusion". ITER.